Marko 13:32-36
Marko 13:32-36 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Lakini habari ya siku ile na saa ile hakuna aijuaye, hata malaika walio mbinguni, wala Mwana, ila Baba. Angalieni, kesheni, [ombeni], kwa kuwa hamjui wakati ule utakapokuwapo. Mfano wake ni kama mtu mwenye kusafiri, ameiacha nyumba yake, amewapa watumwa wake amri, na kila mtu kazi yake, naye amemwamuru bawabu akeshe. Kesheni basi, kwa maana hamjui ajapo bwana wa nyumba, kwamba ni jioni, au kwamba ni usiku wa manane, au awikapo jogoo, au asubuhi; asije akawasili ghafla akawakuta mmelala.
Marko 13:32-36 Biblia Habari Njema (BHN)
“Lakini, juu ya siku au saa hiyo hakuna mtu ajuaye itakuja lini; wala malaika wa mbinguni, wala Mwana; Baba peke yake ndiye ajuaye. Muwe waangalifu na kesheni, maana hamjui wakati huo utafika lini. Itakuwa kama mtu anayeondoka nyumbani kwenda safari akiwaachia watumishi wake madaraka, kila mmoja na kazi yake; akamwambia na mlinzi wa mlango awe macho. Kesheni, basi, kwa maana hamjui mwenye nyumba atarudi lini; huenda ikawa jioni, usiku wa manane, alfajiri au asubuhi. Kesheni ili akija ghafla asije akawakuta mmelala.
Marko 13:32-36 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Walakini habari ya siku ile na saa ile hakuna aijuaye, hata malaika walio mbinguni, wala Mwana, ila Baba. Angalieni, kesheni, [ombeni], kwa kuwa hamjui wakati ule utakapokuwapo. Mfano wake ni kama mtu mwenye kusafiri, ameiacha nyumba yake, amewapa watumwa wake amri, na kila mtu kazi yake, naye amemwamuru bawabu akeshe. Kesheni basi, kwa maana hamjui ajapo bwana wa nyumba, kwamba ni jioni, au kwamba ni usiku wa manane, au awikapo jimbi, au asubuhi; asije akawasili ghafula akawakuta mmelala.
Marko 13:32-36 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
“Kwa habari ya siku ile na saa hakuna yeyote ajuaye, hata malaika walio mbinguni wala Mwana, ila Baba peke yake. Jihadharini! Kesheni! Kwa maana hamjui wakati ule utakapowadia. Ni kama mtu anayesafiri. Anaiacha nyumba yake na kuwaachia watumishi wake kuiangalia, kila mtu na kazi yake, kisha akamwamuru yule bawabu aliye mlangoni akeshe. “Basi kesheni kwa sababu hamjui ni lini mwenye nyumba atakaporudi: iwapo ni jioni, au ni usiku wa manane, au alfajiri awikapo jogoo, au mapambazuko. Kama akija ghafula, asije akawakuta mmelala.