Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Marko 11:12-23

Marko 11:12-23 Biblia Habari Njema (BHN)

Kesho yake, walipokuwa wanatoka Bethania, Yesu aliona njaa. Basi, akaona kwa mbali mtini wenye majani mengi. Akauendea ili aone kama ulikuwa na tunda lolote. Alipoufikia, aliukuta bila tunda lolote ila tu majani matupu, kwa vile hayakuwa majira yake ya matunda. Hapo akauambia mtini, “Tangu leo hata milele mtu yeyote asile matunda kwako.” Nao wanafunzi wake walisikia maneno hayo. Basi, wakafika Yerusalemu. Yesu akaingia hekaluni akaanza kuwafukuza nje watu waliokuwa wanauza na kununua vitu humo. Akazipindua meza za wale waliokuwa wakibadilishana fedha, na viti vya wale waliokuwa wakiuza njiwa. Hakumruhusu mtu yeyote kupitia hekaluni akichukua kitu. Kisha akawafundisha, “Imeandikwa: ‘Nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala kwa ajili ya mataifa yote!’ Lakini nyinyi mmeifanya kuwa pango la wanyanganyi!” Makuhani wakuu na waalimu wa sheria waliposikia hayo, walianza kutafuta njia ya kumwangamiza. Lakini walimwogopa kwa sababu umati wa watu ulishangazwa na mafundisho yake. Ilipokuwa jioni, Yesu na wanafunzi wake waliondoka mjini. Asubuhi na mapema, walipokuwa wanapita, waliuona ule mtini umenyauka wote, hata mizizi. Petro aliukumbuka, akamwambia Yesu, “Mwalimu, tazama! Ule mtini ulioulaani, umenyauka!” Yesu akawaambia, “Mwaminini Mungu. Nawaambieni kweli, mtu akiuambia mlima huu: ‘Ngoka ukajitose baharini,’ bila kuona shaka moyoni mwake, ila akaamini kwamba mambo yote anayosema yanafanyika, atafanyiwa jambo hilo.

Shirikisha
Soma Marko 11

Marko 11:12-23 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Kesho yake walipokuwa wakitoka Bethania, Yesu alikuwa na njaa. Akauona mtini kwa mbali, naye akaenda ili aone kama ulikuwa na matunda. Alipoufikia, akakuta una majani tu, kwa kuwa hayakuwa majira ya tini. Akauambia ule mti, “Tangu leo mtu yeyote asile kamwe matunda kutoka kwako.” Wanafunzi wake walimsikia akisema hayo. Walipofika Yerusalemu, Yesu akaingia katika eneo la Hekalu, akaanza kuwafukuza wale waliokuwa wakinunua na kuuza humo ndani. Akazipindua meza za wale waliokuwa wakibadilisha fedha, na pia viti vya wale waliokuwa wakiuza njiwa, wala hakumruhusu mtu yeyote kuchukua bidhaa kupitia ukumbi wa Hekalu. Naye alipokuwa akiwafundisha, akasema, “Je, haikuandikwa kuwa: “ ‘Nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala kwa mataifa yote’? Lakini ninyi mmeifanya kuwa ‘pango la wanyangʼanyi.’ ” Viongozi wa makuhani na walimu wa sheria wakapata habari hizi, nao wakaanza kutafuta njia ya kumuua, kwa kuwa walikuwa wakimwogopa, kwa sababu umati wote ulikuwa unashangazwa na mafundisho yake. Ilipofika jioni, Yesu na wanafunzi wake wakatoka nje ya mji. Asubuhi yake walipokuwa wakipita, wakauona ule mtini umenyauka kutoka juu hadi kwenye mizizi yake. Petro akakumbuka na kumwambia Yesu, “Rabi, tazama! Ule mtini ulioulaani umenyauka!” Yesu akawajibu, “Mwaminini Mungu. Amin, nawaambia, mtu yeyote atakayeuambia mlima huu, ‘Ngʼoka ukatupwe baharini,’ wala asione shaka moyoni mwake, bali aamini kwamba hayo asemayo yametukia, atatimiziwa.

Shirikisha
Soma Marko 11