Mathayo 14:6-13
Mathayo 14:6-13 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Hata ilipofika sikukuu ya kuzaliwa kwake Herode, binti Herodia alicheza mbele ya watu, akampendeza Herode. Hata akaahidi kwa kiapo ya kwamba atampa lo lote atakaloliomba. Naye, huku akichochewa na mamaye, akasema, Nipe hapa katika kombe kichwa cha Yohana Mbatizaji. Naye mfalme akasikitika; lakini kwa ajili ya viapo vyake, na kwa ajili ya wale walioketi chakulani pamoja naye, akaamuru apewe; akatuma mtu, akamkata kichwa Yohana mle gerezani. Kichwa chake kikaletwa katika kombe, akapewa yule kijana; akakichukua kwa mamaye. Wanafunzi wake wakaenda, wakamchukua yule maiti, wakamzika; kisha wakaenda wakampasha Yesu habari. Naye Yesu aliposikia; hayo, aliondoka huko katika chombo, akaenda mahali pasipo watu, faraghani. Na makutano waliposikia, walimfuata kwa miguu kutoka mijini mwao.
Mathayo 14:6-13 Biblia Habari Njema (BHN)
Katika sherehe za sikukuu ya kuzaliwa kwake Herode, binti ya Herodia alicheza mbele ya wageni. Herode alifurahiwa, hata akaahidi kwa kiapo kumpa huyo msichana chochote atakachoomba. Naye, huku akichochewa na mama yake, akaomba, “Nipe papa hapa katika sinia kichwa cha Yohane Mbatizaji.” Mfalme alihuzunika, lakini kwa sababu ya kile kiapo chake na kwa sababu ya wale wageni karamuni, akaamuru apewe. Basi, Herode akatuma mtu gerezani amkate kichwa Yohane. Kichwa chake kikaletwa katika sinia, wakampa yule msichana, naye akampelekea mama yake. Wanafunzi wa Yohane wakaja, wakauchukua mwili wake, wakauzika. Kisha wakaenda kumpasha habari Yesu. Yesu alipopata habari hiyo, aliondoka mahali pale kwa mashua, akaenda mahali pa faragha peke yake. Lakini watu walipata habari, wakamfuata kwa miguu toka mijini.
Mathayo 14:6-13 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Hata ilipofika sikukuu ya kuzaliwa kwake Herode, binti ya Herodia alicheza mbele ya watu, akampendeza Herode. Hata akaahidi kwa kiapo ya kwamba atampa lolote atakaloliomba. Naye, huku akichochewa na mamaye, akasema, Nipe hapa katika kombe kichwa cha Yohana Mbatizaji. Naye mfalme akasikitika; lakini kwa ajili ya viapo vyake, na kwa ajili ya wale walioketi karamuni pamoja naye, akaamuru apewe; akatuma mtu, akamkata kichwa Yohana mle gerezani. Kichwa chake kikaletwa katika kombe, akapewa yule msichana; akakileta kwa mamaye. Wanafunzi wake wakaenda, wakamchukua yule maiti, wakamzika; kisha wakaenda wakampasha Yesu habari. Naye Yesu aliposikia hayo, aliondoka huko katika mashua, akaenda mahali pasipo watu, faraghani. Na makutano waliposikia, walimfuata kwa miguu kutoka mijini mwao.
Mathayo 14:6-13 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Katika siku ya kuadhimisha sikukuu ya kuzaliwa kwa Herode, binti wa Herodia alicheza mbele ya watu waliohudhuria, akamfurahisha sana Herode, kiasi kwamba aliahidi kwa kiapo kumpa huyo binti chochote angeomba. Huyo binti, akiwa amechochewa na mama yake, akasema, “Nipe kichwa cha Yohana Mbatizaji kwenye sinia.” Mfalme akasikitika, lakini kwa sababu ya viapo alivyoapa mbele ya wageni, akaamuru kwamba apatiwe ombi lake. Hivyo akaagiza Yohana Mbatizaji akatwe kichwa mle gerezani. Kichwa chake kikaletwa kwenye sinia, akapewa yule binti, naye akampelekea mama yake. Wanafunzi wa Yohana wakaja na kuuchukua mwili wake kwenda kuuzika. Kisha wakaenda wakamwambia Yesu. Yesu aliposikia yaliyokuwa yametukia, aliondoka kwa chombo akaenda mahali pasipo na watu ili awe peke yake. Lakini watu walipopata habari, wakamfuata kwa miguu kupitia nchi kavu kutoka miji.