Luka 2:22-40
Luka 2:22-40 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kisha, zilipotimia siku za kutakasika kwao, kama ilivyo Torati ya Musa walikwenda naye hata Yerusalemu, wamweke kwa Bwana, (kama ilivyoandikwa katika sheria ya Bwana, Kila mtoto wa kiume aliye kifungua mimba wa mamaye na aitwe mtakatifu kwa Bwana), wakatoe na sadaka, kama ilivyonenwa katika sheria ya Bwana, Hua wawili au makinda ya njiwa wawili. Na tazama, pale Yerusalemu palikuwa na mtu, jina lake Simeoni, naye ni mtu mwenye haki, mcha Mungu, akiitarajia faraja ya Israeli; na Roho Mtakatifu alikuwa juu yake. Naye alikuwa ameonywa na Roho Mtakatifu ya kwamba hataona mauti kabla ya kumwona Kristo wa Bwana. Basi akaja hekaluni ameongozwa na Roho; na wale wazazi walipomleta mtoto Yesu ndani, ili wamfanyie kama ilivyokuwa desturi ya sheria, yeye mwenyewe alimpokea mikononi mwake, akamshukuru Mungu, akisema, Sasa, Bwana, wamruhusu mtumishi wako, Kwa amani, kama ulivyosema; Kwa kuwa macho yangu yameuona wokovu wako, Uliouweka tayari machoni pa watu wote; Nuru ya kuwa mwangaza wa Mataifa, Na kuwa utukufu wa watu wako Israeli. Na babaye na mamaye walikuwa wakiyastaajabia hayo yaliyonenwa juu yake. Simeoni akawabariki, akamwambia Mariamu mama yake, Tazama, huyu amewekwa kwa kuanguka na kuinuka wengi walio katika Israeli, na kuwa ishara itakayonenewa. Nawe mwenyewe, upanga utaingia moyoni mwako, ili yafunuliwe mawazo ya mioyo mingi. Palikuwa na nabii mwanamke, jina lake Ana, binti Fanueli, wa kabila la Asheri, na umri wake ulikuwa miaka mingi, alikuwa amekaa na mume miaka saba baada ya uanawali wake. Naye ni mjane wa miaka themanini na minne; haondoki katika hekalu, ila huabudu usiku na mchana kwa kufunga na kuomba. Huyu alitokea saa ile ile akamshukuru Mungu, na wote waliokuwa wakiutarajia ukombozi katika Yerusalemu akawatolea habari zake. Basi, walipokwisha kuyatimiza yote kama yalivyoagizwa katika sheria ya Bwana, walirejea Galilaya mpaka mjini kwao, Nazareti. Yule mtoto akakua, akaongezeka nguvu, amejaa hekima, na neema ya Mungu ilikuwa juu yake.
