Marko 4:1-8
Marko 4:1-8 Biblia Habari Njema (BHN)
Yesu alianza kufundisha tena akiwa kando ya ziwa. Umati mkubwa wa watu ulimzunguka hata ikambidi aingie katika mashua na kuketi. Watu wote wakawa wamekaa katika nchi kavu, kando ya ziwa. Aliwafundisha mambo mengi kwa mifano, na katika mafundisho yake aliwaambia, “Sikilizeni! Mpanzi alikwenda kupanda mbegu. Alipokuwa akipanda mbegu, nyingine zilianguka njiani, ndege wakaja wakazila. Nyingine zilianguka penye mawe pasipokuwa na udongo mwingi, zikaota mara kwa kuwa udongo haukuwa na kina. Jua lilipochomoza, zikateketea; na kwa kuwa mizizi yake haikuwa na nguvu, zikanyauka. Nyingine zilianguka kwenye miti ya miiba, nayo ikakua na kuzisonga, nazo hazikuzaa nafaka. Nyingine zilianguka katika udongo mzuri, zikamea, zikakua na kuzaa: Moja punje thelathini, moja sitini na nyingine mia.”
Marko 4:1-8 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Yesu akaanza kufundisha tena kando ya bahari. Umati wa watu uliokuwa umekusanyika kumzunguka ulikuwa mkubwa, kiasi kwamba ilimbidi Yesu aingie kwenye mashua iliyokuwa baharini na kuketi humo, nao watu wote walikuwa ufuoni mwa bahari. Akawafundisha mambo mengi kwa mifano, naye katika mafundisho yake akasema: “Sikilizeni! Mpanzi alitoka kwenda kupanda mbegu zake. Alipokuwa akitawanya mbegu, nyingine zilianguka kando ya njia, nao ndege wakaja na kuzila. Nyingine zilianguka kwenye ardhi yenye mwamba isiyo na udongo wa kutosha. Zikaota haraka, kwa kuwa udongo ulikuwa haba. Lakini jua lilipozidi, mimea ikanyauka na kukauka kwa kuwa mizizi yake haikuwa na kina. Mbegu nyingine zilianguka kwenye miiba, nayo miiba hiyo ikakua, ikaisonga hiyo mimea, hivyo haikutoa mazao. Mbegu nyingine zilianguka kwenye udongo mzuri, zikaota vizuri na kukua, zikatoa mazao, moja mara thelathini, nyingine mara sitini, na nyingine mara mia moja.”
Marko 4:1-8 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Akaanza kufundisha tena kando ya ziwa. Kundi kubwa sana la watu wakamkusanyikia, hata yeye akapanda katika mashua, akakaa ziwani, watu wote walikuwa katika nchi kavu kando ya ziwa. Akawafundisha mambo mengi kwa mifano, akawaambia katika mafundisho yake, Sikilizeni; Tazama, mpanzi alitoka kwenda kupanda; ikawa alipokuwa akipanda, mbegu nyingine ilianguka kando ya njia, wakaja ndege wakaila. Nyingine ikaanguka penye mwamba, pasipokuwa na udongo mwingi; mara ikaota kwa kuwa na udongo haba; hata jua lilipozuka iliungua, na kwa kuwa haina mizizi ikanyauka. Nyingine ikaanguka penye miiba; ile miiba ikamea ikaisonga, isizae matunda. Nyingine zikaanguka penye udongo ulio mzuri, zikazaa matunda, zikimea na kukua, na kuzaa, moja thelathini, moja sitini, na moja mia.
Marko 4:1-8 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Akaanza kufundisha tena kando ya bahari. Wakamkusanyikia mkutano mkubwa mno, hata yeye akapanda chomboni, akakaa baharini, mkutano wote ulikuwako juu ya nchi kavu kando ya bahari. Akawafundisha mambo mengi kwa mifano, akawaambia katika mafundisho yake, Sikilizeni; Tazama, mpanzi alitoka kwenda kupanda; ikawa alipokuwa akipanda, mbegu nyingine ilianguka kando ya njia, wakaja ndege wakaila. Nyingine ikaanguka penye mwamba, pasipokuwa na udongo mwingi; mara ikaota kwa kuwa na udongo haba; hata jua lilipozuka iliungua, na kwa kuwa haina mizizi ikanyauka. Nyingine ikaanguka penye miiba; ile miiba ikamea ikaisonga, isizae matunda. Nyingine zikaanguka penye udongo ulio mzuri, zikazaa matunda, zikimea na kukua, na kuzaa, moja thelathini, moja sitini, na moja mia.