Luka 10:13-37
Luka 10:13-37 Biblia Habari Njema (BHN)
“Ole wako Korazini! Ole wako Bethsaida! Maana, kama miujiza iliyofanyika kwenu ingalifanyika kule Tiro na Sidoni, watu wake wangalikwisha vaa mavazi ya gunia kitambo na kukaa katika majivu kutubu. Hata hivyo, siku ya hukumu nyinyi mtapata adhabu kubwa kuliko ya Tiro na Sidoni. Na wewe Kafarnaumu, je, utajikweza mpaka mbinguni? Utaporomoshwa mpaka kuzimu.” Halafu akasema, “Anayewasikiliza nyinyi, ananisikiliza mimi; na anayekataa kuwapokea nyinyi, anakataa kunipokea mimi. Na yeyote anayekataa kunipokea, anakataa kumpokea yule aliyenituma.” Baadaye, wale sabini na wawili walirudi wamejaa furaha, wakisema, “Bwana, hata pepo wametutii tulipolitaja jina lako.” Yeye akawaambia, “Nilimwona Shetani jinsi alivyokuwa anaporomoka kama umeme kutoka mbinguni. Naam, nimewapeni uwezo wa kukanyaga nyoka na nge, na uwezo juu ya nguvu zote za yule adui; hakuna chochote kitakachowadhuru. Hata hivyo, msifurahi kwa sababu pepo wamewatii, bali furahini kwa sababu majina yenu yameandikwa mbinguni.” Saa ileile, Yesu akafurahi kwa uwezo wa Roho Mtakatifu, akasema, “Nakushukuru ee Baba, Bwana wa mbingu na dunia, maana umewaficha wenye hekima na wenye elimu mambo haya, ukawafumbulia wadogo. Naam, Baba, ndivyo ilivyokupendeza.” Kisha akasema, “Baba yangu amenikabidhi vitu vyote. Hakuna amjuaye Mwana ila Baba, wala amjuaye Baba ila Mwana, na yeyote yule ambaye Mwana atapenda kumfunulia.” Halafu akawaelekea wafuasi wake akawaambia, “Heri wanaoona yale mnayoyaona nyinyi! Hakika, manabii na wafalme walitamani kuona yale mnayoyaona nyinyi wasiyaone, na kusikia yale mnayoyasikia wasiyasikie.” Baadaye mwanasheria mmoja alisimama, akamwuliza akitaka kumtega, “Mwalimu, nifanye nini ili nipate uhai wa milele?” Yeye akamwuliza, “Imeandikwa nini katika sheria? Unaelewaje?” Akamjibu, “Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, kwa roho yako yote, kwa nguvu zako zote na kwa akili yako yote. Na, mpende jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe.” Yesu akamwambia, “Vema! Fanya hivyo, nawe utaishi.” Lakini yeye akitaka kujihakikishia kuwa mwema akamwuliza Yesu, “Na jirani yangu ni nani?” Yesu akamjibu, “Mtu mmoja alikuwa anashuka kutoka Yerusalemu kwenda Yeriko. Alipokuwa njiani, alivamiwa na majambazi, wakamnyanganya mali yake na kumpiga, wakamwacha amelala pale nusu mfu. Kumbe, kuhani mmoja akawa anapita barabara ileile, akamwona, akapita kando. Hali kadhalika na Mlawi mmoja, alipofika mahali hapo akamwona, akapita kando. Lakini Msamaria mmoja aliyekuwa anasafiri, alifika pale yule mtu alipokuwa, naye alipomwona, alimwonea huruma. Akamwendea, akamtibu majeraha yake kwa kumtia mafuta na divai na kuyafunga; halafu akampandisha juu ya punda wake, akampeleka katika nyumba moja ya wageni akamwuguza. Kesho yake akatoa fedha dinari mbili akampa yule mwenye nyumba, akamwambia, ‘Mwuguze mtu huyu; na chochote utakachotumia zaidi, nitakulipa nitakaporudi.’” Kisha Yesu akauliza, “Kati ya hao watatu, ni yupi aliyeonesha kuwa jirani yake yule aliyevamiwa na majambazi?” Yule mwalimu wa sheria akamjibu, “Ni yule aliyemwonea huruma.” Yesu akamwambia, “Nenda ukafanye vivyo hivyo.”
