Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Marko 1:2-20

Marko 1:2-20 Biblia Habari Njema (BHN)

Ilianza kama ilivyoandikwa katika kitabu cha nabii Isaya: “Mungu alisema, ‘Namtuma mjumbe wangu akutangulie, ambaye atakutayarishia njia yako.’ Sauti ya mtu anaita jangwani: ‘Mtayarishieni Bwana njia yake, nyosheni barabara zake.’” Yohane Mbatizaji alitokea jangwani, akahubiri kwamba watu watubu na kubatizwa ili Mungu awasamehe dhambi zao. Watu kutoka sehemu zote za Yudea na wenyeji wote wa Yerusalemu walimwendea, wakaziungama dhambi zao, naye akawabatiza katika mto Yordani. Yohane alikuwa amevaa vazi lililofumwa kwa manyoya ya ngamia, na ukanda wa ngozi kiunoni mwake. Chakula chake kilikuwa nzige na asali ya mwituni. Naye alihubiri akisema, “Baada yangu anakuja mwenye nguvu zaidi kuliko mimi, ambaye mimi sistahili hata kuinama na kufungua kamba za viatu vyake. Mimi ninawabatiza kwa maji, lakini yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu.” Siku hizo, Yesu alifika kutoka Nazareti, mji wa Galilaya, akabatizwa na Yohane katika mto Yordani. Mara tu alipotoka majini, aliona mbingu zimefunguliwa, na Roho akishuka juu yake kama njiwa. Sauti ikasikika kutoka mbinguni: “Wewe ni Mwanangu mpendwa, nimependezwa nawe.” Mara akaongozwa na Roho kwenda jangwani, akakaa huko siku arubaini akijaribiwa na Shetani. Alikuwa huko pamoja na wanyama wa porini, nao malaika wakawa wanamhudumia. Yohane alipokwisha fungwa gerezani, Yesu alikwenda Galilaya, akahubiri Habari Njema ya Mungu, akisema, “Wakati umetimia, na ufalme wa Mungu umekaribia. Tubuni na kuiamini Habari Njema!” Alipokuwa anapita kando ya ziwa Galilaya, aliwaona wavuvi wawili: Simoni na Andrea ndugu yake wakivua samaki kwa wavu. Yesu akawaambia, “Nifuateni nami nitawafanya nyinyi kuwa wavuvi wa watu.” Mara wakaziacha nyavu zao, wakamfuata. Alipokwenda mbele kidogo, aliwaona Yakobo na Yohane, wana wa Zebedayo. Nao pia walikuwa ndani ya mashua yao wakizitengeneza nyavu zao. Yesu akawaita mara, nao wakamwacha baba yao Zebedayo katika mashua pamoja na wafanyakazi, wakamfuata.

Shirikisha
Soma Marko 1

Marko 1:2-20 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Kama ilivyoandikwa katika nabii Isaya, Tazama, namtuma mjumbe wangu Mbele ya uso wako, Atakayeitengeneza njia yako. Sauti ya mtu aliaye nyikani, Itengenezeni njia ya Bwana, Yanyosheni mapito yake. Yohana alitokea, akibatiza nyikani, na kuuhubiri ubatizo wa toba liletalo ondoleo la dhambi. Wakamwendea nchi yote ya Yudea, nao wa Yerusalemu wote, wakabatizwa katika mto wa Yordani, wakiziungama dhambi zao. Na Yohana alikuwa amevaa singa za ngamia na mshipi wa ngozi kiunoni mwake, akala nzige na asali ya mwituni. Akahubiri akisema, Yuaja nyuma yangu aliye na nguvu kuliko mimi, ambaye mimi sistahili kuinama na kuilegeza gidamu ya viatu vyake. Mimi niliwabatiza kwa maji; bali yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu. Ikawa siku zile, Yesu alikuja kutoka Nazareti ya Galilaya, akabatizwa na Yohana katika Yordani. Mara alipopanda kutoka majini, akaona mbingu zinapasuka, na Roho, kama hua, akishuka juu yake; na sauti ikatoka mbinguni, Wewe ndiwe Mwanangu, mpendwa wangu; nimependezwa nawe. Mara Roho akamtoa aende nyikani. Akawako huko jangwani siku arubaini, hali akijaribiwa na Shetani; naye alikuwa pamoja na wanyama wa mwituni, na malaika walikuwa wakimhudumia. Hata baada ya Yohana kutiwa gerezani, Yesu akaenda Galilaya, akiihubiri Habari Njema ya Mungu, akisema, Wakati umetimia, na ufalme wa Mungu umekaribia; tubuni, na kuiamini Injili. Naye alipokuwa akipita kando ya bahari ya Galilaya, akamwona Simoni na Andrea nduguye, wakitupa jarife baharini; kwa maana walikuwa wavuvi. Yesu akawaambia, Njooni mnifuate, nami nitawafanya kuwa wavuvi wa watu. Mara wakaziacha nyavu zao, wakamfuata. Akaendelea mbele kidogo, akamwona Yakobo wa Zebedayo, na Yohana nduguye, nao pia walikuwa katika mashua, wakizitengeneza nyavu zao. Mara akawaita, wakamwacha baba yao Zebedayo ndani ya mashua pamoja na wafanya kazi wakaenda, wakamfuata.

