Luka 19:35-40
Luka 19:35-40 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Wakampeleka kwa Yesu, wakatandika nguo zao juu ya mwana-punda, wakampandisha Yesu. Na alipokuwa akienda walitandaza nguo zao njiani. Hata alipokuwa amekaribia matelemko ya mlima wa Mizeituni, kundi zima la wanafunzi wake walianza kufurahi na kumsifu Mungu kwa sauti kuu, kwa ajili ya matendo yote ya uwezo waliyoyaona, wakasema, Ndiye mbarikiwa Mfalme ajaye kwa jina la Bwana; amani mbinguni, na utukufu huko juu. Baadhi ya Mafarisayo waliokuwa katika mkutano wakamwambia, Mwalimu, uwakanye wanafunzi wako. Akajibu, akasema, Nawaambia ninyi, wakinyamaza hawa, mawe yatapiga kelele.
Luka 19:35-40 Biblia Habari Njema (BHN)
Basi, wakampelekea Yesu yule mwanapunda. Kisha wakatandika mavazi yao juu yake, wakampandisha Yesu juu yake. Yesu akaendelea na safari, na watu wakatandaza mavazi yao barabarani. Alipofika karibu na Yerusalemu, katika mteremko wa mlima wa Mizeituni, umati wote na wanafunzi wake wakaanza kushangilia na kumtukuza Mungu kwa sauti kubwa kwa sababu ya mambo makuu waliyoyaona; wakawa wanasema: “Abarikiwe Mfalme ajaye kwa jina la Bwana. Amani mbinguni, na utukufu juu mbinguni!” Hapo baadhi ya Mafarisayo waliokuwako katika lile kundi la watu wakamwambia Yesu, “Mwalimu, wanyamazishe wanafunzi wako!” Yesu akawajibu, “Nawaambieni, kama hawa wakinyamaza, hakika hayo mawe yatapaza sauti.”
Luka 19:35-40 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Wakampeleka kwa Yesu, wakatandika nguo zao juu ya mwanapunda, wakampandisha Yesu. Na alipokuwa akienda walitandaza nguo zao njiani. Na alipokuwa amekaribia mteremko wa mlima wa Mizeituni, kundi zima la wanafunzi wake walianza kufurahi na kumsifu Mungu kwa sauti kuu, kwa ajili ya matendo yote ya uwezo waliyoyaona, wakasema, Ndiye mbarikiwa Mfalme ajaye kwa jina la Bwana; amani mbinguni, na utukufu huko juu. Baadhi ya Mafarisayo waliokuwa katika mkutano wakamwambia, Mwalimu, uwakanye wanafunzi wako. Akajibu, akasema, Nawaambia ninyi, wakinyamaza hawa, mawe yatanena kwa sauti kuu.
Luka 19:35-40 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Wakamleta kwa Yesu, nao baada ya kutandika mavazi yao juu ya huyo mwana-punda, wakampandisha Yesu juu yake. Alipokuwa akienda akiwa amempanda, watu wakatandaza mavazi yao barabarani. Alipokaribia mahali yanapoanzia materemko ya Mlima wa Mizeituni, umati wote wa wafuasi wake wakaanza kumsifu Mungu kwa furaha kwa sauti kuu kwa ajili ya matendo yote ya miujiza waliyoyaona. Wakasema: “Amebarikiwa Mfalme ajaye kwa Jina la Bwana!” “Amani mbinguni na utukufu huko juu sana.” Baadhi ya Mafarisayo waliokuwamo miongoni mwa ule umati wa watu wakamwambia, “Mwalimu, waamuru wanafunzi wako wanyamaze.” Yesu akawajibu, “Nawaambia ninyi, kama hawa wakinyamaza, mawe yatapiga kelele.”