Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Luka 1:8-38

Luka 1:8-38 Biblia Habari Njema (BHN)

Siku moja, ilipokuwa zamu yake kutoa huduma ya ukuhani mbele ya Mungu, Zakaria alichaguliwa kwa kura, kama ilivyokuwa desturi, kuingia hekaluni ili afukize ubani. Watu, umati mkubwa, walikuwa wamekusanyika nje wanasali wakati huo wa kufukiza ubani. Malaika wa Bwana akamtokea humo ndani, akasimama upande wa kulia wa madhabahu ya kufukizia ubani. Zakaria alipomwona alifadhaika, hofu ikamwingia. Lakini malaika akamwambia, “Zakaria, usiogope, kwa maana sala yako imesikilizwa, na Elisabeti mkeo atakuzalia mtoto wa kiume, nawe utampa jina Yohane. Utakuwa na furaha kubwa na watu wengi watashangilia kwa sababu ya kuzaliwa kwake. Atakuwa mkubwa mbele ya Bwana. Hatakunywa divai wala kileo, atajazwa Roho Mtakatifu tangu tumboni mwa mama yake. Atawaelekeza wengi wa watu wa Israeli kwa Bwana Mungu wao. Atamtangulia Bwana akiongozwa na nguvu na roho kama ya Elia. Atawapatanisha kina baba na watoto wao; atawafanya wasiotii wawe na fikira za uadilifu, na hivyo amtayarishie Bwana watu wake.” Zakaria akamwambia huyo malaika, “Ni kitu gani kitakachonihakikishia jambo hilo? Mimi ni mzee, hali kadhalika na mke wangu.” Malaika akamjibu, “Mimi ni Gabrieli, nisimamaye mbele ya Mungu; nimetumwa niseme nawe, nikuletee hizi habari njema. Sikiliza, utakuwa bubu kwa sababu huyasadiki haya maneno yatakayotimia kwa wakati wake. Hutaweza kusema mpaka hayo niliyokuambia yatakapotimia.” Wakati huo, wale watu walikuwa wanamngoja Zakaria huku wakishangaa juu ya kukawia kwake hekaluni. Alipotoka nje, hakuweza kusema nao. Ikawa dhahiri kwao kwamba alikuwa ameona maono hekaluni. Lakini akawa anawapa ishara kwa mikono, akabaki bubu. Zamu yake ya kuhudumu ilipokwisha, alirudi nyumbani. Baadaye Elisabeti mkewe akapata mimba. Akajificha nyumbani kwa muda wa miezi mitano, akisema: “Hivi ndivyo alivyonitendea Bwana; ameniangalia na kuniondolea aibu niliyokuwa nayo mbele ya watu.” Mnamo mwezi wa sita, malaika Gabrieli alitumwa na Mungu aende kwenye mji uitwao Nazareti huko Galilaya, kwa msichana mmoja bikira aitwaye Maria, mchumba wa mtu mmoja jina lake Yosefu, wa ukoo wa Daudi. Malaika akamwendea, akamwambia, “Salamu, ewe uliyejaliwa neema na Mungu! Bwana yuko nawe!” Maria aliposikia maneno hayo alifadhaika sana, akawaza: Maneno hayo yanamaanisha nini? Malaika akamwambia, “Usiogope Maria, kwa maana Mungu amekujalia neema. Utachukua mimba, utamzaa mtoto wa kiume, nawe utampa jina Yesu. Yeye atakuwa mkubwa na ataitwa Mwana wa Mungu Mkuu. Bwana Mungu atampa kiti cha mfalme Daudi, babu yake. Kwa hivyo atautawala ukoo wa Yakobo milele, na ufalme wake hautakuwa na mwisho.” Maria akamjibu, “Yatawezekanaje hayo, hali mimi ni bikira?” Malaika akamjibu, “Roho Mtakatifu atakushukia, na uwezo wake Mungu Mkuu utakujia kama kivuli; kwa sababu hiyo, mtoto atakayezaliwa ataitwa Mtakatifu, Mwana wa Mungu. Ujue pia kwamba hata Elisabeti, jamaa yako, naye amepata mimba ingawa ni mzee, na sasa ni mwezi wa sita kwake yeye ambaye watu walimfahamu kuwa tasa. Kwa maana hakuna jambo lisilowezekana kwa Mungu.” Maria akasema, “Mimi ni mtumishi wa Bwana, nitendewe kama ulivyosema.” Kisha yule malaika akaenda zake.

