Luka 5:12-32
Luka 5:12-32 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ikawa, alipokuwa katika mmojawapo wa miji ile, tazama, palikuwa na mtu amejaa ukoma; naye alipomwona Yesu alianguka kifudifudi, akamwomba akisema, Bwana, ukitaka, waweza kunitakasa. Naye akaunyosha mkono wake, akamgusa akisema, Nataka; takasika. Na mara ukoma wake ukamwondoka. Akamkataza asimwambie mtu, ila, Nenda ukajionyeshe kwa kuhani; ukatoe kwa ajili ya kutakasika kwako kama Musa alivyoamuru, iwe ushuhuda kwao. Lakini habari zake zikazidi kuenea, wakakutanika makutano mengi wamsikilize na kuponywa magonjwa yao. Lakini yeye alikuwa akijiepua, akaenda mahali pasipokuwa na watu, akaomba. Ikawa siku zile mojawapo alikuwa akifundisha, na Mafarisayo na waalimu wa torati walikuwa wameketi hapo, waliotoka katika kila kijiji cha Galilaya, na Uyahudi, na Yerusalemu; na uweza wa Bwana ulikuwapo apate kuponya. Na tazama, wakaja watu wanamchukua kitandani mtu mwenye kupooza; wakataka kumpeleka ndani na kumweka mbele yake. Hata walipokosa nafasi ya kumpeleka ndani kwa ajili ya lile kundi la watu, walipanda juu ya dari wakampisha katika matofali ya juu, wakamshusha yeye na kitanda chake katikati mbele ya Yesu. Naye alipoiona imani yao, alimwambia, Ee rafiki, umesamehewa dhambi zako. Basi, wale waandishi na Mafarisayo wakaanza kuhojiana wakisema, Ni nani huyu asemaye maneno ya kukufuru? N’nani awezaye kusamehe dhambi isipokuwa Mungu peke yake? Na Yesu alijua hoja zao, akajibu akawaambia, Mnahojiana nini mioyoni mwenu? Lililo jepesi ni lipi? Kusema, Umesamehewa dhambi zako, au kusema, Ondoka, uende? Lakini, mpate kujua ya kwamba Mwana wa Adamu anayo amri duniani ya kusamehe dhambi, (alimwambia yule mwenye kupooza). Nakuambia, Ondoka, ujitwike kitanda chako, ukaende zako nyumbani kwako. Mara hiyo akasimama mbele yao, akajitwika kile alichokilalia, akaenda zake nyumbani kwake, huku akimtukuza Mungu. Ushangao ukawashika wote, wakamtukuza Mungu; wakajaa hofu, wakisema, Leo tumeona mambo ya ajabu. Baada ya hayo akatoka, akaona mtoza ushuru, jina lake Lawi, ameketi forodhani, akamwambia, Nifuate. Akaacha vyote, akaondoka, akamfuata. Na Lawi akamfanyia karamu kubwa nyumbani mwake; palikuwa na mkutano mkuu wa watoza ushuru na watu wengineo waliokuwa wameketi chakulani pamoja nao. Ikawa Mafarisayo na waandishi wao kuwanung’unikia wanafunzi wake, wakisema, Mbona mnakula na kunywa pamoja na watoza ushuru na wenye dhambi? Yesu akajibu akawaambia, Wenye afya hawana haja na tabibu, isipokuwa walio hawawezi. Sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi, wapate kutubu.
