Luka 8:16-18
Luka 8:16-18 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Hakuna mtu ambaye akiisha washa taa huifunika kwa chombo, au kuiweka mvunguni, bali huiweka juu ya kiango, ili waingiao wapate kuona nuru yake. Kwa maana hakuna neno lililositirika ambalo halitafunuliwa; wala lililofichwa ambalo halitajulikana na kutokea wazi. Jiangalieni basi jinsi msikiavyo; kwa kuwa mwenye kitu atapewa, na yule asiye na kitu atanyang’anywa hata kile ambacho anadhaniwa kuwa nacho.
Luka 8:16-18 Biblia Habari Njema (BHN)
“Watu hawawashi taa na kuifunika kwa debe au kuiweka mvunguni. Lakini huiweka juu ya kinara ili watu wanapoingia ndani wapate kuona mwanga. “Chochote kilichofichwa kitafichuliwa, na siri yoyote itagunduliwa na kujulikana hadharani. “Kwa hiyo, jihadharini jinsi mnavyosikia; maana aliye na kitu ataongezewa, lakini yule asiye na kitu, hata kile anachodhani anacho, kitachukuliwa.”
Luka 8:16-18 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Hakuna mtu ambaye akiisha washa taa huifunika kwa mtungi, au kuiweka mvunguni, bali huiweka juu ya kiango, ili waingiao wapate kuona nuru yake. Kwa maana hakuna neno lililositirika ambalo halitafunuliwa; wala lililofichwa ambalo halitajulikana na kuwekwa wazi. Jiangalieni basi jinsi msikiavyo; kwa kuwa mwenye kitu atapewa, na yule asiye na kitu atanyang'anywa hata kile ambacho anadhaniwa kuwa nacho.
Luka 8:16-18 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
“Hakuna mtu awashaye taa na kuificha ndani ya gudulia au kuiweka mvunguni mwa kitanda. Badala yake, huiweka juu ya kinara, ili wale waingiao ndani waone mwanga. Kwa maana hakuna jambo lolote lililofichika ambalo halitafichuliwa, wala lolote lililositirika ambalo halitajulikana na kuwekwa wazi. Kwa hiyo, kuweni waangalifu mnavyosikia. Kwa maana yeyote aliye na kitu atapewa zaidi. Lakini yule asiye na kitu, hata kile anachodhani anacho atanyangʼanywa.”