Marko 1:9-20
Marko 1:9-20 Biblia Habari Njema (BHN)
Siku hizo, Yesu alifika kutoka Nazareti, mji wa Galilaya, akabatizwa na Yohane katika mto Yordani. Mara tu alipotoka majini, aliona mbingu zimefunguliwa, na Roho akishuka juu yake kama njiwa. Sauti ikasikika kutoka mbinguni: “Wewe ni Mwanangu mpendwa, nimependezwa nawe.” Mara akaongozwa na Roho kwenda jangwani, akakaa huko siku arubaini akijaribiwa na Shetani. Alikuwa huko pamoja na wanyama wa porini, nao malaika wakawa wanamhudumia. Yohane alipokwisha fungwa gerezani, Yesu alikwenda Galilaya, akahubiri Habari Njema ya Mungu, akisema, “Wakati umetimia, na ufalme wa Mungu umekaribia. Tubuni na kuiamini Habari Njema!” Alipokuwa anapita kando ya ziwa Galilaya, aliwaona wavuvi wawili: Simoni na Andrea ndugu yake wakivua samaki kwa wavu. Yesu akawaambia, “Nifuateni nami nitawafanya nyinyi kuwa wavuvi wa watu.” Mara wakaziacha nyavu zao, wakamfuata. Alipokwenda mbele kidogo, aliwaona Yakobo na Yohane, wana wa Zebedayo. Nao pia walikuwa ndani ya mashua yao wakizitengeneza nyavu zao. Yesu akawaita mara, nao wakamwacha baba yao Zebedayo katika mashua pamoja na wafanyakazi, wakamfuata.
Marko 1:9-20 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ikawa siku zile, Yesu alikuja kutoka Nazareti ya Galilaya, akabatizwa na Yohana katika Yordani. Mara alipopanda kutoka majini, akaona mbingu zinapasuka, na Roho, kama hua, akishuka juu yake; na sauti ikatoka mbinguni, Wewe ndiwe Mwanangu, mpendwa wangu; nimependezwa nawe. Mara Roho akamtoa aende nyikani. Akawako huko jangwani siku arubaini, hali akijaribiwa na Shetani; naye alikuwa pamoja na wanyama wa mwituni, na malaika walikuwa wakimhudumia. Hata baada ya Yohana kutiwa gerezani, Yesu akaenda Galilaya, akiihubiri Habari Njema ya Mungu, akisema, Wakati umetimia, na ufalme wa Mungu umekaribia; tubuni, na kuiamini Injili. Naye alipokuwa akipita kando ya bahari ya Galilaya, akamwona Simoni na Andrea nduguye, wakitupa jarife baharini; kwa maana walikuwa wavuvi. Yesu akawaambia, Njooni mnifuate, nami nitawafanya kuwa wavuvi wa watu. Mara wakaziacha nyavu zao, wakamfuata. Akaendelea mbele kidogo, akamwona Yakobo wa Zebedayo, na Yohana nduguye, nao pia walikuwa katika mashua, wakizitengeneza nyavu zao. Mara akawaita, wakamwacha baba yao Zebedayo ndani ya mashua pamoja na wafanya kazi wakaenda, wakamfuata.
Marko 1:9-20 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ikawa siku zile, Yesu alikuja kutoka Nazareti ya Galilaya, akabatizwa na Yohana katika Yordani. Mara alipopanda kutoka majini, akaona mbingu zinapasuka, na Roho, kama hua, akishuka juu yake; na sauti ikatoka mbinguni, Wewe ndiwe Mwanangu, mpendwa wangu; nimependezwa nawe. Mara Roho akamtoa aende nyikani. Akawako huko jangwani siku arobaini, hali akijaribiwa na Shetani; naye alikuwa pamoja na wanyama wa mwitu, na malaika walikuwa wakimhudumia. Hata baada ya Yohana kutiwa gerezani, Yesu akaenda Galilaya, akiihubiri Habari Njema ya Mungu, akisema, Wakati umetimia, na ufalme wa Mungu umekaribia; tubuni, na kuiamini Injili. Naye alipokuwa akipita kando ya bahari ya Galilaya, akamwona Simoni na Andrea nduguye, wakitupa jarife baharini; kwa maana walikuwa wavuvi. Yesu akawaambia, Njoni mnifuate, nami nitawafanya kuwa wavuvi wa watu. Mara wakaziacha nyavu zao, wakamfuata. Akaendelea mbele kidogo, akamwona Yakobo wa Zebedayo, na Yohana nduguye, nao pia walikuwa chomboni, wakizitengeneza nyavu zao. Mara akawaita, wakamwacha baba yao Zebedayo ndani ya chombo pamoja na watu wa mshahara, wakaenda, wakamfuata.
Marko 1:9-20 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Wakati huo Yesu akaja kutoka Nazareti ya Galilaya, naye akabatizwa na Yohana katika Mto Yordani. Yesu alipokuwa akitoka ndani ya maji, aliona mbingu zikifunguka na Roho akishuka juu yake kama hua. Nayo sauti kutoka mbinguni ikasema, “Wewe ni Mwanangu mpendwa; nami nimependezwa nawe sana.” Wakati huo huo, Roho akamwongoza Yesu kwenda nyikani, naye akawa huko nyikani kwa muda wa siku arobaini, akijaribiwa na Shetani. Alikaa na wanyama wa mwituni, nao malaika wakamhudumia. Baada ya Yohana kukamatwa na kutiwa gerezani, Yesu aliingia Galilaya akaanza kuhubiri habari njema ya Mungu, akisema, “Wakati umewadia, Ufalme wa Mungu umekaribia. Tubuni na kuiamini Habari Njema.” Yesu alipokuwa akitembea kando ya Bahari ya Galilaya, aliwaona Simoni na Andrea nduguye wakizitupa nyavu zao baharini, kwa kuwa wao walikuwa wavuvi. Yesu akawaambia, “Njooni, nifuateni nami nitawafanya mwe wavuvi wa watu.” Mara wakaacha nyavu zao, wakamfuata. Alipokwenda mbele kidogo, akamwona Yakobo mwana wa Zebedayo na Yohana nduguye, wakiwa kwenye mashua yao wakizitengeneza nyavu zao. Papo hapo akawaita, nao wakamwacha Zebedayo baba yao kwenye mashua pamoja na watumishi wa kuajiriwa, nao wakamfuata Yesu.