Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Luka 6:12-49

Luka 6:12-49 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Ikawa siku zile aliondoka akaenda mlimani ili kuomba, akakesha usiku kucha katika kumwomba Mungu. Hata kulipokuwa mchana aliwaita wanafunzi wake; akachagua kumi na wawili miongoni mwao, ambao aliwaita Mitume; Simoni, aliyemwita jina la pili Petro, na Andrea nduguye, na Yakobo na Yohana, na Filipo na Bartolomayo, na Mathayo na Tomaso, na Yakobo wa Alfayo, na Simoni aitwaye Zelote, na Yuda wa Yakobo, na Yuda Iskariote, ndiye aliyekuwa msaliti. Akashuka pamoja nao, akasimama mahali tambarare, pamoja na wanafunzi wake wengi, na makutano makubwa ya watu waliotoka Uyahudi wote na Yerusalemu, na pwani ya Tiro na Sidoni; waliokuja kumsikiliza na kuponywa magonjwa yao; na wale waliosumbuliwa na pepo wachafu; waliponywa. Na makutano yote walikuwa wakitaka kumgusa, kwa sababu uweza ulikuwa ukimtoka ukiwaponya wote. Akainua macho yake akawatazama wanafunzi wake, akasema, Heri ninyi mlio maskini, kwa sababu ufalme wa Mungu ni wenu. Heri ninyi mlio na njaa sasa, kwa sababu mtashiba. Heri ninyi mliao sasa, kwa sababu mtacheka. Heri ninyi watu watakapowachukia, na kuwatenga, na kuwashutumu, na kulitupa nje jina lenu kama neno ovu, kwa ajili ya Mwana wa Adamu. Furahiwani siku ile na kuruka-ruka, kwa kuwa, tazama, thawabu yenu ni kubwa mbinguni, maana, baba zao waliwatenda manabii vivyo hivyo. Lakini, ole wenu ninyi mlio na mali, kwa kuwa faraja yenu mmekwisha kuipata. Ole wenu ninyi ambao mmeshiba sasa, kwa kuwa mtaona njaa. Ole wenu ninyi mnaocheka sasa, kwa kuwa mtaomboleza na kulia. Ole wenu ninyi watu wote watakapowasifu, kwa kuwa baba zao waliwatenda manabii wa uongo mambo kama hayo. Lakini nawaambia ninyi mnaosikia, Wapendeni adui zenu, watendeeni mema wale ambao wawachukia ninyi, wabarikieni wale ambao wawalaani ninyi, waombeeni wale ambao wawaonea ninyi. Akupigaye shavu moja, mgeuzie la pili, naye akunyang’anyaye joho yako, usimzuilie na kanzu. Mpe kila akuombaye, na akunyang’anyaye vitu vyako, usitake akurudishie. Na kama mnavyotaka watu wawatendee ninyi, watendeeni vivyo hivyo. Maana mkiwapenda wale wawapendao ninyi, mwaonyesha fadhili gani? Kwa kuwa hata wenye dhambi huwapenda wale wawapendao. Nanyi mkiwatendea mema wale wawatendeao mema, mwaonyesha fadhili gani? Hata wenye dhambi hufanya vivyo hivyo. Na mkiwakopesha watu huku mkitumaini kupata kitu kwao, mwaonyesha fadhili gani? Hata wenye dhambi huwakopesha wenye dhambi, ili warudishiwe vile vile. Bali wapendeni adui zenu, tendeni mema, na kukopesha msitumaini kupata malipo, na thawabu yenu itakuwa nyingi; nanyi mtakuwa wana wa Aliye juu, kwa kuwa yeye ni mwema kwa wasiomshukuru, na waovu. Basi, iweni na huruma, kama Baba yenu alivyo na huruma. Msihukumu, nanyi hamtahukumiwa; msilaumu, nanyi hamtalaumiwa; achilieni, nanyi mtaachiliwa. Wapeni watu vitu, nanyi mtapewa; kipimo cha kujaa na kushindiliwa, na kusukwa-sukwa hata kumwagika, ndicho watu watakachowapa vifuani mwenu. Kwa kuwa kipimo kile kile mpimacho ndicho mtakachopimiwa. Akawaambia mithali, Je! Aliye kipofu aweza kuongoza kipofu? Hawatatumbukia shimoni