Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mathayo 25:14-29

Mathayo 25:14-29 Biblia Habari Njema (BHN)

“Wakati huo itakuwa kama mtu mmoja aliyetaka kusafiri ngambo: Aliwaita watumishi wake, akawakabidhi mali yake. Alimpa kila mmoja kadiri ya uwezo wake: Mmoja fedha talanta tano, mwingine talanta mbili na mwingine talanta moja, kisha akasafiri. Mara yule aliyekabidhiwa fedha talanta tano akafanya kazi nazo akapata faida talanta tano. Hali kadhalika na yule aliyekabidhiwa talanta mbili akapata faida talanta mbili. Lakini yule aliyekabidhiwa fedha talanta moja akaenda, akachimba shimo ardhini, akaificha fedha ya bwana wake. “Baada ya muda mrefu, yule bwana alirudi, akaanza kukagua hesabu ya matumizi na mapato ya fedha yake. Mtumishi aliyekabidhiwa fedha talanta tano akaja amechukua talanta tano faida, akamwambia, ‘Bwana, ulinikabidhi talanta tano, hapa pana talanta tano zaidi faida niliyopata.’ Bwana wake akamwambia, ‘Vema, mtumishi mwema na mwaminifu. Umekuwa mwaminifu katika mambo madogo, nitakukabidhi makubwa. Njoo ufurahi pamoja na bwana wako.’ “Mtumishi aliyekabidhiwa talanta mbili akaja, akatoa talanta mbili faida, akisema, ‘Bwana, ulinikabidhi talanta mbili. Chukua talanta mbili zaidi faida niliyopata.’ Bwana wake akamwambia, ‘Vema, mtumishi mwema na mwaminifu. Umekuwa mwaminifu katika mambo madogo, nitakukabidhi makubwa. Njoo ufurahi pamoja na bwana wako.’ “Lakini yule aliyekabidhiwa fedha talanta moja akaja, akasema, ‘Bwana, najua wewe ni mtu mgumu; wewe huvuna pale ambapo hukupanda, na kukusanya pale ambapo hukutawanya. Niliogopa, nikaificha fedha yako katika ardhi. Chukua basi mali yako.’ “Bwana wake akamwambia, ‘Wewe ni mtumishi mwovu na mvivu! Unajua kuwa mimi huvuna mahali ambapo sikupanda, na hukusanya pale ambapo sikutawanya. Ilikupasa basi, kuiweka fedha yangu katika benki, nami ningelichukua mtaji wangu na faida yake! Basi, mnyanganyeni hiyo fedha mkampe yule mwenye talanta kumi. Maana, aliye na kitu atapewa na kuzidishiwa. Lakini yule asiye na kitu, hata kile alicho nacho kitachukuliwa.

Shirikisha
Soma Mathayo 25

Mathayo 25:14-29 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Maana itakuwa kama mfano wa mtu aliyetaka kusafiri, akawaita watumwa wake, akaweka kwao mali zake. Akampa mmoja talanta tano, na mmoja talanta mbili, na mmoja talanta moja; kila mtu kwa kadiri ya uwezo wake; akasafiri. Mara yule aliyepokea talanta tano akaenda, akafanya biashara nazo, akachuma faida talanta nyingine tano. Vile vile na yule mwenye mbili, yeye naye akachuma nyingine mbili faida. Lakini yule aliyepokea moja alikwenda akafukua chini, akaificha fedha ya bwana wake. Baada ya siku nyingi akaja bwana wa watumwa wale, akafanya hesabu nao. Akaja yule aliyepokea talanta tano, akaleta talanta nyingine tano, akisema, Bwana, uliweka kwangu talanta tano; tazama, talanta nyingine tano nilizopata faida. Bwana wake akamwambia, Vema, mtumwa mwema na mwaminifu; ulikuwa mwaminifu kwa machache, nitakuweka juu ya mengi; ingia katika furaha ya bwana wako. Akaja na yule aliyepokea talanta mbili, akasema, Bwana, uliweka kwangu talanta mbili; tazama, talanta nyingine mbili nilizopata faida. Bwana wake akamwambia, Vema, mtumwa mwema na mwaminifu; ulikuwa mwaminifu kwa machache, nitakuweka juu ya mengi; ingia katika furaha ya bwana wako. Akaja na yule aliyepokea talanta moja, akasema, Bwana, nilitambua ya kuwa wewe u mtu mgumu, wavuna usipopanda, wakusanya usipotawanya; basi nikaogopa, nikaenda nikaificha talanta yako katika ardhi; tazama, unayo iliyo yako. Bwana wake akajibu, akamwambia, Wewe mtumwa mbaya na mlegevu, ulijua ya kuwa navuna nisipopanda, nakusanya nisipotawanya; basi, ilikupasa kuiweka fedha yangu kwa watoao riba; nami nikija ningalipata iliyo yangu na faida yake. Basi, mnyang'anyeni talanta hiyo, mpeni yule aliye nazo talanta kumi. Kwa maana kila mwenye kitu atapewa, na kuongezewa tele; lakini asiye na kitu, hata kile alicho nacho atanyang'anywa.