Luka 2:22-40 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Ulipotimia wakati wa utakaso wake Maria kwa mujibu wa Sheria ya Mose, basi Yosefu na Maria walimpeleka mtoto Yerusalemu, ili kumweka wakfu kwa Bwana (kama ilivyoandikwa katika Sheria ya Bwana, kwamba, “Kila mtoto wa kiume kifungua mimba atawekwa wakfu kwa Bwana”), na pia kutoa dhabihu kulingana na yale yaliyonenwa katika Sheria ya Bwana: “Hua wawili au makinda mawili ya njiwa.” Basi alikuwako huko Yerusalemu mtu mmoja jina lake Simeoni, ambaye alikuwa mwenye haki na mcha Mungu, akitarajia faraja ya Israeli, na Roho Mtakatifu alikuwa juu yake. Roho Mtakatifu alikuwa amemfunulia kuwa hatakufa kabla hajamwona Kristo wa Bwana. Simeoni, akiwa ameongozwa na Roho Mtakatifu, alikwenda Hekaluni. Wazazi walipomleta mtoto Yesu ili kumfanyia kama ilivyokuwa desturi ya Sheria, ndipo Simeoni akampokea mtoto mikononi mwake na kumsifu Mungu, akisema: “Bwana Mwenyezi, kama ulivyoahidi, sasa wamruhusu mtumishi wako aende zake kwa amani. Kwa maana macho yangu yameuona wokovu wako, ulioweka tayari machoni pa watu wote, nuru kwa ajili ya ufunuo kwa watu wa Mataifa na kwa ajili ya utukufu kwa watu wako Israeli.” Naye Yosefu na mama yake mtoto wakastaajabu kwa yale yaliyokuwa yamesemwa kumhusu huyo mtoto. Kisha Simeoni akawabariki, akamwambia Maria mama yake, “Mtoto huyu amewekwa kwa makusudi ya kuanguka na kuinuka kwa wengi katika Israeli. Atakuwa ishara ambayo watu watanena dhidi yake, ili mawazo ya mioyo mingi yadhihirike. Nao upanga utauchoma moyo wako.” Tena alikuwako Hekaluni nabii mmoja mwanamke, jina lake Ana binti Fanueli, wa kabila la Asheri. Alikuwa mzee sana; naye alikuwa ameolewa na kuishi na mume kwa miaka saba tu, kisha mumewe akafa. Hivyo alikuwa mjane na umri wake ulikuwa miaka themanini na minne. Yeye hakuondoka humo Hekaluni usiku wala mchana, bali alikuwa akimwabudu Mungu, akifunga na kuomba. Wakati huo huo, Ana alikuja akaanza kusifu, akimshukuru Mungu na kusema habari za huyo mtoto kwa watu wote waliokuwa wakitarajia ukombozi wa Yerusalemu. Yosefu na Maria walipokuwa wamekamilisha mambo yote yaliyotakiwa na Sheria ya Bwana, walirudi mjini kwao Nazareti huko Galilaya. Naye yule mtoto akakua na kuongezeka nguvu, akiwa amejaa hekima, na neema ya Mungu ilikuwa juu yake.
Luka 2:22-40 Biblia Habari Njema (BHN)
Siku zilipotimia za Yosefu na Maria kutakaswa kama walivyotakiwa na sheria, wazazi hao walimchukua mtoto, wakaenda naye Yerusalemu ili wamweke mbele za Bwana. Katika sheria ya Bwana imeandikwa: “Kila mzaliwa wa kwanza wa kiume atawekwa wakfu kwa Bwana.” Pia walikwenda ili watoe sadaka: Hua wawili au makinda mawili ya njiwa, kama ilivyotakiwa katika sheria ya Bwana. Wakati huo huko Yerusalemu kulikuwa na mtu mmoja, mwema na mcha Mungu, jina lake Simeoni. Yeye alikuwa akitazamia kwa hamu ukombozi wa Israeli. Roho Mtakatifu alikuwa pamoja naye. Roho Mtakatifu alikuwa amemhakikishia kwamba hatakufa kabla ya kumwona Kristo wa Bwana. Basi, akiongozwa na Roho Mtakatifu, Simeoni aliingia hekaluni; na wazazi wa Yesu walipomleta hekaluni mtoto wao ili wamfanyie kama ilivyotakiwa na sheria, Simeoni alimpokea mtoto Yesu mikononi mwake huku akimtukuza Mungu, akisema: “Sasa Bwana, umetimiza ahadi yako, umruhusu mtumishi wako aende kwa amani. Maana kwa macho yangu nimeuona wokovu ulioleta, ambao umeutayarisha uonekane na watu wote: Mwanga utakaowaangazia watu wa mataifa, na utukufu kwa watu wako Israeli.” Baba yake Yesu na mama yake walikuwa wakistaajabia maneno aliyosema Simeoni juu ya mtoto. Simeoni akawabariki, akamwambia Maria mama yake, “Mtoto huyu atakuwa sababu ya kupotea na kuokoka kwa watu wengi katika Israeli. Naye atakuwa ishara itakayopingwa na watu; na hivyo mawazo ya watu wengi yataonekana wazi. Nawe mwenyewe, uchungu ulio kama upanga mkali utauchoma moyo wako.” Palikuwa na nabii mmoja mwanamke, mzee sana, jina lake Ana, binti Fanueli, wa kabila la Asheri. Alikuwa ameishi na mumewe kwa miaka saba tangu alipoolewa. Halafu alibaki mjane hadi wakati huo akiwa mzee wa miaka themanini na minne. Wakati huo wote alikaa hekaluni akifunga na kusali usiku na mchana. Saa hiyohiyo, alijitokeza mbele, akamshukuru Mungu, na kueleza habari za huyo mtoto kwa watu wote waliokuwa wanatazamia ukombozi wa Yerusalemu. Hao wazazi walipokwisha fanya yote yaliyoamriwa na sheria ya Bwana, walirudi makwao Nazareti, wilayani Galilaya. Mtoto akakua, akazidi kupata nguvu, akajaa hekima, na neema ya Mungu ilikuwa naye.