Luka 5:12-32 Biblia Habari Njema (BHN)
Ikawa, Yesu alipokuwa katika mmojawapo wa miji ya huko, mtu mmoja mwenye ukoma mwili mzima akamwona. Basi, mtu huyo akaanguka kifudifudi akamwomba Yesu: “Bwana, ukitaka, waweza kunitakasa.” Yesu akanyosha mkono, akamgusa na kusema, “Nataka! Takasika!” Mara ule ukoma ukamwacha. Naye Yesu akamwamuru: “Usimwambie mtu yeyote; bali nenda ukajioneshe kwa kuhani, ukatoe sadaka kwa ajili ya kutakasika kwako kama alivyoamuru Mose kuwathibitishia kwamba umepona.” Lakini habari za Yesu zilizidi kuenea kila mahali. Watu makundi mengi wakakusanyika ili kumsikiliza na kuponywa magonjwa yao. Lakini yeye alikwenda zake mahali pasipo na watu, akawa anasali huko. Siku moja, Yesu alikuwa akifundisha. Mafarisayo na waalimu wa sheria kutoka katika kila kijiji cha Galilaya, Yudea na Yerusalemu, walikuwa wameketi hapo. Nguvu ya Bwana ilikuwa pamoja naye kwa ajili ya kuponya wagonjwa. Mara watu wakaja, wamemchukua mtu mmoja aliyepooza maungo, amelala kitandani; wakajaribu kumwingiza ndani, wamweke mbele ya Yesu. Lakini, kwa sababu ya wingi wa watu, hawakuweza kuingia ndani. Basi, wakapanda juu ya paa, wakaondoa vigae, wakamshusha huyo aliyepooza pamoja na kitanda chake, wakamweka mbele ya Yesu. Yesu alipoona jinsi walivyokuwa na imani kubwa, akamwambia huyo mtu, “Rafiki, umesamehewa dhambi zako.” Waalimu wa sheria na Mafarisayo wakaanza kujiuliza: “Nani huyu anayesema maneno ya kufuru? Hakuna mtu awezaye kusamehe dhambi ila Mungu peke yake!” Yesu alitambua mawazo yao, akawauliza, “Mnawaza nini mioyoni mwenu? Ni lipi lililo rahisi zaidi: Kusema, ‘Umesamehewa dhambi,’ au kusema, ‘Simama utembee?’ Basi, nataka mjue kwamba Mwana wa Mtu anao uwezo wa kuwasamehe watu dhambi duniani.” Hapo akamwambia huyo mtu aliyepooza, “Simama, chukua kitanda chako, uende zako nyumbani.” Mara, huyo mtu aliyepooza akasimama mbele yao wote, akachukua kitanda chake akaenda nyumbani kwake huku akimtukuza Mungu. Wote wakashangaa na kushikwa na hofu; wakamtukuza Mungu wakisema: “Tumeona maajabu leo.” Baada ya hayo, Yesu akatoka nje, akamwona mtozaushuru mmoja aitwaye Lawi, ameketi ofisini. Yesu akamwambia, “Nifuate!” Naye akaacha yote akamfuata. Lawi akamwandalia Yesu karamu kubwa nyumbani mwake. Na kundi kubwa la watozaushuru na watu wengine walikuwa wameketi pamoja nao. Mafarisayo na waalimu wa sheria wakawanungunikia wanafunzi wake wakisema: “Kwa nini mnakula na kunywa pamoja na watozaushuru na wenye dhambi?” Yesu akawajibu, “Wenye afya hawamhitaji daktari; wanaomhitaji ni wale walio wagonjwa. Sikuja kuwaita watu wema, bali wenye dhambi, wapate kutubu.”
Luka 5:12-32 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ikawa, alipokuwa katika mmojawapo wa miji ile, tazama, palikuwa na mtu amejaa ukoma; naye alipomwona Yesu alianguka kifudifudi, akamwomba akisema, Bwana, ukitaka, waweza kunitakasa. Naye akaunyosha mkono wake, akamgusa akisema, Nataka; takasika. Na mara ukoma wake ukamwondoka. Akamkataza asimwambie mtu, ila, Nenda ukajioneshe kwa kuhani; ukatoe sadaka kwa ajili ya kutakasika kwako kama Musa alivyoamuru, iwe ushuhuda kwao. Lakini habari zake zikazidi kuenea, wakakutanika makutano mengi wamsikilize na kuponywa magonjwa yao. Lakini yeye alikuwa akijiepua, akaenda mahali pasipokuwa na watu, akaomba. Ikawa siku zile mojawapo alikuwa akifundisha, na Mafarisayo na waalimu wa torati walikuwa wameketi hapo, waliotoka katika kila kijiji cha Galilaya, na Yudea, na Yerusalemu; na uweza wa Bwana ulikuwapo apate kuponya. Na tazama, wakaja watu wanamchukua kitandani mtu mwenye kupooza; wakataka kumpeleka ndani na kumweka mbele yake. Hata walipokosa nafasi ya kumpeleka ndani kwa ajili ya lile kundi la watu, walipanda juu ya dari wakampitisha katika matofali ya juu, wakamshusha yeye na kitanda chake katikati mbele ya Yesu. Naye alipoiona imani yao, alimwambia, Ee rafiki, umesamehewa dhambi zako. Basi, wale Waandishi na Mafarisayo wakaanza kuulizana wakisema, Ni nani huyu asemaye maneno ya kukufuru? Ni nani awezaye kusamehe dhambi isipokuwa Mungu peke yake? Na Yesu alijua hoja zao, akajibu akawaambia, Mnajiuliza nini mioyoni mwenu? Lililo jepesi ni lipi? Kusema, Umesamehewa dhambi zako, au kusema, Ondoka, uende? Lakini, mpate kujua ya kwamba Mwana wa Adamu anayo amri duniani ya kusamehe dhambi, (alimwambia yule mwenye kupooza). Nakuambia, Ondoka, ujitwike kitanda chako, ukaende zako nyumbani kwako. Mara hiyo akasimama mbele yao, akajitwika kile alichokilalia, akaenda zake nyumbani kwake, huku akimtukuza Mungu. Mshangao ukawashika wote, wakamtukuza Mungu; wakajaa hofu, wakisema, Leo tumeona mambo ya ajabu. Baada ya hayo akatoka, akaona mtoza ushuru, jina lake Lawi, ameketi forodhani, akamwambia, Nifuate. Akaacha vyote, akaondoka, akamfuata. Na Lawi akamfanyia karamu kubwa nyumbani mwake; palikuwa na mkutano mkuu wa watoza ushuru na watu wengineo waliokuwa wameketi chakulani pamoja nao. Ikawa Mafarisayo na waandishi wao kuwanung'unikia wanafunzi wake, wakisema, Mbona mnakula na kunywa pamoja na watoza ushuru na wenye dhambi? Yesu akajibu akawaambia, Wenye afya hawana haja na tabibu, isipokuwa walio wagonjwa. Sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi, wapate kutubu.