Shirikisha
Soma Marko 1

Marko 1:2-20 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Kama ilivyoandikwa katika nabii Isaya, Tazama, namtuma mjumbe wangu Mbele ya uso wako, Atakayeitengeneza njia yako. Sauti ya mtu aliaye nyikani, Itengenezeni njia ya Bwana, Yanyosheni mapito yake. Yohana alitokea, akibatiza nyikani, na kuuhubiri ubatizo wa toba liletalo ondoleo la dhambi. Wakamwendea nchi yote ya Uyahudi, nao wa Yerusalemu wote, wakabatizwa katika mto wa Yordani, wakiziungama dhambi zao. Na Yohana alikuwa amevaa singa za ngamia na mshipi wa ngozi kiunoni mwake, akala nzige na asali ya mwitu. Akahubiri akisema, Yuaja nyuma yangu aliye na nguvu kuliko mimi, ambaye mimi sistahili kuinama na kuilegeza gidamu ya viatu vyake. Mimi niliwabatiza kwa maji; bali yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu. Ikawa siku zile, Yesu alikuja kutoka Nazareti ya Galilaya, akabatizwa na Yohana katika Yordani. Mara alipopanda kutoka majini, akaona mbingu zinapasuka, na Roho, kama hua, akishuka juu yake; na sauti ikatoka mbinguni, Wewe ndiwe Mwanangu, mpendwa wangu; nimependezwa nawe. Mara Roho akamtoa aende nyikani. Akawako huko jangwani siku arobaini, hali akijaribiwa na Shetani; naye alikuwa pamoja na wanyama wa mwitu, na malaika walikuwa wakimhudumia. Hata baada ya Yohana kutiwa gerezani, Yesu akaenda Galilaya, akiihubiri Habari Njema ya Mungu, akisema, Wakati umetimia, na ufalme wa Mungu umekaribia; tubuni, na kuiamini Injili. Naye alipokuwa akipita kando ya bahari ya Galilaya, akamwona Simoni na Andrea nduguye, wakitupa jarife baharini; kwa maana walikuwa wavuvi. Yesu akawaambia, Njoni mnifuate, nami nitawafanya kuwa wavuvi wa watu. Mara wakaziacha nyavu zao, wakamfuata. Akaendelea mbele kidogo, akamwona Yakobo wa Zebedayo, na Yohana nduguye, nao pia walikuwa chomboni, wakizitengeneza nyavu zao. Mara akawaita, wakamwacha baba yao Zebedayo ndani ya chombo pamoja na watu wa mshahara, wakaenda, wakamfuata.

Shirikisha
Soma Marko 1

Marko 1:2-20 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Kama ilivyoandikwa katika kitabu cha nabii Isaya: “Tazama, nitamtuma mjumbe wangu mbele yako, atakayetengeneza njia mbele yako”: “sauti ya mtu aliaye nyikani. ‘Itengenezeni njia ya Bwana, yanyoosheni mapito yake.’ ” Yohana alikuja, akibatiza huko nyikani, akihubiri ubatizo wa toba kwa ajili ya msamaha wa dhambi. Watu kutoka Uyahudi wote na sehemu zote za Yerusalemu walikuwa wakimwendea. Nao wakaziungama dhambi zao, akawabatiza katika Mto Yordani. Yohana alivaa mavazi yaliyotengenezwa kwa singa za ngamia na mkanda wa ngozi kiunoni mwake. Chakula chake kilikuwa nzige na asali ya mwitu. Naye alihubiri akisema, “Baada yangu atakuja yeye aliye na uwezo kuniliko mimi, ambaye sistahili hata kuinama na kulegeza kamba za viatu vyake. Mimi nawabatiza kwa maji, lakini yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu.” Wakati huo Yesu akaja kutoka Nazareti ya Galilaya, naye akabatizwa na Yohana katika Mto Yordani. Yesu alipokuwa akitoka ndani ya maji, aliona mbingu zikifunguka na Roho akishuka juu yake kama hua. Nayo sauti kutoka mbinguni ikasema, “Wewe ni Mwanangu mpendwa; nami nimependezwa nawe sana.” Wakati huo huo, Roho akamwongoza Yesu kwenda nyikani, naye akawa huko nyikani kwa muda wa siku arobaini, akijaribiwa na Shetani. Alikaa na wanyama wa mwituni, nao malaika wakamhudumia. Baada ya Yohana kukamatwa na kutiwa gerezani, Yesu aliingia Galilaya akaanza kuhubiri habari njema ya Mungu, akisema, “Wakati umewadia, Ufalme wa Mungu umekaribia. Tubuni na kuiamini Habari Njema.” Yesu alipokuwa akitembea kando ya Bahari ya Galilaya, aliwaona Simoni na Andrea nduguye wakizitupa nyavu zao baharini, kwa kuwa wao walikuwa wavuvi. Yesu akawaambia, “Njooni, nifuateni nami nitawafanya mwe wavuvi wa watu.” Mara wakaacha nyavu zao, wakamfuata. Alipokwenda mbele kidogo, akamwona Yakobo mwana wa Zebedayo na Yohana nduguye, wakiwa kwenye mashua yao wakizitengeneza nyavu zao. Papo hapo akawaita, nao wakamwacha Zebedayo baba yao kwenye mashua pamoja na watumishi wa kuajiriwa, nao wakamfuata Yesu.

Shirikisha
Soma Marko 1