Marko 15:1-47
Marko 15:1-47 Biblia Habari Njema (BHN)
Kulipopambazuka, makuhani wakuu walifanya shauri pamoja na wazee, waalimu wa sheria na Baraza lote, wakamfunga Yesu pingu, wakampeleka na kumkabidhi kwa Pilato. Pilato akamwuliza Yesu, “Je, wewe ni Mfalme wa Wayahudi?” Yesu akajibu, “Wewe umesema.” Makuhani wakuu wakamshtaki Yesu mambo mengi. Pilato akamwuliza tena Yesu, “Je, hujibu neno? Tazama wanavyotoa mashtaka mengi juu yako.” Lakini Yesu hakujibu neno, hata Pilato akashangaa. Kila wakati wa sikukuu ya Pasaka, Pilato alikuwa na desturi ya kuwafungulia mfungwa mmoja waliyemtaka. Basi, kulikuwa na mtu mmoja aitwaye Baraba, ambaye alikuwa amefungwa pamoja na waasi wengine kwa kusababisha uasi na mauaji. Watu wengi wakamwendea Pilato wakamwomba awafanyie kama kawaida yake. Pilato akawauliza, “Je, mwataka niwafungulieni Mfalme wa Wayahudi?” Alisema hivyo kwa sababu alijua wazi kwamba makuhani wakuu walimkabidhi Yesu kwake kwa sababu ya wivu. Lakini makuhani wakuu wakawachochea watu wamwombe Pilato awafungulie Baraba. Pilato akawauliza tena, “Basi, sasa mwataka nifanye nini na mtu huyu mnayemwita Mfalme wa Wayahudi?” Watu wote wakapaza sauti tena: “Msulubishe!” Lakini Pilato akawauliza, “Kwa nini! Amefanya ubaya gani?” Lakini wao wakazidi kupaza sauti, “Msulubishe!” Pilato alitaka kuuridhisha huo umati wa watu; basi, akamwachilia Baraba kutoka gerezani. Akaamuru Yesu apigwe viboko, kisha akamtoa asulubiwe. Kisha askari walimpeleka Yesu ndani ukumbini, katika ikulu, wakakusanya kikosi kizima cha askari. Wakamvika vazi la rangi ya zambarau, wakasokota taji ya miiba, wakamwekea kichwani. Wakaanza kumsalimu, “Shikamoo Mfalme wa Wayahudi!” Wakampiga kichwani kwa mwanzi, wakamtemea mate; wakampigia magoti na kumsujudia. Baada ya kumdhihaki, walimvua lile joho, wakamvika nguo zake, kisha wakampeleka kumsulubisha. Walipokuwa njiani, walikutana na mtu mmoja aitwaye Simoni, mwenyeji wa Kurene. Yeye alikuwa baba yao Aleksanda na Rufo, na wakati huo alikuwa akitoka shambani. Basi, wakamlazimisha achukue msalaba wa Yesu. Kisha wakampeleka Yesu mpaka mahali palipoitwa Golgotha, maana yake, mahali pa Fuvu la Kichwa. Wakampa divai iliyochanganywa na manemane, lakini yeye alikataa kunywa. Basi, wakamsulubisha, wakagawana mavazi yake kwa kuyapigia kura waamue nani angepata nini. Ilikuwa saa tatu asubuhi walipomsulubisha. Na shtaka dhidi yake lilikuwa limeandikwa, “Mfalme wa Wayahudi.” Pamoja naye waliwasulubisha wanyanganyi wawili, mmoja upande wake wa kulia na mwingine upande wake wa kushoto. [ Hapo yakatimia Maandiko Matakatifu yanayosema, “Aliwekwa kundi moja na waovu.”] Watu waliokuwa wanapita mahali hapo walimtukana, wakitikisa vichwa vyao na kusema, “Aha! Wewe mwenye kuvunja hekalu na kulijenga kwa siku tatu! Sasa, shuka msalabani ujiokoe mwenyewe!” Nao makuhani wakuu pamoja na waalimu wa sheria walimdhihaki wakisema, “Aliwaokoa wengine, lakini kujiokoa mwenyewe hawezi! Ati yeye ni Kristo, Mfalme wa Israeli! Basi, na ashuke kutoka msalabani ili tuone na kuamini.” Hata watu wale waliosulubiwa pamoja naye walimtukana. Tangu saa sita mchana mpaka