Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Luka 7:36-50

Luka 7:36-50 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Mtu mmoja katika Mafarisayo alimwalika ale chakula kwake; akaingia katika nyumba yake yule Farisayo, akaketi chakulani. Na tazama, mwanamke mmoja wa mji ule, aliyekuwa mwenye dhambi, alipopata habari ya kuwa ameketi chakulani katika nyumba ya yule Farisayo, alileta chupa ya marimari yenye marhamu. Akasimama nyuma karibu na miguu yake, akilia, akaanza kumdondoshea miguu machozi yake, na kuipangusa kwa nywele za kichwa chake, akiibusubusu miguu yake na kuipaka yale marhamu. Basi, yule Farisayo aliyemwalika alipoona vile, alisema moyoni mwake, Mtu huyu kama angekuwa nabii, angemtambua mwanamke huyu amgusaye, ni nani, naye ni wa namna gani, ya kwamba ni mwenye dhambi. Yesu akajibu akamwambia, Simoni, nina neno nitakalo kukuambia. Akasema, Mwalimu, nena. Akasema, Mtu mmoja mkopeshaji alikuwa na wadeni wawili; mmoja amwia dinari mia tano, na wa pili hamsini. Nao walipokuwa hawana cha kumlipa, aliwasamehe wote wawili. Katika hao wawili ni yupi atakayempenda zaidi? Simoni akajibu akasema, Nadhani ni yule ambaye alimsamehe nyingi. Akamwambia, Umeamua haki. Akamgeukia yule mwanamke, akamwambia Simoni, Wamwona mwanamke huyu? Niliingia nyumbani kwako, hukunipa maji kwa miguu yangu; bali huyu amenidondoshea machozi miguu yangu, na kuipangusa kwa nywele za kichwa chake. Wewe hukunibusu; lakini huyu tangu nilipoingia hakuacha kunibusu sana miguu yangu. Hukunipaka kichwa changu mafuta; bali huyu amenipaka miguu yangu marhamu. Kwa ajili ya hayo nakuambia, Amesamehewa dhambi zake ambazo ni nyingi, kwa kuwa amependa sana; lakini asamehewaye kidogo, huyo hupenda kidogo. Kisha alimwambia mwanamke, Umesamehewa dhambi zako. Ndipo wale walioketi chakulani pamoja naye walianza kusema mioyoni mwao, Ni nani huyu hata asamehe dhambi? Akamwambia yule mwanamke, Imani yako imekuokoa, nenda zako kwa amani.

Shirikisha
Soma Luka 7

Luka 7:36-50 Biblia Habari Njema (BHN)

Mfarisayo mmoja alimwalika Yesu kula chakula nyumbani kwake. Akaingia nyumbani kwa huyo Mfarisayo, akakaa kula chakula. Basi, katika mji ule kulikuwa na mama mmoja mwenye dhambi. Alipopata habari kwamba Yesu yuko nyumbani kwa huyo Mfarisayo, alichukua chupa ya alabasta yenye marashi. Akaja, akasimama karibu na miguu yake Yesu, akilia, na machozi yake yakamdondokea Yesu miguuni. Huyo mwanamke akaipangusa miguu ya Yesu kwa nywele zake. Kisha akaibusu na kuipaka yale marashi. Yule Mfarisayo aliyemwalika Yesu alipoona hayo, akawaza moyoni mwake, “Kama mtu huyu angekuwa kweli nabii angejua huyu mwanamke ni wa namna gani, ya kwamba ni mwenye dhambi.” Yesu akamwambia huyo Mfarisayo, “Simoni, ninacho kitu cha kukuambia.” Naye Simoni akamwambia, “Ndio Mwalimu, sema.” Yesu akasema, “Watu wawili walikuwa wamemkopa mtu fedha: Mmoja alikuwa amekopa denari 500, na mwingine hamsini. Waliposhindwa kulipa madeni yao, huyo mtu aliwasamehe wote wawili. Sasa ni yupi kati ya hao wawili atampenda zaidi huyo bwana?” Simoni akamjibu, “Ni dhahiri kwamba yule aliyesamehewa deni kubwa zaidi atampenda zaidi yule bwana.” Yesu akamwambia, “Sawa.” Halafu akamgeukia yule mwanamke na kumwambia Simoni, “Unamwona huyu mwanamke, sivyo? Basi, mimi nilipoingia hapa nyumbani kwako hukunipa maji ya kunawa miguu yangu; lakini mwanamke huyu ameniosha miguu yangu kwa machozi yake na kunipangusa kwa nywele zake. Wewe hukunisalimu kwa kunibusu, lakini huyu mwanamke tangu nilipoingia hapa amekuwa akiibusu miguu yangu. Wewe hukunionesha ukarimu wako kwa kunipaka mafuta kichwani, lakini huyu mwanamke amefanya hivyo kwa kunipaka mafuta miguu yangu. Kwa hiyo nakuambia amesamehewa dhambi zake nyingi kwa kuwa ameonesha upendo mkubwa. Mwenye kusamehewa kidogo, hupenda kidogo.” Basi, Yesu akamwambia yule mwanamke, “Umesamehewa dhambi zako.” Ndipo wale waliokuwa pamoja naye mezani wakaulizana, “Ni mtu wa namna gani huyu awezaye kusamehe dhambi?” Naye Yesu akamwambia yule mwanamke, “Imani yako imekuokoa; nenda kwa amani.”

