Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Luka 12:1-12

Luka 12:1-12 Biblia Habari Njema (BHN)

Wakati watu kwa maelfu walipokuwa wamekusanyika hata wakawa wanakanyagana, Yesu aliwaambia kwanza wanafunzi wake, “Jihadharini na chachu ya Mafarisayo, yaani unafiki. Kila kilichofunikwa kitafunuliwa, kila kilichofichika kitafichuliwa. Kwa hiyo, kila mliyosema gizani, watu watayasikia katika mwanga, na kila mliyonongona faraghani milango imefungwa, yatatangazwa juu ya nyumba. “Nawaambieni nyinyi rafiki zangu: Msiwaogope wale wanaoua mwili, wasiweze kufanya kitu kingine zaidi. Nitawaonesheni yule ambaye ni lazima kumwogopa: Mwogopeni yule ambaye baada ya kuua ana uwezo wa kumtupa mtu katika moto wa Jehanamu. Naam, ninawaambieni, mwogopeni huyo. Inajulikana kwamba shomoro watano huuzwa kwa sarafu ndogo kumi, au sivyo? Lakini mbele ya Mungu hasahauliki hata mmoja. Lakini hata nywele za vichwa vyenu zimehesabiwa zote. Msiogope, basi; nyinyi mna thamani kuliko shomoro wengi! “Nawaambieni kweli, kila mtu anayekiri hadharani kwamba yeye ni wangu, Mwana wa Mtu naye atakiri mbele ya malaika wa Mungu kwamba mtu huyo ni wake. Lakini, mtu yeyote anayenikana mbele ya watu, naye atakanwa mbele ya malaika wa Mungu. “Yeyote anayesema neno la kumpinga Mwana wa Mtu atasamehewa; lakini anayemkufuru Roho Mtakatifu hatasamehewa. “Watakapowapeleka nyinyi mbele ya masunagogi na mbele ya wakuu na watawala, msiwe na wasiwasi juu ya jinsi mtakavyojitetea au jinsi mtakavyosema. Kwa maana wakati huo Roho Mtakatifu atawafundisheni kile mnachopaswa kusema.”

Shirikisha
Soma Luka 12

Luka 12:1-12 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Wakati huo, umati mkubwa wa watu maelfu, walipokuwa wamekusanyika hata wakawa wanakanyagana, Yesu akaanza kuzungumza kwanza na wanafunzi wake, akawaambia: “Jihadharini na chachu ya Mafarisayo, yaani, unafiki wao. Hakuna jambo lolote lililositirika ambalo halitafunuliwa, au lililofichwa ambalo halitajulikana. Kwa hiyo, lolote mlilosema gizani litasikiwa nuruni. Na kile mlichonongʼona masikioni mkiwa kwenye vyumba vya ndani, kitatangazwa juu ya paa. “Nawaambieni rafiki zangu, msiwaogope wale wauao mwili, lakini baada ya hilo hawawezi kufanya lolote zaidi. Lakini nitawaambia nani wa kumwogopa: Mwogopeni yule ambaye baada ya kuua mwili, ana mamlaka ya kuwatupa motoni. Naam, nawaambia, mwogopeni huyo! Mnajua kwamba shomoro watano huuzwa kwa senti mbili? Lakini Mungu hamsahau hata mmoja wao. Naam, hata nywele za vichwa vyenu zote zimehesabiwa. Hivyo msiogope, kwa maana ninyi ni wa thamani kubwa kuliko shomoro wengi. “Ninawaambia kwamba yeyote atakayenikiri mbele ya watu, Mwana wa Adamu naye atamkiri mbele za malaika wa Mungu. Lakini yeye atakayenikana mimi mbele ya watu, Mwana wa Adamu naye atamkana mbele ya malaika wa Mungu. Naye kila atakayenena neno baya dhidi ya Mwana wa Adamu atasamehewa, lakini yeyote atakayemkufuru Roho Mtakatifu hatasamehewa. “Watakapowapeleka katika masinagogi, na mbele ya watawala na wenye mamlaka, msiwe na wasiwasi kuhusu namna mtakavyojitetea au mtakavyosema. Kwa maana Roho Mtakatifu atawafundisha wakati huo huo mnachopaswa kusema.”

Shirikisha
Soma Luka 12