Luka 18:1-8
Luka 18:1-8 Biblia Habari Njema (BHN)
Basi, Yesu aliwasimulia mfano kuonesha kwamba ni lazima kusali daima bila kukata tamaa. Alisema: “Katika mji mmoja kulikuwa na hakimu ambaye hakuwa anamcha Mungu wala kumjali binadamu. Katika mji huohuo, kulikuwa pia na mama mmoja mjane ambaye alimwendea huyo hakimu mara nyingi akimwomba amtetee apate haki yake kutoka kwa adui yake. Kwa muda mrefu huyo hakimu hakupenda kumtetea huyo mjane; lakini, mwishowe akajisemea: ‘Ingawa mimi simchi Mungu wala simjali binadamu, lakini kwa vile huyu mjane ananisumbua, nitamtetea; la sivyo ataendelea kufika hapa, na mwisho atanichosha kabisa!’” Basi, Bwana akaendelea kusema, “Sikieni jinsi alivyosema huyo hakimu mbaya. Je, ndio kusema Mungu hatawatetea wale aliowachagua, ambao wanamlilia mchana na usiku? Je, atakawia kuwasikiliza? Nawaambieni atawatetea upesi. Hata hivyo, je, kutakuwako na imani duniani wakati Mwana wa Mtu atakapokuja?”
Luka 18:1-8 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Akawaambia mfano, ya kwamba imewapasa kumwomba Mungu sikuzote, wala wasikate tamaa. Akasema, Palikuwa na hakimu katika mji fulani, hamchi Mungu, wala hajali watu. Na katika mji huo palikuwa na mwanamke mjane, aliyekuwa akimwendeaendea, akisema, Nipatie haki na adui wangu. Naye kwa muda alikataa; halafu akasema moyoni mwake, Ijapokuwa simchi Mungu wala sijali watu, lakini, kwa kuwa mjane huyu ananiudhi, nitampatia haki yake, asije akanichosha kwa kunijia daima. Bwana akasema, Sikilizeni asemavyo yule hakimu dhalimu. Na Mungu, je! Hatawapatia haki wateule wake wanaomlilia mchana na usiku, naye ni mvumilivu kwao? Nawaambia, atawapatia haki upesi; lakini, atakapokuja Mwana wa Adamu, je! Ataiona imani duniani?
Luka 18:1-8 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Akawaambia mfano, ya kwamba imewapasa kumwomba Mungu sikuzote, wala wasikate tamaa. Akasema, Palikuwa na kadhi katika mji fulani, hamchi Mungu, wala hajali watu. Na katika mji huo palikuwa na mwanamke mjane, aliyekuwa akimwendea-endea, akisema, Nipatie haki na adui wangu. Naye kwa muda alikataa; halafu akasema moyoni mwake, Ijapokuwa simchi Mungu wala sijali watu, lakini, kwa kuwa mjane huyu ananiudhi, nitampatia haki yake, asije akanichosha kwa kunijia daima. Bwana akasema, Sikilizeni asemavyo yule kadhi dhalimu. Na Mungu, je! Hatawapatia haki wateule wake wanaomlilia mchana na usiku, naye ni mvumilivu kwao? Nawaambia, atawapatia haki upesi; walakini, atakapokuja Mwana wa Adamu, je! Ataiona imani duniani?
Luka 18:1-8 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Kisha Yesu akawapa wanafunzi wake mfano ili kuwaonyesha kuwa yawapasa kuomba pasipo kukata tamaa. Akawaambia, “Katika mji mmoja alikuwepo hakimu ambaye hakumwogopa Mungu wala kumjali mtu. Katika mji huo alikuwako mjane mmoja ambaye alikuwa akija kwake mara kwa mara akimwomba, ‘Tafadhali nipatie haki kati yangu na adui yangu.’ “Kwa muda mrefu yule hakimu alikataa. Lakini hatimaye akasema moyoni mwake, ‘Ijapokuwa simwogopi Mungu wala simjali mwanadamu, lakini kwa kuwa huyu mjane ananisumbuasumbua, nitahakikisha amepata haki yake ili asiendelee kunichosha kwa kunijia mara kwa mara!’ ” Bwana akasema, “Sikilizeni asemavyo huyu hakimu dhalimu. Je, Mungu hatawatendea haki wateule wake wanaomlilia usiku na mchana? Je, atakawia kuwasaidia? Ninawaambia, atawapatia haki upesi. Lakini je, Mwana wa Adamu atakapokuja ataikuta imani duniani?”