Shirikisha
Soma Luka 1

Luka 1:8-38 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Basi ikawa, alipokuwa akifanya kazi ya ukuhani wakati wa zamu yake mbele za Mungu, kama ilivyokuwa desturi ya ukuhani, kura ilimwangukia kuingia katika hekalu la Bwana ili kufukiza uvumba. Na makutano yote ya watu walikuwa wakisali nje saa ya kufukiza uvumba. Akatokewa na malaika wa Bwana, amesimama upande wa kulia wa madhabahu ya kufukizia. Zakaria alipomwona alifadhaika, hofu ikamwingia. Lakini yule malaika akamwambia, Usiogope, Zakaria, maana dua yako imesikiwa, na mkeo Elisabeti atakuzalia mtoto wa kiume, na jina lake utamwita Yohana. Nawe utakuwa na furaha na shangwe, na watu wengi watakufurahia kuzaliwa kwake. Kwa sababu atakuwa mkuu mbele za Bwana; hatakunywa divai wala kileo; naye atajazwa Roho Mtakatifu hata tangu tumboni mwa mamaye. Na wengi katika Waisraeli atawarejesha kwa Bwana Mungu wao. Naye atatangulia mbele zake katika roho ya Eliya, na nguvu zake, ili kuigeuza mioyo ya baba iwaelekee watoto, na kuwatilia waasi akili za wenye haki, na kumwekea Bwana tayari watu waliotayarishwa. Zakaria akamwambia malaika, Nitajuaje neno hilo? Maana mimi ni mzee, na mke wangu ni mkongwe wa siku nyingi. Malaika akamjibu akamwambia, Mimi ni Gabrieli, nisimamaye mbele za Mungu; nami nimetumwa niseme nawe, na kukupasha habari hizi njema. Na tazama! Utakuwa bubu, usiweze kusema, mpaka siku ile yatakapotukia hayo, kwa sababu hukuyasadiki maneno yangu; nayo yatatimizwa kwa wakati wake. Na wale watu walikuwa wakimngojea Zakaria, wakastaajabia kukawia kwake mle hekaluni. Alipotoka akiwa hawezi kusema nao, walitambua ya kuwa ameona maono ndani ya hekalu, naye aliendelea kuwaashiria akakaa bubu. Ikawa siku za huduma yake zilipokuwa zimetimia akaenda nyumbani kwake. Hata baada ya siku zile mkewe Elisabeti alichukua mimba akatawa miezi mitano, akisema, Hivi ndivyo alivyonitendea Bwana katika siku zile alizoniangalia ili kuniondolea aibu yangu mbele ya watu. Mwezi wa sita, malaika Gabrieli alitumwa na Mungu kwenda mpaka katika mji wa Galilaya, jina lake Nazareti, kwa mwanamwali bikira aliyekuwa ameposwa na mtu, jina lake Yusufu, wa ukoo wa Daudi; na jina lake bikira huyo ni Mariamu. Akaingia nyumbani kwake akasema, Salamu, uliyepewa neema, Bwana yu pamoja nawe. Naye akafadhaika sana kwa ajili ya maneno yake, akawaza moyoni, Salamu hii ni ya namna gani? Malaika akamwambia, Usiogope, Mariamu, kwa maana umepata neema kwa Mungu. Tazama, utachukua mimba na kuzaa mtoto wa kiume; na jina lake utamwita Yesu. Huyo atakuwa mkuu, ataitwa Mwana wa Aliye Juu, na Bwana Mungu atampa kiti cha enzi cha Daudi, baba yake. Ataimiliki nyumba ya Yakobo hata milele, na ufalme wake utakuwa hauna mwisho. Mariamu akamwambia malaika, Litakuwaje neno hili, maana sijui mume? Malaika akajibu akamwambia, Roho Mtakatifu atakujia juu yako, na nguvu zake Aliye Juu zitakufunika kama kivuli; kwa sababu hiyo hicho kitakachozaliwa kitaitwa kitakatifu, Mwana wa Mungu. Tena, tazama, jamaa yako Elisabeti naye amechukua mimba ya mtoto wa kiume katika uzee wake; na mwezi huu ni wa sita kwake yeye aliyeitwa tasa; kwa kuwa hakuna neno lisilowezekana kwa Mungu. Mariamu akasema, Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana; na iwe kwangu kama ulivyosema. Kisha malaika akaondoka akaenda zake.

