Luka 1:3-80
Luka 1:3-80 Biblia Habari Njema (BHN)
Inafaa nami pia, Mheshimiwa, baada ya kuchunguza kwa makini mambo yote tangu mwanzo, nikuandikie kwa mpango, ili nawe uweze kujionea mwenyewe ukweli wa mambo yale uliyofundishwa. Wakati Herode alipokuwa mfalme wa Yudea, kulikuwa na kuhani mmoja jina lake Zakaria, wa kikundi cha ukuhani cha Abiya. Mke wake alikuwa anaitwa Elisabeti, naye alikuwa wa ukoo wa kuhani Aroni. Wote wawili walikuwa wanyofu mbele ya Mungu, wakiishi kwa kufuata amri na maagizo yote ya Bwana bila lawama. Lakini hawakuwa wamejaliwa watoto kwa vile Elisabeti alikuwa tasa, nao wote wawili walikuwa wazee sana. Siku moja, ilipokuwa zamu yake kutoa huduma ya ukuhani mbele ya Mungu, Zakaria alichaguliwa kwa kura, kama ilivyokuwa desturi, kuingia hekaluni ili afukize ubani. Watu, umati mkubwa, walikuwa wamekusanyika nje wanasali wakati huo wa kufukiza ubani. Malaika wa Bwana akamtokea humo ndani, akasimama upande wa kulia wa madhabahu ya kufukizia ubani. Zakaria alipomwona alifadhaika, hofu ikamwingia. Lakini malaika akamwambia, “Zakaria, usiogope, kwa maana sala yako imesikilizwa, na Elisabeti mkeo atakuzalia mtoto wa kiume, nawe utampa jina Yohane. Utakuwa na furaha kubwa na watu wengi watashangilia kwa sababu ya kuzaliwa kwake. Atakuwa mkubwa mbele ya Bwana. Hatakunywa divai wala kileo, atajazwa Roho Mtakatifu tangu tumboni mwa mama yake. Atawaelekeza wengi wa watu wa Israeli kwa Bwana Mungu wao. Atamtangulia Bwana akiongozwa na nguvu na roho kama ya Elia. Atawapatanisha kina baba na watoto wao; atawafanya wasiotii wawe na fikira za uadilifu, na hivyo amtayarishie Bwana watu wake.” Zakaria akamwambia huyo malaika, “Ni kitu gani kitakachonihakikishia jambo hilo? Mimi ni mzee, hali kadhalika na mke wangu.” Malaika akamjibu, “Mimi ni Gabrieli, nisimamaye mbele ya Mungu; nimetumwa niseme nawe, nikuletee hizi habari njema. Sikiliza, utakuwa bubu kwa sababu huyasadiki haya maneno yatakayotimia kwa wakati wake. Hutaweza kusema mpaka hayo niliyokuambia yatakapotimia.” Wakati huo, wale watu walikuwa wanamngoja Zakaria huku wakishangaa juu ya kukawia kwake hekaluni. Alipotoka nje, hakuweza kusema nao. Ikawa dhahiri kwao kwamba alikuwa ameona maono hekaluni. Lakini akawa anawapa ishara kwa mikono, akabaki bubu. Zamu yake ya kuhudumu ilipokwisha, alirudi nyumbani. Baadaye Elisabeti mkewe akapata mimba. Akajificha nyumbani kwa muda wa miezi mitano, akisema: “Hivi ndivyo alivyonitendea Bwana; ameniangalia na kuniondolea aibu niliyokuwa nayo mbele ya watu.” Mnamo mwezi wa sita, malaika Gabrieli alitumwa na Mungu aende kwenye mji uitwao Nazareti huko Galilaya, kwa msichana mmoja bikira aitwaye Maria, mchumba wa mtu mmoja jina lake Yosefu, wa ukoo wa Daudi. Malaika akamwendea, akamwambia, “Salamu, ewe uliyejaliwa neema na Mungu! Bwana yuko nawe!” Maria aliposikia maneno hayo alifadhaika