Mathayo 16:1-4
Mathayo 16:1-4 Biblia Habari Njema (BHN)
Mafarisayo na Masadukayo walimwendea Yesu, na kwa kumjaribu, wakamwomba awaoneshe ishara kutoka mbinguni. Lakini Yesu akawajibu, [“Ikifika jioni nyinyi husema: ‘Hali ya hewa itakuwa nzuri kwa maana anga ni jekundu!’ Na alfajiri mwasema: ‘Leo hali ya hewa itakuwa ya dhoruba, maana anga ni jekundu na tena mawingu yametanda!’ Basi, nyinyi mnajua sana kusoma majira kwa kuangalia hali ya anga, lakini kutambua dalili za nyakati hizi hamjui.] Kizazi kiovu kisicho na uaminifu! Kinataka ishara, lakini hakitapewa ishara yoyote isipokuwa ishara ile ya Yona.” Basi, akawaacha, akaenda zake.
Mathayo 16:1-4 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Wakamjia Mafarisayo na Masadukayo, wakamjaribu, wakamwomba awaoneshe ishara itokayo mbinguni. Akajibu, akawaambia, [Jioni ikifika, mnasema, hali ya anga itakuwa mzuri; kwa kuwa mbingu ni nyekundu. Na asubuhi, mnasema, Leo kutakuwa na dhoruba; kwa maana mbingu ni nyekundu, tena kumetanda. Enyi wanafiki, mnajua kuutambua uso wa mbingu; lakini, je! Ishara za nyakati hizi hamwezi kuzitambua?] Kizazi kibaya na cha zinaa chataka ishara; wala hakitapewa ishara, isipokuwa ishara ya Yona. Akawaacha, akaenda zake.
Mathayo 16:1-4 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Wakamjia Mafarisayo na Masadukayo, wakamjaribu, wakamwomba awaonyeshe ishara itokayo mbinguni. Akajibu, akawaambia, [Kukiwa jioni, mwasema, Kutakuwa na kianga; kwa maana mbingu ni nyekundu. Na asubuhi, mwasema, Leo kutakuwa na dhoruba; kwa maana mbingu ni nyekundu, tena kumetanda. Enyi wanafiki, mwajua kuutambua uso wa mbingu; lakini, je! Ishara za zamani hizi hamwezi kuzitambua?] Kizazi kibaya na cha zinaa chataka ishara; wala hakitapewa ishara, isipokuwa ishara ya Yona. Akawaacha, akaenda zake.
Mathayo 16:1-4 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Mafarisayo na Masadukayo wakamjia Yesu na kumjaribu kwa kumwomba awaonyeshe ishara kutoka mbinguni. Yesu akawajibu, “Ifikapo jioni, mnasema, ‘Hali ya hewa itakuwa nzuri, kwa kuwa anga ni nyekundu.’ Nanyi wakati wa asubuhi mnasema, ‘Leo kutakuwa na dhoruba, kwa sababu anga ni nyekundu na mawingu yametanda.’ Mnajua jinsi ya kupambanua kule kuonekana kwa anga, lakini hamwezi kupambanua dalili za nyakati. Kizazi kiovu na cha uzinzi kinatafuta ishara, lakini hakitapewa ishara yoyote isipokuwa ishara ya Yona.” Yesu akawaacha, akaenda zake.