Shirikisha
Soma Luka 1

Luka 1:8-38 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Basi ikawa, alipokuwa akifanya kazi ya ukuhani katika taratibu ya zamu yake mbele za Mungu, kama ilivyokuwa desturi ya ukuhani, kura ilimwangukia kuingia katika hekalu la Bwana ili kufukiza uvumba. Na makutano yote ya watu walikuwa wakisali nje saa ya kufukiza uvumba. Akatokewa na malaika wa Bwana, amesimama upande wa kuume wa madhabahu ya kufukizia. Zakaria alipomwona alifadhaika, hofu ikamwingia. Lakini yule malaika akamwambia, Usiogope, Zakaria, maana dua yako imesikiwa, na mkeo Elisabeti atakuzalia mtoto mwanamume, na jina lake utamwita Yohana. Nawe utakuwa na furaha na shangwe, na watu wengi watakufurahia kuzaliwa kwake. Kwa sababu atakuwa mkuu mbele za Bwana; hatakunywa divai wala kileo; naye atajazwa Roho Mtakatifu hata tangu tumboni mwa mamaye. Na wengi katika Waisraeli atawarejeza kwa Bwana Mungu wao. Naye atatangulia mbele zake katika roho ya Eliya, na nguvu zake, ili kuigeuza mioyo ya baba iwaelekee watoto, na kuwatilia waasi akili za wenye haki, na kumwekea Bwana tayari watu waliotengenezwa. Zakaria akamwambia malaika, Nitajuaje neno hilo? Maana mimi ni mzee, na mke wangu ni mkongwe wa siku nyingi. Malaika akamjibu akamwambia, Mimi ni Gabrieli, nisimamaye mbele za Mungu; nami nimetumwa niseme nawe, na kukupasha habari hizi njema. Na tazama! Utakuwa bubu, usiweze kusema, mpaka siku ile yatakapotukia hayo, kwa sababu hukuyasadiki maneno yangu; nayo yatatimizwa kwa wakati wake. Na wale watu walikuwa wakimngojea Zakaria, wakastaajabia kukawia kwake mle hekaluni. Alipotoka hali hawezi kusema nao, walitambua ya kuwa ameona maono ndani ya hekalu, naye aliendelea kuwaashiria akakaa bubu. Ikawa siku za huduma yake zilipokuwa zimetimia akaenda nyumbani kwake. Hata baada ya siku zile mkewe Elisabeti alichukua mimba akatawa miezi mitano, akisema, Hivi ndivyo alivyonitendea Bwana katika siku zile alizoniangalia ili kuniondolea aibu yangu mbele ya watu. Mwezi wa sita, malaika Gabrieli alitumwa na Mungu kwenda mpaka mji wa Galilaya, jina lake Nazareti, kwa mwanamwali bikira aliyekuwa ameposwa na mtu, jina lake Yusufu, wa mbari ya Daudi; na jina lake bikira huyo ni Mariamu. Akaingia nyumbani kwake akasema, Salamu, uliyepewa neema, Bwana yu pamoja nawe. Naye akafadhaika sana kwa ajili ya maneno yake, akawaza moyoni, Salamu hii ni ya namna gani? Malaika akamwambia, Usiogope, Mariamu, kwa maana umepata neema kwa Mungu. Tazama, utachukua mimba na kuzaa mtoto mwanamume; na jina lake utamwita Yesu. Huyo atakuwa mkuu, ataitwa Mwana wa Aliye juu, na Bwana Mungu atampa kiti cha enzi cha Daudi, baba yake. Ataimiliki nyumba ya Yakobo hata milele, na ufalme wake utakuwa hauna mwisho. Mariamu akamwambia malaika, Litakuwaje neno hili, maana sijui mume? Malaika akajibu akamwambia, Roho Mtakatifu atakujilia juu yako, na nguvu zake Aliye juu zitakufunika kama kivuli; kwa sababu hiyo hicho kitakachozaliwa kitaitwa kitakatifu, Mwana wa Mungu. Tena, tazama, jamaa yako Elisabeti naye amechukua mimba ya mtoto mwanamume katika uzee wake; na mwezi huu ni wa sita kwake yeye aliyeitwa tasa; kwa kuwa hakuna neno lisilowezekana kwa Mungu. Mariamu akasema, Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana; na iwe kwangu kama ulivyosema. Kisha malaika akaondoka akaenda zake.