sana, akawaza: Maneno hayo yanamaanisha nini? Malaika akamwambia, “Usiogope Maria, kwa maana Mungu amekujalia neema. Utachukua mimba, utamzaa mtoto wa kiume, nawe utampa jina Yesu. Yeye atakuwa mkubwa na ataitwa Mwana wa Mungu Mkuu. Bwana Mungu atampa kiti cha mfalme Daudi, babu yake. Kwa hivyo atautawala ukoo wa Yakobo milele, na ufalme wake hautakuwa na mwisho.” Maria akamjibu, “Yatawezekanaje hayo, hali mimi ni bikira?” Malaika akamjibu, “Roho Mtakatifu atakushukia, na uwezo wake Mungu Mkuu utakujia kama kivuli; kwa sababu hiyo, mtoto atakayezaliwa ataitwa Mtakatifu, Mwana wa Mungu. Ujue pia kwamba hata Elisabeti, jamaa yako, naye amepata mimba ingawa ni mzee, na sasa ni mwezi wa sita kwake yeye ambaye watu walimfahamu kuwa tasa. Kwa maana hakuna jambo lisilowezekana kwa Mungu.” Maria akasema, “Mimi ni mtumishi wa Bwana, nitendewe kama ulivyosema.” Kisha yule malaika akaenda zake. Siku kadhaa baadaye, Maria alifunga safari akaenda kwa haraka hadi mji mmoja ulioko katika milima ya Yudea. Huko, aliingia katika nyumba ya Zakaria, akamsalimu Elisabeti. Mara tu Elisabeti aliposikia sauti ya Maria, mtoto mchanga tumboni mwake Elisabeti akaruka. Naye Elisabeti akajazwa Roho Mtakatifu, akasema kwa sauti kubwa, “Umebarikiwa kuliko wanawake wote, naye utakayemzaa amebarikiwa. Mimi ni nani hata mama wa Bwana wangu afike kwangu? Nakuambia, mara tu niliposikia sauti yako, mtoto mchanga tumboni mwangu aliruka kwa furaha. Heri yako wewe uliyesadiki kwamba yatatimia yale Bwana aliyokuambia.” Naye Maria akasema, “Moyo wangu wamtukuza Bwana, roho yangu inafurahi kwa sababu ya Mungu Mwokozi wangu. Kwa kuwa amemwangalia kwa huruma mtumishi wake mnyenyekevu. Hivyo tangu sasa watu wote wataniita mwenye heri. Kwa kuwa Mungu Mwenye Nguvu amenifanyia makuu, jina lake ni takatifu. Huruma yake kwa watu wanaomcha hudumu kizazi hata kizazi. Amefanya mambo makuu kwa mkono wake: Amewatawanya wenye kiburi katika mawazo ya mioyo yao; amewashusha wenye nguvu kutoka viti vyao vya enzi, akawakweza wanyenyekevu. Wenye njaa amewashibisha mema, matajiri amewaondoa mikono mitupu. Amemsaidia Israeli mtumishi wake, akikumbuka huruma yake, kama alivyowaahidia wazee wetu, Abrahamu na wazawa wake hata milele.” Maria alikaa na Elisabeti kwa muda upatao miezi mitatu, halafu akarudi nyumbani kwake. Wakati wa kujifungua kwake Elisabeti ulifika, akajifungua mtoto wa kiume. Jirani na watu wa jamaa yake walipopata habari kwamba Bwana amemwonea huruma kubwa, walifurahi pamoja naye. Halafu siku ya nane walifika kumtahiri mtoto, wakataka kumpa jina la baba yake, Zakaria. Lakini mama yake akasema, “Sivyo, bali ataitwa Yohane.” Wakamwambia, “Mbona hakuna yeyote katika ukoo wake mwenye jina hilo?” Basi, wakamwashiria baba yake wapate kujua alitaka mtoto wake apewe jina gani. Naye akaomba kibao cha kuandikia, akaandika hivi: “Yohane ndilo