Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mathayo 28:1-20

Mathayo 28:1-20 Biblia Habari Njema (BHN)

Baada ya Sabato, karibu na mapambazuko ya siku ile ya Jumapili, Maria Magdalene na yule Maria mwingine walikwenda kutazama lile kaburi. Ghafla kukatokea tetemeko kubwa la nchi; malaika wa Bwana alishuka kutoka mbinguni, akalivingirisha lile jiwe, akalikalia. Alionekana kama umeme na mavazi yake yalikuwa meupe kama theluji. Walinzi wa lile kaburi wakatetemeka kwa hofu kubwa, hata wakawa kama wamekufa. Lakini yule malaika akawaambia wale wanawake, “Nyinyi msiogope! Najua kwamba mnamtafuta Yesu aliyesulubiwa. Hayupo hapa maana amefufuka kama alivyosema. Njoni mkaone mahali alipokuwa amelala. Basi, nendeni upesi mkawaambie wanafunzi wake kwamba amefufuka kutoka kwa wafu, na sasa anawatangulieni kule Galilaya; huko mtamwona. Haya, mimi nimekwisha waambieni.” Wakiwa wenye hofu na furaha kubwa, hao wanawake walitoka upesi kaburini, wakakimbia kwenda kuwaambia wanafunzi wake. Mara, Yesu akakutana nao, akasema: “Salamu.” Hao wanawake wakamwendea, wakapiga magoti mbele yake, wakashika miguu yake. Kisha Yesu akawaambia, “Msiogope! Nendeni mkawaambie ndugu zangu waende Galilaya, na huko wataniona.” Wale wanawake walipokuwa wanakwenda zao, baadhi ya walinzi wa lile kaburi walikwenda mjini kutoa taarifa kwa makuhani wakuu juu ya mambo yote yaliyotukia. Basi, wakakutana pamoja na wazee, na baada ya kushauriana, wakawapa wale askari kiasi kikubwa cha fedha wakisema, “Nyinyi mtasema hivi: ‘Wanafunzi wake walikuja usiku, wakamwiba sisi tukiwa tumelala.’ Na kama mkuu wa mkoa akijua jambo hili, sisi tutasema naye na kuhakikisha kuwa nyinyi hamtapata matatizo.” Wale walinzi wakazichukua zile fedha, wakafanya kama walivyofundishwa. Habari hiyo imeenea kati ya Wayahudi mpaka leo. Wale wanafunzi kumi na mmoja walikwenda Galilaya kwenye ule mlima aliowaagizia Yesu. Walipomwona wakamwabudu, ingawa wengine walikuwa na mashaka. Yesu akaja karibu, akawaambia, “Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani. Nendeni basi, mkawafanye watu wa mataifa yote wawe wanafunzi wangu, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na la Mwana, na la Roho Mtakatifu. Wafundisheni kushika maagizo yote niliyowapeni. Nami nipo pamoja nanyi siku zote; naam, mpaka mwisho wa nyakati.”

Shirikisha
Soma Mathayo 28

Mathayo 28:1-20 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Na sabato ilipokwisha, ikipambazuka siku ya kwanza ya juma, Mariamu Magdalene, na Mariamu yule wa pili, walikwenda kulitazama kaburi. Na tazama, palikuwa na tetemeko kubwa la ardhi; kwa sababu malaika wa Bwana alishuka kutoka mbinguni, akaja akalivingirisha lile jiwe akalikalia. Na sura yake ilikuwa kama umeme, na mavazi yake meupe kama theluji. Na kwa kumwogopa, wale walinzi wakatetemeka, wakawa kama wafu. Malaika akajibu, akawaambia wale wanawake, Msiogope ninyi; kwa maana najua ya kuwa mnamtafuta Yesu aliyesulubiwa. Hayupo hapa; maana amefufuka kama alivyosema. Njooni, mpatazame mahali alipolazwa. Nanyi nendeni upesi, mkawaambie wanafunzi wake, Amefufuka katika wafu. Tazama, awatangulia kwenda Galilaya; ndiko mtakakomwona. Haya, nimekwisha waambia. Wakaondoka upesi kutoka kaburini, kwa hofu na furaha nyingi, wakaenda mbio kuwapasha wanafunzi wake habari. Na tazama, Yesu akakutana nao, akisema, Salamu! Wakakaribia wakamshika miguu, wakamsujudia. Kisha Yesu akawaambia, Msiogope; nendeni, mkawaambie ndugu zangu waende Galilaya, ndiko watakakoniona. Nao wale walipokuwa wakienda, tazama, baadhi ya walinzi waliingia mjini, wakawaambia wakuu wa makuhani juu ya mambo yote yaliyotendeka. Wakakusanyika pamoja na wazee, wakafanya shauri, wakawapa askari fedha nyingi, wakisema, Semeni, ya kwamba wanafunzi wake walikuja usiku, wakamwiba, sisi tulipokuwa tumelala. Na jambo hili likisikika kwa mtawala, sisi tutasema naye, nanyi hamtapata shida. Basi wakazitwaa zile fedha, wakafanya kama walivyofundishwa. Na neno hilo likaenea kati ya Wayahudi hata leo. Na wale wanafunzi kumi na mmoja wakaenda Galilaya hadi katika mlima ule aliowaagiza Yesu. Nao walipomwona, walimsujudia; lakini baadhi yao walikuwa na mashaka. Yesu akaja kwao, akasema nao, akawaambia, Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani. Basi, nendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu; na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari.

