Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Luka 21:1-19

Luka 21:1-19 Biblia Habari Njema (BHN)

Yesu alitazama kwa makini, akawaona matajiri walivyokuwa wanatia sadaka zao katika hazina ya hekalu, akamwona pia mama mmoja mjane akitumbukiza humo sarafu mbili ndogo. Basi, akasema, “Nawaambieni kweli, mama huyu mjane maskini ametia katika hazina kiasi kikubwa kuliko walichotia wote. Kwa maana, wengine wote wametoa sadaka zao kutokana na ziada ya mali zao, lakini huyu mama, ingawa ni maskini, ametoa kila kitu alichohitaji kwa kuishi.” Baadhi ya wanafunzi walikuwa wanazungumza juu ya hekalu, jinsi lilivyopambwa kwa mawe ya thamani, pamoja na sadaka zilizotolewa kwa Mungu. Yesu akasema, “Haya yote mnayoyaona – zitakuja siku ambapo hakuna hata jiwe moja litakalosalia juu ya lingine; kila kitu kitaharibiwa.” Basi, wakamwuliza, “Mwalimu, mambo hayo yatatokea lini? Na ni ishara gani zitakazoonesha kwamba karibu mambo hayo yatokee?” Yesu akawajibu, “Jihadharini, msije mkadanganyika. Maana wengi watatokea na kulitumia jina langu, kila mmoja akidai kwamba yeye ni mimi, na kwamba wakati ule umekaribia. Lakini nyinyi msiwafuate! Basi, mtakaposikia habari za vita na misukosuko, msitishike; maana ni lazima hayo yatokee kwanza, lakini mwisho wa yote, bado.” Halafu akaendelea kusema: “Taifa moja litapigana na taifa lingine, na ufalme mmoja utapigana na ufalme mwingine. Kila mahali kutakuwa na mitetemeko mikubwa ya ardhi, njaa na tauni. Kutakuwa na vituko vya kutisha na ishara kubwa angani. Lakini kabla ya kutokea hayo yote, watawatieni nguvuni, watawatesa na kuwapelekeni katika masunagogi na kuwatia gerezani; mtapelekwa mbele ya wafalme na watawala kwa ajili ya jina langu, mpate kunishuhudia kwao. Muwe na msimamo huu mioyoni mwenu: Hakuna kufikiria kabla ya wakati juu ya jinsi mtakavyojitetea, kwa sababu mimi mwenyewe nitawapeni ufasaha wa maneno na hekima, hata maadui zenu hawataweza kustahimili wala kupinga. Wazazi wenu, ndugu, jamaa na rafiki zenu watawasaliti nyinyi; na baadhi yenu mtauawa. Watu wote watawachukieni nyinyi kwa sababu ya jina langu. Lakini, hata unywele mmoja wa vichwa vyenu hautapotea. Kwa uvumilivu wenu, mtayaokoa maisha yenu.

Shirikisha
Soma Luka 21

Luka 21:1-19 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Akainua macho yake akawaona matajiri wakitia sadaka zao katika sanduku la hazina. Akamwona mjane mmoja maskini akitia mle senti mbili. Akasema, Hakika nawaambia, huyu mjane maskini ametia zaidi kuliko wote; maana, hao wote walitoa sadaka katika mali iliyowazidi, bali huyu katika umaskini wake ametia vyote alivyokuwa navyo. Na watu kadhaa walipokuwa wakiongea habari za hekalu, jinsi lilivyopambwa kwa mawe mazuri na sadaka za watu, alisema, Haya mnayoyatazama, siku zitakuja ambapo halitasalia jiwe juu ya jiwe ambalo halitabomolewa. Wakamwuliza wakisema, Mwalimu, mambo hayo yatakuwa lini? Nayo ni nini ishara ya kuwa mambo hayo yako karibu kutukia? Akasema, Angalieni, msije mkadanganyika, kwa sababu wengi watakuja kwa jina langu, wakisema, Mimi ndiye; tena, Majira yamekaribia. Basi msiwafuate hao. Nanyi mtakaposikia habari za vita na fitina, msitishwe; maana, hayo hayana budi kutukia kwanza, lakini ule mwisho hauji upesi. Kisha aliwaambia, Taifa litaondoka kupigana na taifa, na ufalme kupigana na ufalme; kutakuwa na mitetemeko mikubwa ya ardhi; na njaa na tauni mahali pengi; na mambo ya kutisha na ishara kuu kutoka mbinguni. Lakini, kabla hayo yote hayajatokea, watawakamata na kuwaudhi; watawapeleka mbele ya masinagogi, na kuwaua magerezani, mkipelekwa mbele ya wafalme na watawala kwa ajili ya jina langu. Na hayo yatakuwa ushuhuda kwenu. Basi, kusudieni mioyoni mwenu, kutofikiri-fikiri kwanza mtakavyojibu; kwa sababu mimi nitawapa kinywa na hekima ambayo watesi wenu wote hawataweza kushindana nayo wala kuipinga. Nanyi mtasalitiwa na wazazi wenu, na ndugu zenu, na jamaa zenu, na rafiki zenu, nao watawaua baadhi yenu. Nanyi mtachukiwa na watu wote kwa ajili ya jina langu. Lakini hautapotea hata unywele mmoja wa vichwa vyenu. Nanyi kwa subira yenu mtaziponya nafsi zenu.

