Mathayo 22:15-22
Mathayo 22:15-22 Biblia Habari Njema (BHN)
Kisha, Mafarisayo wakaenda zao, wakashauriana jinsi ya kumnasa Yesu kwa maneno yake. Basi, wakawatuma wafuasi wao pamoja na wafuasi wa kikundi cha Herode. Wakamwuliza, “Mwalimu, tunajua kwamba wewe ni mtu mwaminifu, na kwamba wafundisha njia ya Mungu kwa uaminifu; humwogopi mtu yeyote, maana cheo cha mtu si kitu kwako. Haya, tuambie maoni yako. Je, ni halali au la, kulipa kodi kwa Kaisari?” Lakini Yesu alitambua uovu wao, akawaambia, “Enyi wanafiki mbona mnanijaribu? Nionesheni fedha ya kulipia kodi.” Nao wakamtolea sarafu ya fedha. Basi, Yesu akawauliza, “Sura na chapa hii ni ya nani?” Wakamjibu, “Ni ya Kaisari.” Hapo Yesu akawaambia, “Basi, ya Kaisari mpeni Kaisari, na ya Mungu mpeni Mungu.” Waliposikia hivyo wakashangaa; wakamwacha, wakaenda zao.
Mathayo 22:15-22 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ndipo Mafarisayo wakaenda zao, wakafanya shauri, jinsi ya kumtega kwa maneno. Wakatuma kwake wanafunzi wao pamoja na Maherodi, wakasema, Mwalimu, tunajua ya kuwa wewe u mtu wa kweli, na njia ya Mungu waifundisha katika kweli, wala hujali cheo cha mtu awaye yote, kwa maana hutazami sura za watu. Basi utuambie, Waonaje? Ni halali kumpa Kaisari kodi, ama sivyo? Lakini Yesu akaufahamu uovu wao, akasema, Mbona mnanijaribu, enyi wanafiki? Nionesheni fedha ya kodi. Nao wakamletea dinari. Akawaambia, Ni ya nani sanamu hii, na anwani hii? Wakamwambia, Ni ya Kaisari. Akawaambia, Basi, mpeni Kaisari yaliyo ya Kaisari, na Mungu yaliyo ya Mungu. Waliposikia, walistaajabu, wakamwacha, wakaenda zao.
Mathayo 22:15-22 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ndipo Mafarisayo wakaenda zao, wakafanya shauri, jinsi ya kumtega kwa maneno. Wakatuma kwake wanafunzi wao pamoja na Maherodi, wakasema, Mwalimu, twajua ya kuwa wewe u mtu wa kweli, na njia ya Mungu waifundisha katika kweli, wala hujali cheo cha mtu awaye yote, kwa maana hutazami sura za watu. Basi utuambie, Waonaje? Ni halali kumpa Kaisari kodi, ama sivyo? Lakini Yesu akaufahamu uovu wao, akasema, Mbona mnanijaribu, enyi wanafiki? Nionyesheni fedha ya kodi. Nao wakamletea dinari. Akawaambia, Ni ya nani sanamu hii, na anwani hii? Wakamwambia, Ni ya Kaisari. Akawaambia, Basi, mlipeni Kaisari yaliyo ya Kaisari, na Mungu yaliyo ya Mungu. Waliposikia, walistaajabu, wakamwacha, wakaenda zao.
Mathayo 22:15-22 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Ndipo Mafarisayo wakatoka nje wakaandaa mpango wa kumtega Yesu katika maneno yake. Wakatuma wanafunzi wao kwake pamoja na Maherode. Nao wakasema, “Mwalimu, tunajua kwamba wewe ni mtu mwadilifu na unafundisha njia ya Mungu katika kweli bila kuyumbishwa na mtu wala kuonyesha upendeleo. Tuambie basi, wewe unaonaje? Je, ni halali kulipa kodi kwa Kaisari, au la?” Lakini Yesu, akijua makusudi yao mabaya, akawaambia, “Enyi wanafiki, kwa nini mnajaribu kunitega? Nionyesheni hiyo sarafu inayotumika kwa kulipia kodi.” Wakamletea dinari. Naye akawauliza, “Sura hii ni ya nani? Na maandishi haya ni ya nani?” Wakamjibu, “Ni vya Kaisari.” Basi Yesu akawaambia, “Mpeni Kaisari kilicho cha Kaisari, naye Mungu mpeni kilicho cha Mungu.” Waliposikia hili, wakashangaa. Hivyo wakamwacha, wakaenda zao.