Shirikisha
Soma Mathayo 28

Mathayo 28:1-20 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Hata sabato ilipokwisha, ikipambazuka siku ya kwanza ya juma, Mariamu Magdalene, na Mariamu yule wa pili, walikwenda kulitazama kaburi. Na tazama, palikuwa na tetemeko kubwa la nchi; kwa sababu malaika wa Bwana alishuka kutoka mbinguni, akaja akalivingirisha lile jiwe akalikalia. Na sura yake ilikuwa kama umeme, na mavazi yake meupe kama theluji. Na kwa kumwogopa, wale walinzi wakatetemeka, wakawa kama wafu. Malaika akajibu, akawaambia wale wanawake, Msiogope ninyi; kwa maana najua ya kuwa mnamtafuta Yesu aliyesulibiwa. Hayupo hapa; kwani amefufuka kama alivyosema. Njoni, mpatazame mahali alipolazwa. Nanyi nendeni upesi, mkawaambie wanafunzi wake, Amefufuka katika wafu. Tazama, awatangulia kwenda Galilaya; ndiko mtakakomwona. Haya, nimekwisha waambia. Wakaondoka upesi kutoka kaburini, kwa hofu na furaha nyingi, wakaenda mbio kuwapasha wanafunzi wake habari. Na tazama, Yesu akakutana nao, akisema, Salamu! Wakakaribia wakamshika miguu, wakamsujudia. Kisha Yesu akawaambia, Msiogope; enendeni, mkawaambie ndugu zangu waende Galilaya, ndiko watakakoniona. Nao wale walipokuwa wakienda, tazama, baadhi ya askari waliingia mjini, wakawapasha wakuu wa makuhani habari za mambo yote yaliyotendeka. Wakakusanyika pamoja na wazee, wakafanya shauri, wakawapa askari fedha nyingi, wakisema, Semeni, ya kwamba wanafunzi wake walikuja usiku, wakamwiba, sisi tulipokuwa tumelala. Na neno hili likisikilikana kwa liwali, sisi tutasema naye, nanyi tutawaondolea wasiwasi. Basi wakazitwaa zile fedha, wakafanya kama walivyofundishwa. Na neno hilo likaenea kati ya Wayahudi hata leo. Na wale wanafunzi kumi na mmoja wakaenda Galilaya mpaka mlima ule aliowaagiza Yesu. Nao walipomwona, walimsujudia; lakini baadhi yao waliona shaka. Yesu akaja kwao, akasema nao, akawaambia, Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani. Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu; na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari.

Shirikisha
Soma Mathayo 28

Mathayo 28:1-20 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Baada ya Sabato, alfajiri mapema siku ya kwanza ya juma, Maria Magdalene na yule Maria mwingine walikwenda kulitazama kaburi. Ghafula, pakawa na tetemeko kubwa la ardhi, kwa sababu malaika wa Bwana alishuka kutoka mbinguni, akaenda penye kaburi, akalivingirisha lile jiwe na kulikalia. Sura ya huyo malaika ilikuwa kama umeme, na mavazi yake yalikuwa meupe kama theluji. Wale walinzi wa kaburi walimwogopa sana, wakatetemeka hata wakawa kama wafu. Yule malaika akawaambia wale wanawake, “Msiogope, kwa maana ninajua kuwa mnamtafuta Yesu aliyesulubiwa. Hayupo hapa, kwa kuwa amefufuka, kama vile alivyosema. Njooni mpatazame mahali alipokuwa amelazwa. Kisha nendeni upesi mkawaambie wanafunzi wake kwamba, ‘Amefufuka kutoka kwa wafu, naye awatangulia kwenda Galilaya. Huko ndiko mtamwona. Sasa nimekwisha kuwaambia.’ ” Hivyo wale wanawake wakaondoka pale kaburini wakiwa wamejawa na hofu, bali wakiwa na furaha nyingi. Wakaenda mbio kuwaeleza wanafunzi wake habari hizo. Ghafula, Yesu akakutana nao, akasema, “Salamu!” Wale wanawake wakamkaribia, wakaishika miguu yake, wakamwabudu. Ndipo Yesu akawaambia, “Msiogope. Nendeni mkawaambie ndugu zangu waende Galilaya, ndiko watakakoniona.” Wakati wale wanawake walikuwa njiani wakienda, baadhi ya wale askari waliokuwa wakilinda kaburi walienda mjini na kuwaeleza viongozi wa makuhani kila kitu kilichokuwa kimetukia. Baada ya viongozi wa makuhani kukutana na wazee na kutunga hila, waliwapa wale askari kiasi kikubwa cha fedha wakiwaambia, “Inawapasa mseme, ‘Wanafunzi wake walikuja wakati wa usiku na kumwiba sisi tulipokuwa tumelala.’ Kama habari hizi zikimfikia mtawala, sisi tutamwondolea mashaka nanyi hamtapata tatizo lolote.” Kwa hiyo wale askari wakazipokea hizo fedha nao wakafanya kama walivyoelekezwa. Habari hii imeenea miongoni mwa Wayahudi mpaka leo. Basi wale wanafunzi kumi na mmoja wakaenda hadi Galilaya kwenye ule mlima ambao Yesu alikuwa amewaagiza. Walipomwona, wakamwabudu; lakini baadhi yao wakaona shaka. Yesu akawajia na kusema, “Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani. Kwa sababu hii, enendeni mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa Jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu, nanyi wafundisheni kuyashika mambo yote niliyowaamuru ninyi. Hakika mimi niko pamoja nanyi siku zote, hadi mwisho wa nyakati.”

Shirikisha
Soma Mathayo 28