wote wawili? Mwanafunzi hawi mkuu kuliko mwalimu wake, lakini kila mtu ambaye amehitimu hulingana na mwalimu wake. Basi, mbona wakitazama kibanzi kilicho ndani ya jicho la ndugu yako, na boriti iliyo ndani ya jicho lako mwenyewe huiangalii? Au, utawezaje kumwambia ndugu yako, Ndugu yangu, niache nikitoe kibanzi kilicho ndani ya jicho lako, nawe huiangalii boriti iliyo ndani ya jicho lako mwenyewe? Mnafiki wewe, itoe kwanza ile boriti katika jicho lako mwenyewe, ndipo utakapoona vema kukitoa kile kibanzi kilichomo katika jicho la ndugu yako. Kwa maana hakuna mti mzuri uzaao matunda mabaya, wala mti mbaya uzaao matunda mazuri; kwa kuwa kila mti hutambulikana kwa matunda yake; maana, katika miiba hawachumi tini, wala katika michongoma hawachumi zabibu. Mtu mwema katika hazina njema ya moyo wake hutoa yaliyo mema, na mtu mwovu katika hazina mbovu ya moyo wake hutoa yaliyo maovu; kwa kuwa mtu, kinywa chake hunena yale yaujazayo moyo wake. Na kwa nini mnaniita, Bwana, Bwana, walakini hamyatendi nisemayo? Kila mtu ajaye kwangu, na kuyasikia maneno yangu na kuyatenda, nitawaonyesha mfano wake. Mfano wake ni mtu ajengaye nyumba, na kuchimba chini sana, na kuweka msingi juu ya mwamba; na kulipokuja gharika, mto uliishukia nyumba ile kwa nguvu, usiweze kuitikisa; kwa kuwa imejengwa vizuri. Lakini yule aliyesikia ila hakutenda, mfano wake ni mtu aliyejenga nyumba juu ya ardhi pasipokuwa na msingi, mto ukaishukia kwa nguvu, ikaanguka mara; na maangamizi yake nyumba ile yakawa makubwa.

Shirikisha
Soma Luka 6

Luka 6:12-49 Biblia Habari Njema (BHN)

Siku moja Yesu alikwenda mlimani kusali, akakesha huko usiku kucha akisali. Kesho yake aliwaita wanafunzi wake, na miongoni mwao akawachagua watu kumi na wawili ambao aliwaita mitume: Simoni (ambaye Yesu alimpa jina Petro) na Andrea ndugu yake, Yakobo na Yohane, Filipo na Bartholomayo, Mathayo na Thoma, Yakobo wa Alfayo na Simoni (aliyeitwa Zelote), Yuda wa Yakobo na Yuda Iskarioti ambaye baadaye alikuwa msaliti. Baada ya kushuka mlimani pamoja nao, Yesu alisimama mahali palipokuwa tambarare. Hapo kulikuwa na kundi kubwa la wanafunzi wake na umati wa watu waliotoka pande zote za Yudea na Yerusalemu na pwani ya Tiro na Sidoni. Wote walifika kumsikiliza Yesu na kuponywa magonjwa yao. Aliwaponya pia wote waliokuwa wanasumbuliwa na pepo wachafu. Watu wote walitaka kumgusa, kwa maana nguvu ilikuwa inatoka ndani yake na kuwaponya wote. Yesu akawageukia wanafunzi wake, akasema: “Heri nyinyi mlio maskini, maana ufalme wa Mungu ni wenu. Heri nyinyi mnaosikia njaa sasa, maana baadaye mtashiba. Heri nyinyi mnaolia sasa, maana baadaye mtacheka kwa furaha. “Heri yenu nyinyi iwapo watu watawachukia, watawatenga, watawatukana na kuwaharibieni jina kwa ajili ya Mwana wa Mtu. Wakati hayo yatakapotokea, furahini na kucheza, maana hakika tuzo lenu ni kubwa mbinguni. Kwa maana wazee wao waliwatendea manabii vivyo hivyo. Lakini ole wenu nyinyi mlio matajiri, maana mmekwisha pata faraja yenu. Ole wenu nyinyi mnaoshiba sasa, maana baadaye mtasikia njaa. Ole wenu nyinyi mnaocheka kwa furaha sasa, maana baadaye mtaomboleza na kulia. Ole wenu nyinyi iwapo watu wote wanawasifu, maana