Marko 14:1-52
Marko 14:1-52 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Baada ya siku mbili ilikuwa sikukuu ya Pasaka, na mikate isiyochachwa; wakuu wa makuhani na waandishi wakatafuta njia ya kumkamata kwa hila na kumwua. Kwa maana walisema, Isiwe kwa wakati wa sikukuu, isije ikatokea ghasia katika watu. Naye alipokuwapo Bethania, nyumbani mwa Simoni mkoma, ameketi chakulani, alikuja mwanamke mwenye kibweta cha marhamu ya nardo safi ya thamani nyingi; akakivunja kibweta akaimimina kichwani pake. Palikuwa na watu waliochukizwa katika nafsi zao wakisema, Kwani kupoteza marhamu namna hii? Maana marhamu hii ingaliweza kuuzwa kwa dinari mia tatu na kuzidi, wakapewa maskini. Wakamnung’unikia sana yule mwanamke. Yesu akasema, Mwacheni; mbona mnamtaabisha? Amenitendea kazi njema; maana sikuzote mnao maskini pamoja nanyi, na kila mpendapo mwaweza kuwatendea mema; lakini mimi hamnami sikuzote. Ametenda alivyoweza; ametangulia kuupaka mwili wangu marhamu kwa ajili ya maziko. Amin, nawaambia, Kila ihubiriwapo Injili katika ulimwengu wote, na hili alilotenda huyu litatajwa kwa kumbukumbu lake. Yuda Iskariote, yule mmoja katika wale Thenashara, akaenda zake kwa wakuu wa makuhani, apate kumsaliti kwao. Nao waliposikia walifurahi, wakaahidi kumpa fedha. Akatafuta njia ya kumsaliti wakati wa kufaa. Hata siku ya kwanza ya mikate isiyochachwa, walipoichinja pasaka, wanafunzi wake wakamwambia, Ni wapi utakapo tuende tukuandalie uile pasaka? Akatuma wawili katika wanafunzi wake, akawaambia, Nendeni zenu mjini; atakutana nanyi mwanamume amechukua mtungi wa maji; mfuateni; na po pote atakapoingia, mwambieni mwenye nyumba, Mwalimu asema, Ki wapi chumba changu cha wageni, niile pasaka humo, pamoja na wanafunzi wangu? Naye mwenyewe atawaonyesha orofa kubwa, imeandikwa tayari; humo tuandalieni. Wanafunzi wakatoka, wakaenda mjini, wakaona kama alivyowaambia, wakaiandaa pasaka. Basi ilipokuwa jioni yuaja pamoja na wale Thenashara. Nao walipokuwa wameketi chakulani, wakila, Yesu alisema, Amin, nawaambia, Mmoja wenu, naye anakula pamoja nami, atanisaliti. Wakaanza kuhuzunika, wakamwambia mmoja mmoja, Je! Ni mimi? Akawaambia, Ni mmoja wa hao Thenashara, ambaye achovya pamoja nami katika kombe. Kwa maana Mwana wa Adamu aenda zake kama alivyoandikiwa; lakini ole wake mtu yule ambaye amsaliti Mwana wa Adamu; ingekuwa heri kwake mtu yule kama asingalizaliwa. Nao walipokuwa wakila, alitwaa mkate, akabariki, akaumega, akawapa, akasema, Twaeni; huu ndio mwili wangu. Akatwaa kikombe, akashukuru, akawapa; wakakinywea wote. Akawaambia, Hii ndiyo damu yangu ya agano, imwagikayo kwa ajili ya wengi. Amin, nawaambia ninyi, Sitakunywa tena kabisa uzao wa mzabibu, hata siku ile nitakapounywa mpya katika ufalme wa Mungu. Nao walipokwisha kuimba walitoka kwenda mlima wa Mizeituni. Yesu akawaambia, Mtakunguwazwa ninyi nyote kwa ajili yangu usiku huu; kwa kuwa imeandikwa, Nitampiga mchungaji, na kondoo watatawanyika. Lakini baada ya kufufuka kwangu, nitawatangulia kwenda Galilaya. Petro akamwambia, Hata wajapokunguwazwa wote, lakini siyo mimi. Yesu akamwambia, Amin, nakuambia wewe, Leo, usiku huu, kabla ya kuwika jogoo mara mbili, utanikana