Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mathayo 21:33-46

Mathayo 21:33-46 Biblia Habari Njema (BHN)

Yesu akasema, “Sikilizeni mfano mwingine. Mtu mmoja mwenye nyumba alilima shamba la mizabibu; akalizungushia ukuta, akachimba kisima cha kusindikia divai, akajenga humo mnara pia. Kisha akalikodisha kwa wakulima, akasafiri kwenda hadi nchi ya mbali. Wakati wa mavuno ulipofika, aliwatuma watumishi wake kwa wale wakulima, ili wakachukue sehemu ya mavuno yake. Wale wakulima wakawakamata hao watumishi; mmoja wakampiga, mwingine wakamuua na mwingine wakampiga mawe. Huyo mtu akawatuma tena watumishi wengine, wengi kuliko wa safari ya kwanza. Wale wakulima wakawatendea namna ileile. Mwishowe akamtuma mwanawe huku akifikiri: ‘Watamjali mwanangu.’ Lakini wale wakulima walipomwona mwanawe wakasemezana wao kwa wao: ‘Huyu ndiye mrithi; na tumuue ili tuuchukue urithi wake!’ Basi, wakamkamata, wakamtoa nje ya lile shamba la mizabibu, wakamuua. “Sasa, huyo mwenye shamba la mizabibu atakapokuja, atawafanyaje hao wakulima?” Wao wakamjibu, “Atawaangamiza vibaya hao waovu, na lile shamba atawapa wakulima wengine ambao watampa sehemu ya mavuno wakati wake.” Hapo Yesu akawaambia, “Je, hamkusoma jambo hili katika Maandiko Matakatifu? ‘Jiwe walilokataa waashi sasa limekuwa jiwe kuu la msingi. Bwana ndiye aliyefanya jambo hili, nalo ni la ajabu sana kwetu!’ “Kwa hiyo nawaambieni, ufalme wa Mungu utaondolewa kwenu na kupewa watu wa mataifa mengine wenye kutoa matunda yake.” Atakayeanguka juu ya jiwe hilo atavunjika vipandevipande; na likimwangukia mtu yeyote, litamponda” (taz. Luka 20:18). Makuhani wakuu na Mafarisayo waliposikia hiyo mifano yake walitambua kwamba alikuwa anawasema wao. Kwa hiyo wakawa wanatafuta njia ya kumtia nguvuni, lakini waliwaogopa watu kwa sababu wao walimtambua yeye kuwa nabii.

Shirikisha
Soma Mathayo 21

Mathayo 21:33-46 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

“Sikilizeni mfano mwingine: Kulikuwa na mtu mmoja mwenye shamba ambaye alipanda shamba la mizabibu. Akajenga ukuta kulizunguka, akatengeneza shinikizo ndani yake na akajenga mnara wa ulinzi. Kisha akalikodisha hilo shamba la mizabibu kwa wakulima fulani, naye akaondoka, akasafiri kwenda nchi nyingine. Wakati wa mavuno ulipokaribia, akawatuma watumishi wake kwa hao wapangaji ili kukusanya matunda yake. “Wale wapangaji wakawakamata wale watumishi, wakampiga mmoja, wakamuua mwingine, na yule wa tatu wakampiga mawe. Kisha akawatuma kwao watumishi wengine, wengi kuliko wale wa kwanza, nao wale wapangaji wakawatendea vilevile. Mwisho wa yote, akamtuma mwanawe kwao, akisema, ‘Watamheshimu mwanangu.’ “Lakini wale wapangaji walipomwona mwanawe, wakasemezana wao kwa wao, ‘Huyu ndiye mrithi. Njooni tumuue, ili tuchukue urithi wake.’ Hivyo wakamchukua, wakamtupa nje ya shamba la mizabibu, wakamuua. “Kwa hiyo, huyo mwenye shamba la mizabibu atakapokuja, atawafanyia nini hao wakulima?” Wakamjibu, “Kwa huzuni kuu atawaangamiza kabisa hao wadhalimu na kulipangisha shamba lake la mizabibu kwa wakulima wengine ambao watampatia fungu lake la matunda wakati wa mavuno.” Yesu akawaambia, “Je, hamjasoma katika Maandiko kwamba: “ ‘Jiwe walilolikataa waashi limekuwa jiwe kuu la pembeni. Bwana ndiye alitenda jambo hili, nalo ni la ajabu machoni petu’? “Kwa hiyo ninawaambia, Ufalme wa Mungu utaondolewa kwenu na kupewa watu wengine wawezao kuzaa matunda yake. Yeye aangukaye juu ya jiwe hili atavunjika vipande vipande, lakini yule litakayemwangukia atasagwa kabisa.” Viongozi wa Makuhani na Mafarisayo waliposikia mifano ya Yesu, walitambua kuwa alikuwa akiwasema wao. Wakatafuta njia ya kumkamata, lakini wakaogopa umati wa watu, kwa kuwa watu walimwona Yesu kuwa ni nabii.