wazee wao waliwafanyia manabii wa uongo vivyo hivyo. “Lakini nawaambieni nyinyi mnaonisikiliza, wapendeni maadui zenu, watendeeni mema wale wanaowachukieni. Watakieni baraka wale wanaowalaani, na waombeeni wale wanaowatendea vibaya. Mtu akikupiga shavu moja mgeuzie pia la pili. Mtu akikunyanganya koti lako mwachie pia shati lako. Yeyote anayekuomba mpe, na mtu akikunyanganya mali yako usimtake akurudishie. Jinsi mnavyotaka watu wawatendee nyinyi, watendeeni wao vivyo hivyo. “Na ikiwa mnawapenda tu wale wanaowapenda nyinyi, je, mtapata tuzo gani? Hakuna! Kwa maana hata wenye dhambi huwapenda wale wanaowapenda wao. Tena, kama mkiwatendea mema wale tu wanaowatendeeni mema, mtapata tuzo gani? Hata wenye dhambi hufanya hayo. Na kama mnawakopesha wale tu mnaotumaini watawalipeni, je, mtapata tuzo gani? Hata wenye dhambi huwakopesha wenye dhambi wenzao ili warudishiwe kima kilekile. Ila nyinyi wapendeni maadui zenu na kuwatendea mema; kopesheni bila kutazamia kurudishiwa, na tuzo lenu litakuwa kubwa, nanyi mtakuwa watoto wa Mungu aliye juu. Kwa maana yeye ni mwema kwa wale wasio na shukrani na walio wabaya. Muwe na huruma kama Baba yenu alivyo na huruma. “Msiwahukumu wengine, nanyi hamtahukumiwa; msiwalaumu wengine, nanyi hamtalaumiwa; wasameheni wengine, nanyi mtasamehewa. Wapeni wengine wanavyohitaji, nanyi mtapewa. Naam, mtapokea mikononi mwenu kipimo kilichojaa, kikashindiliwa na kusukwasukwa hata kumwagika. Kwa maana kipimo kilekile mnachotumia kwa wengine ndicho atakachotumia Mungu kwenu.” Akawaambia mfano huu: “Je, kipofu anaweza kumwongoza kipofu mwenzake? La! Wote wataanguka shimoni. Mwanafunzi hampiti mwalimu wake, lakini kila mwanafunzi akisha hitimu huwa kama mwalimu wake. Kwa nini wakiona kibanzi jichoni mwa ndugu yako, na papo hapo huioni boriti iliyoko jichoni mwako? Au, wawezaje kumwambia ndugu yako, ‘Ndugu, ngoja nikuondoe kibanzi jichoni mwako,’ na huku huioni boriti iliyomo katika jicho lako mwenyewe? Mnafiki wewe! Toa kwanza boriti iliyomko jichoni mwako, na hapo ndipo utaona sawasawa kiasi cha kuweza kuondoa kibanzi kilicho jichoni mwa ndugu yako. “Mti mzuri hauzai matunda mabaya, wala mti mbaya hauzai matunda mazuri. Watu huutambua mti kutokana na matunda yake. Ni wazi kwamba watu hawachumi tini katika michongoma, wala hawachumi zabibu katika mbigili. Mtu mwema hutoa yaliyo mema kutoka katika hazina bora iliyomo moyoni mwake; na mtu mbaya hutoa yaliyo mabaya kutoka katika hazina mbaya iliyo moyoni mwake, kwa maana mtu huongea kutokana na yale yaliyojaa moyoni mwake. “Mbona mwaniita ‘Bwana, Bwana,’ na huku hamtimizi yale ninayosema? Nitawapeni mfano unaofaa kuonesha alivyo yeyote yule anayekuja kwangu, akasikia maneno yangu na kuyatimiza: Huyo anafanana na mtu ajengaye nyumba, ambaye amechimba chini na kuweka msingi wake juu ya mwamba; kukatokea mafuriko ya mto, mkondo wa maji ukaipiga nyumba ile, lakini haukuweza kuitikisa, kwa sababu ilikuwa imejengwa imara. Lakini yeyote anayesikia maneno yangu asifanye chochote, huyo anafanana na mtu aliyejenga nyumba juu ya udongo, bila msingi. Mafuriko ya mto yakatokea, mkondo wa maji ukaipiga nyumba ile, ikaanguka na kuharibika kabisa!”