Luka 5:12-32 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Ikawa siku moja Yesu alipokuwa katika mji fulani, mtu mmoja mwenye ukoma mwili mzima akamjia. Alipomwona Yesu, alianguka chini mpaka uso wake ukagusa ardhi, akamsihi akisema, “Bwana, ukitaka, waweza kunitakasa.” Yesu akanyoosha mkono wake, akamgusa yule mtu, akamwambia, “Nataka. Takasika!” Na mara ukoma wake ukatakasika. Yesu akamwagiza akisema, “Usimwambie mtu yeyote, bali nenda ukajionyeshe kwa kuhani na ukatoe sadaka alizoagiza Mose kwa utakaso wako, ili kuwa ushuhuda kwao.” Lakini habari zake Yesu zikazidi sana kuenea kotekote kuliko wakati mwingine wowote. Makutano makubwa ya watu yalikuwa yakikusanyika ili kumsikiliza na kuponywa magonjwa yao. Lakini mara kwa mara Yesu alijitenga nao ili kwenda mahali pa faragha kuomba. Siku moja Yesu alipokuwa akifundisha, Mafarisayo na walimu wa sheria, waliokuwa wametoka kila kijiji cha Galilaya na kutoka Uyahudi na Yerusalemu, walikuwa wameketi huko. Nao uweza wa Bwana ulikuwa juu yake kuponya wagonjwa. Wakaja watu wamembeba mgonjwa aliyepooza kwenye mkeka. Wakajaribu kumwingiza ndani ili wamweke mbele ya Yesu. Walipokuwa hawawezi kufanya hivyo kwa sababu ya umati wa watu, wakapanda juu ya paa, wakaondoa baadhi ya matofali, wakamteremsha yule mgonjwa kwa mkeka wake hadi katikati ya ule umati pale mbele ya Yesu. Yesu alipoiona imani yao, akamwambia yule mgonjwa, “Rafiki, dhambi zako zimesamehewa.” Mafarisayo na wale walimu wa sheria wakaanza kuuliza, “Ni nani mtu huyu anayesema maneno ya kukufuru? Ni nani awezaye kusamehe dhambi isipokuwa Mungu peke yake?” Yesu akijua mawazo yao akawauliza, “Kwa nini mnawaza hivyo mioyoni mwenu? Je, ni lipi lililo rahisi zaidi, kumwambia, ‘Umesamehewa dhambi zako,’ au kusema, ‘Inuka, uende’? Lakini ili mpate kujua kwamba Mwana wa Adamu anayo mamlaka duniani kusamehe dhambi…” Akamwambia yule aliyepooza, “Nakuambia, inuka, chukua mkeka wako, uende nyumbani kwako.” Mara yule mtu aliyekuwa amepooza akasimama mbele yao wote, akachukua mkeka wake, akaenda zake nyumbani, huku akimtukuza Mungu. Kila mmoja akashangaa na kumtukuza Mungu. Wakajawa na hofu ya Mungu, wakasema, “Leo tumeona mambo ya ajabu.” Baada ya haya, Yesu alitoka na kumwona mtoza ushuru mmoja jina lake Lawi akiwa amekaa forodhani, mahali pake pa kutoza ushuru. Akamwambia, “Nifuate.” Naye Lawi akaacha kila kitu, akaondoka, akamfuata. Kisha Lawi akamfanyia Yesu karamu kubwa nyumbani kwake, nao umati mkubwa wa watoza ushuru na watu wengine walikuwa wakila pamoja nao. Lakini Mafarisayo na walimu wa sheria waliokuwa wa dhehebu lao wakawalalamikia wanafunzi wa Yesu, wakisema, “Mbona mnakula na kunywa pamoja na watoza ushuru na ‘wenye dhambi’?” Yesu akawajibu, “Wenye afya hawahitaji tabibu, bali walio wagonjwa. Sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi wapate kutubu.”