Luka 10:13-37 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ole wako Korazini! Ole wako, Bethsaida! Kwa kuwa kama miujiza hiyo iliyofanyika kwenu ingalifanyika katika Tiro na Sidoni, wangalitubu tangu hapo, huku wakikaa katika nguo za magunia na majivu. Lakini, siku ya hukumu itakuwa rahisi Tiro na Sidoni kustahimili adhabu zake kuliko ninyi. Nawe Kapernaumu, je! Utakuzwa hata mbinguni? Utashushwa hata kuzimu. Awasikilizaye ninyi anisikiliza mimi, naye awakataaye ninyi anikataa mimi; naye anikataaye mimi amkataa yeye aliyenituma. Ndipo wale sabini waliporudi kwa furaha, wakisema, Bwana, hata pepo wanatutii kwa jina lako. Akawaambia, Nilimwona Shetani, akianguka kutoka mbinguni kama umeme. Tazama, nimewapa amri ya kukanyaga nyoka na nge, na nguvu zote za yule adui, wala hakuna kitu kitakachowadhuru. Lakini, msifurahi kwa vile pepo wanavyowatii; bali furahini kwa sababu majina yenu yameandikwa mbinguni. Saa ile ile alishangilia katika Roho Mtakatifu, akasema, Nakushukuru, Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa mambo haya umewaficha wenye hekima na akili; umewafunulia watoto wachanga; Naam, Baba, kwa kuwa ndivyo ilivyokupendeza. Akasema, Nimekabidhiwa vyote na Baba yangu, wala hakuna amjuaye Mwana ila Baba; wala hakuna amjuaye Baba ila Mwana, na yeyote ambaye Mwana apenda kumfunulia. Akawageukia wanafunzi wake, akasema nao kwa faragha, Heri macho yaonayo mnayoyaona ninyi. Kwa kuwa nawaambia ya kwamba manabii wengi na wafalme walitamani kuyaona mnayoyaona ninyi wasiyaone; na kuyasikia mnayoyasikia ninyi wasiyasikie. Na tazama, mwanasheria mmoja alisimama amjaribu; akisema, Mwalimu, nifanye nini ili niurithi uzima wa milele? Akamwambia, Imeandikwa nini katika torati? Wasomaje? Akajibu akasema, Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote, na kwa akili zako zote; na jirani yako kama nafsi yako. Akamwambia, Umejibu vema; fanya hivi nawe utaishi. Naye akitaka kujidai haki, alimwuliza Yesu, Na jirani yangu ni nani? Yesu akajibu akasema, Mtu mmoja alishuka toka Yerusalemu kwenda Yeriko, akaangukia kati ya wanyang'anyi; wakamvua nguo, wakamtia jeraha, wakaenda zao, wakamwacha akiwa karibu kufa. Kwa nasibu kuhani mmoja alishuka kwa njia ile; na alipomwona alipita kando. Na Mlawi vivyo hivyo, alipofika pale akamwona, akapita kando. Lakini, Msamaria mmoja katika kusafiri kwake alifika hapo alipokuwa; na alipomwona alimhurumia, akakaribia, akamfunga majeraha yake, akayatia mafuta na divai; akampandisha juu ya mnyama wake, akampeleka mpaka nyumba ya wageni, akamtunza. Hata siku ya pili akatoa dinari mbili, akampa mwenye nyumba ya wageni, akisema, Mtunze huyu, na chochote utakachogharimiwa zaidi, mimi nitakaporudi nitakulipa. Waonaje wewe, katika hao watatu, ni yupi aliyekuwa jirani yake yule aliyeangukia kati ya wanyang'anyi? Akasema, Ni huyo aliyemwonea huruma. Yesu akamwambia, Nenda zako, nawe ukafanye vivyo hivyo.