Shirikisha
Soma Luka 6

Luka 6:12-49 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Ikawa siku zile aliondoka akaenda mlimani ili kuomba, akakesha usiku kucha akimwomba Mungu. Na kulipokucha aliwaita wanafunzi wake; akachagua kumi na wawili miongoni mwao, ambao aliwaita mitume; Simoni, aliyemwita jina la pili Petro, na Andrea nduguye, na Yakobo na Yohana, na Filipo na Bartholomayo, na Mathayo na Tomaso, na Yakobo wa Alfayo, na Simoni aitwaye Zelote, na Yuda wa Yakobo, na Yuda Iskarioti, ndiye aliyekuwa msaliti. Akashuka pamoja nao, akasimama mahali tambarare, pamoja na wanafunzi wake wengi, na makutano makubwa ya watu waliotoka Yudea wote na Yerusalemu, na pwani ya Tiro na Sidoni; waliokuja kumsikiliza na kuponywa magonjwa yao; na wale waliosumbuliwa na pepo wachafu; waliponywa. Na makutano yote walikuwa wakitaka kumgusa, kwa sababu uweza ulikuwa ukimtoka ukiwaponya wote. Akainua macho yake akawatazama wanafunzi wake, akasema, Heri ninyi mlio maskini, kwa sababu ufalme wa Mungu ni wenu. Heri ninyi mlio na njaa sasa, kwa sababu mtashiba. Heri ninyi mliao sasa, kwa sababu mtacheka. Heri ninyi watu watakapowachukia, na kuwatenga, na kuwashutumu, na kulitupa nje jina lenu kama neno ovu, kwa ajili ya Mwana wa Adamu. Furahieni siku ile na kurukaruka, kwa kuwa, tazama, thawabu yenu ni kubwa mbinguni, maana, baba zao waliwatenda manabii vivyo hivyo. Lakini, ole wenu ninyi mlio na mali, kwa kuwa faraja yenu mmekwisha kuipata. Ole wenu ninyi ambao mmeshiba sasa, kwa kuwa mtaona njaa. Ole wenu ninyi mnaocheka sasa, kwa kuwa mtaomboleza na kulia. Ole wenu ninyi watu wote watakapowasifu, kwa kuwa baba zao waliwatenda manabii wa uongo mambo kama hayo. Lakini nawaambia ninyi mnaosikia, Wapendeni adui zenu, watendeeni mema wale ambao wawachukia ninyi, wabarikieni wale ambao wawalaani ninyi, waombeeni wale ambao wawaonea ninyi. Akupigaye shavu moja, mgeuzie la pili, naye akunyang'anyaye joho yako, usimzuilie na kanzu. Mpe kila akuombaye, na akunyang'anyaye vitu vyako, usitake akurudishie. Na kama mnavyotaka watu wawatendee ninyi, watendeeni vivyo hivyo. Maana mkiwapenda wale wawapendao ninyi, mwaonesha fadhili gani? Kwa kuwa hata wenye dhambi huwapenda wale wawapendao. Nanyi mkiwatendea mema wale wawatendeao mema, mwaonesha fadhili gani? Hata wenye dhambi hufanya vivyo hivyo. Na mkiwakopesha watu huku mkitumaini kupata kitu kwao, mwaonesha fadhili gani? Hata wenye dhambi huwakopesha wenye dhambi, ili warudishiwe vile vile. Bali wapendeni adui zenu, tendeni mema, na kukopesha msitumaini kupata malipo, na thawabu yenu itakuwa nyingi; nanyi mtakuwa wana wa Aliye Juu, kwa kuwa yeye ni mwema kwa wasiomshukuru, na waovu. Basi, iweni na huruma, kama Baba yenu alivyo na huruma. Msihukumu, nanyi hamtahukumiwa; msilaumu, nanyi hamtalaumiwa; sameheni, nanyi mtasamehewa. Wapeni watu vitu, nanyi mtapewa; kipimo cha kujaa na kushindiliwa, na kusukwasukwa hata kumwagika, ndicho watu watakachowapa vifuani mwenu. Kwa kuwa kipimo kile kile mpimacho ndicho mtakachopimiwa. Akawaambia mithali, Je! Aliye kipofu aweza kuongoza kipofu? Hawatatumbukia