Shirikisha
Soma Luka 1

Luka 1:8-38 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Siku moja ilipokuwa zamu ya kikundi cha Zekaria, yeye akifanya kazi ya ukuhani Hekaluni mbele za Mungu, alichaguliwa kwa kura kwa kufuata desturi za ukuhani, kuingia Hekaluni mwa Bwana ili kufukiza uvumba. Nao wakati wa kufukiza uvumba ulipowadia, wale wote waliokuwa wamekusanyika ili kuabudu walikuwa nje wakiomba. Ndipo malaika wa Bwana, akiwa amesimama upande wa kuume wa madhabahu ya kufukizia uvumba, akamtokea Zekaria. Zekaria alipomwona huyo malaika, akafadhaika sana, akajawa na hofu. Lakini malaika akamwambia, “Usiogope, Zekaria, kwa maana Mungu amesikia maombi yako. Mkeo Elizabeti atakuzalia mtoto wa kiume, nawe utamwita jina lake Yohana. Yeye atakuwa furaha na shangwe kwako, nao watu wengi watashangilia kwa sababu ya kuzaliwa kwake. Kwa kuwa atakuwa mkuu mbele za Bwana, kamwe hataonja mvinyo wala kinywaji chochote cha kulevya, naye atajazwa Roho Mtakatifu hata kabla ya kuzaliwa kwake. Naye atawageuza wengi wa wana wa Israeli warudi kwa Bwana Mungu wao. Naye atatangulia mbele za Bwana katika roho na nguvu ya Eliya, ili kuigeuza mioyo ya baba kuwaelekea watoto wao, na wasiotii warejee katika hekima ya wenye haki, ili kuliweka tayari taifa lililoandaliwa kwa ajili ya Bwana.” Zekaria akamuuliza malaika, “Jambo hilo linawezekanaje? Mimi ni mzee na mke wangu pia ana umri mkubwa.” Malaika akamjibu, akamwambia, “Mimi ni Gabrieli, nisimamaye mbele za Mungu, nami nimetumwa kwako ili nikuambie habari hizi njema. Basi sasa kwa kuwa hujaamini maneno yangu ambayo yatatimizwa kwa wakati wake, utakuwa bubu hadi siku ile mambo haya yatakapotukia.” Wakati huo watu walikuwa wanamngojea Zekaria nje huku wakishangaa kukawia kwake mle Hekaluni. Alipotoka akawa hawezi kusema nao, wao wakatambua kuwa ameona maono ndani ya Hekalu. Lakini kwa kuwa alikuwa bubu, akawa anawaashiria kwa mikono. Muda wake wa kuhudumu Hekaluni ulipomalizika, akarudi nyumbani kwake. Baada ya muda usio mrefu, Elizabeti mkewe akapata mimba, naye akajitenga kwa miezi mitano. Akasema, “Hili ndilo Bwana alilonitendea aliponiangalia kwa upendeleo na kuniondolea aibu yangu mbele ya watu.” Mwezi wa sita baada ya Elizabeti kupata mimba, Mungu alimtuma malaika Gabrieli aende Galilaya katika mji wa Nazareti, kwa mwanamwali bikira aliyekuwa ameposwa na mtu mmoja jina lake Yosefu wa nyumba ya Daudi. Jina la huyu mwanamwali bikira ni Maria. Naye malaika akaja kwake akamwambia: “Salamu, wewe uliyebarikiwa, Bwana yu pamoja nawe!” Maria akafadhaishwa sana na maneno haya, akajiuliza moyoni, “Salamu hii ni ya namna gani?” Ndipo malaika akamwambia, “Usiogope, Maria, umepata kibali kwa Mungu. Tazama, utachukua mimba, nawe utamzaa mtoto mwanaume na utamwita jina lake Yesu. Yeye atakuwa mkuu, naye ataitwa Mwana wa Aliye Juu Sana. BWANA Mungu atampa kiti cha enzi cha Daudi baba yake. Ataimiliki nyumba ya Yakobo milele, na ufalme wake hautakuwa na mwisho.” Maria akamuuliza huyo malaika, “Maadamu mimi ni bikira, jambo hili litawezekanaje?” Malaika akamjibu, “Roho Mtakatifu atakujilia juu yako, nazo nguvu zake Yeye Aliye Juu Sana zitakufunika kama kivuli. Kwa hiyo mtoto atakayezaliwa atakuwa mtakatifu, naye ataitwa Mwana wa Mungu. Tazama, jamaa yako Elizabeti amechukua mimba katika uzee wake, na huu ni mwezi wake wa sita, yeye aliyeitwa tasa. Kwa maana kwa Mungu hakuna lisilowezekana.” Maria akasema, “Tazama, mimi ni mtumishi wa Bwana. Na iwe kwangu kama ulivyosema.” Kisha malaika akaondoka, akamwacha.

Shirikisha
Soma Luka 1