Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Luka 12:22-34

Luka 12:22-34 Biblia Habari Njema (BHN)

Kisha Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Kwa sababu hiyo nawaambieni, msiwe na wasiwasi juu ya chakula mnachohitaji ili kuishi, wala juu ya mavazi mnayohitaji kwa ajili ya miili yenu. Kwa sababu uzima ni bora kuliko chakula, na mwili ni bora kuliko mavazi. Chukueni kwa mfano, kunguru: Hawapandi, hawavuni wala hawana ghala yoyote. Hata hivyo, Mungu huwalisha. Nyinyi mna thamani zaidi kuliko ndege! Ni nani kati yenu kwa kuwa na wasiwasi sana anaweza kuongeza kidogo urefu wa maisha yake? Basi, kama hamwezi kufanya jambo dogo kama hilo, kwa nini kuwa na wasiwasi juu ya yale mengine? Angalieni maua jinsi yanavyomea. Hayafanyi kazi wala hayafumi. Lakini nawaambieni, hata Solomoni mwenyewe na fahari zake zote hakupata kuvikwa vizuri kama ua mojawapo. Ikiwa basi, Mungu hulivika hivyo jani la shambani ambalo leo liko na kesho latupwa motoni, je, si atawafanyia nyinyi zaidi? Enyi watu wenye imani haba! “Basi, msivurugike akili, mkihangaika juu ya mtakachokula au mtakachokunywa. Kwa maana hayo yote yanahangaikiwa na watu wote wasiomjua Mungu. Baba yenu anajua kwamba mnahitaji vitu hivyo. Shughulikeni kwanza juu ya ufalme wa Mungu, na hayo mtapewa kwa ziada. “Msiogope, enyi kundi dogo! Maana Baba yenu amependa kuwapeni ufalme. Uzeni mali yenu mkawape maskini hizo fedha. Jifanyieni mifuko isiyochakaa, na kujiwekea hazina mbinguni ambako haitapungua. Huko wezi hawakaribii, wala nondo hawaharibu. Pale ilipo hazina yako, ndipo pia utakapokuwa moyo wako.

Shirikisha
Soma Luka 12

Luka 12:22-34 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Kisha Yesu akawaambia wanafunzi wake: “Kwa hiyo nawaambia, msisumbukie maisha yenu kwamba mtakula nini; au msumbukie miili yenu kwamba mtavaa nini. Maisha ni zaidi ya chakula, na mwili ni zaidi ya mavazi. Fikirini ndege! Wao hawapandi wala hawavuni, hawana ghala wala popote pa kuhifadhi nafaka; lakini Mungu huwalisha. Ninyi ni wa thamani zaidi kuliko ndege! Ni nani miongoni mwenu ambaye kwa kujitaabisha kwake anaweza kujiongezea hata saa moja zaidi katika maisha yake? Kama hamwezi kufanya jambo dogo kama hilo, kwa nini basi kuyasumbukia hayo mengine? “Angalieni maua jinsi yameavyo: Hayafanyi kazi wala hayafumi. Lakini nawaambia, hata Solomoni katika fahari yake yote hakuvikwa vizuri kama mojawapo ya hayo maua. Basi ikiwa Mungu huyavika hivi majani ya shambani, ambayo leo yapo, na kesho yanatupwa motoni, si atawavika ninyi vizuri zaidi, enyi wa imani haba! Wala msisumbuke mioyoni mwenu mtakula nini au mtakunywa nini. Msiwe na wasiwasi juu ya haya. Watu wa mataifa ya duniani husumbuka sana kuhusu vitu hivi vyote, lakini Baba yenu anafahamu kuwa mnahitaji haya yote. Bali utafuteni Ufalme wa Mungu, na haya yote atawapa pia. “Msiogope enyi kundi dogo, kwa maana Baba yenu ameona vyema kuwapa ninyi Ufalme. Uzeni mali zenu mkawape maskini. Jifanyieni mifuko isiyochakaa, mkajiwekee hazina mbinguni isiyokwisha, mahali ambapo mwizi hakaribii wala nondo haharibu. Kwa sababu mahali hazina yako ilipo, hapo ndipo moyo wako utakapokuwa pia.

Shirikisha
Soma Luka 12