saa tisa giza likaikumba nchi yote. Saa tisa alasiri Yesu akalia kwa sauti kubwa, akasema, “Eloi, Eloi, lema sabakthani?” Maana yake, “Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?” Baadhi ya watu waliosimama pale waliposikia hivyo, walisema, “Sikiliza! Anamwita Elia.” Mtu mmoja akakimbia, akaichovya sifongo katika siki, akaiweka juu ya mwanzi, akampa anywe akisema, “Hebu tuone kama Elia atakuja kumteremsha msalabani!” Yesu akapaza sauti kubwa, akakata roho. Basi, pazia la hekalu likapasuka vipande viwili toka juu mpaka chini. Jemadari mmoja aliyekuwa amesimama mbele yake alipoona kwamba Yesu alikata roho namna hiyo, akasema, “Kweli mtu huyu alikuwa Mwana wa Mungu!” Walikuwako pia wanawake waliotazama kwa mbali, miongoni mwao akiwa Maria Magdalene, Salome, na Maria mama wa kina Yakobo mdogo na Yose. Hawa walimfuata Yesu alipokuwa Galilaya na kumtumikia. Kulikuwa na wanawake wengine wengi waliokuja Yerusalemu pamoja naye. Wakati wa jioni ulikuwa umekwisha fika. Hiyo ilikuwa siku ya Maandalio, yaani siku inayotangulia Sabato. Hapo akaja Yosefu mwenyeji wa Arimathaya, mjumbe wa Baraza Kuu, aliyeheshimika sana. Yeye pia alikuwa anatazamia kuja kwa ufalme wa Mungu. Basi, alimwendea Pilato bila woga, akaomba apewe mwili wa Yesu. Pilato alishangaa kusikia kwamba Yesu alikuwa amekwisha kufa. Basi, akamwita jemadari, akamwuliza kama Yesu alikuwa amekufa kitambo. Pilato alipoarifiwa na huyo jemadari kwamba Yesu alikuwa amekwisha kufa, akamruhusu Yosefu kuuchukua mwili wake. Hapo Yosefu akanunua sanda ya kitani, akauteremsha chini huo mwili, akauzungushia sanda. Akauweka katika kaburi lililokuwa limechongwa mwambani, kisha akavingirisha jiwe kubwa mbele ya mlango. Nao Maria Magdalene na Maria mama yake Yose walipaona hapo alipolazwa.
Marko 15:1-47 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Mara kulipokuwa asubuhi wakuu wa makuhani walifanya shauri pamoja na wazee na waandishi na baraza nzima, wakamfunga Yesu, wakamchukua, wakamleta mbele ya Pilato. Pilato akamwuliza, Wewe ndiwe mfalme wa Wayahudi? Akajibu, akamwambia, Wewe wasema. Nao wakuu wa makuhani walikuwa wakimshitaki mambo mengi. Pilato akamwuliza tena akisema, Hujibu neno? Tazama ni mambo mangapi wanayokushitaki! Wala Yesu hakujibu neno tena, hata Pilato akastaajabu. Basi wakati wa sikukuu huwafungulia mfungwa mmoja, wamwombaye. Palikuwa na mtu aitwaye Baraba, aliyefungwa pamoja na waasi, waliosababisha mauaji katika uhalifu huo. Makutano wakaja, wakaanza kuomba awafanyie kama vile alivyozoea. Pilato akawajibu, akisema, Je! Mnataka niwafungulie mfalme wa Wayahudi? Kwa maana alitambua ya kuwa wakuu wa makuhani wamemtoa kwa husuda. Lakini wakuu wa makuhani wakawachochea watu, kuwa afadhali awafungulie Baraba. Pilato akajibu tena akawaambia, Basi nimtendeje huyu mnayemnena kuwa ni mfalme wa Wayahudi? Wakapiga kelele tena, Msulubishe. Pilato akawaambia, Kwani ni ubaya gani alioutenda? Wakazidi sana kupiga kelele, Msulubishe. Pilato kwa kupenda kuwaridhisha watu, akawafungulia Baraba; akamtoa Yesu, baada ya kumpiga mijeledi, ili asulubiwe. Nao askari wakamchukua ndani ya