Luka 23:44-56
Luka 23:44-56 Biblia Habari Njema (BHN)
Ilikuwa yapata saa sita mchana; jua likaacha kuangaza, giza likaifunika nchi yote mpaka saa tisa, na pazia lililokuwa limetundikwa hekaluni likapasuka vipande viwili. Yesu akalia kwa sauti kubwa: “Baba, mikononi mwako naiweka roho yangu.” Alipokwisha sema hayo, akakata roho. Hapo, yule jemadari alipoona yaliyotukia akamsifu Mungu akisema: “Hakika huyu alikuwa mtu mwema.” Watu wale wote waliokuwa wamekusanyika hapo kwa ajili ya tukio hilo, walipoona hayo yaliyotukia, walirudi makwao wakijipiga vifua kwa huzuni. Marafiki zake wote pamoja na wale wanawake walioandamana naye kutoka Galilaya, walisimama kwa mbali kutazama tukio hilo. Kulikuwa na mtu mmoja jina lake Yosefu, mwenyeji wa kijiji kimoja cha Wayahudi kiitwacho Arimathaya. Alikuwa mtu mwema anayeheshimika. Alikuwa akitazamia kuja kwa ufalme wa Mungu. Ingawa alikuwa mmoja wa Baraza Kuu la Wayahudi, hakuwa amekubaliana nao katika kitendo chao. Basi, yeye alikwenda kwa Pilato, akaomba apewe mwili wa Yesu. Kisha akaushusha mwili huo kutoka msalabani, akauzungushia sanda ya kitani, akauweka katika kaburi lililokuwa limechongwa kwenye mwamba, ambalo halikuwa limetumika. Siku hiyo ilikuwa Ijumaa, na maandalio ya siku ya Sabato yalikuwa yanaanza. Wale wanawake walioandamana na Yesu kutoka Galilaya walimfuata Yosefu, wakaliona lile kaburi na jinsi mwili wake Yesu ulivyowekwa. Halafu, walirudi nyumbani, wakatayarisha manukato na marashi ya kuupaka mwili wa Yesu. Siku ya Sabato walipumzika kama ilivyoamriwa na sheria.
Luka 23:44-56 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Hapo ilikuwa yapata saa sita, kukawa giza juu ya nchi yote hadi saa tisa, jua limepungua nuru yake; pazia la hekalu likapasuka katikati. Yesu akalia kwa sauti kuu, akasema, Ee Baba, mikononi mwako naiweka roho yangu. Alipokwisha kusema hayo alikata roho. Yule jemadari alipoona yaliyotukia, alimtukuza Mungu, akisema, Hakika yake, mtu huyu alikuwa mwenye haki. Na makutano yote ya watu waliokuwa wamekutanika kutazama mambo hayo, walipoona yaliyotendeka, wakaenda zao kwao, wakijipigapiga vifua. Na wote waliojuana naye, na wale wanawake walioandamana naye toka Galilaya, wakasimama kwa mbali, wakitazama mambo hayo. Na tazama, akatoka mtu mmoja, jina lake Yusufu, ambaye ni mtu wa baraza, mtu mwema, mwenye haki; (wala hakulikubali shauri na tendo lao), naye ni mtu wa Arimathaya, mji mmoja wa Wayahudi, tena anautazamia ufalme wa Mungu; mtu huyo alikwenda kwa Pilato, akataka kupewa mwili wa Yesu. Akaushusha, akauzinga sanda ya kitani, akauweka katika kaburi lililochongwa mwambani, ambalo hajalazwa mtu bado ndani yake. Na siku ile ilikuwa siku ya Maandalio, na sabato ikaanza kuingia. Na wale wanawake waliokuja naye toka Galilaya walifuata, wakaliona kaburi, na jinsi mwili wake ulivyowekwa. Wakarudi, wakatayarisha manukato na marhamu. Na siku ya sabato walistarehe kama ilivyoamriwa.