Shirikisha
Soma Mathayo 25

Mathayo 25:14-29 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Maana ni mfano wa mtu atakaye kusafiri, aliwaita watumwa wake, akaweka kwao mali zake. Akampa mmoja talanta tano, na mmoja talanta mbili, na mmoja talanta moja; kila mtu kwa kadiri ya uwezo wake; akasafiri. Mara yule aliyepokea talanta tano akaenda, akafanya biashara nazo, akachuma faida talanta nyingine tano. Vile vile na yule mwenye mbili, yeye naye akachuma nyingine mbili faida. Lakini yule aliyepokea moja alikwenda akafukua chini, akaificha fedha ya bwana wake. Baada ya siku nyingi akaja bwana wa watumwa wale, akafanya hesabu nao. Akaja yule aliyepokea talanta tano, akaleta talanta nyingine tano, akisema, Bwana, uliweka kwangu talanta tano; tazama, talanta nyingine tano nilizopata faida. Bwana wake akamwambia, Vema, mtumwa mwema na mwaminifu; ulikuwa mwaminifu kwa machache, nitakuweka juu ya mengi; ingia katika furaha ya bwana wako. Akaja na yule aliyepokea talanta mbili, akasema, Bwana, uliweka kwangu talanta mbili; tazama, talanta nyingine mbili nilizopata faida. Bwana wake akamwambia, Vema, mtumwa mwema na mwaminifu; ulikuwa mwaminifu kwa machache, nitakuweka juu ya mengi; ingia katika furaha ya bwana wako. Akaja na yule aliyepokea talanta moja, akasema, Bwana, nalitambua ya kuwa wewe u mtu mgumu, wavuna usipopanda, wakusanya usipotawanya; basi nikaogopa, nikaenda nikaificha talanta yako katika ardhi; tazama, unayo iliyo yako. Bwana wake akajibu, akamwambia, Wewe mtumwa mbaya na mlegevu, ulijua ya kuwa navuna nisipopanda, nakusanya nisipotawanya; basi, ilikupasa kuiweka fedha yangu kwa watoao riba; nami nikija ningalipata iliyo yangu na faida yake. Basi, mnyang’anyeni talanta hiyo, mpeni yule aliye nazo talanta kumi. Kwa maana kila mwenye kitu atapewa, na kuongezewa tele; lakini asiye na kitu, hata kile alicho nacho atanyang’anywa.

Shirikisha
Soma Mathayo 25

Mathayo 25:14-29 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

“Tena, Ufalme wa Mbinguni ni kama mtu aliyetaka kusafiri, naye akawaita watumishi wake na kuweka mali yake kwenye uangalizi wao. Mmoja akampa talanta tano, mwingine talanta mbili, na mwingine talanta moja. Kila mmoja alipewa kwa kadiri ya uwezo wake. Kisha yeye akasafiri. Yule aliyepewa talanta tano akaenda mara moja akafanya nazo biashara akapata talanta nyingine tano zaidi. Yule aliyepewa talanta mbili akafanya vivyo hivyo, akapata nyingine mbili zaidi. Lakini yule mtumishi aliyekuwa amepokea talanta moja, alikwenda akachimba shimo ardhini na kuificha ile fedha ya bwana wake. “Baada ya muda mrefu, yule bwana wa wale watumishi akarudi na kufanya hesabu nao. Yule mtumishi aliyepokea talanta tano akaja, akaleta nyingine tano zaidi. Akasema, ‘Bwana uliweka kwenye uangalizi wangu talanta tano. Tazama, nimepata faida ya talanta tano zaidi.’ “Bwana wake akamwambia, ‘Umefanya vizuri sana, mtumishi mwema na mwaminifu! Umekuwa mwaminifu kwa vitu vichache; nami nitakuweka kuwa msimamizi wa vitu vingi. Njoo ushiriki katika furaha ya bwana wako!’ “Yule mwenye talanta mbili naye akaja. Akasema, ‘Bwana, uliweka kwenye uangalizi wangu talanta mbili. Tazama nimepata hapa talanta mbili zaidi.’ “Bwana wake akajibu, ‘Umefanya vizuri sana, mtumishi mwema na mwaminifu. Umekuwa mwaminifu kwa vitu vichache; nami nitakuweka kuwa msimamizi wa vitu vingi. Njoo ushiriki katika furaha ya bwana wako!’ “Kisha yule mtumishi aliyepokea talanta moja akaja, akasema, ‘Bwana, nilijua kwamba wewe ni mtu mgumu, unayevuna mahali usipopanda na kukusanya mahali usipotawanya mbegu. Kwa hiyo niliogopa, nikaenda, nikaificha talanta yako ardhini. Tazama, hii hapa ile iliyo mali yako.’ “Bwana wake akajibu, ‘Wewe mtumishi mwovu na mvivu! Ulijua kwamba ninavuna mahali nisipopanda na kukusanya mahali nisipotawanya mbegu. Vyema basi, ingekupasa kuweka fedha yangu kwa watoa riba, ili nirudipo, nichukue ile iliyo yangu na faida yake. “ ‘Basi mnyangʼanyeni hiyo talanta, mkampe yule mwenye talanta kumi. Kwa maana kila mtu aliye na kitu atapewa zaidi, naye atakuwa navyo tele. Lakini yule asiye na kitu, hata kile alicho nacho atanyangʼanywa.

Shirikisha
Soma Mathayo 25