behewa, ndiyo Praitorio (yaani, makao makuu ya mtawala), wakakusanya pamoja kikosi kizima. Wakamvika vazi la rangi ya zambarau, wakasokota taji la miiba, wakamtia kichwani; wakaanza kumsalimu, Salamu, Mfalme wa Wayahudi! Wakampiga mwanzi wa kichwa, wakamtemea mate, wakapiga magoti, wakamsujudia. Hata wakiisha kumdhihaki, wakamvua lile vazi la rangi ya zambarau, wakamvika mavazi yake mwenyewe; wakampeleka nje ili wamsulubishe. Wakamshurutisha mtu aliyekuwa akipita, akitoka mashambani, Simoni Mkirene, baba yao Iskanda na Rufo, ili auchukue msalaba wake. Wakamleta mpaka mahali paitwapo Golgotha, yaani, Fuvu la kichwa. Wakampa mvinyo iliyotiwa manemane, asiipokee. Wakamsulubisha, wakagawa mavazi yake, wakayapigia kura kila mtu atwae nini. Basi ilikuwa saa tatu, nao wakamsulubisha. Palikuwa na anwani ya mashitaka yake iliyoandikwa juu, MFALME WA WAYAHUDI. Na pamoja naye walisulubisha wanyang'anyi wawili, mmoja mkono wake wa kulia na mmoja mkono wake wa kushoto. [ Basi andiko likatimizwa linenalo, Alihesabiwa pamoja na waasi.] Nao waliokuwa wakipita njiani wakamtukana, wakitikisatikisa vichwa, wakisema, Ahaa! Wewe mwenye kulivunja hekalu na kulijenga katika siku tatu, jiponye nafsi yako, ushuke msalabani. Kadhalika na wakuu wa makuhani wakamdhihaki wao kwa wao, pamoja na waandishi, wakisema, Aliponya wengine; hawezi kujiponya mwenyewe. Kristo, mfalme wa Israeli, na ashuke sasa msalabani tupate kuona na kuamini. Hata wale waliosulubiwa pamoja naye wakamsuta. Na ilipokuwa saa sita, palikuwa na giza juu ya nchi yote, hadi saa tisa. Na saa tisa Yesu akapaza sauti yake kwa nguvu, Eloi, Eloi, lama sabakthani? Maana yake, Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha? Na baadhi yao waliosimama pale, walisema, Tazama, anamwita Eliya. Na mmoja akaenda mbio, akajaza sifongo siki, akaitia juu ya mwanzi, akamnywesha, akisema, Acheni, na tuone kwamba Eliya anakuja kumteremsha. Naye Yesu akatoa sauti kuu, akakata roho. Pazia la hekalu likapasuka vipande viwili toka juu hadi chini. Basi yule kamanda, aliyesimama hapo akimwelekea, alipoona ya kuwa alikata roho jinsi hii, akasema, Hakika mtu huyu alikuwa Mwana wa Mungu. Palikuwako na wanawake wakitazama kwa mbali; miongoni mwao alikuwemo Mariamu Magdalene, na Mariamu mama yao Yakobo mdogo na Yose, na Salome; hao ndio waliofuatana naye huko Galilaya, na kumtumikia; na wengine wengi waliopanda pamoja naye mpaka Yerusalemu. Ilipofika wakati wa jioni, kwa sababu ni Maandalio, ndiyo siku iliyo kabla ya sabato, akaenda Yusufu, mtu wa Arimathaya, mstahiki, mtu wa baraza ya mashauri, naye mwenyewe anautazamia ufalme wa Mungu; akafanya ujasiri, akaingia mbele ya Pilato akauomba mwili wake Yesu. Lakini Pilato akastaajabu, kama amekwisha kufa. Akamwita yule kamanda, akamwuliza kwamba amekufa kitambo. Hata alipokwisha kupata hakika kutoka kwa yule kamanda, alimpa Yusufu yule maiti. Naye akanunua sanda ya kitani, akamteremsha, akamfungia ile sanda, akamweka katika kaburi lililochongwa mwambani; akavingirisha jiwe mbele ya mlango wa kaburi. Nao Mariamu Magdalene na Mariamu mamaye Yose wakapatazama mahali alipowekwa.
