Marko 10:17-27
Marko 10:17-27 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Alipokuwa akitoka kwenda njiani, mtu mmoja akaja mbio, akampigia magoti, akamwuliza, Mwalimu mwema, nifanye nini nipate kuurithi uzima wa milele? Yesu akamwambia, Kwa nini kuniita mwema? Hakuna aliye mwema ila mmoja, ndiye Mungu. Wazijua amri, Usiue, Usizini, Usiibe, Usishuhudie uongo, Usidanganye, Waheshimu baba yako na mama yako. Akamwambia, Mwalimu, haya yote nimeyashika tangu utoto wangu. Yesu akamkazia macho, akampenda, akamwambia, Umepungukiwa na neno moja. Nenda, ukauze ulivyo navyo vyote, uwape maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni; kisha njoo unifuate. Lakini yeye akakunja uso kwa neno hilo, akaenda zake kwa huzuni; kwa sababu alikuwa na mali nyingi. Yesu akatazama kotekote, akawaambia wanafunzi wake, Jinsi itakavyokuwa shida wenye mali kuingia katika ufalme wa Mungu! Wanafunzi wakashangaa kwa maneno yake. Yesu akajibu tena, akawaambia, Watoto, jinsi ilivyo shida wenye kutegemea mali kuingia katika ufalme wa Mungu! Ni rahisi ngamia kupenya katika tundu ya sindano kuliko tajiri kuingia katika ufalme wa Mungu. Nao wakashangaa mno, wakimwambia, Ni nani, basi, awezaye kuokoka? Yesu akawakazia macho, akasema, Kwa wanadamu haiwezekani, bali kwa Mungu sivyo; maana yote yawezekana kwa Mungu.
Marko 10:17-27 Biblia Habari Njema (BHN)
Yesu alipoanza tena safari yake, mtu mmoja alimjia mbio, akapiga magoti mbele yake, akamwuliza, “Mwalimu mwema, nifanyeje niupate uhai wa milele?” Yesu akamjibu, “Mbona unaniita mwema? Hakuna aliye mwema ila Mungu peke yake. Unazijua amri: ‘Usizini, Usiue, Usiibe, Usitoe ushahidi wa uongo, Usidanganye, Waheshimu baba yako na mama yako.’” Naye akamjibu, “Mwalimu, hayo yote nimeyazingatia tangu ujana wangu.” Yesu akamtazama, akampenda, akamwambia, “Umepungukiwa na kitu kimoja: Nenda ukauze kila kitu ulicho nacho, uwape maskini hizo fedha, nawe utakuwa na hazina mbinguni, kisha uje unifuate.” Aliposikia hayo, alisikitika, akaenda zake akiwa na huzuni, kwa maana alikuwa na mali nyingi. Yesu akatazama pande zote, akawaambia wanafunzi wake, “Jinsi gani itakavyokuwa vigumu kwa matajiri kuingia katika ufalme wa Mungu!” Wanafunzi walishangazwa na maneno yake. Yesu akawaambia tena, “Watoto wangu, ni vigumu sana kuingia katika ufalme wa Mungu! Ni rahisi zaidi ngamia kupenya katika tundu la sindano, kuliko tajiri kuingia katika ufalme wa Mungu.” Wanafunzi wake wakashangaa sana wakaulizana, “Ni nani basi, atakayeweza kuokoka?” Yesu akawatazama, akawaambia, “Kwa binadamu haiwezekani, lakini kwa Mungu si hivyo, maana kwa Mungu mambo yote huwezekana.”
Marko 10:17-27 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Hata alipokuwa akitoka kwenda njiani, mtu mmoja akaja mbio, akampigia magoti, akamwuliza, Mwalimu mwema, nifanye nini nipate kuurithi uzima wa milele? Yesu akamwambia, Kwa nini kuniita mwema? Hakuna aliye mwema ila mmoja, ndiye Mungu. Wazijua amri, Usiue, Usizini, Usiibe, Usishuhudie uongo, Usidanganye, Waheshimu baba yako na mama yako. Akamwambia, Mwalimu, haya yote nimeyashika tangu utoto wangu. Yesu akamkazia macho, akampenda, akamwambia, Umepungukiwa na neno moja. Enenda, ukauze ulivyo navyo vyote, uwape maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni; kisha njoo unifuate. Walakini yeye akakunja uso kwa neno hilo, akaenda zake kwa huzuni; kwa sababu alikuwa na mali nyingi. Yesu akatazama kotekote, akawaambia wanafunzi wake, Jinsi itakavyokuwa shida wenye mali kuingia katika ufalme wa Mungu! Wanafunzi wakashangaa kwa maneno yake. Yesu akajibu tena, akawaambia, Watoto, jinsi ilivyo shida wenye kutegemea mali kuingia katika ufalme wa Mungu! Ni rahisi ngamia kupenya katika tundu ya sindano kuliko tajiri kuingia katika ufalme wa Mungu. Nao wakashangaa mno, wakimwambia, Ni nani, basi, awezaye kuokoka? Yesu akawakazia macho, akasema, Kwa wanadamu haiwezekani, bali kwa Mungu sivyo; maana yote yawezekana kwa Mungu.
Marko 10:17-27 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Yesu alipokuwa anaondoka, mtu mmoja akamkimbilia, akapiga magoti mbele yake, akamuuliza, “Mwalimu mwema, nifanye nini ili niurithi uzima wa milele?” Yesu akamwambia, “Mbona unaniita mwema? Hakuna yeyote aliye mwema ila Mungu peke yake. Unazijua amri: ‘Usiue, usizini, usiibe, usishuhudie uongo, usidanganye, waheshimu baba yako na mama yako.’ ” Akamjibu, “Mwalimu, amri hizi zote nimezishika tangu nikiwa mtoto.” Yesu akamtazama na kumpenda, akamwambia, “Umepungukiwa na kitu kimoja. Nenda ukauze kila kitu ulicho nacho uwape maskini hizo fedha, nawe utakuwa na hazina mbinguni. Kisha njoo, unifuate.” Yule mtu aliposikia hayo, akasikitika sana. Akaondoka kwa huzuni kwa sababu alikuwa na mali nyingi. Yesu akatazama pande zote, akawaambia wanafunzi wake, “Itakuwa vigumu sana kwa wenye mali kuingia katika Ufalme wa Mungu!” Wanafunzi wake wakashangazwa sana na maneno hayo. Lakini Yesu akawaambia tena, “Wanangu, tazama jinsi ilivyo vigumu kwa wale wanaotumainia mali kuingia katika Ufalme wa Mungu. Ni rahisi zaidi kwa ngamia kupita kwenye tundu la sindano kuliko mtu tajiri kuingia katika Ufalme wa Mungu.” Wanafunzi wake wakashangaa sana. Wakaulizana wao kwa wao, “Ni nani basi awezaye kuokoka?” Yesu akawatazama, akawaambia, “Kwa mwanadamu jambo hili haliwezekani, lakini kwa Mungu sivyo. Mambo yote yanawezekana kwa Mungu.”