Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Marko 11:12-25

Marko 11:12-25 Biblia Habari Njema (BHN)

Kesho yake, walipokuwa wanatoka Bethania, Yesu aliona njaa. Basi, akaona kwa mbali mtini wenye majani mengi. Akauendea ili aone kama ulikuwa na tunda lolote. Alipoufikia, aliukuta bila tunda lolote ila tu majani matupu, kwa vile hayakuwa majira yake ya matunda. Hapo akauambia mtini, “Tangu leo hata milele mtu yeyote asile matunda kwako.” Nao wanafunzi wake walisikia maneno hayo. Basi, wakafika Yerusalemu. Yesu akaingia hekaluni akaanza kuwafukuza nje watu waliokuwa wanauza na kununua vitu humo. Akazipindua meza za wale waliokuwa wakibadilishana fedha, na viti vya wale waliokuwa wakiuza njiwa. Hakumruhusu mtu yeyote kupitia hekaluni akichukua kitu. Kisha akawafundisha, “Imeandikwa: ‘Nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala kwa ajili ya mataifa yote!’ Lakini nyinyi mmeifanya kuwa pango la wanyanganyi!” Makuhani wakuu na waalimu wa sheria waliposikia hayo, walianza kutafuta njia ya kumwangamiza. Lakini walimwogopa kwa sababu umati wa watu ulishangazwa na mafundisho yake. Ilipokuwa jioni, Yesu na wanafunzi wake waliondoka mjini. Asubuhi na mapema, walipokuwa wanapita, waliuona ule mtini umenyauka wote, hata mizizi. Petro aliukumbuka, akamwambia Yesu, “Mwalimu, tazama! Ule mtini ulioulaani, umenyauka!” Yesu akawaambia, “Mwaminini Mungu. Nawaambieni kweli, mtu akiuambia mlima huu: ‘Ngoka ukajitose baharini,’ bila kuona shaka moyoni mwake, ila akaamini kwamba mambo yote anayosema yanafanyika, atafanyiwa jambo hilo. Kwa hiyo nawaambieni, mnaposali na kuomba kitu, aminini kwamba mmekipokea, nanyi mtapewa. Mnaposimama kusali, msameheni kila mtu aliyewakosea chochote, ili Baba yenu aliye mbinguni awasamehe nyinyi makosa yenu.” [

Shirikisha
Soma Marko 11

Marko 11:12-25 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Siku iliyofuata walipokuwa wakitoka Bethania, aliona njaa. Akaona kwa mbali mtini wenye majani, akaenda ili labda aone kitu juu yake; na alipoufikia hakuona kitu ila majani; maana si wakati wa tini. Akajibu, akauambia, Tangu leo hata milele mtu asile matunda kwako. Wanafunzi wake wakasikia. Wakafika Yerusalemu, naye akaingia ndani ya hekalu, akaanza kuwafukuza wale waliokuwa wakiuza na kununua ndani ya hekalu, akazipindua meza za wabadili fedha, na viti vyao wauzao njiwa; wala hakumruhusu mtu yeyote kupitia katika hekalu akiwa amebeba kitu. Akafundisha, akasema, Je! Haikuandikwa, Nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala kwa mataifa yote? Bali ninyi mmeifanya kuwa pango la wanyang'anyi. Wakuu wa makuhani na waandishi wakapata habari wakatafuta jinsi ya kumwangamiza; maana walimwogopa, kwa sababu mkutano wote walishangazwa na mafundisho yake. Na kulipokuwa jioni alitoka mjini. Na asubuhi walipokuwa wakipita, waliuona ule mtini umenyauka toka shinani. Petro akakumbuka habari yake, akamwambia, Rabi, tazama, mtini ulioulaani umenyauka. Yesu akajibu, akamwambia, Mwaminini Mungu. Amin, nawaambia, yeyote atakayeuambia mlima huu, Ng'oka ukatupwe baharini, wala asione shaka moyoni mwake, ila aamini kwamba hayo asemayo yametukia, yatakuwa yake. Kwa sababu hiyo nawaambia, Yoyote myaombayo mkisali, aminini ya kwamba mnayapokea, nayo yatakuwa yenu. Nanyi, kila msimamapo na kusali, sameheni, mkiwa na neno juu ya mtu; ili na Baba yenu aliye mbinguni awasamehe na ninyi makosa yenu. [