Marko 15:1-47 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Mara kulipokuwa asubuhi wakuu wa makuhani walifanya shauri pamoja na wazee na waandishi na baraza nzima, wakamfunga Yesu, wakamchukua, wakamleta mbele ya Pilato. Pilato akamwuliza, Wewe ndiwe mfalme wa Wayahudi? Akajibu, akamwambia, Wewe wasema. Nao wakuu wa makuhani walikuwa wakimshitaki mambo mengi. Pilato akamwuliza tena akisema, Hujibu neno? Tazama ni mambo mangapi wanayokushitaki! Wala Yesu hakujibu neno tena, hata Pilato akastaajabu. Basi wakati wa sikukuu huwafungulia mfungwa mmoja, wamwombaye. Palikuwa na mtu aitwaye Baraba, amefungwa pamoja na watu waliofanya fitina, na kufanya uuaji katika fitina ile. Makutano wakaja, wakaanza kuomba awafanyie kama vile alivyozoea. Pilato akawajibu, akisema, Je! Mnataka niwafungulie mfalme wa Wayahudi? Kwa maana alitambua ya kuwa wakuu wa makuhani wamemtoa kwa husuda. Lakini wakuu wa makuhani wakawataharakisha makutano, kwamba afadhali awafungulie Baraba. Pilato akajibu tena akawaambia, Basi nimtendeje huyu mnayemnena kuwa ni mfalme wa Wayahudi? Wakapiga kelele tena, Msulibishe. Pilato akawaambia, Kwani, ni ubaya gani alioutenda? Wakazidi sana kupiga kelele, Msulibishe. Pilato akipenda kuwaridhisha makutano, akawafungulia Baraba; akamtoa Yesu, baada ya kumpiga mijeledi, ili asulibiwe. Nao askari wakamchukua ndani ya behewa, ndiyo Praitorio (yaani, nyumba ya uliwali), wakakusanya pamoja kikosi kizima. Wakamvika vazi la rangi ya zambarau, wakasokota taji ya miiba, wakamtia kichwani; wakaanza kumsalimu, Salamu, Mfalme wa Wayahudi! Wakampiga mwanzi wa kichwa, wakamtemea mate, wakapiga magoti, wakamsujudia. Hata wakiisha kumdhihaki, wakamvua lile vazi la rangi ya zambarau, wakamvika mavazi yake mwenyewe; wakamchukua nje ili wamsulibishe. Wakamshurutisha mtu aliyekuwa akipita, akitoka mashamba, Simoni Mkirene, baba yao Iskanda na Rufo, ili auchukue msalaba wake. Wakamleta mpaka mahali paitwapo Golgotha, yaani, Fuvu la kichwa. Wakampa mvinyo iliyotiwa manemane, asiipokee. Wakamsulibisha, wakagawa mavazi yake, wakayapigia kura kila mtu atwae nini. Basi ilikuwa saa tatu, nao wakamsulibisha. Palikuwa na anwani ya mashitaka yake iliyoandikwa juu, MFALME WA WAYAHUDI. Na pamoja naye walisulibisha wanyang’anyi wawili, mmoja mkono wake wa kuume na mmoja mkono wake wa kushoto. [ Basi andiko likatimizwa linenalo, Alihesabiwa pamoja na waasi.] Nao waliokuwa wakipita njiani wakamtukana, wakitikisa-tikisa vichwa, wakisema, Ahaa! Wewe mwenye kulivunja hekalu na kulijenga katika siku tatu, jiponye nafsi yako, ushuke msalabani. Kadhalika na wakuu wa makuhani wakamdhihaki wao kwa wao, pamoja na waandishi, wakisema, Aliponya wengine; hawezi kujiponya mwenyewe. Kristo, mfalme wa Israeli, na ashuke sasa msalabani tupate kuona na kuamini. Hata wale waliosulibiwa pamoja naye wakamfyolea. Na ilipokuwa saa sita, palikuwa na giza juu ya nchi yote, hata saa tisa. Na saa tisa Yesu akapaza sauti yake kwa nguvu, Eloi, Eloi, lama sabakthani? Maana yake, Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha? Na baadhi yao waliosimama pale, walisema, Tazama, anamwita Eliya. Na mmoja akaenda mbio, akajaza sifongo siki, akaitia juu ya mwanzi, akamnywesha, akisema, Acheni, na