Marko 4:21-34
Marko 4:21-34 Biblia Habari Njema (BHN)
Yesu akaendelea kuwaambia, “Je, watu huwasha taa wakaileta ndani na kuifunika kwa debe au kuiweka mvunguni? La! Huiweka juu ya kinara. Basi, kila kilichofichwa kitafichuliwa, na kila kilichofunikwa kitafunuliwa. Mwenye masikio na asikie!” Akawaambia pia, “Sikilizeni kwa makini mnachosikia! Kipimo kilekile mnachowapimia watu wengine, ndicho mtakachopimiwa; tena mtazidishiwa. Aliye na kitu atapewa zaidi; asiye na kitu, hata kile alicho nacho kitachukuliwa.” Yesu akaendelea kusema, “Ufalme wa Mungu ni kama ifuatavyo. Mtu hupanda mbegu shambani. Usiku hulala, mchana yu macho na wakati huo mbegu zinaota na kukua; yeye hajui inavyofanyika. Udongo wenyewe huiwezesha mimea kukua na kuzaa matunda: Kwanza huchipua jani changa, kisha suke, na mwishowe nafaka ndani ya suke. Nafaka inapoiva, huyo mtu huanza kutumia mundu wake, maana wakati wa mavuno umefika.” Tena, Yesu akasema, “Tuufananishe Ufalme wa Mungu na nini? Tuueleze kwa mifano gani? Ni kama mbegu ya haradali ambayo ni ndogo kuliko mbegu zote. Lakini ikisha pandwa, huota na kuwa mmea mkubwa kuliko mimea yote ya shambani. Matawi yake huwa makubwa hata ndege wa angani huweza kujenga viota vyao katika kivuli chake.” Yesu aliwahubiria ujumbe wake kwa mifano mingine mingi ya namna hiyo; aliongea nao kadiri walivyoweza kusikia. Hakuongea nao chochote bila kutumia mifano; lakini alipokuwa pamoja na wanafunzi wake peke yao alikuwa akiwafafanulia kila kitu.
Marko 4:21-34 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Akawaambia, Mwaonaje? Taa huja ili kuwekwa chini ya pishi, au mvunguni? Si kuwekwa juu ya kiango? Kwa maana hakuna neno lililositirika, ila kusudi lije kudhihirika; wala hakuna lililofichwa, ila kusudi lije kutokea wazi. Mtu akiwa na masikio ya kusikilia, na asikie. Akawaambia, Angalieni msikialo; kipimo kile mpimacho ndicho mtakachopimiwa, na tena mtazidishiwa. Kwa maana mwenye kitu atapewa, naye asiye na kitu, hata kile alicho nacho atanyang'anywa. Akasema, Ufalme wa Mungu, mfano wake ni kama mtu aliyemwaga mbegu juu ya nchi; akawa akilala na kuondoka, usiku na mchana, nayo mbegu ikamea na kukua, asivyojua yeye. Maana nchi huzaa yenyewe; kwanza jani, tena suke, kisha ngano pevu katika suke. Hata matunda yakiiva, mara atapeleka mundu, kwa kuwa mavuno yamefika. Akasema, Tuulinganishe na nini ufalme wa Mungu? Au tuutie katika mfano gani? Ni kama punje ya haradali, ambayo ipandwapo katika nchi, ingawa ni ndogo kuliko mbegu zote zilizo katika nchi, lakini ikiisha kupandwa hukua, ikawa kubwa kuliko miti yote ya mboga, ikafanya matawi makubwa; hata ndege wa angani waweza kukaa chini ya uvuli wake. Kwa mifano mingi ya namna hii alikuwa akisema nao neno lake, kwa kadiri walivyoweza kulisikia; wala pasipo mfano hakusema nao; lakini akawaeleza wanafunzi wake mwenyewe mambo yote kwa faragha.
Marko 4:21-34 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Akawaambia, Mwaonaje? Taa huja ili kuwekwa chini ya pishi, au mvunguni? Si kuwekwa juu ya kiango? Kwa maana hakuna neno lililositirika, ila makusudi lije likadhihirika; wala hakuna lililofichwa, ila makusudi lije likatokea wazi. Mtu akiwa na masikio ya kusikilia, na asikie. Akawaambia, Angalieni msikialo; kipimo kile mpimacho ndicho mtakachopimiwa, na tena mtazidishiwa. Kwa maana mwenye kitu atapewa, naye asiye na kitu, hata kile alicho nacho atanyang’anywa. Akasema, Ufalme wa Mungu, mfano wake ni kama mtu aliyemwaga mbegu juu ya nchi; akawa akilala na kuondoka, usiku na mchana, nayo mbegu ikamea na kukua, asivyojua yeye. Maana nchi huzaa yenyewe; kwanza jani, tena suke, kisha ngano pevu katika suke. Hata matunda yakiiva, mara atapeleka mundu, kwa kuwa mavuno yamefika. Akasema, Tuulinganishe na nini ufalme wa Mungu? Au tuutie katika mfano gani? Ni kama punje ya haradali, ambayo ipandwapo katika nchi, ingawa ni ndogo kuliko mbegu zote zilizo katika nchi, lakini ikiisha kupandwa hukua, ikawa kubwa kuliko miti yote ya mboga, ikafanya matawi makubwa; hata ndege wa angani waweza kukaa chini ya uvuli wake. Kwa mifano mingi ya namna hii alikuwa akisema nao neno lake, kwa kadiri walivyoweza kulisikia; wala pasipo mfano hakusema nao; lakini akawaeleza wanafunzi wake mwenyewe mambo yote kwa faragha.
Marko 4:21-34 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Akawaambia, “Je, taa huwashwa na kufunikwa chini ya kikapu au mvunguni mwa kitanda? Je, haiwashwi na kuwekwa juu ya kinara chake? Kwa kuwa hakuna kilichofichika ambacho hakitafunuliwa, wala hakuna jambo lolote la siri ambalo halitaletwa nuruni. Mwenye masikio ya kusikia, na asikie.” Naye akawaambia, “Kuweni waangalifu na yale mnayosikia. Kipimo kile mpimacho, ndicho mtakachopimiwa ninyi, hata na zaidi. Kwa maana kila mtu aliye na kitu atapewa zaidi, naye atakuwa navyo tele. Lakini yule asiye na kitu, hata kile alicho nacho atanyangʼanywa.” Pia akawaambia, “Ufalme wa Mungu unafanana na mtu apandaye mbegu shambani. Akiisha kuzipanda, usiku na mchana, akiwa amelala au ameamka, mbegu huota na kukua pasipo yeye kujua ikuavyo. Udongo huifanya iote kuwa mche, halafu suke, kisha nafaka kamili kwenye suke. Lakini nafaka inapokuwa imekomaa, mara mkulima huingia shambani na mundu wa kuvunia, maana mavuno yamekuwa tayari.” Akawaambia tena, “Tuufananishe Ufalme wa Mungu na nini? Au tutumie mfano gani ili kuueleza? Ni kama punje ya haradali, ambayo ni mbegu ndogo sana kuliko mbegu zote zinazopandwa ardhini. Lakini ikishaota, hukua ikawa mmea mkubwa kuliko yote ya bustanini, ikawa na matawi makubwa hata ndege wa angani wanaweza kujenga viota kwenye matawi yake.” Kwa mifano mingine mingi kama hii Yesu alinena nao neno lake, kwa kadiri walivyoweza kulielewa. Hakusema nao neno lolote pasipo mfano. Lakini alipokuwa na wanafunzi wake, aliwafafanulia kila kitu.