Mathayo 19:13-26
Mathayo 19:13-26 Biblia Habari Njema (BHN)
Kisha watu wakamletea Yesu watoto wadogo ili awawekee mikono na kuwaombea. Lakini wanafunzi wakawakemea. Yesu akasema, “Waacheni hao watoto waje kwangu, wala msiwazuie; maana ufalme wa mbinguni ni wa watu walio kama watoto hawa.” Basi, akawawekea mikono, kisha akaondoka mahali hapo. Mtu mmoja alimjia Yesu, akamwuliza, “Mwalimu, nifanye kitu gani chema ili niupate uhai wa milele?” Yesu akamwambia, “Mbona unaniuliza kuhusu jambo jema? Kuna mmoja tu aliye mwema. Ukitaka kuingia katika uhai, shika amri.” Yule mtu akamwuliza, “Amri zipi?” Yesu akasema, “Usiue, Usizini, Usiibe, Usitoe ushahidi wa uongo, Waheshimu baba yako na mama yako; na, Mpende jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe.” Huyo kijana akamwambia, “Hayo yote nimeyazingatia; nifanye nini zaidi?” Yesu akamwambia, “Kama unapenda kuwa mkamilifu, nenda ukauze mali yako, uwape maskini fedha hiyo, nawe utakuwa na hazina mbinguni, kisha njoo unifuate.” Huyo kijana aliposikia hayo, akaenda zake akiwa mwenye huzuni, maana alikuwa na mali nyingi. Hapo Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Kweli nawaambieni itakuwa vigumu sana kwa tajiri kuingia katika ufalme wa mbinguni. Tena nawaambieni, ni rahisi zaidi kwa ngamia kupita katika tundu la sindano, kuliko kwa tajiri kuingia katika ufalme wa Mungu.” Wale wanafunzi waliposikia hivyo walishangaa sana, wakamwuliza, “Ni nani basi, awezaye kuokoka?” Yesu akawatazama, akasema, “Kwa binadamu jambo hili haliwezekani, lakini kwa Mungu mambo yote huwezekana.”
Mathayo 19:13-26 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ndipo akaletewa watoto wadogo ili aweke mikono yake juu yao na kuwaombea; wanafunzi wake wakawakemea. Lakini Yesu akasema, Waacheni watoto wadogo waje kwangu; wala msiwazuie; kwa maana walio mfano wa hao, ufalme wa mbinguni ni wao. Akaweka mikono yake juu yao, akatoka huko. Na tazama, mtu mmoja akamwendea akamwambia, Mwalimu, nitende jambo gani jema, ili nipate uzima wa milele? Akamwambia, Kwa nini uniulize kuhusu wema? Aliye mwema ni mmoja. Lakini ukitaka kuingia katika uzima, zishike amri. Akamwambia, Zipi? Yesu akasema, Ni hizi, Usiue, Usizini, Usiibe, Usishuhudie uongo, Waheshimu baba yako na mama yako, na, Mpende jirani yako kama nafsi yako. Yule kijana akamwambia, Haya yote nimeyashika; nimepungukiwa na nini tena? Yesu akamwambia, Ukitaka kuwa mkamilifu, nenda ukauze ulivyo navyo, uwape maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni; kisha njoo unifuate. Yule kijana alipolisikia neno lile, akaenda zake kwa huzuni; kwa sababu alikuwa na mali nyingi. Yesu akawaambia wanafunzi wake, Amin, nawaambieni, ya kwamba itakuwa shida tajiri kuingia katika ufalme wa mbinguni. Nawaambia tena, Ni rahisi zaidi ngamia kupenya tundu ya sindano, kuliko tajiri kuingia katika ufalme wa Mungu. Wanafunzi waliposikia, walishangaa mno, wakisema, Ni nani basi awezaye kuokoka? Yesu akawakazia macho, akawaambia, Kwa wanadamu hilo haliwezekani; bali kwa Mungu yote yawezekana.
