Mathayo 26:17-20
Mathayo 26:17-20 Biblia Habari Njema (BHN)
Siku ya kwanza kabla ya sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu, wanafunzi walimwendea Yesu wakamwuliza, “Unataka tukuandalie wapi chakula cha Pasaka?” Yeye akawajibu, “Nendeni mjini kwa mwanamume fulani, mkamwambie: ‘Mwalimu anasema, wakati wangu umefika; kwako nitakula Pasaka pamoja na wanafunzi wangu.’” Wanafunzi wakafanya kama Yesu alivyowaagiza, wakaandaa Pasaka. Kulipokuwa jioni, Yesu akakaa mezani pamoja na wanafunzi wake kumi na wawili.
Mathayo 26:17-20 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Katika siku ya kwanza ya mikate isiyotiwa chachu, wanafunzi wake wakamwendea Yesu, wakamwambia, Ni wapi utakapo tukuandalie uile Pasaka? Akasema, Nendeni mjini kwa mtu fulani, mkamwambie, Mwalimu asema, Majira yangu ni karibu; kwako nitafanya Pasaka pamoja na wanafunzi wangu. Wanafunzi wakafanya kama Yesu alivyowaagiza, wakaiandaa Pasaka. Basi kulipokuwa jioni aliketi chakulani pamoja na wale Kumi na Wawili.
Mathayo 26:17-20 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Hata siku ya kwanza ya mikate isiyotiwa chachu, wanafunzi wake wakamwendea Yesu, wakamwambia, Ni wapi utakapo tukuandalie uile Pasaka? Akasema, Enendeni mjini kwa mtu fulani, mkamwambie, Mwalimu asema, Majira yangu ni karibu; kwako nitafanya Pasaka pamoja na wanafunzi wangu. Wanafunzi wakafanya kama Yesu alivyowaagiza, wakaiandaa Pasaka. Basi kulipokuwa jioni aliketi chakulani pamoja na wale Thenashara.
Mathayo 26:17-20 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Siku ya kwanza ya Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu, wanafunzi walimjia Yesu wakamuuliza, “Unataka twende wapi ili tukuandalie mahali pa kula Pasaka?” Akajibu, “Nendeni kwa mtu fulani huko mjini, mkamwambie, ‘Mwalimu asema hivi: Saa yangu imekaribia. Nitaiadhimisha Pasaka pamoja na wanafunzi wangu katika nyumba yako.’ ” Hivyo wanafunzi wakafanya kama vile Yesu alivyokuwa amewaelekeza, nao wakaandaa Pasaka. Ilipofika jioni, Yesu alikuwa ameketi mezani pamoja na wale wanafunzi wake kumi na wawili.