Mathayo 22:1-14
Mathayo 22:1-14 Biblia Habari Njema (BHN)
Yesu alisema nao tena kwa kutumia mifano: “Ufalme wa mbinguni umefanana na mfalme aliyemwandalia mwanawe karamu ya harusi. Basi, akawatuma watumishi kuwaita walioalikwa waje harusini, lakini walioalikwa hawakutaka kufika. Akawatuma tena watumishi wengine, akisema, ‘Waambieni wale walioalikwa: Karamu yangu iko tayari sasa; fahali wangu na ndama wanono wamekwisha chinjwa; kila kitu ni tayari; njoni harusini.’ Lakini wao hawakujali, wakaenda zao; mmoja shambani kwake, mwingine kwenye shughuli zake, na wengine wakawakamata wale watumishi wakawatukana, wakawaua. Yule mfalme akakasirika, akawatuma askari wake wakawaangamize wauaji hao na kuuteketeza mji wao. Kisha akawaambia watumishi wake: ‘Karamu ya harusi iko tayari kweli, lakini walioalikwa hawakustahili. Basi, nendeni kwenye barabara na wowote wale mtakaowakuta waiteni waje harusini.’ Wale watumishi wakatoka, wakaenda njiani, wakawaleta watu wote, wabaya na wema. Nyumba ya harusi ikajaa wageni. “Mfalme alipoingia kuwaona wageni, akamwona mtu mmoja ambaye hakuvaa mavazi ya harusi. Mfalme akamwuliza, ‘Rafiki, umeingiaje hapa bila vazi la harusi?’ Lakini yeye akakaa kimya. Hapo mfalme akawaambia watumishi, ‘Mfungeni miguu na mikono mkamtupe nje gizani; huko atalia na kusaga meno.’” Yesu akamaliza kwa kusema, “Wengi wamealikwa, lakini wachache wameteuliwa.”
Mathayo 22:1-14 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Yesu akasema nao tena kwa mifano, akawaambia, “Ufalme wa Mbinguni unaweza kufananishwa na mfalme mmoja aliyemwandalia mwanawe karamu ya arusi. Akawatuma watumishi wake kuwaita wale waliokuwa wamealikwa karamuni, lakini wakakataa kuja. “Kisha akawatuma watumishi wengine akisema, ‘Waambieni wale walioalikwa kwamba nimeandaa chakula. Nimekwisha kuchinja mafahali wangu na vinono, karamu iko tayari. Karibuni kwa karamu ya arusi.’ “Lakini hawakuzingatia, wakaenda zao: huyu shambani mwake na mwingine kwenye biashara zake. Wengine wao wakawakamata wale watumishi wake, wakawatesa na kuwaua. Yule mfalme akakasirika sana, akapeleka jeshi lake likawaangamiza wale wauaji na kuuteketeza mji wao kwa moto. “Kisha akawaambia watumishi wake, ‘Karamu ya arusi imeshakuwa tayari, lakini wale niliowaalika hawakustahili kuja. Kwa hiyo nendeni katika njia panda mkamwalike karamuni yeyote mtakayemwona.’ Wale watumishi wakaenda barabarani, wakawakusanya watu wote waliowaona, wema na wabaya. Ukumbi wa arusi ukajaa wageni. “Lakini mfalme alipoingia ndani ili kuwaona wageni, akamwona mle mtu mmoja ambaye hakuwa amevaa vazi la arusi. Mfalme akamuuliza, ‘Rafiki, uliingiaje humu bila vazi la arusi?’ Yule mtu hakuwa na la kusema. “Ndipo mfalme akawaambia watumishi wake, ‘Mfungeni mikono na miguu mkamtupe nje, kwenye giza. Huko kutakuwa na kilio na kusaga meno.’ “Kwa maana walioitwa ni wengi, lakini walioteuliwa ni wachache.”
Mathayo 22:1-14 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Yesu akajibu, akawaambia tena kwa mifano, akisema, Ufalme wa mbinguni unafanana na mfalme mmoja aliyemfanyia mwanawe arusi. Akawatuma watumwa wake wawaite walioalikwa kuja arusini; nao wakakataa kuja. Akatuma tena watu kwa wengine, akisema, Waambieni wale walioalikwa, Tazameni, nimeandaa karamu yangu; ng'ombe zangu na vinono vimekwisha kuchinjwa, na vyote vimekuwa tayari, njoni arusini. Lakini hawakujali, wakaenda zao, mmoja shambani kwake, mmoja kwenye biashara yake; nao waliosalia wakawakamata watumwa wake, wakawadhulumu na kuwaua. Basi yule mfalme akaghadhibika; akatuma majeshi yake, akawaangamiza wauaji wale, akauteketeza mji wao. Kisha akawaambia watumwa wake, Arusi iko tayari, lakini wale walioalikwa hawakustahili. Basi Nendeni hata njia panda za barabara, na wote mwaonao waiteni arusini. Watumwa wale wakatoka wakaenda njia kuu, wakakusanya wote waliowaona, waovu kwa wema; arusi ikajaa wageni. Lakini alipoingia yule mfalme ili kuwatazama wageni wake, akaona mle mtu mmoja asiyevaa vazi la arusi. Akamwambia, Rafiki, uliingiaje humu nawe huna vazi la arusi? Naye akatekewa. Mfalme akawaambia watumishi, Mfungeni mikono na miguu, mchukueni mkamtupe katika giza la nje; ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno. Kwa maana waitwao ni wengi, bali wateule ni wachache.
Mathayo 22:1-14 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Yesu akajibu, akawaambia tena kwa mithali, akisema, Ufalme wa mbinguni umefanana na mfalme mmoja aliyemfanyia mwanawe arusi. Akawatuma watumwa wake wawaite walioalikwa kuja arusini; nao wakakataa kuja. Akatuma tena watu kwa wengine, akisema, Waambieni wale walioalikwa, Tazameni, nimeandaa karamu yangu; ng’ombe zangu na vinono vimekwisha kuchinjwa, na vyote vimekuwa tayari, njoni arusini. Lakini hawakujali, wakaenda zao, mmoja shambani kwake, mmoja kwenye biashara yake; nao waliosalia wakawakamata watumwa wake, wakawatenda jeuri, na kuwaua. Basi yule mfalme akaghadhibika; akapeleka majeshi yake, akawaangamiza wauaji wale, akauteketeza mji wao. Kisha akawaambia watumwa wake, Arusi i tayari, lakini wale walioalikwa hawakustahili. Basi enendeni hata njia panda za barabara, na wote mwaonao waiteni arusini. Watumwa wale wakatoka wakaenda njia kuu, wakakusanya wote waliowaona, waovu kwa wema; arusi ikajaa wageni. Lakini alipoingia yule mfalme ili kuwatazama wageni wake, akaona mle mtu mmoja asiyevaa vazi la arusi. Akamwambia, Rafiki, uliingiaje humu nawe huna vazi la arusi? Naye akatekewa. Mfalme akawaambia watumishi, Mfungeni mikono na miguu, mchukueni mkamtupe katika giza la nje; ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno. Kwa maana waitwao ni wengi, bali wateule ni wachache.