Shirikisha
Soma Luka 7

Luka 7:36-50 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Mtu mmoja katika Mafarisayo alimwalika ale chakula kwake; akaingia katika nyumba yake yule Farisayo, akaketi chakulani. Na tazama, mwanamke mmoja wa mji ule, aliyekuwa mwenye dhambi, alipopata habari ya kuwa ameketi chakulani katika nyumba ya yule Farisayo, alileta chupa ya marimari yenye marhamu. Akasimama nyuma karibu na miguu yake, akilia, akaanza kumdondoshea miguu machozi yake, na kuipangusa kwa nywele za kichwa chake, akiibusu-busu miguu yake na kuipaka yale marhamu. Basi, yule Farisayo aliyemwalika alipoona vile, alisema moyoni mwake, Mtu huyu kama angekuwa nabii, angemtambua mwanamke huyu amgusaye, ni nani, naye ni wa namna gani, ya kwamba ni mwenye dhambi. Yesu akajibu akamwambia, Simoni, nina neno nitakalo kukuambia. Akasema, Mwalimu, nena. Akasema, Mtu mmoja mkopeshaji alikuwa na wadeni wawili; mmoja amwia dinari mia tano, na wa pili hamsini. Nao walipokuwa hawana cha kumlipa, aliwasamehe wote wawili. Katika hao wawili ni yupi atakayempenda zaidi? Simoni akajibu akasema, Nadhani ni yule ambaye alimsamehe nyingi. Akamwambia, Umeamua haki. Akamgeukia yule mwanamke, akamwambia Simoni, Wamwona mwanamke huyu? Niliingia nyumbani kwako, hukunipa maji kwa miguu yangu; bali huyu amenidondoshea machozi miguu yangu, na kuipangusa kwa nywele za kichwa chake. Wewe hukunibusu; lakini huyu tangu nilipoingia hakuacha kunibusu sana miguu yangu. Hukunipaka kichwa changu mafuta; bali huyu amenipaka miguu yangu marhamu. Kwa ajili ya hayo nakuambia, Amesamehewa dhambi zake ambazo ni nyingi, kwa kuwa amependa sana; lakini asamehewaye kidogo, huyo hupenda kidogo. Kisha alimwambia mwanamke, Umesamehewa dhambi zako. Ndipo wale walioketi chakulani pamoja naye walianza kusema mioyoni mwao, Ni nani huyu hata asamehe dhambi? Akamwambia yule mwanamke, Imani yako imekuokoa, enenda zako kwa amani.

Shirikisha
Soma Luka 7

Luka 7:36-50 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Basi Farisayo mmoja alimwalika Yesu nyumbani kwake kwa chakula. Hivyo Yesu akaenda nyumbani mwa yule Farisayo na kukaa katika nafasi yake mezani. Naye mwanamke mmoja kwenye ule mji, ambaye alikuwa mwenye dhambi, alipojua kwamba Yesu alikuwa akila chakula nyumbani kwa yule Farisayo, akaleta chupa ya marhamu yenye manukato. Yule mwanamke akasimama nyuma ya miguu ya Yesu akilia. Akailowanisha miguu yake kwa machozi yake, kisha akaifuta kwa nywele zake, akaibusu na kuimiminia manukato. Yule Farisayo aliyemwalika Yesu alipoona yanayotendeka, akawaza moyoni mwake, “Kama huyu mtu angekuwa nabii, angejua kwamba ni nani anayemgusa, na kwamba yeye ni mwanamke wa namna gani, na ya kuwa huyu mwanamke ni mwenye dhambi.” Yesu akanena akamwambia, “Simoni, nina jambo la kukuambia.” Simoni akajibu, “Mwalimu, sema.” “Palikuwa na mtu mmoja aliyewakopesha watu wawili fedha: Mmoja alidaiwa dinari 500 na mwingine dinari hamsini. Wote wawili walipokuwa hawawezi kulipa, aliyafuta madeni yao wote wawili. Sasa ni yupi kati yao atakayempenda yule aliyewasamehe zaidi?” Simoni akajibu, “Nadhani ni yule aliyesamehewa deni kubwa zaidi.” Naye Yesu akamwambia, “Umehukumu kwa usahihi.” Kisha akamgeukia yule mwanamke, akamwambia Simoni, “Je, unamwona mwanamke huyu? Nilipoingia nyumbani mwako, hukunipa maji ya kunawa miguu yangu, lakini huyu ameninawisha miguu kwa machozi yake, na kunifuta kwa nywele zake. Hukunisalimu kwa busu, lakini huyu mwanamke hajaacha kuibusu miguu yangu tangu nilipoingia. Hukunipaka mafuta kichwani mwangu, lakini yeye ameipaka miguu yangu manukato. Kwa hiyo, nakuambia, dhambi zake zilizokuwa nyingi zimesamehewa, kwani ameonyesha upendo mwingi. Lakini yule aliyesamehewa kidogo, hupenda kidogo.” Kisha akamwambia yule mwanamke, “Dhambi zako zimesamehewa.” Lakini wale waliokuwa wameketi pamoja naye chakulani wakaanza kusemezana wao kwa wao, “Huyu ni nani ambaye hata anasamehe dhambi?” Yesu akamwambia yule mwanamke, “Imani yako imekuokoa; nenda kwa amani.”

Shirikisha
Soma Luka 7