Luka 5:4-11
Luka 5:4-11 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Na alipokwisha kunena, alimwambia Simoni, Tweka mpaka kilindini, mkashushe nyavu zenu mvue samaki. Simoni akajibu akamwambia, Bwana mkubwa, tumefanya kazi ya kuchosha usiku kucha, tusipate kitu; lakini kwa neno lako nitazishusha nyavu. Basi, walipofanya hivyo walipata samaki wengi mno, nyavu zao zikaanza kukatika; wakawapungia mikono washiriki wenzao waliokuwa katika mashua nyingine, waje kuwasaidia; wakaja, wakazijaza mashua zote mbili, hata zikakaribia kuzama. Simoni Petro alipoona hayo, alianguka magotini mbele ya Yesu, akisema, Ondoka kwangu, kwa kuwa mimi ni mtu mwenye dhambi, Bwana. Maana alishikwa na mshangao, yeye na wote waliokuwa pamoja naye, kwa sababu ya wingi wa samaki waliowapata; na kadhalika Yakobo na Yohana, wana wa Zebedayo, waliokuwa washirika wa Simoni. Yesu akamwambia Simoni, Usiogope, tangu sasa utakuwa ukivua watu. Hata walipokwisha kuziegesha mashua zao pwani, wakaacha vyote wakamfuata.
Luka 5:4-11 Biblia Habari Njema (BHN)
Alipomaliza kufundisha, akamwambia Simoni, “Endesha mashua mpaka kilindini, mkatupe nyavu zenu mpate kuvua samaki.” Simoni akamjibu, “Bwana, tumejitahidi kuvua samaki usiku kucha bila kupata kitu, lakini kwa kuwa umesema, nitatupa nyavu.” Baada ya kufanya hivyo, wakavua samaki wengi, hata nyavu zao zikaanza kukatika. Wakawaita wenzao waliokuwa katika mashua nyingine waje kuwasaidia. Wakaja, wakazijaza mashua zote mbili samaki, hata karibu zingezama. Simoni Petro alipoona hayo, akapiga magoti mbele ya Yesu akisema, “Ondoka mbele yangu, ee Bwana, kwa kuwa mimi ni mwenye dhambi!” Simoni pamoja na wenzake wote walishangaa kwa kupata samaki wengi vile. Hali kadhalika Yakobo na Yohane, wana wa Zebedayo, waliokuwa wavuvi wenzake Simoni. Yesu akamwambia Simoni, “Usiogope; tangu sasa utakuwa ukivua watu.” Basi, baada ya kuzileta zile mashua ukingoni mwa ziwa, wakaacha yote, wakamfuata.
Luka 5:4-11 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Hata alipokwisha kunena, alimwambia Simoni, Tweka mpaka kilindini, mkashushe nyavu zenu mvue samaki. Simoni akajibu akamwambia, Bwana mkubwa, tumefanya kazi ya kuchosha usiku kucha, tusipate kitu; lakini kwa neno lako nitazishusha nyavu. Basi, walipofanya hivyo walipata samaki wengi mno, nyavu zao zikaanza kukatika; wakawapungia mikono washirika wao waliokuwa katika chombo cha pili, waje kuwasaidia; wakaja, wakavijaza vyombo vyote viwili, hata vikataka kuzama. Simoni Petro alipoona hayo, alianguka magotini pa Yesu, akisema, Ondoka kwangu, kwa kuwa mimi ni mtu mwenye dhambi, Bwana. Maana alishikwa na ushangao, yeye na wote waliokuwa pamoja naye, kwa sababu ya wingi wa samaki walioupata; na kadhalika Yakobo na Yohana, wana wa Zebedayo, waliokuwa washirika wa Simoni. Yesu akamwambia Simoni, Usiogope, tangu sasa utakuwa ukivua watu. Hata walipokwisha kuviegesha pwani vyombo vyao, wakaacha vyote wakamfuata.
Luka 5:4-11 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Alipomaliza kunena, akamwambia Simoni, “Sasa peleka mashua hadi kilindini kisha mshushe nyavu zenu mkavue samaki.” Simoni akamjibu, “Bwana, tumefanya kazi ya kuchosha usiku kucha na hatukuvua chochote. Lakini, kwa neno lako nitazishusha nyavu.” Nao walipozishusha nyavu zao, wakavua samaki wengi sana, nyavu zao zikajaa zikaanza kukatika. Wakawaashiria wavuvi wenzao kwenye ile mashua nyingine ili waje kuwasaidia. Wakaja, wakajaza mashua zote mbili samaki hata zikaanza kuzama. Simoni Petro alipoona haya yaliyotukia, alianguka miguuni mwa Yesu na kumwambia, “Bwana, ondoka kwangu. Mimi ni mtu mwenye dhambi!” Kwa kuwa yeye na wavuvi wenzake walikuwa wameshangazwa sana na wingi wa samaki waliokuwa wamepata. Vivyo hivyo wenzake Simoni, yaani Yakobo na Yohana, wana wa Zebedayo, walishangazwa pia. Ndipo Yesu akamwambia Simoni, “Usiogope, tangu sasa utakuwa mvuvi wa watu.” Hivyo wakasogeza mashua zao mpaka ufuoni mwa bahari, wakaacha kila kitu na kumfuata.