Luka 10:13-37 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ole wako Korazini! Ole wako, Bethsaida! Kwa kuwa kama miujiza hiyo iliyofanyika kwenu ingalifanyika katika Tiro na Sidoni, wangalitubu tangu hapo, huku wakiketi katika nguo za kigunia na majivu. Lakini, siku ya hukumu itakuwa rahisi Tiro na Sidoni kustahimili adhabu zake kuliko ninyi. Nawe Kapernaumu, je! Utakuzwa hata mbinguni? Utashushwa hata kuzimu. Awasikilizaye ninyi anisikiliza mimi, naye awakataaye ninyi anikataa mimi; naye anikataaye mimi amkataa yeye aliyenituma. Ndipo wale sabini waliporudi kwa furaha, wakisema, Bwana, hata pepo wanatutii kwa jina lako. Akawaambia, Nilimwona Shetani, akianguka kutoka mbinguni kama umeme. Tazama, nimewapa amri ya kukanyaga nyoka na nge, na nguvu zote za yule adui, wala hakuna kitu kitakachowadhuru. Lakini, msifurahi kwa vile pepo wanavyowatii; bali furahini kwa sababu majina yenu yameandikwa mbinguni. Saa ile ile alishangilia kwa Roho Mtakatifu, akasema, Nakushukuru, Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa mambo haya umewaficha wenye hekima na akili; umewafunulia watoto wachanga; Naam, Baba, kwa kuwa ndivyo ilivyokupendeza. Akasema, Nimekabidhiwa vyote na Baba yangu, wala hakuna amjuaye Mwana ila Baba; wala hakuna amjuaye Baba ila Mwana, na ye yote ambaye Mwana apenda kumfunulia. Akawageukia wanafunzi wake, akasema nao kwa faragha, Heri macho yaonayo mnayoyaona ninyi. Kwa kuwa nawaambia ya kwamba manabii wengi na wafalme walitamani kuyaona mnayoyaona ninyi wasiyaone; na kuyasikia mnayoyasikia ninyi wasiyasikie. Na tazama, mwana-sheria mmoja alisimama amjaribu; akisema, Mwalimu, nifanye nini ili niurithi uzima wa milele? Akamwambia, Imeandikwa nini katika torati? Wasomaje? Akajibu akasema, Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote, na kwa akili zako zote; na jirani yako kama nafsi yako. Akamwambia, Umejibu vema; fanya hivi nawe utaishi. Naye akitaka kujidai haki, alimwuliza Yesu, Na jirani yangu ni nani? Yesu akajibu akasema, Mtu mmoja alishuka toka Yerusalemu kwenda Yeriko, akaangukia kati ya wanyang’anyi; wakamvua nguo, wakamtia jeraha, wakaenda zao, wakimwacha karibu ya kufa. Kwa nasibu kuhani mmoja alishuka kwa njia ile; na alipomwona alipita kando. Na Mlawi vivyo hivyo, alipofika pale akamwona, akapita kando. Lakini, Msamaria mmoja katika kusafiri kwake alifika hapo alipo; na alipomwona alimhurumia, akakaribia, akamfunga jeraha zake, akizitia mafuta na divai; akampandisha juu ya mnyama wake, akampeleka mpaka nyumba ya wageni, akamtunza. Hata siku ya pili akatoa dinari mbili, akampa mwenye nyumba ya wageni, akisema, Mtunze huyu, na cho chote utakachogharimiwa zaidi, mimi nitakaporudi nitakulipa. Waonaje wewe, katika hao watatu, ni yupi aliyekuwa jirani yake yule aliyeangukia kati ya wanyang’anyi? Akasema, Ni huyo aliyemwonea huruma. Yesu akamwambia, Enenda zako, nawe ukafanye vivyo hivyo.
