Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mika 6:1-16

Mika 6:1-16 Biblia Habari Njema (BHN)

Sikilizeni anachosema Mwenyezi-Mungu: “Wewe nabii, nenda ukailalamikie milima, navyo vilima visikie sauti yako.” Sikilizeni kesi ya Mwenyezi-Mungu enyi milima, sikilizeni enyi misingi ya kudumu ya dunia! Mwenyezi-Mungu anayo kesi dhidi ya watu wake. Yeye atatoa mashtaka dhidi ya Waisraeli. Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Enyi watu wangu, nimewatendea nini? Nimewachosha kwa kitu gani? Nijibuni! Mimi niliwatoa nchini Misri; niliwakomboa kutoka utumwani; niliwapeni Mose, Aroni na Miriamu kuwaongoza. Enyi watu wangu, kumbukeni njama za Balaki mfalme wa Moabu, na jinsi Balaamu mwana wa Beori alivyomjibu. Kumbukeni yaliyotukia njiani kati ya Shitimu na Gilgali. Kumbukeni mtambue matendo yangu ya kuwaokoa!” Nimwendee Mwenyezi-Mungu na kitu gani, nipate kumwabudu Mungu aliye juu? Je, nimwendee na sadaka za kuteketezwa, nimtolee ndama wa mwaka mmoja? Je, Mwenyezi-Mungu atapendezwa nikimtolea maelfu ya kondoo madume, au mito elfu na elfu ya mafuta? Je, nimtolee mzaliwa wangu wa kwanza kwa ajili ya kosa langu, naam, mtoto wangu kwa ajili ya dhambi yangu? Mungu amekuonesha yaliyo mema, ewe mtu; anachotaka Mwenyezi-Mungu kwako ni hiki: Kutenda mambo ya haki, kupenda kuwa na huruma, na kuishi kwa unyenyekevu na Mungu wako. Mwenyezi-Mungu anawaita wakazi wa mji, na ni jambo la busara sana kumcha yeye: “Sikilizeni, enyi watu wa Yuda; sikilizeni enyi mliokusanyika mjini. “Je, nitavumilia maovu yaliyorundikwa nyumbani mwao, mali zilizopatikana kwa udanganyifu, na matumizi ya mizani danganyifu, jambo ambalo ni chukizo? Je, naweza kusema hawana hatia watu wanaotumia mizani ya danganyifu na mawe ya kupimia yasiyo halali? Matajiri wa miji wamejaa dhuluma, wakazi wake husema uongo, kila wasemacho ni udanganyifu. Kwa hiyo nami, nimeanza kuwaangusha chini, na kuwaangamiza kwa sababu ya dhambi zenu. Mtakula lakini hamtashiba; ndani mwenu njaa itazidi kuwauma. Mkiweka akiba haitahifadhiwa, na mkihifadhi kitu nitakiharibu kwa vita. Mtapanda mbegu, lakini hamtavuna. Mtasindika zeituni, lakini hamtatumia hayo mafuta. Mtasindika zabibu, lakini hamtakunywa hiyo divai. Nyinyi mnafuata mfano mbaya wa mfalme Omri na mfano wa jamaa ya mfalme Ahabu na mfano mbaya wa jamaa ya mwanawe, Ahabu, na mmefuata mashauri yao. Kwa hiyo nitawaleteeni maangamizi, na kila mtu atawadharau. Watu watawadhihaki kila mahali.”

