Luka 24:36-48
Luka 24:36-48 Biblia Habari Njema (BHN)
Walipokuwa wakiwaambia hayo, Yesu mwenyewe akasimama kati yao, akawaambia “Amani iwe nanyi.” Wakashtuka na kushikwa na hofu wakidhani wameona mzimu. Lakini yeye akawaambia, “Kwa nini mnafadhaika? Mbona mnakuwa na mashaka mioyoni mwenu? Angalieni mikono na miguu yangu, ya kwamba ni mimi mwenyewe. Nipapaseni mkaone, maana mzimu hauna mwili na mifupa kama mnionavyo.” Baada ya kusema hayo, akawaonesha mikono na miguu. Wakiwa bado katika hali ya kutosadiki kwa sababu ya furaha yao, na wakiwa wanastaajabu, akawauliza, “Mnacho chakula chochote hapa?” Wakampa kipande cha samaki wa kuokwa. Akakichukua, akala, wote wakimwona. Halafu akawaambia, “Hii ndiyo maana ya maneno niliyowaambia nilipokuwa pamoja nanyi: Kwamba ilikuwa lazima kukamilisha yote yaliyoandikwa juu yangu katika sheria ya Mose na katika vitabu vya manabii na katika kitabu cha Zaburi.” Kisha, akaziangazia akili zao ili wapate kuelewa Maandiko Matakatifu. Akawaambia, “Ndivyo ilivyoandikwa, kwamba Kristo atateswa na siku ya tatu atafufuka kutoka kwa wafu, na kwamba ni lazima, kwa jina lake, mataifa yote kuanzia Yerusalemu, yahubiriwe kwamba watu wanapaswa kutubu na kusamehewa dhambi. Nyinyi ni mashahidi wa mambo hayo.
Luka 24:36-48 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Na walipokuwa katika kusema habari hiyo, yeye mwenyewe alisimama katikati yao, akawaambia, Amani iwe kwenu. Wakashituka, wakaogopa sana, wakidhani ya kwamba wanaona roho. Akawaambia, Mbona mnafadhaika? Na kwa nini mnaona shaka mioyoni mwenu? Tazameni mikono yangu na miguu yangu, ya kuwa ni mimi mwenyewe. Nishikenishikeni, mwone; kwa kuwa roho haina mwili na mifupa kama mnavyoniona mimi kuwa nayo. Na baada ya kusema hayo aliwaonesha mikono yake na miguu yake. Basi walipokuwa hawajaamini kwa furaha, huku wakistaajabu, aliwaambia, Mna chakula chochote hapa? Wakampa kipande cha samaki wa kuokwa. Akakitwaa, akala mbele yao. Kisha akawaambia, Hayo ndiyo maneno yangu niliyowaambia nilipokuwa ningali pamoja nanyi, ya kwamba ni lazima yatimizwe yote niliyoandikiwa katika Torati ya Musa, na katika vitabu vya Manabii na Zaburi. Ndipo akawafunua akili zao wapate kuelewa maandiko. Akawaambia, Ndivyo ilivyoandikwa, kwamba Kristo atateswa na kufufuka siku ya tatu; na kwamba mataifa yote watahubiriwa kwa jina lake habari ya toba na ondoleo la dhambi, kuanza tangu Yerusalemu. Nanyi ndinyi mashahidi wa mambo haya.
Luka 24:36-48 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Na walipokuwa katika kusema habari hiyo, yeye mwenyewe alisimama katikati yao, akawaambia, Amani iwe kwenu. Wakashituka, wakaogopa sana, wakidhani ya kwamba wanaona roho. Akawaambia, Mbona mnafadhaika? Na kwa nini mnaona shaka mioyoni mwenu? Tazameni mikono yangu na miguu yangu, ya kuwa ni mimi mwenyewe. Nishikenishikeni, mwone; kwa kuwa roho haina mwili na mifupa kama mnavyoniona mimi kuwa nayo. Na baada ya kusema hayo aliwaonyesha mikono yake na miguu yake. Basi walipokuwa hawajaamini kwa furaha, huku wakistaajabu, aliwaambia, Mna chakula cho chote hapa? Wakampa kipande cha samaki wa kuokwa. Akakitwaa, akala mbele yao. Kisha akawaambia, Hayo ndiyo maneno yangu niliyowaambia nilipokuwa nikali pamoja nanyi, ya kwamba ni lazima yatimizwe yote niliyoandikiwa katika Torati ya Musa, na katika Manabii na Zaburi. Ndipo akawafunulia akili zao wapate kuelewa na maandiko. Akawaambia, Ndivyo ilivyoandikwa, kwamba Kristo atateswa na kufufuka siku ya tatu; na kwamba mataifa yote watahubiriwa kwa jina lake habari ya toba na ondoleo la dhambi, kuanza tangu Yerusalemu. Nanyi ndinyi mashahidi wa mambo haya.
Luka 24:36-48 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Walipokuwa bado wanazungumza hayo, Yesu mwenyewe akasimama katikati yao, akasema, “Amani iwe nanyi!” Wakashtuka na kuogopa wakidhani kwamba wameona mzuka. Lakini Yesu akawauliza, “Kwa nini mnaogopa? Kwa nini mna shaka mioyoni mwenu? Tazameni mikono yangu na miguu yangu, mwone kuwa ni mimi hasa. Niguseni mwone; kwa maana mzuka hauna nyama na mifupa, kama mnionavyo kuwa navyo.” Aliposema haya, akawaonyesha mikono na miguu yake. Wakashindwa kuamini kwa ajili ya furaha na mshangao waliokuwa nao. Akawauliza, “Mna chakula chochote hapa?” Wakampa kipande cha samaki aliyeokwa, naye akakichukua na kukila mbele yao. Akawaambia, “Haya ndiyo yale niliyowaambia nilipokuwa bado niko pamoja nanyi, kwamba yote yaliyoandikwa kunihusu mimi katika Sheria ya Mose, Manabii na Zaburi hayana budi kutimizwa.” Ndipo akafungua fahamu zao ili waweze kuyaelewa Maandiko. Akawaambia, “Haya ndiyo yaliyoandikwa: Kristo atateswa na siku ya tatu atafufuka kutoka kwa wafu. Toba na msamaha wa dhambi zitatangaziwa mataifa yote kupitia jina lake kuanzia Yerusalemu. Ninyi ni mashahidi wa mambo haya.