Luka 2:22-40 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kisha, zilipotimia siku za kutakasika kwao, kama ilivyo torati ya Musa walikwenda naye hata Yerusalemu, wamweke kwa Bwana, (kama ilivyoandikwa katika sheria ya Bwana, Kila mtoto mwanamume aliye kifungua mimba ya mamaye na aitwe mtakatifu kwa Bwana), wakatoe na sadaka, kama ilivyonenwa katika sheria ya Bwana, Hua wawili au makinda ya njiwa wawili. Na tazama, pale Yerusalemu palikuwa na mtu, jina lake Simeoni, naye ni mtu mwenye haki, mcha Mungu, akiitarajia faraja ya Israeli; na Roho Mtakatifu alikuwa juu yake. Naye alikuwa ameonywa na Roho Mtakatifu ya kwamba hataona mauti kabla ya kumwona Kristo wa Bwana. Basi akaja hekaluni ameongozwa na Roho; na wale wazazi walipomleta mtoto Yesu ndani, ili wamfanyie kama ilivyokuwa desturi ya sheria, yeye mwenyewe alimpokea mikononi mwake, akamshukuru Mungu, akisema, Sasa, Bwana, wamruhusu mtumishi wako, Kwa amani, kama ulivyosema; Kwa kuwa macho yangu yameuona wokovu wako, Uliouweka tayari machoni pa watu wote; Nuru ya kuwa mwangaza wa Mataifa, Na kuwa utukufu wa watu wako Israeli. Na babaye na mamaye walikuwa wakiyastaajabia hayo yaliyonenwa juu yake. Simeoni akawabariki, akamwambia Mariamu mama yake, Tazama, huyu amewekwa kwa kuanguka na kuinuka wengi walio katika Israeli, na kuwa ishara itakayonenewa. Nawe mwenyewe, upanga utaingia moyoni mwako, ili yafunuliwe mawazo ya mioyo mingi. Palikuwa na nabii mke, jina lake Ana, binti Fanueli, wa kabila ya Asheri, na umri wake ulikuwa miaka mingi, alikuwa amekaa na mume miaka saba baada ya uanawali wake. Naye ni mjane wa miaka themanini na minne; haondoki katika hekalu, ila huabudu usiku na mchana kwa kufunga na kuomba. Huyu alitokea saa ile ile akamshukuru Mungu, na wote waliokuwa wakiutarajia ukombozi katika Yerusalemu akawatolea habari zake. Basi, walipokwisha kuyatimiza yote kama yalivyoagizwa katika sheria ya Bwana, walirejea Galilaya mpaka mjini kwao, Nazareti. Yule mtoto akakua, akaongezeka nguvu, amejaa hekima, na neema ya Mungu ilikuwa juu yake.