Mathayo 19:13-26 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ndipo akaletewa watoto wadogo ili aweke mikono yake juu yao na kuwaombea; wanafunzi wake wakawakemea. Lakini Yesu akasema, Waacheni watoto wadogo waje kwangu; wala msiwazuie; kwa maana walio mfano wa hao, ufalme wa mbinguni ni wao. Akaweka mikono yake juu yao, akatoka huko. Na tazama, mtu mmoja akamwendea akamwambia, Mwalimu, nitende jambo gani jema, ili nipate uzima wa milele? Akamwambia Kwani kuniuliza habari ya wema? Aliye mwema ni mmoja. Lakini ukitaka kuingia katika uzima, zishike amri. Akamwambia, Zipi? Yesu akasema, Ni hizi, Usiue, Usizini, Usiibe, Usishuhudie uongo, Waheshimu baba yako na mama yako, na, Mpende jirani yako kama nafsi yako. Yule kijana akamwambia, Haya yote nimeyashika; nimepungukiwa na nini tena? Yesu akamwambia, Ukitaka kuwa mkamilifu, enenda ukauze ulivyo navyo, uwape maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni; kisha njoo unifuate. Yule kijana alipolisikia neno lile, akaenda zake kwa huzuni; kwa sababu alikuwa na mali nyingi. Yesu akawaambia wanafunzi wake, Amin, nawaambieni, ya kwamba itakuwa shida tajiri kuingia katika ufalme wa mbinguni. Nawaambia tena, Ni rahisi zaidi ngamia kupenya tundu ya sindano, kuliko tajiri kuingia katika ufalme wa Mungu. Wanafunzi waliposikia, walishangaa mno, wakisema, Ni nani basi awezaye kuokoka? Yesu akawakazia macho, akawaambia, Kwa wanadamu hilo haliwezekani; bali kwa Mungu yote yawezekana.
Mathayo 19:13-26 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Kisha watoto wadogo wakaletwa kwa Yesu ili aweke mikono yake juu yao na awaombee. Lakini wanafunzi wake wakawakemea wale waliowaleta. Yesu akasema, “Waacheni watoto wadogo waje kwangu, wala msiwazuie, kwa maana Ufalme wa Mbinguni ni wa wale walio kama hawa.” Naye akaweka mikono yake juu yao, na akaondoka huko. Mtu mmoja akamjia Yesu na kumuuliza, “Mwalimu mwema, nifanye jambo gani jema ili nipate uzima wa milele?” Yesu akamjibu, “Mbona unaniuliza habari ya mema? Aliye mwema ni Mmoja tu. Lakini ukitaka kuingia uzimani, zitii amri.” Yule mtu akamuuliza, “Amri zipi?” Yesu akamjibu, “Usiue, usizini, usiibe, usishuhudie uongo, waheshimu baba yako na mama yako, na umpende jirani yako kama nafsi yako.” Yule kijana akasema, “Hizi zote nimezishika. Je, bado nimepungukiwa na nini?” Yesu akamwambia, “Kama ukitaka kuwa mkamilifu, nenda, ukauze vitu vyote ulivyo navyo, na hizo fedha uwape maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni. Kisha njoo, unifuate.” Yule kijana aliposikia hayo, akaenda zake kwa huzuni, kwa sababu alikuwa na mali nyingi. Ndipo Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Amin, nawaambia, itakuwa vigumu kwa mtu tajiri kuingia katika Ufalme wa Mbinguni. Tena nawaambia, ni rahisi zaidi kwa ngamia kupita kwenye tundu la sindano kuliko mtu tajiri kuingia katika Ufalme wa Mungu.” Wanafunzi wake waliposikia haya, walishangaa sana na kuuliza, “Ni nani basi awezaye kuokoka?” Lakini Yesu akawatazama, akawaambia, “Kwa mwanadamu jambo hili haliwezekani, lakini mambo yote yanawezekana kwa Mungu.”