jina lake.” Wote wakastaajabu. Papo hapo, midomo na ulimi wake Zakaria vikafunguliwa, akawa anaongea akimsifu Mungu. Hofu ikawaingia jirani wote, na habari hizo zikaenea kila mahali katika milima ya Yudea. Wote waliosikia mambo hayo, waliyatafakari mioyoni mwao wakisema: “Mtoto huyu atakuwa mtu wa namna gani?” Maana, hakika nguvu ya Bwana ilikuwa pamoja naye. Zakaria, baba yake mtoto, akajazwa Roho Mtakatifu, akatamka unabii huu: “Atukuzwe Bwana Mungu wa Israeli, kwani amewajia na kuwakomboa watu wake. Ametupatia Mwokozi shujaa, mzawa wa Daudi mtumishi wake. Aliahidi hapo kale kwa njia ya manabii wake watakatifu, kwamba atatuokoa mikononi mwa maadui zetu na kutoka mikononi mwa wote wanaotuchukia. Alisema atawahurumia wazee wetu, na kukumbuka agano lake takatifu. Alimwapia Abrahamu babu yetu, kwamba atatujalia sisi tukombolewe mikononi mwa maadui zetu, tupate kumtumikia bila hofu, tuwe wanyofu na waadilifu mbele yake, siku zote za maisha yetu. Nawe mwanangu, utaitwa, nabii wa Mungu Mkuu, utamtangulia Bwana kumtayarishia njia yake; kuwatangazia watu kwamba wataokolewa kwa kuondolewa dhambi zao. Mungu wetu ni mpole na mwenye huruma. Atatuchomozea mwanga kutoka juu, na kuwaangazia wote wanaokaa katika giza kuu la kifo, aongoze hatua zetu katika njia ya amani.” Mtoto akakua, akapata nguvu rohoni. Alikaa jangwani mpaka alipojionesha rasmi kwa watu wa Israeli.
Luka 1:3-80 Swahili Revised Union Version (SRUV)
nimeona vema mimi nami, kwa kuwa nimejitafutia usahihi wa mambo hayo yote tangu mwanzo, kukuandikia kwa taratibu, Theofilo mtukufu, upate kujua hakika ya mambo yale uliyofundishwa. Zamani za Herode, mfalme wa Yudea, palikuwa na kuhani mmoja, jina lake Zakaria, wa kikundi cha ukuhani cha Abiya, na mkewe alikuwa mmojawapo wa uzao wa Haruni, jina lake Elisabeti. Na wote wawili walikuwa wenye haki mbele za Mungu, wakiishi katika amri zote za Bwana na maagizo yake bila lawama. Nao walikuwa hawana mtoto, maana Elisabeti alikuwa tasa, na wote wawili ni wazee sana. Basi ikawa, alipokuwa akifanya kazi ya ukuhani wakati wa zamu yake mbele za Mungu, kama ilivyokuwa desturi ya ukuhani, kura ilimwangukia kuingia katika hekalu la Bwana ili kufukiza uvumba. Na makutano yote ya watu walikuwa wakisali nje saa ya kufukiza uvumba. Akatokewa na malaika wa Bwana, amesimama upande wa kulia wa madhabahu ya kufukizia. Zakaria alipomwona alifadhaika, hofu ikamwingia. Lakini yule malaika akamwambia, Usiogope, Zakaria, maana dua yako imesikiwa, na mkeo Elisabeti atakuzalia mtoto wa kiume, na jina lake utamwita Yohana. Nawe utakuwa na furaha na shangwe, na watu wengi watakufurahia kuzaliwa kwake. Kwa sababu atakuwa mkuu mbele za Bwana; hatakunywa divai wala kileo; naye atajazwa Roho Mtakatifu hata tangu tumboni mwa mamaye. Na wengi katika Waisraeli atawarejesha kwa Bwana Mungu wao. Naye atatangulia mbele zake