mara tatu. Naye akazidi sana kusema, Ijaponipasa kufa nawe, hata hivyo sitakukana kamwe. Na wote wakasema vile vile. Kisha wakaja mpaka bustani iitwayo Gethsemane; akawaambia wanafunzi wake, Ketini hapa muda niombapo. Akamtwaa Petro na Yakobo na Yohana pamoja naye, akaanza kufadhaika sana na kuhangaika. Akawaambia, Roho yangu ina huzuni nyingi kiasi cha kufa; kaeni hapa mkeshe. Akaendelea mbele kidogo, akaanguka kifudifudi, akiomba ya kuwa, ikiwezekana, saa hiyo imwepuke. Akasema, Aba, Baba, yote yawezekana kwako; uniondolee kikombe hiki; walakini, si kama nitakavyo mimi, bali utakavyo wewe. Akaja akawakuta wamelala usingizi, akamwambia Petro, Je! Simoni, umelala? Hukuweza kukesha saa moja? Kesheni mwombe, msije mkaingia majaribuni, roho i radhi ila mwili ni dhaifu. Akaenda zake tena, akaomba, akisema neno lilo hilo. Akaja tena akawakuta wamelala, maana macho yao yamekuwa mazito, wala hawakujua la kumjibu. Akaja mara ya tatu, akawaambia, Laleni sasa, mpumzike; yatosha, saa imekuja; tazama, Mwana wa Adamu anatiwa mikononi mwao wenye dhambi. Ondokeni, twendeni zetu; tazama, yule anayenisaliti amekaribia. Basi alipokuwa katika kusema, mara Yuda alifika, mmoja wa wale Thenashara, na pamoja naye mkutano, wana panga na marungu, wametoka kwa wakuu wa makuhani, na waandishi, na wazee. Na yule anayemsaliti alikuwa amewapa ishara, akisema, Nitakayembusu, huyo ndiye; mkamateni, mkamchukue salama. Basi alipokuja, mara akamwendea, akasema, Rabi, akambusu. Wakanyosha mikono yao wakamkamata. Na mmoja wao waliokuwapo akafuta upanga, akampiga mtumwa wa Kuhani Mkuu, akamkata sikio. Yesu akajibu, akawaambia, Je! Ni kama juu ya mnyang’anyi mmetoka wenye panga na marungu, kunitwaa mimi? Kila siku nalikuwa mbele yenu hekaluni nikifundisha, msinikamate; lakini haya yamekuwa ili maandiko yapate kutimia. Ndipo wakamwacha, wakakimbia wote. Na kijana mmoja alimfuata, amejitanda mwili wake nguo ya kitani; wakamkamata; naye akaiacha ile nguo ya kitani, akakimbia yu uchi.
Marko 14:1-52 Biblia Habari Njema (BHN)
Ilikuwa siku mbili tu kabla ya sikukuu ya Pasaka na ya mikate isiyotiwa chachu. Makuhani wakuu na waalimu wa sheria walikuwa wakitafuta njia ya kumtia Yesu nguvuni kwa hila, wamuue. Lakini walisema, “Tusimtie nguvuni wakati wa sikukuu, watu wasije wakafanya ghasia.” Yesu alikuwa Bethania, nyumbani kwa Simoni Mkoma. Alipokuwa mezani kula chakula, mama mmoja aliyekuwa na chupa ya alabasta yenye marashi ya nardo safi ya thamani kubwa alikuja, akaivunja hiyo chupa, akammiminia Yesu marashi hayo kichwani. Baadhi ya watu waliokuwa hapo walikasirika, wakajisemea, “Kwa nini kupoteza ovyo marashi haya? Yangaliweza kuuzwa kwa fedha kiasi cha dinari 300, wakapewa maskini!” Wakamkemea huyo mama. Lakini Yesu akawaambia, “Mwacheni; kwa nini mnamsumbua? Amenitendea jambo jema. Maskini mnao daima pamoja nanyi; mnaweza kuwasaidia wakati wowote mnaopenda. Lakini mimi sitakuwapo pamoja nanyi daima. Yeye amefanya alivyoweza; ameupaka mwili wangu marashi kuutayarisha kwa mazishi. Nawaambieni kweli, popote ulimwenguni Habari Njema itakapohubiriwa, kitendo hiki alichofanya kitatajwa kwa kumkumbuka yeye.” Kisha Yuda Iskarioti, mmoja