Shirikisha
Soma Marko 11

Marko 11:12-25 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Hata asubuhi yake walipotoka Bethania aliona njaa. Akaona kwa mbali mtini wenye majani, akaenda ili labda aone kitu juu yake; na alipoufikilia hakuona kitu ila majani; maana si wakati wa tini. Akajibu, akauambia, Tangu leo hata milele mtu asile matunda kwako. Wanafunzi wake wakasikia. Wakafika Yerusalemu, naye akaingia ndani ya hekalu, akaanza kuwafukuza wale waliokuwa wakiuza na kununua ndani ya hekalu, akazipindua meza za wabadili fedha, na viti vyao wauzao njiwa; wala hakuacha mtu achukue chombo kati ya hekalu. Akafundisha, akasema, Je! Haikuandikwa, Nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala kwa mataifa yote? Bali ninyi mmeifanya kuwa pango la wanyang’anyi. Wakuu wa makuhani na waandishi wakapata habari wakatafuta jinsi ya kumwangamiza; maana walimwogopa, kwa sababu mkutano wote walishangaa kwa mafundisho yake. Na kulipokuwa jioni alitoka mjini. Na asubuhi walipokuwa wakipita, waliuona ule mtini umenyauka toka shinani. Petro akakumbuka habari yake, akamwambia, Rabi, tazama, mtini ulioulaani umenyauka. Yesu akajibu, akamwambia, Mwaminini Mungu. Amin, nawaambia, Ye yote atakayeuambia mlima huu, Ng’oka ukatupwe baharini, wala asione shaka moyoni mwake, ila aamini kwamba hayo asemayo yametukia, yatakuwa yake. Kwa sababu hiyo nawaambia, Yo yote myaombayo mkisali, aminini ya kwamba mnayapokea, nayo yatakuwa yenu. Nanyi, kila msimamapo na kusali, sameheni, mkiwa na neno juu ya mtu; ili na Baba yenu aliye mbinguni awasamehe na ninyi makosa yenu. [

Shirikisha
Soma Marko 11

Marko 11:12-25 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Kesho yake walipokuwa wakitoka Bethania, Yesu alikuwa na njaa. Akauona mtini kwa mbali, naye akaenda ili aone kama ulikuwa na matunda. Alipoufikia, akakuta una majani tu, kwa kuwa hayakuwa majira ya tini. Akauambia ule mti, “Tangu leo mtu yeyote asile kamwe matunda kutoka kwako.” Wanafunzi wake walimsikia akisema hayo. Walipofika Yerusalemu, Yesu akaingia katika eneo la Hekalu, akaanza kuwafukuza wale waliokuwa wakinunua na kuuza humo ndani. Akazipindua meza za wale waliokuwa wakibadilisha fedha, na pia viti vya wale waliokuwa wakiuza njiwa, wala hakumruhusu mtu yeyote kuchukua bidhaa kupitia ukumbi wa Hekalu. Naye alipokuwa akiwafundisha, akasema, “Je, haikuandikwa kuwa: “ ‘Nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala kwa mataifa yote’? Lakini ninyi mmeifanya kuwa ‘pango la wanyangʼanyi.’ ” Viongozi wa makuhani na walimu wa sheria wakapata habari hizi, nao wakaanza kutafuta njia ya kumuua, kwa kuwa walikuwa wakimwogopa, kwa sababu umati wote ulikuwa unashangazwa na mafundisho yake. Ilipofika jioni, Yesu na wanafunzi wake wakatoka nje ya mji. Asubuhi yake walipokuwa wakipita, wakauona ule mtini umenyauka kutoka juu hadi kwenye mizizi yake. Petro akakumbuka na kumwambia Yesu, “Rabi, tazama! Ule mtini ulioulaani umenyauka!” Yesu akawajibu, “Mwaminini Mungu. Amin, nawaambia, mtu yeyote atakayeuambia mlima huu, ‘Ngʼoka ukatupwe baharini,’ wala asione shaka moyoni mwake, bali aamini kwamba hayo asemayo yametukia, atatimiziwa. Kwa sababu hiyo nawaambia, yoyote mtakayoyaomba mkisali, aminini ya kwamba mmeyapokea, nayo yatakuwa yenu. Nanyi kila msimamapo kusali, sameheni mkiwa na neno na mtu, ili naye Baba yenu aliye mbinguni awasamehe ninyi makosa yenu. [

Shirikisha
Soma Marko 11