Luka 7:18-23
Luka 7:18-23 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Wanafunzi wa Yohana wakamletea habari za hayo yote. Ndipo Yohana alipowaita wawili katika wanafunzi wake, akawatuma kwa Yesu akiuliza, Wewe ndiwe yule ajaye, au tumtazamie mwingine? Nao walipofika kwake, walisema, Yohana Mbatizaji ametutuma kwako, akisema, Wewe ndiwe yule ajaye, au tumtazamie mwingine? Na saa ile ile aliwaponya wengi magonjwa yao, na misiba, na pepo wabaya; na vipofu wengi aliwakirimia kuona. Ndipo alipojibu, akawaambia, Nendeni mkamweleze Yohana hayo mliyoyaona na kuyasikia; vipofu wanapata kuona, viwete wanatembea, wenye ukoma wanatakasika, viziwi wanasikia, wafu wanafufuliwa, maskini wanahubiriwa habari njema. Naye heri mtu ye yote asiyechukizwa nami.
Luka 7:18-23 Biblia Habari Njema (BHN)
Wanafunzi wa Yohane walimhabarisha Yohane juu ya mambo hayo yote. Naye Yohane, baada ya kuwaita wawili kati ya wanafunzi wake, aliwatuma kwa Bwana wamwulize: “Wewe ndiye yule anayekuja, au tumngoje mwingine?” Wale wanafunzi walipomfikia Yesu wakamwambia, “Yohane Mbatizaji ametutuma kwako tukuulize: ‘Wewe ndiye yule anayekuja, au tumngoje mwingine?’” Wakati huohuo, Yesu alikuwa anawaponya watu wengi waliokuwa wanateseka kwa magonjwa na waliopagawa na pepo wabaya na kuwawezesha vipofu wengi kuona. Basi, Yesu akawajibu, “Nendeni mkamwambie Yohane yale mliyojionea na kuyasikia: Vipofu wanaona, viwete wanatembea, wenye ukoma wanatakaswa, viziwi wanasikia, wafu wanafufuliwa, na maskini wanahubiriwa Habari Njema. Heri mtu yule ambaye hana mashaka nami!”
Luka 7:18-23 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Wanafunzi wa Yohana wakamletea habari za hayo yote. Ndipo Yohana alipowaita wawili katika wanafunzi wake, akawatuma kwa Yesu akiuliza, Wewe ndiwe yule ajaye, au tumtazamie mwingine? Nao walipofika kwake, walisema, Yohana Mbatizaji ametutuma kwako, akisema, Wewe ndiwe yule ajaye, au tumtazamie mwingine? Na saa ile ile aliwaponya wengi magonjwa yao, na misiba, na pepo wabaya; na vipofu wengi aliwakirimia kuona. Ndipo alipojibu, akawaambia, Nendeni mkamweleze Yohana hayo mliyoyaona na kuyasikia; vipofu wanapata kuona, viwete wanatembea, wenye ukoma wanatakasika, viziwi wanasikia, wafu wanafufuliwa, maskini wanahubiriwa Habari Njema. Naye heri mtu yeyote asiyechukizwa nami.
Luka 7:18-23 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Wanafunzi wa Yohana Mbatizaji wakamweleza Yohana mambo haya yote. Hivyo Yohana akawaita wanafunzi wake wawili na kuwatuma kwa Bwana ili kumuuliza, “Wewe ndiye yule aliyekuwa aje, au tumngojee mwingine?” Wale watu walipofika kwa Yesu wakamwambia, “Yohana Mbatizaji ametutuma tukuulize, ‘Wewe ndiye yule aliyekuwa aje, au tumngojee mwingine?’ ” Wakati huo huo, Yesu aliwaponya wengi waliokuwa na magonjwa, maradhi na pepo wachafu, na pia akawafungua vipofu wengi macho wakapata kuona. Hivyo akawajibu wale wajumbe, “Rudini mkamwambie Yohana yote mnayoyaona na kuyasikia: Vipofu wanapata kuona, viwete wanatembea, wenye ukoma wanatakaswa, viziwi wanasikia, wafu wanafufuliwa na maskini wanahubiriwa habari njema. Amebarikiwa mtu yule asiyechukizwa na mimi.”