Luka 14:16-24
Luka 14:16-24 Biblia Habari Njema (BHN)
Yesu akamjibu, “Mtu mmoja alifanya karamu kubwa, akawaalika watu wengi. Wakati wa karamu ulipofika alimtuma mtumishi wake akawaambie walioalikwa, ‘Njoni, kila kitu ni tayari.’ Lakini wote, mmoja baada ya mwingine, wakaanza kuomba radhi. Wa kwanza akamwambia mtumishi: ‘Nimenunua shamba, na hivyo sina budi niende kuliangalia; nakuomba uniwie radhi.’ Mwingine akasema: ‘Nimenunua ng'ombe jozi tano wa kulima, sasa nimo njiani kwenda kuwajaribu; nakuomba uniwie radhi.’ Na mwingine akasema: ‘Nimeoa kwa hiyo siwezi kuja.’ Mtumishi huyo akarudi na kumwarifu bwana wake jambo hilo. Yule mwenye nyumba alikasirika, akamwambia mtumishi wake: ‘Nenda upesi kwenye barabara na vichochoro vya mji, uwalete hapa ndani maskini, viwete, vipofu na vilema wengine.’ Baadaye, mtumishi huyo akasema: ‘Bwana, mambo yamefanyika kama ulivyoamuru, lakini bado iko nafasi.’ Yule bwana akamwambia mtumishi: ‘Nenda katika barabara na vichochoro vya mji uwashurutishe watu kuingia ili nyumba yangu ijae. Kwa maana, nawaambieni, hakuna hata mmoja wa wale walioalikwa atakayeonja karamu yangu.’”
Luka 14:16-24 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Akamwambia, Mtu mmoja alifanya karamu kubwa akaalika watu wengi, akamtuma mtumwa wake saa ya chakula awaambie wale walioalikwa, Njooni, kwa kuwa vitu vyote vimekwisha kuwekwa tayari. Wakaanza wote kutoa udhuru kwa nia moja. Wa kwanza alimwambia, Nimenunua shamba, sharti niende nikalitazame; tafadhali unisamehe. Mwingine akasema, Nimenunua ng'ombe jozi tano, ninakwenda kuwajaribu; tafadhali unisamehe. Mwingine akasema, Nimeoa mke, na kwa sababu hiyo siwezi kuja. Yule mtumwa akaenda, akamwambia Bwana wake kuhusu mambo hayo. Basi, yule mwenye nyumba akakasirika, akamwambia mtumwa wake, Toka upesi, uende katika njia kuu na vichochoro vya mji, ukawalete hapa maskini, na vilema, na vipofu, na viwete. Mtumwa akasema, Bwana, hayo uliyoagiza yamekwisha tendeka, na hata sasa ingaliko nafasi. Bwana akamwambia mtumwa, Toka nje uende barabarani na mipakani, ukawashurutishe kuingia ndani, nyumba yangu ipate kujaa. Maana nawaambia ya kwamba katika wale walioalikwa, hakuna hata mmoja atakayeionja karamu yangu.
Luka 14:16-24 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Akamwambia, Mtu mmoja alifanya karamu kubwa akaalika watu wengi, akamtuma mtumwa wake saa ya chakula awaambie wale walioalikwa, Njoni, kwa kuwa vitu vyote vimekwisha kuwekwa tayari. Wakaanza wote kutoa udhuru kwa nia moja. Wa kwanza alimwambia, Nimenunua shamba, sharti niende nikalitazame; tafadhali unisamehe. Mwingine akasema, Nimenunua ng’ombe jozi tano, ninakwenda kuwajaribu; tafadhali unisamehe. Mwingine akasema, Nimeoa mke, na kwa sababu hiyo siwezi kuja. Yule mtumwa akaenda, akampa bwana wake habari ya mambo hayo. Basi, yule mwenye nyumba akakasirika, akamwambia mtumwa wake, Toka upesi, uende katika njia kuu na vichochoro vya mji, ukawalete hapa maskini, na vilema, na vipofu, na viwete. Mtumwa akasema, Bwana, hayo uliyoagiza yamekwisha tendeka, na hata sasa ingaliko nafasi. Bwana akamwambia mtumwa, Toka nje uende barabarani na mipakani, ukawashurutishe kuingia ndani, nyumba yangu ipate kujaa. Maana nawaambia ya kwamba katika wale walioalikwa, hapana hata mmoja atakayeionja karamu yangu.
Luka 14:16-24 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Yesu akamjibu, “Mtu mmoja alikuwa anaandaa karamu kubwa, akaalika watu wengi. Wakati wa karamu ulipofika, akamtuma mtumishi wake akawaambie wale walioalikwa, ‘Karibuni, kila kitu ki tayari sasa.’ “Lakini wote, kila mmoja, wakaanza kutoa udhuru: Wa kwanza akasema, ‘Nimenunua shamba, lazima niende kuliona. Tafadhali niwie radhi.’ “Mwingine akasema, ‘Ndipo tu nimenunua jozi tano za ngʼombe wa kulimia, nami ninakwenda kuwajaribu, tafadhali niwie radhi.’ Naye mwingine akasema, ‘Nimeoa mke, kwa hiyo siwezi kuja.’ “Yule mtumishi akarudi, akampa bwana wake taarifa. Ndipo yule mwenye nyumba akakasirika, akamwagiza yule mtumishi wake, akisema, ‘Nenda upesi kwenye mitaa na vichochoro vya mjini uwalete maskini, vilema, vipofu na viwete.’ “Yule mtumishi akamwambia, ‘Bwana, yale uliyoniagiza nimefanya, lakini bado ipo nafasi.’ “Ndipo yule bwana akamwambia mtumishi wake, ‘Nenda kwenye barabara na vijia vilivyoko nje ya mji na uwalazimishe watu waingie ili nyumba yangu ipate kujaa. Kwa maana nawaambia, hakuna hata mmoja wa wale walioalikwa atakayeionja karamu yangu.’ ”