wa wale kumi na wawili, alikwenda kwa makuhani wakuu ili kumsaliti Yesu. Makuhani wakuu waliposikia habari hizo, walifurahi, wakamwahidi kumpa fedha. Basi, Yuda akaanza kutafuta nafasi ya kumsaliti. Siku ya kwanza ya sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu, wakati ambapo mwanakondoo wa Pasaka huchinjwa, wanafunzi wake walimwuliza, “Wataka tukuandalie wapi karamu ya Pasaka?” Basi Yesu akawatuma wawili wa wanafunzi wake akiwaambia, “Nendeni mjini, na humo mtakutana na mwanamume mmoja anayebeba mtungi wa maji. Mfuateni mpaka katika nyumba atakayoingia, mkamwambie mwenye nyumba, ‘Mwalimu anasema: Wapi chumba changu ambamo nitakula Pasaka pamoja na wanafunzi wangu?’ Naye atawaonesha chumba kikubwa ghorofani kilichotayarishwa na kupambwa. Tuandalieni humo.” Wanafunzi wakaondoka, wakaenda mjini, wakakuta kila kitu sawa kama Yesu alivyokuwa amewaambia. Wakaandaa karamu ya Pasaka. Ilipokuwa jioni, Yesu alifika pamoja na wanafunzi wake kumi na wawili. Walipokuwa mezani wakila, Yesu alisema, “Kweli nawaambieni, mmoja wenu anayekula pamoja nami, atanisaliti.” Hapo wanafunzi wake wakaanza kuhuzunika, wakamwuliza mmojammoja, “Je, ni mimi?” Yesu akawaambia, “Ni mmoja wenu nyinyi kumi na wawili, anayechovya mkate pamoja nami katika bakuli. Kweli Mwana wa Mtu anakwenda zake kama Maandiko Matakatifu yanavyosema juu yake; lakini, ole wake mtu yule anayemsaliti Mwana wa Mtu! Ingalikuwa afadhali kwa mtu huyo kama hangalizaliwa!” Walipokuwa wanakula, Yesu alitwaa mkate, akashukuru, akaumega na kuwapa wanafunzi wake akisema, “Twaeni; huu ni mwili wangu.” Kisha akatwaa kikombe cha divai, akamshukuru Mungu, akawapa; wote wakanywa kutoka kikombe hicho. Akawaambia, “Hii ni damu yangu inayothibitisha agano la Mungu, damu inayomwagwa kwa ajili ya watu wengi. Kweli nawaambieni, sitakunywa tena divai ya zabibu mpaka siku ile nitakapoinywa upya katika ufalme wa Mungu.” Kisha wakaimba wimbo, wakaondoka, wakaenda katika mlima wa Mizeituni. Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Nyinyi nyote mtakuwa na mashaka nami; maana Maandiko Matakatifu yasema: ‘Nitampiga mchungaji, nao kondoo watatawanyika.’ Lakini nikisha fufuka, nitawatangulieni kule Galilaya.” Petro akamwambia “Hata kama wote watakuwa na mashaka nawe na kukuacha, mimi sitakukana kamwe!” Yesu akamwambia, “Kweli nakuambia, usiku huu, kabla jogoo hajawika mara mbili, utanikana mara tatu.” Lakini Petro akasisitiza, “Hata kama ni lazima nife pamoja nawe, sitakuacha kamwe.” Wanafunzi wote pia wakasema vivyo hivyo. Basi, wakafika katika bustani iliyoitwa Gethsemane. Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Kaeni hapa wakati mimi nasali.” Kisha akawachukua Petro, Yakobo na Yohane; akaanza kufadhaika sana na kuhangaika. Akawaambia, “Nina huzuni kubwa moyoni hata karibu kufa. Kaeni hapa na kukesha.” Akaenda mbele kidogo, akajitupa chini kifudifudi, akasali kwamba, kama ingewezekana, asiipitie saa hiyo ya mateso. Akasema, “Baba yangu, kwako mambo yote yanawezekana. Uniondolee kikombe hiki; lakini isiwe kama nitakavyo mimi, bali utakavyo wewe.” Kisha akarudi kwa wanafunzi wale watatu, akawakuta wamelala. Basi, akamwuliza