shimoni wote wawili? Mwanafunzi hawi mkuu kuliko mwalimu wake, lakini kila mtu ambaye amehitimu hulingana na mwalimu wake. Basi, mbona wakitazama kibanzi kilicho ndani ya jicho la ndugu yako, na boriti iliyo ndani ya jicho lako mwenyewe huiangalii? Au, utawezaje kumwambia ndugu yako, Ndugu yangu, niache nikitoe kibanzi kilicho ndani ya jicho lako, nawe huiangalii boriti iliyo ndani ya jicho lako mwenyewe? Mnafiki wewe, itoe kwanza ile boriti katika jicho lako mwenyewe, ndipo utakapoona vema kukitoa kile kibanzi kilichomo katika jicho la ndugu yako. Kwa maana hakuna mti mzuri uzaao matunda mabaya, wala mti mbaya uzaao matunda mazuri; kwa kuwa kila mti hutambulikana kwa matunda yake; maana, katika miiba hawachumi tini, wala katika michongoma hawachumi zabibu. Mtu mwema katika hazina njema ya moyo wake hutoa yaliyo mema, na mtu mwovu katika hazina mbovu ya moyo wake hutoa yaliyo maovu; kwa kuwa mtu, kinywa chake hunena yale yaujazayo moyo wake. Na kwa nini mnaniita, Bwana, Bwana, lakini hamyatendi nisemayo? Kila mtu ajaye kwangu, na kuyasikia maneno yangu na kuyatenda, nitawaonesha mfano wake. Mfano wake ni mtu ajengaye nyumba, na kuchimba chini sana, na kuweka msingi juu ya mwamba; na kulipokuja gharika, mto uliipiga nyumba ile kwa nguvu, usiweze kuitikisa; kwa kuwa imejengwa vizuri. Lakini yule aliyesikia ila hakutenda, mfano wake ni mtu aliyejenga nyumba juu ya ardhi pasipokuwa na msingi, mto ukaipiga kwa nguvu, ikaanguka mara; na maangamizi yake nyumba ile yakawa makubwa.

Shirikisha
Soma Luka 6

Luka 6:12-49 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Ikawa katika siku hizo Yesu alikwenda mlimani kuomba, akakesha usiku kucha akimwomba Mungu. Kulipopambazuka, akawaita wanafunzi wake, naye akachagua kumi na wawili, ambao pia aliwaita mitume: Simoni aliyemwita Petro, Andrea nduguye, Yakobo, Yohana, Filipo, Bartholomayo, Mathayo, Tomaso, Yakobo mwana wa Alfayo, Simoni aliyeitwa Zelote, Yuda mwana wa Yakobo, na Yuda Iskariote ambaye alikuwa msaliti. Akashuka pamoja nao, akasimama mahali penye uwanja tambarare. Hapo palikuwa na idadi kubwa ya wanafunzi wake na umati mkubwa wa watu kutoka sehemu zote za Uyahudi, kutoka Yerusalemu, na kutoka pwani ya Tiro na Sidoni. Walikuwa wamekuja kumsikiliza na kuponywa magonjwa yao. Wale waliokuwa wakiteswa na pepo wachafu akawaponya. Watu wote walikuwa wanajitahidi kumgusa kwa sababu nguvu zilikuwa zikimtoka na kuwaponya wote. Akawatazama wanafunzi wake, akasema: “Mmebarikiwa ninyi mlio maskini, kwa sababu Ufalme wa Mungu ni wenu. Mmebarikiwa ninyi mlio na njaa sasa, kwa sababu mtashibishwa. Mmebarikiwa ninyi mnaolia sasa, kwa sababu mtacheka. Mmebarikiwa ninyi, watu watakapowachukia, watakapowatenga na kuwatukana na kulikataa jina lenu kama neno ovu, kwa ajili ya Mwana wa Adamu. “Furahini na kurukaruka kwa shangwe, kwa sababu thawabu yenu ni kubwa mbinguni, kwa kuwa hivyo ndivyo baba zao walivyowatenda manabii. “Lakini ole wenu ninyi mlio matajiri, kwa sababu mmekwisha kupokea faraja yenu. Ole wenu ninyi mlioshiba sasa, maana mtaona njaa. Ole wenu ninyi mnaocheka