katika roho ya Eliya, na nguvu zake, ili kuigeuza mioyo ya baba iwaelekee watoto, na kuwatilia waasi akili za wenye haki, na kumwekea Bwana tayari watu waliotayarishwa. Zakaria akamwambia malaika, Nitajuaje neno hilo? Maana mimi ni mzee, na mke wangu ni mkongwe wa siku nyingi. Malaika akamjibu akamwambia, Mimi ni Gabrieli, nisimamaye mbele za Mungu; nami nimetumwa niseme nawe, na kukupasha habari hizi njema. Na tazama! Utakuwa bubu, usiweze kusema, mpaka siku ile yatakapotukia hayo, kwa sababu hukuyasadiki maneno yangu; nayo yatatimizwa kwa wakati wake. Na wale watu walikuwa wakimngojea Zakaria, wakastaajabia kukawia kwake mle hekaluni. Alipotoka akiwa hawezi kusema nao, walitambua ya kuwa ameona maono ndani ya hekalu, naye aliendelea kuwaashiria akakaa bubu. Ikawa siku za huduma yake zilipokuwa zimetimia akaenda nyumbani kwake. Hata baada ya siku zile mkewe Elisabeti alichukua mimba akatawa miezi mitano, akisema, Hivi ndivyo alivyonitendea Bwana katika siku zile alizoniangalia ili kuniondolea aibu yangu mbele ya watu. Mwezi wa sita, malaika Gabrieli alitumwa na Mungu kwenda mpaka katika mji wa Galilaya, jina lake Nazareti, kwa mwanamwali bikira aliyekuwa ameposwa na mtu, jina lake Yusufu, wa ukoo wa Daudi; na jina lake bikira huyo ni Mariamu. Akaingia nyumbani kwake akasema, Salamu, uliyepewa neema, Bwana yu pamoja nawe. Naye akafadhaika sana kwa ajili ya maneno yake, akawaza moyoni, Salamu hii ni ya namna gani? Malaika akamwambia, Usiogope, Mariamu, kwa maana umepata neema kwa Mungu. Tazama, utachukua mimba na kuzaa mtoto wa kiume; na jina lake utamwita Yesu. Huyo atakuwa mkuu, ataitwa Mwana wa Aliye Juu, na Bwana Mungu atampa kiti cha enzi cha Daudi, baba yake. Ataimiliki nyumba ya Yakobo hata milele, na ufalme wake utakuwa hauna mwisho. Mariamu akamwambia malaika, Litakuwaje neno hili, maana sijui mume? Malaika akajibu akamwambia, Roho Mtakatifu atakujia juu yako, na nguvu zake Aliye Juu zitakufunika kama kivuli; kwa sababu hiyo hicho kitakachozaliwa kitaitwa kitakatifu, Mwana wa Mungu. Tena, tazama, jamaa yako Elisabeti naye amechukua mimba ya mtoto wa kiume katika uzee wake; na mwezi huu ni wa sita kwake yeye aliyeitwa tasa; kwa kuwa hakuna neno lisilowezekana kwa Mungu. Mariamu akasema, Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana; na iwe kwangu kama ulivyosema. Kisha malaika akaondoka akaenda zake. Basi, Mariamu akaondoka siku hizo, akaenda hadi katika nchi yenye milima kwa haraka mpaka mji mmoja wa Yudea, akaingia nyumbani kwa Zakaria akamwamkia Elisabeti. Ikawa Elisabeti aliposikia kule kuamkia kwake Mariamu, kitoto kichanga kikaruka ndani ya tumbo lake; Elisabeti akajazwa Roho Mtakatifu; akapaza sauti kwa nguvu akasema, Umebarikiwa wewe katika wanawake, naye mzao wa tumbo lako amebarikiwa. Limenitokeaje neno hili, hata mama wa Bwana wangu anijie mimi? Maana sauti ya