Luka 4:14-21
Luka 4:14-21 Biblia Habari Njema (BHN)
Hapo Yesu alirudi Galilaya akiwa amejaa nguvu za Roho Mtakatifu, na habari zake zikaenea katika sehemu zote za jirani. Naye akawa anawafundisha watu katika masunagogi yao, akasifiwa na wote. Basi, Yesu alikwenda Nazareti, mahali alipolelewa, na siku ya Sabato, aliingia katika sunagogi kama ilivyokuwa desturi yake. Akasimama ili asome Maandiko Matakatifu kwa sauti. Akapokea kitabu cha nabii Isaya, akakifungua na akakuta mahali palipoandikwa: “Roho wa Bwana yu juu yangu, kwani ameniweka wakfu niwaletee maskini Habari Njema. Amenituma niwatangazie mateka uhuru wao, na vipofu watapata kuona tena; amenituma niwakomboe wanaoonewa, na kutangaza mwaka wa neema ya Bwana.” Baada ya kusoma, akafunga kile kitabu, akampa mtumishi, kisha akaketi; watu wote wakamkodolea macho. Naye akaanza kuwaambia, “Andiko hili mlilosikia limetimia leo.”
Luka 4:14-21 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Yesu akarudi kwa nguvu za Roho, akaendea Galilaya; habari zake zikaenea katika nchi zote za kandokando. Naye alikuwa akifundisha katika masinagogi yao, akitukuzwa na watu wote. Akaenda Nazareti, hapo alipolelewa; na siku ya sabato akaingia katika sinagogi kama ilivyokuwa desturi yake, akasimama ili asome. Akapewa kitabu cha nabii Isaya, akakifungua kitabu, akapata mahali palipoandikwa, Roho wa Bwana yu juu yangu, Kwa maana amenitia mafuta kuwahubiria maskini Habari Njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, Na vipofu kupata kuona tena, Kuwaacha huru waliosetwa, Na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa. Akakifunga kitabu, akamrudishia mtumishi, akaketi; na watu wote waliokuwamo katika sinagogi wakamkazia macho. Akaanza kuwaambia, Leo maandiko haya yametimia masikioni mwenu.
Luka 4:14-21 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Yesu akarudi kwa nguvu za Roho, akenda Galilaya; habari zake zikaenea katika nchi zote za kandokando. Naye alikuwa akifundisha katika masinagogi yao, akitukuzwa na watu wote. Akaenda Nazareti, hapo alipolelewa; na siku ya sabato akaingia katika sinagogi kama ilivyokuwa desturi yake, akasimama ili asome. Akapewa chuo cha nabii Isaya, akakifungua chuo, akatafuta mahali palipoandikwa, Roho wa Bwana yu juu yangu, Kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, Na vipofu kupata kuona tena, Kuwaacha huru waliosetwa, Na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa. Akakifunga chuo, akamrudishia mtumishi, akaketi; na watu wote waliokuwamo katika sinagogi wakamkazia macho. Akaanza kuwaambia, Leo maandiko haya yametimia masikioni mwenu.
Luka 4:14-21 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Kisha Yesu akarudi mpaka Galilaya, akiwa amejaa nguvu za Roho Mtakatifu, nazo habari zake zikaenea katika sehemu zote za nchi za kandokando. Akaanza kufundisha kwenye masinagogi yao, na kila mmoja akamsifu. Yesu akaenda Nazareti, alipolelewa, na siku ya Sabato alikwenda katika sinagogi kama ilivyokuwa desturi yake. Akasimama ili asome, naye akapewa kitabu cha nabii Isaya, akakifungua na kukuta mahali palipoandikwa: “Roho wa Bwana yu juu yangu, kwa sababu amenitia mafuta kuwahubiria maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, na vipofu kupata kuona tena, kuwaweka huru wanaoonewa, na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubalika.” Kisha akakifunga kitabu, akamrudishia mtumishi na akaketi. Watu wote waliokuwamo katika sinagogi wakamkazia macho. Ndipo akaanza kwa kuwaambia, “Leo Andiko hili limetimia mkiwa mnasikia.”