Petro, “Simoni, je, umelala? Hukuweza kukesha hata saa moja?” Kisha akawaambia, “Kesheni na kusali ili msije mkaingia katika majaribu. Roho inataka, lakini mwili ni dhaifu.” Akaenda kusali tena akirudia maneno yaleyale. Kisha akarudi tena, akawakuta wamelala. Macho yao yalikuwa yamebanwa na usingizi. Hawakujua la kumjibu. Alipowajia mara ya tatu aliwaambia, “Mnalala bado na kupumzika? Sasa imetosha! Saa imefika! Mwana wa Mtu anakabidhiwa kwa watu waovu. Amkeni, twende zetu. Tazameni, yule atakayenisaliti amekaribia.” Yesu alipokuwa bado anasema, Yuda, mmoja wa wale kumi na wawili, akafika pamoja na umati wa watu wenye mapanga na marungu. Watu hao walikuwa wametumwa na makuhani wakuu, waalimu wa sheria na wazee. Msaliti Yuda alikuwa amewapa ishara: “Yule nitakayembusu ndiye; mkamateni na kumpeleka chini ya ulinzi.” Yuda alipofika tu, alimwendea Yesu moja kwa moja, akamwambia, “Mwalimu!” Kisha akambusu. Basi, hao watu wakamkamata Yesu, wakamtia nguvuni. Mmoja wa wale waliokuwa wamesimama hapo pamoja na Yesu, akachomoa upanga wake, akampiga mtumishi wa kuhani mkuu, akamkata sikio. Yesu akawaambia, “Je, mmekuja na mapanga na marungu kunikamata kana kwamba mimi ni mnyanganyi? Kila siku nilikuwa pamoja nanyi nikifundisha hekaluni, wala hamkunikamata. Lakini sasa lazima Maandiko Matakatifu yatimie.” Hapo wanafunzi wote wakamwacha, wakakimbia. Kulikuwa na kijana mmoja aliyekuwa anamfuata Yesu akiwa amevaa shuka. Nao wakajaribu kumkamata. Lakini yeye akaponyoka, akaiachilia ile shuka, akakimbia uchi.
Marko 14:1-52 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Baada ya siku mbili ilikuwa sikukuu ya Pasaka, na mikate isiyochachwa; wakuu wa makuhani na waandishi wakatafuta njia ya kumkamata kwa hila na kumwua. Kwa maana walisema, Isiwe kwa wakati wa sikukuu, isije ikatokea ghasia katika watu. Naye alipokuwapo Bethania, nyumbani mwa Simoni mwenye ukoma, akiwa amekaa mezani, alikuja mwanamke mwenye chupa ya marhamu yenye manukato ya nardo safi ya thamani kubwa; akaivunja chupa akaimimina kichwani pake. Palikuwa na watu waliochukizwa katika nafsi zao wakisema, Kwa nini kupoteza marhamu namna hii? Maana marhamu hii ingaliweza kuuzwa kwa dinari mia tatu na kuzidi, wakapewa maskini. Wakamnung'unikia sana yule mwanamke. Yesu akasema, Mwacheni; mbona mnamsumbua? Amenitendea kazi njema; maana sikuzote mnao maskini pamoja nanyi, na kila mpendapo mwaweza kuwatendea mema; lakini mimi hamko nami sikuzote. Ametenda alivyoweza; ametangulia kuupaka mwili wangu marhamu kwa ajili ya maziko. Amin, nawaambia, Kila ihubiriwapo Injili katika ulimwengu wote, na hili alilotenda huyu litatajwa kwa kumbukumbu lake. Yuda Iskarioti, yule mmoja katika wale Kumi na Wawili, akaenda zake kwa wakuu wa makuhani, apate kumsaliti kwao. Nao waliposikia walifurahi, wakaahidi kumpa fedha. Akatafuta njia ya kumsaliti wakati wa kufaa. Katika siku ya kwanza ya mikate isiyochachwa, walipoichinja Pasaka, wanafunzi wake wakamwambia, Ni wapi utakapo tuende tukuandalie uile Pasaka? Akatuma wawili katika wanafunzi wake, akawaambia, Nendeni zenu mjini; atakutana nanyi mwanamume amebeba mtungi wa maji; mfuateni; na popote atakapoingia, mwambieni mwenye nyumba, Mwalimu