kuamkia kwako ilipoingia masikioni mwangu, kitoto kichanga kikaruka kwa shangwe ndani ya tumbo langu. Naye heri aliyesadiki; kwa maana yatatimizwa aliyoambiwa na Bwana. Mariamu akasema, Moyo wangu wamwadhimisha Bwana, Na roho yangu imemfurahia Mungu, Mwokozi wangu; Kwa kuwa ameutazama Unyonge wa mjakazi wake. Kwa maana, tazama, tokea sasa Vizazi vyote wataniita mbarikiwa; Kwa kuwa Mwenye nguvu amenitendea makuu, Na jina lake ni takatifu. Na rehema zake hudumu vizazi hata vizazi Kwa hao wanaomcha. Amefanya nguvu kwa mkono wake; Amewatawanya walio na kiburi katika mawazo ya mioyo yao; Amewaangusha wakuu katika viti vyao vya enzi; Na wanyonge amewainua. Wenye njaa amewashibisha mema, Na wenye mali amewaondoa mikono mitupu. Amemsaidia Israeli, mtumishi wake; Ili kukumbuka rehema zake; Kama alivyowaambia baba zetu, Abrahamu na uzao wake hata milele. Mariamu akakaa naye kadiri ya miezi mitatu, kisha akarudi kwenda nyumbani kwake. Ikawa, siku za kuzaa kwake Elisabeti zilipotimia, alizaa mtoto mwanamume. Wakasikia jirani zake na jamaa zake ya kwamba Bwana amemwongezea rehema zake, wakafurahi pamoja naye. Ikawa siku ya nane wakaja kumtahiri mtoto; wakataka kumpa jina la babaye, Zakaria. Mamaye akajibu akasema La, sivyo; bali, ataitwa Yohana. Wakamwambia, Hapana mtu katika jamaa zako aitwaye jina hilo. Wakamwashiria babaye wajue atakavyo kumwita. Akataka kibao, akaandika ya kwamba, Jina lake ni Yohana. Wakastaajabu wote. Papo hapo kinywa chake kikafunguliwa na ulimi wake pia, akaanza kunena akimsifu Mungu. Wakaingiwa na hofu wote waliokuwa wakikaa karibu nao; na mambo hayo yote yakatangazwa katika nchi yote ya Yudea yenye milima. Na wote walioyasikia wakayaweka mioyoni mwao, wakisema, Mtoto huyu atakuwa wa namna gani? Kwa sababu mkono wa Bwana ulikuwa pamoja naye. Na Zakaria, baba yake, akajazwa Roho Mtakatifu, akatabiri, akisema, Atukuzwe Bwana, Mungu wa Israeli, Kwa kuwa amewajia watu wake, na kuwakomboa. Ametusimamishia pembe ya wokovu Katika mlango wa Daudi, mtumishi wake. Kama alivyosema tangu mwanzo Kwa kinywa cha manabii wake watakatifu; Tuokolewe na adui zetu Na mikononi mwao wote wanaotuchukia; Ili kuwatendea rehema baba zetu, Na kulikumbuka agano lake takatifu; Kiapo alichomwapia Abrahamu, baba yetu, Ya kwamba atatujalia sisi, Tuokoke mikononi mwa adui zetu, Na kumwabudu pasipo hofu, Kwa utakatifu na kwa haki Mbele zake siku zetu zote. Nawe, mtoto, utaitwa nabii wake Aliye Juu, Kwa maana utatangulia mbele za uso wa Bwana umtengenezee njia zake; Uwajulishe watu wake wokovu, Kwa kusamehewa dhambi zao. Kwa njia ya rehema za Mungu wetu, Ambazo kwa hizo mwangaza utokao juu umetufikia, Kuwaangaza wakaao katika giza na uvuli wa mauti, Na kuiongoza miguu yetu kwenye njia ya amani. Yule mtoto akakua, akaongezeka nguvu rohoni, akakaa majangwani hadi siku ile alipotokeza hadharani kwa Israeli.
