Luka 2:41-52
Luka 2:41-52 Biblia Habari Njema (BHN)
Wazazi wake walikuwa na desturi ya kwenda Yerusalemu kila mwaka wakati wa sikukuu ya Pasaka. Mtoto alipokuwa na umri wa miaka kumi na miwili, wote walikwenda kwenye sikukuu hiyo kama ilivyokuwa desturi. Baada ya sikukuu, walianza safari ya kurudi makwao, lakini Yesu alibaki Yerusalemu bila wazazi wake kuwa na habari. Walidhani alikuwa pamoja na kundi la wasafiri, wakaenda mwendo wa kutwa, halafu wakaanza kumtafuta miongoni mwa jamaa na marafiki. Kwa kuwa hawakumwona, walirudi Yerusalemu wakimtafuta. Siku ya tatu, walimkuta hekaluni kati ya waalimu, akiwasikiliza na kuwauliza maswali. Wote waliosikia maneno yake walistaajabia akili yake na majibu yake ya hekima. Wazazi wake walipomwona walishangaa. Maria, mama yake, akamwuliza, “Mwanangu, kwa nini umetutendea hivyo? Baba yako na mimi tumekuwa tukikutafuta kwa huzuni.” Yeye akawajibu, “Kwa nini mlinitafuta? Hamkujua kwamba inanipasa kuwa katika nyumba ya Baba yangu?” Lakini wazazi wake hawakuelewa maana ya maneno aliyowaambia. Basi, akarudi pamoja nao hadi Nazareti, akawa anawatii. Mama yake akaweka mambo hayo yote moyoni mwake. Naye Yesu akaendelea kukua katika hekima na kimo; akazidi kupendwa na Mungu na watu.
Luka 2:41-52 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi, wazee wake huenda Yerusalemu kila mwaka, wakati wa sikukuu ya Pasaka. Na alipofikisha umri wa miaka kumi na miwili, walipanda kama ilivyokuwa desturi ya sikukuu; na walipokwisha kuzitimiza siku, wakati wa kurudi kwao, yule mtoto Yesu alibaki nyuma huko Yerusalemu, na wazee wake walikuwa hawana habari. Nao wakadhani ya kuwa yumo katika msafara; wakaenda mwendo wa kutwa, wakawa wakimtafuta katika jamaa zao na wenzao; na walipomkosa, wakarudi Yerusalemu, huku wakimtafuta. Ikawa baada ya siku tatu wakamwona hekaluni, ameketi katikati ya waalimu, akiwasikiliza na kuwauliza maswali. Nao wote waliomsikia walistaajabia fahamu zake na majibu yake. Na walipomwona walishangaa, na mama yake akamwambia, Mwanangu, mbona umetutenda hivi? Tazama, baba yako na mimi tulikuwa tukikutafuta kwa huzuni. Akawaambia, Kwa nini mnitafute? Hamkujua ya kuwa imenipasa kuwamo katika nyumba ya Baba yangu? Nao hawakuelewa neno hilo alilowaambia. Akashuka pamoja nao mpaka Nazareti, naye alikuwa akiwatii; na mamaye aliyaweka hayo yote moyoni mwake. Naye Yesu akazidi kuendelea katika hekima na kimo, akimpendeza Mungu na wanadamu.
Luka 2:41-52 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi, wazee wake huenda Yerusalemu kila mwaka, wakati wa sikukuu ya Pasaka. Na alipopata umri wake miaka kumi na miwili, walipanda kama ilivyokuwa desturi ya sikukuu; na walipokwisha kuzitimiza siku, wakati wa kurudi kwao, yule mtoto Yesu alibaki nyuma huko Yerusalemu, na wazee wake walikuwa hawana habari. Nao wakadhani ya kuwa yumo katika msafara; wakaenenda mwendo wa kutwa, wakawa wakimtafuta katika jamaa zao na wenzao; na walipomkosa, wakarejea Yerusalemu, huku wakimtafuta. Ikawa baada ya siku tatu wakamwona hekaluni, ameketi katikati ya waalimu, akiwasikiliza na kuwauliza maswali. Nao wote waliomsikia walistaajabia fahamu zake na majibu yake. Na walipomwona walishangaa, na mama yake akamwambia, Mwanangu, mbona umetutenda hivi? Tazama, baba yako na mimi tulikuwa tukikutafuta kwa huzuni. Akawaambia, Kwani kunitafuta? Hamkujua ya kuwa imenipasa kuwamo katika nyumba ya Baba yangu? Nao hawakuelewa na neno hilo alilowaambia. Akashuka pamoja nao mpaka Nazareti, naye alikuwa akiwatii; na mamaye aliyaweka hayo yote moyoni mwake. Naye Yesu akazidi kuendelea katika hekima na kimo, akimpendeza Mungu na wanadamu.
Luka 2:41-52 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Kila mwaka Yosefu na Maria mama yake Yesu walikuwa na desturi ya kwenda Yerusalemu kwa ajili ya Sikukuu ya Pasaka. Yesu alipokuwa na umri wa miaka kumi na miwili, walipanda kwenda kwenye Sikukuu hiyo kama ilivyokuwa desturi. Baada ya Sikukuu kumalizika, wakati Yosefu na Maria mama yake walipokuwa wakirudi nyumbani, Yesu alibaki Yerusalemu lakini hawakutambua. Wao wakidhani kuwa yuko miongoni mwa wasafiri, walienda mwendo wa kutwa nzima. Ndipo wakaanza kumtafuta miongoni mwa jamaa zao na marafiki. Walipomkosa walirudi Yerusalemu ili kumtafuta. Baada ya siku tatu wakamkuta ndani ya Hekalu, akiwa ameketi katikati ya walimu wa sheria, akiwasikiliza na kuwauliza maswali. Wote waliomsikia walistaajabishwa na uwezo wake mkubwa wa kuelewa, na majibu aliyoyatoa. Yosefu na Maria mama yake walipomwona walishangaa. Mama yake akamuuliza, “Mwanangu, mbona umetufanyia hivi? Tazama, mimi na baba yako tumekuwa tukikutafuta kwa wasiwasi mkubwa kila mahali.” Yesu akawaambia, “Kwa nini kunitafuta? Hamkujua kwamba imenipasa kuwa katika nyumba ya Baba yangu?” Lakini wao hawakuelewa maana ya lile alilowaambia. Ndipo akashuka pamoja nao hadi Nazareti, naye alikuwa mtiifu kwao. Lakini mama yake akayaweka moyoni mwake mambo haya yote. Naye Yesu akakua katika hekima na kimo, akimpendeza Mungu na wanadamu.