Marko 12:1-5
Marko 12:1-5 Biblia Habari Njema (BHN)
Yesu alianza kusema nao kwa mifano: “Mtu mmoja alilima shamba la mizabibu. Akalizungushia ukuta, na katikati yake akachimba kisima cha kusindikia divai, akajenga mnara pia. Akalikodisha shamba hilo kwa wakulima, akasafiri hadi nchi ya mbali. Wakati wa mavuno, alimtuma mtumishi wake kwa wale wakulima, akamletee sehemu ya mazao ya shamba lake. Wale wakulima wakamkamata, wakampiga, wakamrudisha mikono mitupu. Akamtuma tena mtumishi mwingine; huyu pia wakamwumiza kichwa na kumtendea vibaya. Yule mwenye shamba akatuma mtumishi mwingine tena ambaye hao wakulima walimuua. Wengine wengi waliotumwa, baadhi yao walipigwa, na wengi wakauawa.
Marko 12:1-5 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Akaanza kusema nao kwa mifano; Mtu mmoja alipanda shamba la mizabibu, akalizungushia ua, akachimba shimo la shinikizo, akajenga mnara, akapangisha wakulima, akasafiri. Na kwa wakati wake akatuma mtumwa kwa wale wakulima, ili apokee kwa wakulima katika matunda ya mizabibu. Wakamtwaa, wakampiga, wakamtoa nje, bila chochote. Akatuma tena kwao mtumwa mwingine, na huyo wakamtia majeraha ya kichwa, wakamfanyia jeuri. Akamtuma mwingine, huyo wakamwua; na wengine wengi, hawa wakiwapiga na hawa wakiwaua.
Marko 12:1-5 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Akaanza kusema nao kwa mifano; Mtu mmoja alipanda shamba la mizabibu, akazungusha ugo, akachimba shimo la shinikizo, akajenga mnara, akapangisha wakulima, akasafiri. Hata kwa wakati wake akatuma mtumwa kwa wale wakulima, ili apokee kwa wakulima katika matunda ya mizabibu. Wakamtwaa, wakampiga, wakamtoa nje, hana kitu. Akatuma tena kwao mtumwa mwingine, na huyo wakamtia jeraha za kichwa, wakamfanyia jeuri. Akamtuma mwingine, huyo wakamwua; na wengine wengi, hawa wakiwapiga na hawa wakiwaua.
Marko 12:1-5 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Yesu akaanza kusema nao kwa mifano, akawaambia: “Mtu mmoja alipanda shamba la mizabibu. Akajenga ukuta kulizunguka, akachimba shimo ndani yake kwa ajili ya shinikizo la kusindika divai, na akajenga mnara wa ulinzi. Kisha akalikodisha shamba hilo la mizabibu kwa wakulima fulani, kisha akasafiri kwenda nchi nyingine. Wakati wa mavuno ulipofika, mwenye shamba akamtuma mtumishi wake kwa hao wapangaji ili kuchukua sehemu yake ya mavuno ya shamba la mizabibu kutoka kwa hao wapangaji. Lakini wale wakulima walimkamata yule mtumishi, wakampiga, wakamfukuza mikono mitupu. Kisha yule mwenye shamba akamtuma mtumishi mwingine kwao; nao wale wakulima wakampiga kichwani na kumfanyia mambo ya aibu. Kisha akamtuma mtumishi mwingine, naye huyo wakamuua. Akawatuma wengine wengi; baadhi yao wakawapiga, na wengine wakawaua.