Luka 23:44-56 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Hapo ilikuwa yapata saa sita, kukawa giza juu ya nchi yote hata saa kenda, jua limepungua nuru yake; pazia la hekalu likapasuka katikati. Yesu akalia kwa sauti kuu, akasema, Ee Baba, mikononi mwako naiweka roho yangu. Alipokwisha kusema hayo alikata roho. Yule akida alipoona yaliyotukia, alimtukuza Mungu, akisema, Hakika yake, mtu huyu alikuwa mwenye haki. Na makutano yote ya watu waliokuwa wamekutanika kutazama mambo hayo, walipoona yaliyotendeka, wakaenda zao kwao, wakijipiga-piga vifua. Na wote waliojuana naye, na wale wanawake walioandamana naye toka Galilaya, wakasimama kwa mbali, wakitazama mambo hayo. Na tazama, akatoka mtu mmoja, jina lake Yusufu, ambaye ni mtu wa baraza, mtu mwema, mwenye haki; (wala hakulikubali shauri na tendo lao), naye ni mtu wa Arimathaya, mji mmoja wa Wayahudi, tena anautazamia ufalme wa Mungu; mtu huyo alikwenda kwa Pilato, akataka kupewa mwili wa Yesu. Akaushusha, akauzinga sanda ya kitani, akauweka katika kaburi lililochongwa mwambani, ambalo hajalazwa mtu bado ndani yake. Na siku ile ilikuwa siku ya Maandalio, na sabato ikaanza kuingia. Na wale wanawake waliokuja naye toka Galilaya walifuata, wakaliona kaburi, na jinsi mwili wake ulivyowekwa. Wakarudi, wakafanya tayari manukato na marhamu. Na siku ya sabato walistarehe kama ilivyoamriwa.
Luka 23:44-56 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Ilikuwa kama saa sita mchana, nalo giza likafunika nchi yote hadi saa tisa, kwa sababu jua liliacha kutoa nuru. Pazia la Hekalu likachanika vipande viwili. Yesu akapaza sauti yake akasema, “Baba, mikononi mwako naikabidhi roho yangu.” Baada ya kusema haya, akakata roho. Yule jemadari alipoona yaliyotukia, akamsifu Mungu, akasema, “Hakika, mtu huyu alikuwa mwenye haki.” Watu wote waliokuwa wamekusanyika hapo kushuhudia tukio hili walipoyaona hayo, wakapigapiga vifua vyao kwa huzuni na kwenda zao. Lakini wale wote waliomfahamu, pamoja na wale wanawake waliokuwa wamemfuata kutoka Galilaya, walisimama kwa mbali wakiyatazama mambo haya. Basi kulikuwa na mtu mmoja mwema na mwenye haki, jina lake Yosefu. Yeye alikuwa mjumbe wa Baraza la Wayahudi, lakini yeye hakuwa amekubaliana na maamuzi na vitendo vya viongozi wenzake. Huyu alikuwa mwenyeji wa Arimathaya huko Uyahudi, naye alikuwa anaungojea Ufalme wa Mungu kwa matarajio makubwa. Yosefu alikwenda kwa Pilato, akaomba apewe mwili wa Yesu. Akaushusha kutoka msalabani, akaufunga katika kitambaa cha kitani safi, na kuuweka katika kaburi lililochongwa kwenye mwamba, ambalo halikuwa limezikiwa mtu mwingine bado. Ilikuwa Siku ya Maandalizi, nayo Sabato ilikuwa karibu kuanza. Wale wanawake waliokuwa wamekuja pamoja na Yesu wakimfuata kutoka Galilaya wakamfuata Yosefu, wakaliona kaburi na jinsi mwili wa Yesu ulivyolazwa. Kisha wakarudi nyumbani, wakaandaa manukato na marhamu ya kuupaka huo mwili. Lakini wakapumzika siku ya Sabato kama ilivyoamriwa.