tuone kwamba Eliya anakuja kumtelemsha. Naye Yesu akatoa sauti kuu, akakata roho. Pazia la hekalu likapasuka vipande viwili toka juu hata chini. Basi yule akida, aliyesimama hapo akimwelekea, alipoona ya kuwa alikata roho jinsi hii, akasema, Hakika mtu huyu alikuwa Mwana wa Mungu. Palikuwako na wanawake wakitazama kwa mbali; miongoni mwao alikuwamo Mariamu Magdalene, na Mariamu mama yao Yakobo mdogo na Yose, na Salome; hao ndio waliofuatana naye huko Galilaya, na kumtumikia; na wengine wengi waliopanda pamoja naye mpaka Yerusalemu. Hata ikiisha kuwa jioni, kwa sababu ni Maandalio, ndiyo siku iliyo kabla ya sabato, akaenda Yusufu, mtu wa Arimathaya, mstahiki, mtu wa baraza ya mashauri, naye mwenyewe anautazamia ufalme wa Mungu; akafanya ujasiri, akaingia mbele ya Pilato akauomba mwili wake Yesu. Lakini Pilato akastaajabu, kwamba amekwisha kufa. Akamwita yule akida, akamwuliza kwamba amekufa kitambo. Hata alipokwisha kupata hakika kwa yule akida, alimpa Yusufu yule maiti. Naye akanunua sanda ya kitani, akamtelemsha, akamfungia ile sanda, akamweka katika kaburi lililochongwa mwambani; akavingirisha jiwe mbele ya mlango wa kaburi. Nao Mariamu Magdalene na Mariamu mamaye Yose wakapatazama mahali alipowekw
Marko 15:1-47 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Asubuhi na mapema, viongozi wa makuhani, pamoja na wazee, walimu wa sheria na Baraza lote, wakafikia uamuzi. Wakamfunga Yesu, wakamchukua na kumkabidhi kwa Pilato. Pilato akamuuliza, “Je, wewe ndiye Mfalme wa Wayahudi?” Yesu akajibu, “Wewe umesema.” Viongozi wa makuhani wakamshtaki kwa mambo mengi. Pilato akamuuliza tena, “Je, huna la kujibu? Tazama ni mashtaka mangapi wanayaleta juu yako.” Lakini Yesu hakujibu lolote, hivyo Pilato akashangaa. Ilikuwa desturi wakati wa Sikukuu ya Pasaka kumfungulia mfungwa yeyote ambaye watu wangemtaka. Wakati huo, mtu aliyeitwa Baraba alikuwa amefungwa gerezani pamoja na waasi wengine waliokuwa wametekeleza uuaji wakati wa maasi. Ule umati wa watu ukamjia Pilato na kumwomba awafanyie kama ilivyokuwa desturi yake. Pilato akawauliza, “Mnataka niwafungulie huyu Mfalme wa Wayahudi?” Kwa maana yeye alitambua kuwa viongozi wa makuhani walikuwa wamemtia Yesu mikononi mwake kwa ajili ya wivu. Lakini viongozi wa makuhani wakauchochea ule umati wa watu wamwombe awafungulie Baraba badala yake. Pilato akawauliza tena, “Basi mnataka nifanye nini na huyu mtu mnayemwita Mfalme wa Wayahudi?” Wakapiga kelele wakisema, “Msulubishe!” Pilato akawauliza, “Kwa nini? Amefanya kosa gani?” Lakini wao wakapiga kelele kwa nguvu zaidi, wakisema, “Msulubishe!” Pilato, akitaka kuuridhisha ule umati wa watu, akawafungulia Baraba. Naye baada ya kuamuru Yesu achapwe mijeledi, akamtoa ili asulubishwe. Askari wakampeleka Yesu hadi kwenye ukumbi wa ndani wa jumba la kifalme, ndio Praitorio, wakakusanya kikosi kizima cha askari. Wakamvalisha Yesu joho la zambarau, wakasokota taji ya miiba, wakamvika kichwani. Wakaanza kumsalimu kwa dhihaka, “Salamu, mfalme wa Wayahudi!” Wakampiga kwa fimbo ya mwanzi tena na tena kichwani na kumtemea mate. Wakapiga magoti mbele yake, wakamsujudia kwa kumdhihaki. Walipokwisha kumdhihaki, wakamvua lile joho la zambarau, wakamvika tena nguo zake. Kisha wakamtoa