asema, Kiko wapi chumba changu cha wageni, niile Pasaka humo, pamoja na wanafunzi wangu? Naye mwenyewe atawaonesha ghorofa kubwa, iliyotayarishwa; humo tuandalieni. Wanafunzi wakatoka, wakaenda mjini, wakaona kama alivyowaambia, wakaiandaa Pasaka. Basi ilipokuwa jioni akaja pamoja na wale Kumi na Wawili. Nao walipokuwa wameketi chakulani, wakila, Yesu alisema, Amin, nawaambia, Mmoja wenu, naye anakula pamoja nami, atanisaliti. Wakaanza kuhuzunika, wakamwambia mmoja mmoja, Je! Ni mimi? Akawaambia, Ni mmoja wa hao Kumi na Wawili, ambaye achovya pamoja nami katika kombe. Kwa maana Mwana wa Adamu aenda zake kama alivyoandikiwa; lakini ole wake mtu yule ambaye amsaliti Mwana wa Adamu; ingekuwa heri kwake mtu yule kama asingalizaliwa. Nao walipokuwa wakila, alitwaa mkate, akabariki, akaumega, akawapa, akasema, Twaeni; huu ndio mwili wangu. Akatwaa kikombe, akashukuru, akawapa; wakakinywea wote. Akawaambia, Hii ndiyo damu yangu ya agano, imwagikayo kwa ajili ya wengi. Amin, nawaambia ninyi, Sitakunywa tena kabisa uzao wa mzabibu, hata siku ile nitakapounywa mpya katika ufalme wa Mungu. Nao walipokwisha kuimba walitoka kwenda katika mlima wa Mizeituni. Yesu akawaambia, Mtakunguwazwa ninyi nyote kwa ajili yangu usiku huu; kwa kuwa imeandikwa, Nitampiga mchungaji, na kondoo watatawanyika. Lakini baada ya kufufuka kwangu, nitawatangulia kwenda Galilaya. Petro akamwambia, Hata wajapokunguwazwa wote, lakini siyo mimi. Yesu akamwambia, Amin, nakuambia wewe, Leo, usiku huu, kabla ya kuwika jogoo mara mbili, utanikana mara tatu. Naye akazidi sana kusema, Ijaponipasa kufa nawe, hata hivyo sitakukana kamwe. Na wote wakasema vile vile. Kisha wakaja mpaka katika bustani iitwayo Gethsemane; akawaambia wanafunzi wake, Ketini hapa pindi niombapo. Akamtwaa Petro na Yakobo na Yohana pamoja naye, akaanza kufadhaika sana na kuhangaika. Akawaambia, Roho yangu ina huzuni nyingi kiasi cha kufa; kaeni hapa mkeshe. Akaendelea mbele kidogo, akaanguka kifudifudi, akiomba ya kuwa, ikiwezekana, saa hiyo imwepuke. Akasema, Aba, Baba, yote yawezekana kwako; uniondolee kikombe hiki; lakini, si kama nitakavyo mimi, bali utakavyo wewe. Akaja akawakuta wamelala usingizi, akamwambia Petro, Je! Simoni, umelala? Hukuweza kukesha saa moja? Kesheni na kuomba, msije mkaingia majaribuni, roho i radhi ila mwili ni dhaifu. Akaenda zake tena, akaomba, akisema neno lilo hilo. Akaja tena akawakuta wamelala, maana macho yao yamekuwa mazito, wala hawakujua la kumjibu. Akaja mara ya tatu, akawaambia, Laleni sasa, mpumzike; yatosha, saa imekuja; tazama, Mwana wa Adamu anatiwa mikononi mwao wenye dhambi. Ondokeni, twendeni zetu; tazama, yule anayenisaliti amekaribia. Basi alipokuwa katika kusema, mara Yuda alifika, mmoja wa wale Kumi na Wawili, na pamoja naye mkutano, wakiwa na panga na marungu, wametoka kwa wakuu wa makuhani, na waandishi, na wazee. Na yule anayemsaliti alikuwa amewapa ishara, akisema, Nitakayembusu, huyo ndiye; mkamateni na kumpeleka chini ya ulinzi. Basi alipokuja, mara akamwendea, akasema, Rabi, akambusu. Wakanyosha mikono yao wakamkamata. Na mmoja wao waliokuwapo akafuta upanga, akampiga mtumwa wa Kuhani Mkuu, akamkata sikio. Yesu akajibu, akawaambia, Je! Mmekuja na panga na marungu kunikamata kana kwamba mimi ni mnyang'anyi? Kila siku nilikuwa mbele yenu hekaluni nikifundisha, msinikamate; lakini haya yamekuwa ili maandiko yapate kutimia. Ndipo wakamwacha, wakakimbia wote. Na kijana mmoja alimfuata, akiwa amejitanda mwili wake nguo ya kitani; wakamkamata; naye akaiacha ile nguo ya kitani, akakimbia akiwa uchi.