Luka 10:13-37 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
“Ole wako Korazini! Ole wako Bethsaida! Kwa kuwa kama miujiza iliyofanyika kwenu ingefanyika Tiro na Sidoni, miji hiyo ingekuwa imetubu zamani, kwa kuvaa magunia na kujipaka majivu. Lakini itakuwa rahisi zaidi kwa Tiro na Sidoni kustahimili katika siku ya hukumu, kuliko ninyi. Nawe Kapernaumu, je, utainuliwa hadi mbinguni? La hasha! Utashushwa hadi Kuzimu. “Yeye awasikilizaye ninyi anisikiliza mimi; naye awakataaye ninyi amenikataa mimi. Lakini yeye anikataaye mimi amkataa yeye aliyenituma.” Wale sabini na wawili wakarudi kwa furaha, na kusema, “Bwana Isa, hata pepo wachafu wanatutii kwa jina lako.” Isa akawaambia, “Nilimwona Shetani akianguka kutoka mbinguni kama radi. Tazama nimewapa mamlaka ya kukanyaga nyoka na nge na juu ya nguvu zote za adui; wala hakuna kitu chochote kitakachowadhuru. Basi, msifurahi kwa kuwa pepo wachafu wanawatii, bali furahini kwa kuwa majina yenu yameandikwa mbinguni.” Wakati huo Isa akashangilia katika Roho wa Mungu, akasema, “Nakuhimidi Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa umewaficha mambo haya wenye hekima na wenye elimu, nawe ukawafunulia watoto wadogo. Naam, Baba, kwa kuwa hivyo ndivyo ilivyokupendeza. “Nimekabidhiwa vitu vyote na Baba yangu. Hakuna mtu amjuaye Mwana ni nani ila Baba, wala hakuna amjuaye Baba ni nani ila Mwana na yeyote ambaye Mwana anapenda kumfunulia.” Basi Isa akawageukia wanafunzi wake akanena nao faraghani, akawaambia, “Heri macho yanayoona yale mambo mnayoyaona. Kwa maana nawaambia, manabii wengi na wafalme walitamani kuona yale mnayoyaona lakini hawakuyaona, na walitamani kusikia yale mnayoyasikia lakini hawakuyasikia.” Wakati huo mtaalamu mmoja wa Torati alisimama ili kumjaribu Isa, akamuuliza, “Mwalimu, nifanye nini ili niurithi uzima wa milele?” Isa akamjibu, “Imeandikwaje katika Torati? Kwani unasoma nini humo?” Akajibu, “ ‘Mpende Mwenyezi Mungu, Mungu wako, kwa moyo wako wote, kwa roho yako yote, kwa nguvu zako zote, na kwa akili zako zote’; tena, ‘Mpende jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe.’” Isa akamwambia, “Umejibu vyema. Fanya hivyo nawe utaishi.” Lakini yule mtaalamu wa Torati, akitaka kujionesha kuwa mwenye haki, akamuuliza Isa, “Jirani yangu ni nani?” Isa akamjibu akasema, “Mtu mmoja alikuwa akiteremka kutoka Yerusalemu kwenda Yeriko, naye akaangukia mikononi mwa wanyang’anyi. Wakampiga, wakaondoka, wakamwacha akiwa karibu kufa. Kuhani mmoja alikuwa akipitia njia ile, alipomwona huyo mtu, akapita upande mwingine, akamwacha hapo barabarani. Vivyo hivyo, Mlawi mmoja naye alipofika mahali pale, alimwona, akapita upande mwingine, akamwacha hapo barabarani. Lakini Msamaria mmoja aliyekuwa akisafiri alipomwona, alimhurumia. Akaenda alipokuwa na akasafisha majeraha yake kwa divai na mafuta, kisha akayafunga. Ndipo akampandisha kwenye punda wake, akampeleka hadi kwenye nyumba ya wageni na kumtunza. Kesho yake, yule Msamaria akachukua dinari mbili akampa yule mwenye nyumba ya wageni na kusema, ‘Mtunze, nami nirudipo nitakulipa gharama yoyote ya ziada uliyotumia kwa ajili yake.’ “Ni yupi basi miongoni mwa hawa watatu wewe unadhani ni jirani yake yule mtu aliyeangukia mikononi mwa wanyang’anyi?” Yule mtaalamu wa Torati akajibu, “Ni yule aliyemhurumia.” Ndipo Isa akamwambia, “Nenda, ukafanye vivyo hivyo.”