Luka 6:20-29
Luka 6:20-29 Biblia Habari Njema (BHN)
Yesu akawageukia wanafunzi wake, akasema: “Heri nyinyi mlio maskini, maana ufalme wa Mungu ni wenu. Heri nyinyi mnaosikia njaa sasa, maana baadaye mtashiba. Heri nyinyi mnaolia sasa, maana baadaye mtacheka kwa furaha. “Heri yenu nyinyi iwapo watu watawachukia, watawatenga, watawatukana na kuwaharibieni jina kwa ajili ya Mwana wa Mtu. Wakati hayo yatakapotokea, furahini na kucheza, maana hakika tuzo lenu ni kubwa mbinguni. Kwa maana wazee wao waliwatendea manabii vivyo hivyo. Lakini ole wenu nyinyi mlio matajiri, maana mmekwisha pata faraja yenu. Ole wenu nyinyi mnaoshiba sasa, maana baadaye mtasikia njaa. Ole wenu nyinyi mnaocheka kwa furaha sasa, maana baadaye mtaomboleza na kulia. Ole wenu nyinyi iwapo watu wote wanawasifu, maana wazee wao waliwafanyia manabii wa uongo vivyo hivyo. “Lakini nawaambieni nyinyi mnaonisikiliza, wapendeni maadui zenu, watendeeni mema wale wanaowachukieni. Watakieni baraka wale wanaowalaani, na waombeeni wale wanaowatendea vibaya. Mtu akikupiga shavu moja mgeuzie pia la pili. Mtu akikunyanganya koti lako mwachie pia shati lako.
Luka 6:20-29 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Akainua macho yake akawatazama wanafunzi wake, akasema, Heri ninyi mlio maskini, kwa sababu ufalme wa Mungu ni wenu. Heri ninyi mlio na njaa sasa, kwa sababu mtashiba. Heri ninyi mliao sasa, kwa sababu mtacheka. Heri ninyi watu watakapowachukia, na kuwatenga, na kuwashutumu, na kulitupa nje jina lenu kama neno ovu, kwa ajili ya Mwana wa Adamu. Furahieni siku ile na kurukaruka, kwa kuwa, tazama, thawabu yenu ni kubwa mbinguni, maana, baba zao waliwatenda manabii vivyo hivyo. Lakini, ole wenu ninyi mlio na mali, kwa kuwa faraja yenu mmekwisha kuipata. Ole wenu ninyi ambao mmeshiba sasa, kwa kuwa mtaona njaa. Ole wenu ninyi mnaocheka sasa, kwa kuwa mtaomboleza na kulia. Ole wenu ninyi watu wote watakapowasifu, kwa kuwa baba zao waliwatenda manabii wa uongo mambo kama hayo. Lakini nawaambia ninyi mnaosikia, Wapendeni adui zenu, watendeeni mema wale ambao wawachukia ninyi, wabarikieni wale ambao wawalaani ninyi, waombeeni wale ambao wawaonea ninyi. Akupigaye shavu moja, mgeuzie la pili, naye akunyang'anyaye joho yako, usimzuilie na kanzu.
Luka 6:20-29 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Akainua macho yake akawatazama wanafunzi wake, akasema, Heri ninyi mlio maskini, kwa sababu ufalme wa Mungu ni wenu. Heri ninyi mlio na njaa sasa, kwa sababu mtashiba. Heri ninyi mliao sasa, kwa sababu mtacheka. Heri ninyi watu watakapowachukia, na kuwatenga, na kuwashutumu, na kulitupa nje jina lenu kama neno ovu, kwa ajili ya Mwana wa Adamu. Furahiwani siku ile na kuruka-ruka, kwa kuwa, tazama, thawabu yenu ni kubwa mbinguni, maana, baba zao waliwatenda manabii vivyo hivyo. Lakini, ole wenu ninyi mlio na mali, kwa kuwa faraja yenu mmekwisha kuipata. Ole wenu ninyi ambao mmeshiba sasa, kwa kuwa mtaona njaa. Ole wenu ninyi mnaocheka sasa, kwa kuwa mtaomboleza na kulia. Ole wenu ninyi watu wote watakapowasifu, kwa kuwa baba zao waliwatenda manabii wa uongo mambo kama hayo. Lakini nawaambia ninyi mnaosikia, Wapendeni adui zenu, watendeeni mema wale ambao wawachukia ninyi, wabarikieni wale ambao wawalaani ninyi, waombeeni wale ambao wawaonea ninyi. Akupigaye shavu moja, mgeuzie la pili, naye akunyang’anyaye joho yako, usimzuilie na kanzu.
Luka 6:20-29 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Akawatazama wanafunzi wake, akasema: “Mmebarikiwa ninyi mlio maskini, kwa sababu Ufalme wa Mungu ni wenu. Mmebarikiwa ninyi mlio na njaa sasa, kwa sababu mtashibishwa. Mmebarikiwa ninyi mnaolia sasa, kwa sababu mtacheka. Mmebarikiwa ninyi, watu watakapowachukia, watakapowatenga na kuwatukana na kulikataa jina lenu kama neno ovu, kwa ajili ya Mwana wa Adamu. “Furahini na kurukaruka kwa shangwe, kwa sababu thawabu yenu ni kubwa mbinguni, kwa kuwa hivyo ndivyo baba zao walivyowatenda manabii. “Lakini ole wenu ninyi mlio matajiri, kwa sababu mmekwisha kupokea faraja yenu. Ole wenu ninyi mlioshiba sasa, maana mtaona njaa. Ole wenu ninyi mnaocheka sasa, maana mtaomboleza na kulia. Ole wenu watu watakapowasifu, kwani ndivyo baba zao walivyowasifu manabii wa uongo. “Lakini nawaambia ninyi mnaonisikia: Wapendeni adui zenu. Watendeeni mema wanaowachukia. Wabarikini wale wanaowalaani, waombeeni wale wanaowatendea mabaya. Kama mtu akikupiga shavu moja, mgeuzie na la pili pia. Mtu akikunyangʼanya koti lako, usimzuie kuchukua joho pia.