Shirikisha
Soma Mika 6

Mika 6:1-16 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Basi sasa, sikieni asemavyo BWANA; Simama, ujitetee mbele ya milima, vilima navyo na visikie sauti yako. Sikieni, enyi milima, shutuma ya BWANA, na ninyi, enyi misingi ya dunia iliyo imara; kwa maana BWANA ana shutuma na watu wake, naye atahojiana na Israeli. Enyi watu wangu, nimewatenda nini? Nami nimewachosha kwa kitu gani? Shuhudieni juu yangu. Kwa maana nilikupandisha kutoka nchi ya Misri, na kukukomboa utoke katika nyumba ya utumwa, nami niliwatuma Musa, na Haruni, na Miriamu, watangulie mbele yako. Enyi watu wangu, kumbukeni sasa alivyouliza Balaki, mfalme wa Moabu, na alivyojibu Balaamu, mwana wa Beori; kumbukeni yaliyotukia toka Shitimu hadi Gilgali, mpate kuyajua matendo ya haki ya BWANA. Nimwendee BWANA na kitu gani, na kuinama mbele za Mungu aliye juu? Je! Nimwendee na sadaka za kuteketezwa, na ndama wa umri wa mwaka mmoja? Je! BWANA atapendezwa na maelfu ya kondoo dume, au na makumi elfu ya mito ya mafuta? Je! Nimtoe mzaliwa wangu wa kwanza kwa kosa langu, mzawa wa mwili wangu kwa dhambi ya roho yangu? Ee mwanadamu, yeye amekuonesha yaliyo mema; na BWANA anataka nini kwako, ila kutenda haki, na kupenda rehema, na kwenda kwa unyenyekevu na Mungu wako! Sauti ya BWANA inaulilia mji, na mtu mwenye akili ataliona jina lako; isikieni hiyo fimbo na yeye aliyeiagiza. Je! Hata sasa hazina za uovu zingalimo nyumbani mwa wabaya, na kipimo kilichopunguka, ambacho ni chukizo? Je! Naweza kuwa safi nami nina mizani ya udhalimu, na mfuko wa mawe ya kupimia ya udanganyifu? Kwa maana matajiri wake wamejaa jeuri, na wenyeji wake wamesema uongo, na ulimi wao una udanganyifu kichwani mwao. Basi, kwa ajili ya hayo, mimi nami nimekupiga kwa pigo liumizalo sana; nimekufanya kuwa ukiwa, kwa sababu ya dhambi zako. Utakula, lakini hutashiba; ndani yenu njaa itazidi kuwauma; nawe utahama, lakini hutachukua kitu salama; na hicho utakachochukua nitakitoa kwa upanga. Utapanda, lakini hutavuna; utazikanyaga zeituni, lakini hutajipaka mafuta; na hizo zabibu, lakini hutakunywa divai. Kwa maana amri za Omri ndizo zishikwazo, na matendo yote ya nyumba ya Ahabu, nanyi mnakwenda katika mashauri yao; ili nikufanye kuwa ukiwa, na wenyeji waliomo humo kuwa zomeo; nanyi mtayachukua matukano waliyotukanwa watu wangu.

Shirikisha
Soma Mika 6

Mika 6:1-16 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Basi sasa, sikieni asemavyo BWANA; Simama, ujitetee mbele ya milima, vilima navyo na visikie sauti yako. Sikieni, enyi milima, mateto ya BWANA, na ninyi, enyi misingi ya dunia iliyo imara; kwa maana BWANA ana mateto na watu wake, naye atahojiana na Israeli. Enyi watu wangu, nimewatenda nini? Nami nimewachosha kwa habari gani? Shuhudieni juu yangu. Kwa maana nalikupandisha kutoka nchi ya Misri, na kukukomboa utoke katika nyumba ya utumwa, nami naliwapeleka Musa, na Haruni, na Miriamu, watangulie mbele yako. Enyi watu wangu, kumbukeni sasa alivyouliza Balaki, mfalme wa Moabu, na alivyojibu Balaamu, mwana wa Beori; kumbukeni toka Shitimu hata Gilgali, mpate kuyajua matendo ya haki ya BWANA. Nimkaribie BWANA na kitu gani, na kuinama mbele za Mungu aliye juu? Je! Nimkaribie na sadaka za kuteketezwa, na ndama za umri wa mwaka mmoja? Je! BWANA atapendezwa na elfu za kondoo waume, au na elfu kumi za mito ya mafuta? Je! Nimtoe mzaliwa wangu wa kwanza kwa kosa langu, mzao wa mwili wangu kwa dhambi ya roho yangu? Ee mwanadamu, yeye amekuonyesha yaliyo mema; na BWANA anataka nini kwako, ila kutenda haki, na kupenda rehema, na kwenda kwa unyenyekevu na Mungu wako! Sauti ya BWANA inaulilia mji, na mtu mwenye akili ataliona jina lako; isikieni hiyo fimbo na yeye aliyeiagiza. Je! Hata sasa hazina za uovu zingalimo nyumbani mwa wabaya, na kipimo kilichopunguka, ambacho ni chukizo? Je! Naweza kuwa safi nami nina mizani ya udhalimu, na mfuko wa mawe ya kupimia ya udanganyifu? Kwa maana matajiri wake wamejaa jeuri, na wenyeji wake wamesema uongo, na ulimi wao una udanganyifu kichwani mwao. Basi, kwa ajili ya hayo, mimi nami nimekupiga kwa pigo liumizalo sana; nimekufanya kuwa ukiwa, kwa sababu ya dhambi zako. Utakula, lakini hutashiba; na fedheha yako itakuwa kati yako; nawe utahama, lakini hutachukua kitu salama; na hicho utakachochukua nitakitoa kwa upanga. Utapanda, lakini hutavuna; utazikanyaga zeituni, lakini hutajipaka mafuta; na hizo zabibu, lakini hutakunywa divai. Kwa maana amri za Omri ndizo zishikwazo, na matendo yote ya nyumba ya Ahabu, nanyi mnakwenda katika mashauri yao; ili nikufanye kuwa ukiwa, na wenyeji waliomo humo kuwa zomeo; nanyi mtayachukua matukano waliyotukanwa watu wangu.