sasa, maana mtaomboleza na kulia. Ole wenu watu watakapowasifu, kwani ndivyo baba zao walivyowasifu manabii wa uongo. “Lakini nawaambia ninyi mnaonisikia: Wapendeni adui zenu. Watendeeni mema wanaowachukia. Wabarikini wale wanaowalaani, waombeeni wale wanaowatendea mabaya. Kama mtu akikupiga shavu moja, mgeuzie na la pili pia. Mtu akikunyangʼanya koti lako, usimzuie kuchukua joho pia. Mpe kila akuombaye, na kama mtu akichukua mali yako usitake akurudishie. Watendeeni wengine kama ambavyo mngetaka wawatendee ninyi. “Kama mkiwapenda tu wale wanaowapenda, mwapata sifa gani? Hata ‘wenye dhambi’ huwapenda wale wawapendao. Tena mkiwatendea mema wale tu wanaowatendea ninyi mema, mwapata sifa gani? Hata ‘wenye dhambi’ hufanya vivyo hivyo. Tena mnapowakopesha wale tu mnaotegemea wawalipe, mwapata sifa gani? Hata ‘wenye dhambi’ huwakopesha ‘wenye dhambi’ wenzao wakitarajia kulipwa mali yao yote. Lakini wapendeni adui zenu, watendeeni mema, wakopesheni bila kutegemea kurudishiwa mlichokopesha. Ndipo thawabu yenu itakapokuwa kubwa, nanyi mtakuwa wana wa Aliye Juu Sana, kwa sababu yeye ni mwema kwa watu wasio na shukrani na kwa wale waovu. Kuweni na huruma, kama Baba yenu alivyo na huruma. “Msihukumu, nanyi hamtahukumiwa. Msilaumu, nanyi hamtalaumiwa. Sameheni, nanyi mtasamehewa. Wapeni watu vitu, nanyi mtapewa. Kipimo cha kujaa na kushindiliwa na kusukwasukwa hata kumwagika, ndicho watu watakachowapa vifuani mwenu. Kwa kuwa kipimo kile mpimacho, ndicho mtakachopimiwa.” Pia akawapa mfano akasema, “Je, kipofu aweza kumwongoza kipofu? Je, wote wawili hawatatumbukia shimoni? Mwanafunzi hawezi kumzidi mwalimu wake, ila yule aliyehitimu aweza kuwa kama mwalimu wake. “Mbona unatazama kibanzi kilicho ndani ya jicho la ndugu yako, wala huoni boriti iliyo ndani ya jicho lako mwenyewe? Utawezaje kumwambia ndugu yako, ‘Ndugu yangu, acha nitoe kibanzi kilicho ndani ya jicho lako,’ wakati wewe mwenyewe huoni boriti iliyo ndani ya jicho lako? Ewe mnafiki, ondoa boriti ndani ya jicho lako kwanza, ndipo utaweza kuona dhahiri jinsi ya kuondoa kibanzi kilicho ndani ya jicho la ndugu yako. “Hakuna mti mzuri uzaao matunda mabaya, wala hakuna mti mbaya uzaao matunda mazuri. Kila mti hujulikana kwa matunda yake. Kwa maana watu hawachumi tini kwenye miiba, wala zabibu kwenye michongoma. Vivyo hivyo mtu mwema hutoa mambo mema kutoka kwenye hazina ya moyo wake, naye mtu mwovu hutoa mambo maovu kutoka kwenye hazina ya moyo wake. Kwa kuwa mtu hunena kwa kinywa chake yale yaliyoujaza moyo wake. “Kwa nini mnaniita, ‘Bwana, Bwana,’ nanyi hamfanyi ninayowaambia? Nitawaonyesha jinsi alivyo mtu yule anayekuja kwangu na kusikia maneno yangu na kuyatenda. Yeye ni kama mtu aliyejenga nyumba, akachimba chini sana, na kuweka msingi kwenye mwamba. Mafuriko yalipokuja, maji ya ghafula yaliipiga ile nyumba, lakini haikutikisika, kwa sababu ilikuwa imejengwa vizuri. Lakini yeye anayesikia maneno yangu wala asiyatende, ni kama mtu aliyejenga nyumba juu ya ardhi bila kuweka msingi. Mafuriko yalipoikumba nyumba ile, ikaanguka mara na kubomoka kabisa.”

Shirikisha
Soma Luka 6