Marko 1:40-45
Marko 1:40-45 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Akaja kwake mtu mwenye ukoma, akamsihi na kumpigia magoti, na kumwambia, Ukitaka, waweza kunitakasa. Naye akamhurumia, akanyosha mkono wake, akamgusa, akamwambia, Nataka, takasika. Na mara ukoma wake ukamtoka, akatakasika. Akamkataza kwa nguvu, akamwondoa mara, akamwambia, Angalia, usimwambie mtu neno lolote, ila nenda zako ukajioneshe kwa kuhani, ukatoe alivyoamuru Musa kwa ajili ya kutakasika kwako, iwe ushuhuda kwao. Lakini akatoka, akaanza kuhubiri maneno mengi, na kulitangaza lile neno, hata Yesu asiweze tena kuingia mjini waziwazi; bali alikaa nje mahali pasipokuwa na watu, wakamwendea kutoka kila upande.
Marko 1:40-45 Biblia Habari Njema (BHN)
Mtu mmoja mwenye ukoma alimwendea Yesu, akapiga magoti, akamwomba: “Ukitaka, waweza kunitakasa!” Yesu akamwonea huruma, akanyosha mkono wake, akamgusa na kumwambia, “Nataka! Takasika!” Mara ukoma ukamwacha mtu huyo, akatakasika. Kisha Yesu akamwambia aende zake upesi na kumwambia, “Angalia usimwambie mtu yeyote jambo hili, ila nenda ukajioneshe kwa kuhani na ukatoe sadaka kwa ajili ya kutakasika kwako kama alivyoamuru Mose kuwathibitishia kwamba umepona.” Lakini huyo mtu akaenda, akaanza kueneza habari hiyo kila mahali na kusema mambo mengi hata Yesu hakuweza tena kuingia katika mji wowote waziwazi; ikamlazimu kukaa nje, mahali pa faragha. Hata hivyo, watu wakamwendea kutoka kila upande.
Marko 1:40-45 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Akaja kwake mtu mwenye ukoma, akamsihi na kumpigia magoti, na kumwambia, Ukitaka, waweza kunitakasa. Naye akamhurumia, akanyosha mkono wake, akamgusa, akamwambia, Nataka, takasika. Na mara ukoma wake ukamtoka, akatakasika. Akamkataza kwa nguvu, akamwondoa mara, akamwambia, Angalia, usimwambie mtu neno lolote, ila enenda zako ukajionyeshe kwa kuhani, ukatoe alivyoamuru Musa kwa kutakasika kwako, iwe ushuhuda kwao. Lakini akatoka, akaanza kuhubiri maneno mengi, na kulitangaza lile neno, hata Yesu asiweze tena kuingia mjini kwa wazi; bali alikuwako nje mahali pasipokuwa na watu, wakamwendea kutoka kila mahali.
Marko 1:40-45 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Mtu mmoja mwenye ukoma alimjia Yesu, akamwomba akipiga magoti, akamwambia, “Ukitaka, waweza kunitakasa.” Yesu, akiwa amejawa na huruma, akanyoosha mkono wake akamgusa, akamwambia, “Nataka. Takasika!” Mara ukoma ukamtoka, naye akatakasika. Baada ya Yesu kumwonya vikali, akamruhusu aende zake akimwambia, “Hakikisha humwambii mtu yeyote habari hizi, bali nenda ukajionyeshe kwa kuhani, na ukatoe sadaka alizoagiza Mose kwa utakaso wako, ili kuwa ushuhuda kwao.” Lakini yule mtu akaenda akaanza kutangaza habari za kuponywa kwake waziwazi. Kwa hiyo, Yesu hakuweza tena kuingia katika miji waziwazi lakini alikaa sehemu zisizo na watu. Hata hivyo watu wakamfuata huko kutoka kila upande.