Marko 14:1-52 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Zilikuwa zimebaki siku mbili tu kabla ya Sikukuu ya Pasaka, na Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu. Viongozi wa makuhani na walimu wa sheria walikuwa wakitafuta njia ya kumkamata Yesu kwa hila na kumuua. Lakini walisema, “Tusilifanye jambo hili wakati wa Sikukuu, maana watu wanaweza wakafanya ghasia.” Yesu alikuwa Bethania nyumbani kwa Simoni aliyekuwa na ukoma. Wakati alipokuwa ameketi mezani akila chakula cha jioni, mwanamke mmoja aliingia akiwa na chupa ya marhamu yenye manukato ya nardo safi ya thamani kubwa. Akaivunja hiyo chupa, akamiminia hayo manukato kichwani mwa Yesu. Baadhi ya watu waliokuwepo pale walikuwa wakisemezana wao kwa wao, “Upotevu huu wote ni wa nini? Mafuta haya yangeweza kuuzwa kwa zaidi ya dinari 300, na fedha hizo wakapewa maskini.” Wakamkemea vikali huyo mwanamke. Lakini Yesu akawaambia, “Mbona mnamsumbua huyu mwanamke? Mwacheni! Yeye amenitendea jambo zuri sana. Maskini mtakuwa nao siku zote na mnaweza kuwasaidia wakati wowote mnaotaka. Lakini mimi hamtakuwa nami siku zote. Huyu mwanamke amenitendea lile aliloweza. Ameumiminia mwili wangu manukato ili kuniandaa kwa maziko yangu. Amin, nawaambia, mahali popote ulimwenguni ambapo Injili itahubiriwa, jambo hili alilolitenda huyu mwanamke litatajwa pia kwa ukumbusho wake.” Kisha Yuda Iskariote, mmoja wa wale wanafunzi kumi na wawili, akaenda kwa viongozi wa makuhani ili kumsaliti Yesu kwao. Walifurahi sana kusikia jambo hili na wakaahidi kumpa fedha. Hivyo yeye akawa anatafuta wakati uliofaa wa kumsaliti. Siku ya kwanza ya Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu, siku ambayo kwa desturi mwana-kondoo wa Pasaka huchinjwa, wanafunzi wa Yesu wakamuuliza, “Unataka twende wapi ili tukuandalie mahali pa kula Pasaka?” Basi akawatuma wawili miongoni mwa wanafunzi wake, akawaambia, “Nendeni mjini. Huko mtakutana na mwanaume amebeba mtungi wa maji. Mfuateni. Mwambieni mwenye nyumba ile atakayoingia, ‘Mwalimu anauliza: Kiko wapi chumba changu cha wageni, ambamo mimi na wanafunzi wangu tutakula Pasaka?’ Atawaonyesha chumba kikubwa ghorofani, kilichopambwa tena kilicho tayari. Tuandalieni humo.” Wale wanafunzi wakaondoka na kwenda mjini, nao wakakuta kila kitu kama Yesu alivyowaambia. Hivyo wakaiandaa Pasaka. Ilipofika jioni, Yesu akaja pamoja na wale wanafunzi wake kumi na wawili. Walipoketi mezani wakila, Yesu akawaambia, “Amin, nawaambia, mmoja wenu atanisaliti, mmoja anayekula pamoja nami.” Wakaanza kuhuzunika na kumuuliza mmoja baada ya mwingine, “Je, ni mimi Bwana?” Akawajibu, “Ni mmoja miongoni mwenu ninyi kumi na wawili, yule anayechovya mkate kwenye bakuli pamoja nami. Mwana wa Adamu anaenda zake kama vile alivyoandikiwa. Lakini ole wake