Luka 1:3-80 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
nimeona vema mimi nami, kwa kuwa nimejitafutia usahihi wa mambo hayo yote tangu mwanzo, kukuandikia kwa taratibu, Theofilo mtukufu, upate kujua hakika ya mambo yale uliyofundishwa. Zamani za Herode, mfalme wa Uyahudi, palikuwa na kuhani mmoja, jina lake Zakaria, wa zamu ya Abiya, na mkewe alikuwa mmojawapo wa uzao wa Haruni, jina lake Elisabeti. Na wote wawili walikuwa wenye haki mbele za Mungu, wakiendelea katika amri zote za Bwana na maagizo yake bila lawama. Nao walikuwa hawana mtoto, maana Elisabeti alikuwa tasa, na wote wawili ni wazee sana. Basi ikawa, alipokuwa akifanya kazi ya ukuhani katika taratibu ya zamu yake mbele za Mungu, kama ilivyokuwa desturi ya ukuhani, kura ilimwangukia kuingia katika hekalu la Bwana ili kufukiza uvumba. Na makutano yote ya watu walikuwa wakisali nje saa ya kufukiza uvumba. Akatokewa na malaika wa Bwana, amesimama upande wa kuume wa madhabahu ya kufukizia. Zakaria alipomwona alifadhaika, hofu ikamwingia. Lakini yule malaika akamwambia, Usiogope, Zakaria, maana dua yako imesikiwa, na mkeo Elisabeti atakuzalia mtoto mwanamume, na jina lake utamwita Yohana. Nawe utakuwa na furaha na shangwe, na watu wengi watakufurahia kuzaliwa kwake. Kwa sababu atakuwa mkuu mbele za Bwana; hatakunywa divai wala kileo; naye atajazwa Roho Mtakatifu hata tangu tumboni mwa mamaye. Na wengi katika Waisraeli atawarejeza kwa Bwana Mungu wao. Naye atatangulia mbele zake katika roho ya Eliya, na nguvu zake, ili kuigeuza mioyo ya baba iwaelekee watoto, na kuwatilia waasi akili za wenye haki, na kumwekea Bwana tayari watu waliotengenezwa. Zakaria akamwambia malaika, Nitajuaje neno hilo? Maana mimi ni mzee, na mke wangu ni mkongwe wa siku nyingi. Malaika akamjibu akamwambia, Mimi ni Gabrieli, nisimamaye mbele za Mungu; nami nimetumwa niseme nawe, na kukupasha habari hizi njema. Na tazama! Utakuwa bubu, usiweze kusema, mpaka siku ile yatakapotukia hayo, kwa sababu hukuyasadiki maneno yangu; nayo yatatimizwa kwa wakati wake. Na wale watu walikuwa wakimngojea Zakaria, wakastaajabia kukawia kwake mle hekaluni. Alipotoka hali hawezi kusema nao, walitambua ya kuwa ameona maono ndani ya hekalu, naye aliendelea kuwaashiria akakaa bubu. Ikawa siku za huduma yake zilipokuwa zimetimia akaenda nyumbani kwake. Hata baada ya siku zile mkewe Elisabeti alichukua mimba akatawa miezi mitano, akisema, Hivi ndivyo alivyonitendea Bwana katika siku zile alizoniangalia ili kuniondolea aibu yangu mbele ya watu. Mwezi wa sita, malaika Gabrieli alitumwa na Mungu kwenda mpaka mji wa Galilaya, jina lake Nazareti, kwa mwanamwali bikira aliyekuwa ameposwa na mtu, jina lake Yusufu, wa mbari ya Daudi; na jina lake bikira huyo ni Mariamu. Akaingia nyumbani kwake akasema, Salamu, uliyepewa neema, Bwana yu pamoja nawe. Naye akafadhaika sana kwa ajili ya maneno yake, akawaza moyoni, Salamu hii ni ya namna gani? Malaika akamwambia, Usiogope, Mariamu, kwa maana umepata neema kwa Mungu. Tazama, utachukua mimba na kuzaa mtoto mwanamume; na jina lake utamwita Yesu. Huyo atakuwa mkuu, ataitwa Mwana wa Aliye juu, na Bwana Mungu atampa kiti cha enzi cha Daudi, baba yake. Ataimiliki nyumba ya Yakobo hata milele, na ufalme wake utakuwa hauna mwisho. Mariamu akamwambia malaika, Litakuwaje neno hili, maana sijui mume? Malaika akajibu akamwambia, Roho Mtakatifu atakujilia juu yako, na nguvu zake Aliye juu zitakufunika kama kivuli; kwa sababu hiyo hicho kitakachozaliwa kitaitwa kitakatifu, Mwana wa Mungu. Tena, tazama, jamaa yako Elisabeti naye amechukua mimba ya mtoto mwanamume