Shirikisha
Soma Mathayo 21

Mathayo 21:33-46 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Sikilizeni mfano mwingine. Kulikuwa na mtu mwenye shamba, naye alipanda shamba la mizabibu, akalizungushia ua, akachimba shimo la shinikizo ndani yake, akajenga mnara, akapangisha wakulima, akasafiri. Wakati wa kuvuna matunda ulipokuwa karibu, akawatuma watumwa wake kwa wale wakulima, wapokee matunda yake. Wale wakulima wakawakamata watumwa wake, huyu wakampiga, na huyu wakamwua, na huyu wakampiga kwa mawe. Akawatuma tena watumwa wengine wengi kuliko wa kwanza wakawatenda vile vile. Mwishowe akamtuma mwanawe kwao, akisema, Watamstahi mwanangu. Lakini wale wakulima walipomwona yule mwana, wakasemezana wao kwa wao, Huyu ni mrithi; haya na tumwue, tuutwae urithi wake. Wakamkamata, wakamtupa nje ya shamba la mizabibu, wakamwua. Basi atakapokuja yule bwana wa shamba la mizabibu, atawatendaje wale wakulima? Wakamwambia, Atawaangamiza vibaya wale wabaya; na shamba la mizabibu atawapangisha wakulima wengine, watakaomlipa matunda kwa wakati wake. Yesu akawaambia, Hamkupata kusoma katika maandiko, Jiwe walilolikataa waashi, Hilo limekuwa jiwe kuu la pembeni; Neno hili limetoka kwa Bwana, Nalo ni la ajabu machoni petu? Kwa sababu hiyo nawaambia, Ufalme wa Mungu utaondolewa kwenu, nao watapewa taifa lingine lenye kuzaa matunda yake. Naye aangukaye juu ya jiwe hilo atavunjika vipande vipande; naye yeyote ambaye litamwangukia, litamsaga tikitiki. Wakuu wa makuhani na Mafarisayo, waliposikia mifano yake, walitambua ya kuwa anawanenea wao. Nao walipotafuta kumkamata, waliwaogopa makutano, kwa maana wao walimwona kuwa nabii.

Shirikisha
Soma Mathayo 21

Mathayo 21:33-46 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Sikilizeni mfano mwingine. Kulikuwa na mtu mwenye nyumba, naye alipanda shamba la mizabibu, akalizungusha ugo, akachimba shimo la shinikizo ndani yake, akajenga mnara, akapangisha wakulima, akasafiri. Wakati wa matunda ulipokuwa karibu, akawatuma watumwa wake kwa wale wakulima, wapokee matunda yake. Wale wakulima wakawakamata watumwa wake, huyu wakampiga, na huyu wakamwua, na huyu wakampiga kwa mawe. Akawatuma tena watumwa wengine wengi kuliko wa kwanza wakawatenda vile vile. Mwishowe akamtuma mwanawe kwao, akisema, Watamstahi mwanangu. Lakini wale wakulima walipomwona yule mwana, wakasemezana wao kwa wao, Huyu ni mrithi; haya na tumwue, tuutwae urithi wake. Wakamkamata, wakamtupa nje ya shamba la mizabibu, wakamwua. Basi atakapokuja yule bwana wa shamba la mizabibu, atawatendaje wale wakulima? Wakamwambia, Atawaangamiza vibaya wale wabaya; na shamba la mizabibu atawapangisha wakulima wengine, watakaomlipa matunda kwa wakati wake. Yesu akawaambia, Hamkupata kusoma katika maandiko, Jiwe walilolikataa waashi, Hilo limekuwa jiwe kuu la pembeni; Neno hili limetoka kwa Bwana, Nalo ni ajabu machoni petu? Kwa sababu hiyo nawaambia, Ufalme wa Mungu utaondolewa kwenu, nao watapewa taifa lingine lenye kuzaa matunda yake. Naye aangukaye juu ya jiwe hilo atavunjika-vunjika; naye ye yote ambaye litamwangukia, litamsaga tikitiki. Wakuu wa makuhani na Mafarisayo, waliposikia mifano yake, walitambua ya kuwa anawanenea wao. Nao walipotafuta kumkamata, waliwaogopa makutano, kwa maana wao walimwona kuwa nabii.

Shirikisha
Soma Mathayo 21

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha