Luka 4:1-20
Luka 4:1-20 Biblia Habari Njema (BHN)
Yesu alitoka mtoni Yordani akiwa amejaa Roho Mtakatifu, akaongozwa na Roho mpaka jangwani. Huko alijaribiwa na Ibilisi kwa muda wa siku arubaini. Wakati huo wote hakula chochote, na baada ya siku hizo akasikia njaa. Ndipo Ibilisi akamwambia, “Kama wewe ni Mwana wa Mungu, amuru jiwe hili liwe mkate.” Yesu akamjibu, “Imeandikwa: ‘Mtu haishi kwa mkate tu.’” Kisha Ibilisi akamchukua hadi mahali pa juu, akamwonesha kwa mara moja falme zote za ulimwengu. Huyo Shetani akamwambia, “Nitakupa uwezo juu ya falme zote hizi na fahari zake, kwa maana nimepewa hivi vyote; nikitaka kumpa mtu ninaweza. Hivi vyote vitakuwa mali yako wewe, kama ukiniabudu.” Yesu akamjibu, “Imeandikwa: ‘Utamwabudu Bwana Mungu wako, na kumtumikia yeye peke yake.’” Ibilisi akamchukua mpaka Yerusalemu, kwenye mnara wa hekalu, akamwambia, “Kama wewe ni Mwana wa Mungu, jitupe chini kwa maana imeandikwa: ‘Atawaamuru malaika wake wakulinde,’ na tena, ‘Watakuchukua mikononi mwao, usije ukajikwaa mguu kwenye jiwe.’” Lakini Yesu akamjibu, “Imeandikwa: ‘Usimjaribu Bwana Mungu wako.’” Ibilisi alipokwisha mjaribu kwa kila njia, akamwacha kwa muda. Hapo Yesu alirudi Galilaya akiwa amejaa nguvu za Roho Mtakatifu, na habari zake zikaenea katika sehemu zote za jirani. Naye akawa anawafundisha watu katika masunagogi yao, akasifiwa na wote. Basi, Yesu alikwenda Nazareti, mahali alipolelewa, na siku ya Sabato, aliingia katika sunagogi kama ilivyokuwa desturi yake. Akasimama ili asome Maandiko Matakatifu kwa sauti. Akapokea kitabu cha nabii Isaya, akakifungua na akakuta mahali palipoandikwa: “Roho wa Bwana yu juu yangu, kwani ameniweka wakfu niwaletee maskini Habari Njema. Amenituma niwatangazie mateka uhuru wao, na vipofu watapata kuona tena; amenituma niwakomboe wanaoonewa, na kutangaza mwaka wa neema ya Bwana.” Baada ya kusoma, akafunga kile kitabu, akampa mtumishi, kisha akaketi; watu wote wakamkodolea macho.
Luka 4:1-20 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Na Yesu, akiwa amejaa Roho Mtakatifu, alirudi kutoka Yordani, akaongozwa na Roho kwa muda wa siku arubaini nyikani, akijaribiwa na Ibilisi. Na siku hizo alikuwa hali kitu; na zilipotimia, aliona njaa. Ibilisi akamwambia, Ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu, liambie jiwe hili liwe mkate. Yesu akamjibu, Imeandikwa ya kwamba mtu hataishi kwa mkate tu. Akampandisha juu, akamwonesha milki zote za ulimwengu kwa dakika moja. Ibilisi akamwambia, Nitakupa wewe enzi hii yote, na fahari yake, kwa kuwa imo mikononi mwangu, nami humpa yeyote kama nipendavyo. Basi, wewe ukisujudu mbele yangu yote yatakuwa yako. Yesu akajibu akamwambia, Imeandikwa, Msujudie Bwana Mungu wako, umwabudu yeye peke yake. Akamwongoza mpaka Yerusalemu, akamweka juu ya kinara cha hekalu, akamwambia, Ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu, jitupe chini; kwa maana imeandikwa, Atakuagizia malaika zake wakulinde; na ya kwamba, Mikononi mwao watakuchukua, Usije ukajikwaa mguu wako katika jiwe. Yesu akajibu akamwambia, Imenenwa, Usimjaribu Bwana Mungu wako. Basi alipomaliza kila jaribu, Ibilisi akamwacha akaenda zake kwa muda. Yesu akarudi kwa nguvu za Roho, akaendea Galilaya; habari zake zikaenea katika nchi zote za kandokando. Naye alikuwa akifundisha katika masinagogi yao, akitukuzwa na watu wote. Akaenda Nazareti, hapo alipolelewa; na siku ya sabato akaingia katika sinagogi kama ilivyokuwa desturi yake, akasimama ili asome. Akapewa kitabu cha nabii Isaya, akakifungua kitabu, akapata mahali palipoandikwa, Roho wa Bwana yu juu yangu, Kwa maana amenitia mafuta kuwahubiria maskini Habari Njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, Na vipofu kupata kuona tena, Kuwaacha huru waliosetwa, Na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa. Akakifunga kitabu, akamrudishia mtumishi, akaketi; na watu wote waliokuwamo katika sinagogi wakamkazia macho.
Luka 4:1-20 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Na Yesu, hali amejaa Roho Mtakatifu, alirudi kutoka Yordani, akaongozwa na Roho muda wa siku arobaini nyikani, akijaribiwa na Ibilisi. Na siku hizo alikuwa hali kitu; hata zilipotimia, aliona njaa. Ibilisi akamwambia, Ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu, liambie jiwe hili liwe mkate. Yesu akamjibu, Imeandikwa ya kwamba mtu hataishi kwa mkate tu. Akampandisha juu, akamwonyesha milki zote za ulimwengu kwa dakika moja. Ibilisi akamwambia, Nitakupa wewe enzi hii yote, na fahari yake, kwa kuwa imo mikononi mwangu, nami humpa ye yote kama nipendavyo. Basi, wewe ukisujudu mbele yangu yote yatakuwa yako. Yesu akajibu akamwambia, Imeandikwa, Msujudie Bwana Mungu wako, umwabudu yeye peke yake. Akamwongoza mpaka Yerusalemu, akamweka juu ya kinara cha hekalu, akamwambia, Ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu, jitupe chini; kwa maana imeandikwa, Atakuagizia malaika zake wakulinde; na ya kwamba, Mikononi mwao watakuchukua, Usije ukajikwaa mguu wako katika jiwe. Yesu akajibu akamwambia, Imenenwa, Usimjaribu Bwana Mungu wako. Basi alipomaliza kila jaribu, Ibilisi akamwacha akaenda zake kwa muda. Yesu akarudi kwa nguvu za Roho, akenda Galilaya; habari zake zikaenea katika nchi zote za kandokando. Naye alikuwa akifundisha katika masinagogi yao, akitukuzwa na watu wote. Akaenda Nazareti, hapo alipolelewa; na siku ya sabato akaingia katika sinagogi kama ilivyokuwa desturi yake, akasimama ili asome. Akapewa chuo cha nabii Isaya, akakifungua chuo, akatafuta mahali palipoandikwa, Roho wa Bwana yu juu yangu, Kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, Na vipofu kupata kuona tena, Kuwaacha huru waliosetwa, Na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa. Akakifunga chuo, akamrudishia mtumishi, akaketi; na watu wote waliokuwamo katika sinagogi wakamkazia macho.
Luka 4:1-20 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Yesu, akiwa amejaa Roho Mtakatifu, akarudi kutoka Yordani. Akaongozwa na Roho Mtakatifu hadi nyikani, mahali ambako kwa siku arobaini alikuwa akijaribiwa na ibilisi. Kwa siku zote hizo hakula chochote, hivyo baada ya muda huo akaona njaa. Ibilisi akamwambia, “Ikiwa wewe ni Mwana wa Mungu, amuru jiwe hili liwe mkate.” Yesu akajibu akamwambia, “Imeandikwa: ‘Mtu haishi kwa mkate tu.’ ” Ibilisi akampeleka hadi juu ya mlima mrefu akamwonyesha milki zote za dunia kwa mara moja. Akamwambia, “Nitakupa mamlaka juu ya milki hizi na fahari zake zote, kwa maana zimekabidhiwa mkononi mwangu nami ninaweza kumpa yeyote ninayetaka. Hivyo ikiwa utanisujudia na kuniabudu, vyote vitakuwa vyako.” Yesu akamjibu, “Imeandikwa: ‘Mwabudu Bwana Mungu wako na umtumikie yeye peke yake.’ ” Kisha ibilisi akampeleka mpaka Yerusalemu, akamweka juu ya mnara mrefu wa Hekalu, akamwambia, “Kama wewe ndiwe Mwana wa Mungu, jitupe chini kutoka hapa, kwa maana imeandikwa: “ ‘Atakuagizia malaika zake ili wakulinde; nao watakuchukua mikononi mwao, usije ukajikwaa mguu wako katika jiwe.’ ” Yesu akamjibu, “Imesemwa, ‘Usimjaribu Bwana Mungu wako.’ ” Ibilisi alipomaliza kila jaribu, akamwacha Yesu mpaka wakati mwingine ufaao. Kisha Yesu akarudi mpaka Galilaya, akiwa amejaa nguvu za Roho Mtakatifu, nazo habari zake zikaenea katika sehemu zote za nchi za kandokando. Akaanza kufundisha kwenye masinagogi yao, na kila mmoja akamsifu. Yesu akaenda Nazareti, alipolelewa, na siku ya Sabato alikwenda katika sinagogi kama ilivyokuwa desturi yake. Akasimama ili asome, naye akapewa kitabu cha nabii Isaya, akakifungua na kukuta mahali palipoandikwa: “Roho wa Bwana yu juu yangu, kwa sababu amenitia mafuta kuwahubiria maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, na vipofu kupata kuona tena, kuwaweka huru wanaoonewa, na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubalika.” Kisha akakifunga kitabu, akamrudishia mtumishi na akaketi. Watu wote waliokuwamo katika sinagogi wakamkazia macho.