katika uzee wake; na mwezi huu ni wa sita kwake yeye aliyeitwa tasa; kwa kuwa hakuna neno lisilowezekana kwa Mungu. Mariamu akasema, Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana; na iwe kwangu kama ulivyosema. Kisha malaika akaondoka akaenda zake. Basi, Mariamu akaondoka siku hizo, akaenda hata nchi ya milimani kwa haraka mpaka mji mmoja wa Yuda, akaingia nyumbani kwa Zakaria akamwamkia Elisabeti. Ikawa Elisabeti aliposikia kule kuamkia kwake Mariamu, kitoto kichanga kikaruka ndani ya tumbo lake; Elisabeti akajazwa Roho Mtakatifu; akapaza sauti kwa nguvu akasema, Umebarikiwa wewe katika wanawake, naye mzao wa tumbo lako amebarikiwa. Limenitokeaje neno hili, hata mama wa Bwana wangu anijilie mimi? Maana sauti ya kuamkia kwako ilipoingia masikioni mwangu, kitoto kichanga kikaruka kwa shangwe ndani ya tumbo langu. Naye heri aliyesadiki; kwa maana yatatimizwa aliyoambiwa na Bwana. Mariamu akasema, Moyo wangu wamwadhimisha Bwana, Na roho yangu imemfurahia Mungu, Mwokozi wangu; Kwa kuwa ameutazama Unyonge wa mjakazi wake. Kwa maana, tazama, tokea sasa Vizazi vyote wataniita mbarikiwa; Kwa kuwa Mwenye nguvu amenitendea makuu, Na jina lake ni takatifu. Na rehema zake hudumu vizazi hata vizazi Kwa hao wanaomcha. Amefanya nguvu kwa mkono wake; Amewatawanya walio na kiburi katika mawazo ya mioyo yao; Amewaangusha wakuu katika viti vyao vya enzi; Na wanyonge amewakweza. Wenye njaa amewashibisha mema, Na wenye mali amewaondoa mikono mitupu. Amemsaidia Israeli, mtumishi wake; Ili kukumbuka rehema zake; Kama alivyowaambia baba zetu, Ibrahimu na uzao wake hata milele. Mariamu akakaa naye kadiri ya miezi mitatu, kisha akarudi kwenda nyumbani kwake. Ikawa, siku za kuzaa kwake Elisabeti zilipotimia, alizaa mtoto mwanamume. Wakasikia jirani zake na jamaa zake ya kwamba Bwana amemwongezea rehema zake, wakafurahi pamoja naye. Ikawa siku ya nane wakaja kumtahiri mtoto; wakataka kumpa jina la babaye, Zakaria. Mamaye akajibu akasema La, sivyo; bali, ataitwa Yohana. Wakamwambia, Hapana mtu katika jamaa zako aitwaye jina hilo. Wakamwashiria babaye wajue atakavyo kumwita. Akataka kibao, akaandika ya kwamba, Jina lake ni Yohana. Wakastaajabu wote. Papo hapo kinywa chake kikafunguliwa na ulimi wake pia, akaanza kunena akimsifu Mungu. Wakaingiwa na hofu wote waliokuwa wakikaa karibu nao; na mambo hayo yote yakatangazwa katika nchi yote ya milima milima ya Uyahudi. Na wote walioyasikia wakayaweka mioyoni mwao, wakisema, Mtoto huyu atakuwa wa namna gani? Kwa sababu mkono wa Bwana ulikuwa pamoja naye. Na Zakaria, baba yake, akajazwa Roho Mtakatifu, akatabiri, akisema, Atukuzwe Bwana, Mungu wa Israeli, Kwa kuwa amewajia watu wake, na kuwakomboa. Ametusimamishia pembe ya wokovu Katika mlango wa Daudi, mtumishi wake. Kama alivyosema tangu mwanzo Kwa kinywa cha manabii wake watakatifu; Tuokolewe na adui zetu Na mikononi mwao wote wanaotuchukia; Ili kuwatendea rehema baba zetu, Na kulikumbuka agano lake takatifu; Uapo aliomwapia Ibrahimu, baba yetu, Ya kwamba atatujalia sisi, Tuokoke mikononi mwa adui zetu, Na kumwabudu pasipo hofu, Kwa utakatifu na kwa haki Mbele zake siku zetu zote. Nawe, mtoto, utaitwa nabii wake Aliye juu, Kwa maana utatangulia mbele za uso wa Bwana umtengenezee njia zake; Uwajulishe watu wake wokovu, Katika kusamehewa dhambi zao. Kwa njia ya rehema za Mungu wetu, Ambazo kwa hizo mwangaza utokao juu umetufikia, Kuwaangaza wakaao katika giza na uvuli wa mauti, Na kuiongoza miguu yetu kwenye njia ya amani. Yule mtoto akakua, akaongezeka nguvu rohoni, akakaa majangwani hata siku ya kutokea kwake kwa Israeli.