Shirikisha
Soma Mika 6

Mika 6:1-16 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Sikiliza asemalo BWANA: “Simama, tetea shauri lako mbele ya milima; vilima na visikie lile unalotaka kusema. Sikilizeni, ee milima, mashtaka ya BWANA, sikilizeni, enyi misingi ya milele ya dunia. Kwa kuwa BWANA ana shauri dhidi ya watu wake; anatoa mashtaka dhidi ya Israeli. “Watu wangu, nimewatendea nini? Nimewalemea kwa jinsi gani? Mnijibu. Nimewatoa kutoka Misri na kuwakomboa kutoka nchi ya utumwa. Nilimtuma Mose awaongoze, pia Aroni na Miriamu. Watu wangu, kumbukeni jinsi Balaki mfalme wa Moabu alivyofanya shauri na kile Balaamu mwana wa Beori alichojibu. Kumbukeni safari yenu kutoka Shitimu mpaka Gilgali, ili mfahamu matendo ya haki ya BWANA.” Nimjie BWANA na kitu gani na kusujudu mbele za Mungu aliyetukuka? Je, nije mbele zake na sadaka za kuteketezwa, nije na ndama za mwaka mmoja? Je, BWANA atafurahishwa na kondoo dume elfu, au mito elfu kumi ya mafuta? Je, nimtoe mzaliwa wangu wa kwanza kwa ajili ya kosa langu, mtoto wangu mwenyewe kwa ajili ya dhambi ya nafsi yangu? Amekuonyesha yaliyo mema, ee mwanadamu. BWANA anataka nini kwako? Ila kutenda kwa haki na kupenda rehema, na kwenda kwa unyenyekevu na Mungu wako. Sikiliza! BWANA anauita mji: kulicha jina lako ni hekima: “Tii hiyo fimbo na yeye aliyeiamuru. Je, bado nisahau, ee nyumba ya uovu, hazina yako uliyopata kwa udanganyifu na vipimo vilivyopunguka, ambavyo vimelaaniwa? Je, naweza kuhukumu kuwa mtu mwenye mizani ya udanganyifu hana hatia, aliye na mfuko wa mawe ya kupimia ya uongo? Matajiri wake ni wajeuri; watu wake ni waongo na ndimi zao zinazungumza kwa udanganyifu. Kwa hiyo, nimeanza kukuharibu, kuwaangamiza kwa sababu ya dhambi zenu. Mtakula lakini hamtashiba; matumbo yenu bado yatakuwa matupu. Mtaweka akiba lakini hamtaokoa chochote, kwa sababu mtakachoweka akiba nitatoa kwa upanga. Mtapanda lakini hamtavuna; mtakamua zeituni lakini hamtatumia mafuta yake. Mtakamua zabibu lakini hamtakunywa hiyo divai. Mmezishika sheria za Omri na matendo yote ya nyumba ya Ahabu, tena umefuata desturi zao. Kwa hiyo nitakutoa kwa maangamizi na watu wako kuwa dhihaka; mtachukua dharau za mataifa.”

Shirikisha
Soma Mika 6