Luka 24:1-11
Luka 24:1-11 Biblia Habari Njema (BHN)
Jumapili, alfajiri na mapema, wale wanawake walikwenda kaburini wakichukua yale manukato waliyotayarisha. Walikuta lile jiwe limevingirishwa mbali na kaburi. Walipoingia ndani, hawakuuona mwili wa Bwana Yesu. Walipokuwa bado wanashangaa juu ya jambo hilo, mara watu wawili waliovaa mavazi yenye kungaa sana, wakasimama karibu nao. Hao wanawake wakaingiwa na hofu, wakainama chini. Ndipo wale watu wakawaambia, “Kwa nini mnamtafuta aliye hai kati ya wafu? Hayuko hapa; amefufuka. Kumbukeni aliyowaambieni alipokuwa kule Galilaya: ‘Ni lazima Mwana wa Mtu atolewe kwa watu waovu, nao watamsulubisha na siku ya tatu atafufuka.’” Hapo hao wanawake wakayakumbuka maneno yake, wakarudi kutoka kaburini, wakawapa mitume wale kumi na mmoja na wafuasi wengine habari za mambo hayo yote. Hao waliotoa habari hizo kwa mitume ni: Maria Magdalene, Yoana na Maria mama wa Yakobo, pamoja na wanawake wengine walioandamana nao. Mitume waliyachukua maneno hayo kama yasiyo na msingi, hivyo hawakuamini.
Luka 24:1-11 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Siku ya kwanza ya juma, ilipoanza kupambazuka, walikwenda kaburini, wakiyaleta manukato waliyoweka tayari. Wakalikuta lile jiwe limevingirishwa mbali na kaburi, Wakaingia, wasiuone mwili wa Bwana Yesu. Ikawa walipokuwa wakifadhaika kwa ajili ya neno hilo, tazama, watu wawili walisimama karibu nao, wamevaa nguo za kumetameta; nao walipoingiwa na hofu na kuinama kifudifudi hadi nchini, hao waliwaambia, Kwa nini mnamtafuta aliye hai katika wafu? Hayupo hapa, amefufuka. Kumbukeni alivyosema nanyi alipokuwa bado yuko Galilaya, akisema, Imempasa Mwana wa Adamu kutiwa mikononi mwa wenye dhambi, na kusulubiwa, na kufufuka siku ya tatu. Wakayakumbuka maneno yake. Wakaondoka kaburini, wakarudi; wakawaarifu wale kumi na mmoja na wengine wote habari za mambo hayo yote. Nao ni Mariamu Magdalene, na Yoana, na Mariamu mamaye Yakobo, na wale wanawake wengine waliokuwa pamoja nao; hao waliwaambia mitume habari ya mambo hayo.
Luka 24:1-11 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Hata siku ya kwanza ya juma, ilipoanza kupambazuka, walikwenda kaburini, wakiyaleta manukato waliyoweka tayari. Wakalikuta lile jiwe limevingirishwa mbali na kaburi, Wakaingia, wasiuone mwili wa Bwana Yesu. Ikawa walipokuwa wakifadhaika kwa ajili ya neno hilo, tazama, watu wawili walisimama karibu nao, wamevaa nguo za kumeta-meta; nao walipoingiwa na hofu na kuinama kifudifudi hata nchi, hao waliwaambia, Kwa nini mnamtafuta aliye hai katika wafu? Hayupo hapa, amefufuka. Kumbukeni alivyosema nanyi alipokuwa akaliko Galilaya, Lk 9:22; 18:31-33 akisema, Imempasa Mwana wa Adamu kutiwa mikononi mwa wenye dhambi, na kusulibiwa, na kufufuka siku ya tatu. Wakayakumbuka maneno yake. Wakaondoka kaburini, wakarudi; wakawaarifu wale kumi na mmoja na wengine wote habari za mambo hayo yote. Nao ni Mariamu Magdalene, na Yoana, na Mariamu mamaye Yakobo, na wale wanawake wengine waliokuwa pamoja nao; hao waliwaambia mitume habari ya mambo hayo.
Luka 24:1-11 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Mnamo siku ya kwanza ya juma, alfajiri na mapema, wale wanawake walichukua yale manukato waliyokuwa wameyaandaa, wakaenda kaburini. Wakakuta lile jiwe limevingirishwa kutoka kwenye kaburi, lakini walipoingia ndani, hawakuuona mwili wa Bwana Yesu. Walipokuwa wanashangaa juu ya jambo hili, ghafula watu wawili waliokuwa wamevaa mavazi yanayongʼaa kama umeme wakasimama karibu nao. Wale wanawake, wakiwa na hofu, wakainamisha nyuso zao mpaka chini. Lakini wale watu wakawaambia, “Kwa nini mnamtafuta aliye hai miongoni mwa wafu? Hayuko hapa; amefufuka! Kumbukeni alivyowaambia alipokuwa bado yuko pamoja nanyi huko Galilaya kwamba: ‘Ilikuwa lazima Mwana wa Adamu atiwe mikononi mwa watu wenye dhambi na waovu ili asulubiwe, na siku ya tatu afufuke.’ ” Ndipo wakayakumbuka maneno ya Yesu. Waliporudi kutoka huko kaburini, wakawaeleza wale wanafunzi kumi na mmoja pamoja na wengine wote mambo haya yote. Basi Maria Magdalene, Yoana, na Maria mama yake Yakobo, pamoja na wanawake wengine waliofuatana nao ndio waliwaelezea mitume habari hizi. Lakini hawakuwasadiki hao wanawake, kwa sababu maneno yao yalionekana kama upuzi.