nje ili wakamsulubishe. Mtu mmoja kutoka Kirene, jina lake Simoni, baba yao Aleksanda na Rufo, alikuwa anapita zake kuingia mjini kutoka shamba, nao wakamlazimisha kuubeba ule msalaba. Kisha wakampeleka Yesu mpaka mahali palipoitwa Golgotha (maana yake ni Mahali pa Fuvu la Kichwa). Nao wakampa divai iliyochanganywa na manemane, lakini hakuinywa. Basi wakamsulubisha, nazo nguo zake wakagawana miongoni mwao kwa kuzipigia kura ili kuamua ni gani kila mtu ataichukua. Ilikuwa yapata saa tatu asubuhi walipomsulubisha. Tangazo likaandikwa la mashtaka dhidi yake lenye maneno haya: “MFALME WA WAYAHUDI.” Pamoja naye walisulubiwa wanyangʼanyi wawili, mmoja upande wake wa kuume na mwingine upande wa kushoto. [ Nayo maandiko yakatimizwa, yale yasemayo, “Alihesabiwa pamoja na watenda dhambi.]” Watu waliokuwa wakipita njiani wakamtukana huku wakitikisa vichwa vyao na kusema, “Aha! Wewe ambaye utalivunja Hekalu na kulijenga kwa siku tatu, basi shuka kutoka msalabani na ujiokoe mwenyewe!” Vivyo hivyo, viongozi wa makuhani pamoja na walimu wa sheria wakamdhihaki miongoni mwao wakisema, “Aliwaokoa wengine, lakini hawezi kujiokoa mwenyewe! Basi huyu Kristo, huyu Mfalme wa Israeli, ashuke sasa kutoka msalabani, ili tupate kuona na kuamini.” Wale waliosulubiwa pamoja naye pia wakamtukana. Ilipofika saa sita, giza liliifunika nchi yote hadi saa tisa. Mnamo saa tisa, Yesu akapaza sauti, akalia, “Eloi, Eloi, lama sabakthani?” (maana yake, “Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?”) Baadhi ya watu waliokuwa wamesimama karibu waliposikia hayo, wakasema, “Msikieni, anamwita Eliya.” Mtu mmoja akaenda mbio, akachovya sifongo kwenye siki, akaiweka kwenye mwanzi na akampa Yesu ili anywe, akisema, “Basi mwacheni. Hebu tuone kama Eliya atakuja kumshusha kutoka hapo msalabani.” Kisha Yesu akatoa sauti kuu, akakata roho. Pazia la Hekalu likachanika vipande viwili kuanzia juu hadi chini. Basi yule jemadari aliyekuwa amesimama hapo mbele ya msalaba wa Yesu aliposikia ile sauti yake na kuona jinsi alivyokata roho, akasema, “Hakika mtu huyu alikuwa Mwana wa Mungu!” Walikuwepo pia wanawake waliokuwa wakiangalia kwa mbali. Miongoni mwao walikuwepo Maria Magdalene, na Maria mama yao Yakobo mdogo na Yose, pia na Salome. Hawa walifuatana na Yesu na kushughulikia mahitaji yake alipokuwa Galilaya. Pia walikuwepo wanawake wengine wengi waliokuwa wamekuja pamoja naye Yerusalemu. Ilipofika jioni, kwa kuwa ilikuwa Siku ya Maandalizi, yaani siku moja kabla ya Sabato, Yosefu wa Arimathaya, mtu aliyeheshimiwa katika Baraza, na ambaye alikuwa anautarajia Ufalme wa Mungu, akamwendea Pilato kwa ujasiri na kumwomba mwili wa Yesu. Pilato alikuwa akijiuliza kama Yesu alikuwa amekwisha kufa. Hivyo akamwita yule jemadari, akamuuliza iwapo Yesu alikuwa amekwisha kufa. Baada ya kupata habari kutoka kwa yule jemadari kwamba kweli amekwisha kufa, Pilato akampa Yosefu ruhusa ya kuuchukua huo mwili. Hivyo Yosefu akanunua kitambaa cha kitani safi, akaushusha mwili kutoka msalabani, akaufunga katika kile kitambaa cha kitani, na kuuweka ndani ya kaburi lililochongwa kwenye mwamba. Kisha akavingirisha jiwe kwenye ingilio la kaburi. Maria Magdalene na Maria mamaye Yose walipaona mahali pale alipolazwa.