mtu yule amsalitiye Mwana wa Adamu! Ingekuwa heri kwake mtu huyo kama hangezaliwa.” Walipokuwa wanakula, Yesu akachukua mkate, akashukuru, akaumega na kuwapa wanafunzi wake, akisema, “Twaeni mle; huu ndio mwili wangu.” Kisha akakitwaa kikombe, akashukuru, akawapa, nao wote wakanywa kutoka humo. Akawaambia, “Hii ndiyo damu yangu ya agano, imwagikayo kwa ajili ya wengi. Amin, nawaambia, sitakunywa tena katika uzao wa mzabibu, hadi siku ile nitakapounywa mpya katika Ufalme wa Mungu.” Walipokwisha kuimba wimbo, wakatoka wakaenda Mlima wa Mizeituni. Yesu akawaambia, “Ninyi nyote mtaniacha, kwa maana imeandikwa: “ ‘Nitampiga mchungaji, nao kondoo watatawanyika.’ Lakini baada ya kufufuka kwangu, nitawatangulia kwenda Galilaya.” Petro akasema, “Hata kama wengine wote watakuacha, mimi sitakuacha.” Yesu akamwambia, “Amin, nakuambia; leo, usiku huu, kabla jogoo hajawika mara mbili, wewe mwenyewe utanikana mara tatu.” Lakini Petro akasisitiza zaidi, “Hata kama itabidi kufa pamoja nawe, sitakukana kamwe.” Nao wale wengine wote wakasema vivyo hivyo. Wakaenda mahali paitwapo Gethsemane. Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Kaeni hapa, nami niende nikaombe.” Kisha akawachukua pamoja naye Petro, Yakobo na Yohana. Akaanza kuhuzunika sana na kutaabika. Akawaambia, “Moyo wangu umejawa na huzuni kiasi cha kufa. Kaeni hapa na mkeshe.” Akaenda mbele kidogo, akaanguka kifudifudi, akaomba kwamba kama ingewezekana saa hiyo ya mateso imwondokee. Akasema, “ Abba, Baba, mambo yote yawezekana kwako. Niondolee kikombe hiki. Lakini si kama nipendavyo mimi, bali vile upendavyo wewe.” Akarudi kwa wanafunzi wake, akawakuta wamelala. Akamwambia Petro, “Simoni, umelala? Je, hukuweza kukesha hata kwa saa moja? Kesheni na mwombe, msije mkaingia majaribuni. Roho iko radhi, lakini mwili ni mdhaifu.” Akaenda tena kuomba, akisema maneno yale yale. Aliporudi, akawakuta tena wamelala kwa sababu macho yao yalikuwa mazito. Nao hawakujua la kumwambia. Akaja mara ya tatu, akawaambia, “Bado mmelala na kupumzika? Imetosha! Saa imewadia. Tazameni, Mwana wa Adamu anasalitiwa na kutiwa mikononi mwa wenye dhambi. Inukeni, twende zetu! Tazameni, msaliti wangu yuaja!” Yesu alipokuwa bado anazungumza, Yuda, mmoja wa wale wanafunzi Kumi na Wawili, akatokea. Alikuwa amefuatana na umati wa watu wenye panga na marungu, waliokuwa wametumwa na viongozi wa makuhani, walimu wa sheria, na wazee. Basi msaliti alikuwa amewapa hao watu ishara, kwamba: “Yule nitakayembusu ndiye. Mkamateni, mkamchukue chini ya ulinzi.” Mara Yuda akamjia Yesu na kusema, “Rabi.” Akambusu. Wale watu wakamkamata Yesu, wakamweka chini ya ulinzi. Ndipo mmoja wa wale waliokuwa wamesimama karibu aliuchomoa upanga wake na kumpiga mtumishi wa kuhani mkuu, akamkata sikio. Kisha Yesu akawaambia, “Mmekuja na panga na marungu kunikamata kana kwamba mimi ni mnyangʼanyi? Siku kwa siku nilikuwa pamoja nanyi nikifundisha Hekaluni, wala hamkunikamata. Lakini Maandiko sharti yatimie.” Ndipo wanafunzi wake wote wakamwacha, wakakimbia. Kijana mmoja, ambaye hakuwa amevaa kitu isipokuwa alijitanda nguo ya kitani, alikuwa akimfuata Yesu. Walipomkamata, alikimbia uchi, akaliacha vazi lake.