Shirikisha
Soma Luka 21

Luka 21:1-19 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Akainua macho yake akawaona matajiri wakitia sadaka zao katika sanduku la hazina. Akamwona mjane mmoja maskini akitia mle senti mbili. Akasema, Hakika nawaambia, huyu mjane maskini ametia zaidi kuliko wote; maana, hao wote walitia sadakani katika mali iliyowazidi, bali huyu katika umaskini wake ametia vyote alivyokuwa navyo. Na watu kadha wa kadha walipokuwa wakiongea habari za hekalu, jinsi lilivyopambwa kwa mawe mazuri na sadaka za watu, alisema, Haya mnayoyatazama, siku zitakuja ambapo halitasalia jiwe juu ya jiwe ambalo halitabomoshwa. Wakamwuliza wakisema, Mwalimu, mambo hayo yatakuwa lini? Nayo ni nini ishara ya kuwa mambo hayo ya karibu kutukia? Akasema, Angalieni, msije mkadanganyika, kwa sababu wengi watakuja kwa jina langu, wakisema, Mimi ndiye; tena, Majira yamekaribia. Basi msiwafuate hao. Nanyi mtakaposikia habari za vita na fitina, msitishwe; maana, hayo hayana budi kutukia kwanza, lakini ule mwisho hauji upesi. Kisha aliwaambia, Taifa litaondoka kupigana na taifa, na ufalme kupigana na ufalme; kutakuwa na matetemeko makubwa ya nchi; na njaa na tauni mahali mahali; na mambo ya kutisha na ishara kuu kutoka mbinguni. Lakini, kabla hayo yote hayajatokea, watawakamata na kuwaudhi; watawapeleka mbele ya masinagogi, na kuwaua magerezani, mkipelekwa mbele ya wafalme na maliwali kwa ajili ya jina langu. Na hayo yatakuwa ushuhuda kwenu. Basi, kusudieni mioyoni mwenu, kutofikiri-fikiri kwanza mtakavyojibu; kwa sababu mimi nitawapa kinywa na hekima ambayo watesi wenu wote hawataweza kushindana nayo wala kuipinga. Nanyi mtasalitiwa na wazazi wenu, na ndugu zenu, na jamaa zenu, na rafiki zenu, nao watawafisha baadhi yenu. Nanyi mtachukiwa na watu wote kwa ajili ya jina langu. Walakini hautapotea hata unywele mmoja wa vichwa vyenu. Nanyi kwa subira yenu mtaziponya nafsi zenu.

Shirikisha
Soma Luka 21

Luka 21:1-19 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Yesu alipoinua macho yake, aliwaona matajiri wakiweka sadaka zao kwenye sanduku la hazina ya Hekalu. Akamwona pia mjane mmoja maskini akiweka humo sarafu mbili ndogo za shaba. Yesu akasema, “Amin, nawaambia, huyu mjane maskini ameweka humo zaidi ya watu wengine wote. Hawa watu wengine wote wametoa sadaka kutokana na wingi wa mali zao. Lakini huyu mjane ametoa kutokana na umaskini wake vyote alivyokuwa navyo, hata kile alichohitaji ili kuishi.” Baadhi ya wanafunzi wake wakawa wanamwonyesha jinsi Hekalu lilivyopambwa kwa mawe mazuri na kwa vitu vilivyotolewa kuwa sadaka kwa Mungu. Lakini Yesu akawaambia, “Kuhusu haya mnayoyaona hapa, wakati utafika ambapo hakuna jiwe moja litakalobaki juu ya jingine, bali kila moja litabomolewa.” Wakamuuliza, “Mwalimu, mambo haya yatatukia lini? Ni dalili gani itaonyesha kwamba yanakaribia kutendeka?” Yesu akawajibu, “Jihadharini msije mkadanganywa. Maana wengi watakuja kwa Jina langu, wakidai, ‘Mimi ndiye,’ na, ‘Wakati umekaribia.’ Msiwafuate. Lakini msikiapo habari za vita na machafuko, msiogope. Kwa maana hayo ni lazima yatokee kwanza, ila ule mwisho hautakuja wakati huo.” Kisha akawaambia: “Taifa litainuka dhidi ya taifa jingine, na ufalme mmoja dhidi ya ufalme mwingine. Kutakuwa na mitetemeko mikubwa ya ardhi, na njaa kali, na magonjwa ya kuambukiza katika sehemu mbalimbali. Pia kutakuwa na matukio ya kutisha na ishara kuu kutoka mbinguni. “Lakini kabla yote hayajatokea, watawakamata ninyi na kuwatesa. Watawatia mikononi mwa wakuu wa masinagogi na kuwafunga magerezani. Nanyi mtapelekwa mbele ya wafalme na watawala kwa ajili ya Jina langu. Hii itawapa nafasi ya kushuhudia. Lakini kusudieni mioyoni mwenu msisumbuke awali kuhusu mtakalosema mbele ya mashtaka. Kwa maana nitawapa maneno na hekima ambayo hakuna hata adui yenu mmoja atakayeweza kushindana nayo wala kuipinga. Mtasalitiwa hata na wazazi, ndugu, jamaa na marafiki, na baadhi yenu watawaua. Mtachukiwa na watu wote kwa ajili ya Jina langu. Lakini hapatakuwa na unywele mmoja wa kichwa chenu utakaoangamia. Kwa kuvumilia mtaokoa roho zenu.

Shirikisha
Soma Luka 21