Luka 1:3-80 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
mimi nami baada ya kuchunguza kila kitu kwa uangalifu kuanzia mwanzo, niliamua kukuandikia habari za mambo hayo, ewe mtukufu Theofilo, ili upate kujua ukweli kuhusu yale uliyofundishwa. Wakati wa utawala wa Herode mfalme wa Yudea, palikuwa na kuhani mmoja jina lake Zakaria, aliyekuwa wa ukoo wa kikuhani wa Abiya. Elizabeti mkewe alikuwa pia mzao wa Haruni. Zakaria na Elizabeti mkewe wote walikuwa watu wanyofu mbele za Mungu, wakizishika amri zote za Bwana na maagizo yote bila lawama. Lakini walikuwa hawana watoto, kwa sababu Elizabeti alikuwa tasa; nao wote wawili walikuwa wazee sana. Siku moja ilipokuwa zamu ya kikundi cha Zakaria, yeye akifanya kazi ya ukuhani Hekaluni mbele za Mungu, alichaguliwa kwa kura kwa kufuata desturi za ukuhani, kuingia Hekaluni mwa Bwana ili kufukiza uvumba. Nao wakati wa kufukiza uvumba ulipowadia, wale wote waliokuwa wamekusanyika ili kuabudu walikuwa nje wakiomba. Ndipo malaika wa Bwana, akiwa amesimama upande wa kuume wa madhabahu ya kufukizia uvumba, akamtokea Zakaria. Zakaria alipomwona huyo malaika, akafadhaika sana, akajawa na hofu. Lakini malaika akamwambia, “Usiogope, Zakaria, kwa maana Mungu amesikia maombi yako. Mkeo Elizabeti atakuzalia mtoto wa kiume, nawe utamwita jina Yohana. Yeye atakuwa furaha na shangwe kwako, nao watu wengi watashangilia kwa sababu ya kuzaliwa kwake. Kwa kuwa atakuwa mkuu mbele za Bwana, kamwe hataonja mvinyo wala kinywaji chochote cha kulevya, naye atajazwa Roho Mtakatifu hata kabla ya kuzaliwa kwake. Naye atawageuza wengi wa Waisraeli warudi kwa Bwana Mungu wao. Naye atatangulia mbele za Bwana katika roho na nguvu ya Eliya, ili kuigeuza mioyo ya baba kuwaelekea watoto wao, na wasiotii warejee katika hekima ya wenye haki, ili kuwaweka tayari watu walioandaliwa kwa ajili ya Bwana.” Zakaria akamuuliza malaika, “Jambo hilo linawezekanaje? Mimi ni mzee na mke wangu pia ana umri mkubwa.” Malaika akamjibu, akamwambia, “Mimi ni Gabrieli, nisimamaye mbele za Mungu, nami nimetumwa kwako ili nikuambie habari hizi njema. Basi sasa kwa kuwa hujaamini maneno yangu ambayo yatatimizwa kwa wakati wake, utakuwa bubu hadi siku ile mambo haya yatakapotukia.” Wakati huo watu walikuwa wanamngojea Zakaria nje huku wakishangaa kukawia kwake mle Hekaluni. Alipotoka akawa hawezi kusema nao, wao wakatambua kuwa ameona maono ndani ya Hekalu. Lakini kwa kuwa alikuwa bubu, akawa anawaashiria kwa mikono. Muda wake wa kuhudumu Hekaluni ulipomalizika, akarudi nyumbani mwake. Baada ya muda usio mrefu, Elizabeti mkewe akapata mimba, naye akajitenga kwa miezi mitano. Elizabeti akasema, “Hili ndilo Bwana alilonitendea aliponipa kibali na kuniondolea aibu yangu mbele ya watu.” Mwezi wa sita baada ya Elizabeti kupata mimba, Mungu alimtuma malaika Gabrieli aende Galilaya katika mji wa Nazareti, kwa mwanamwali bikira aliyekuwa ameposwa na mtu mmoja jina lake Yusufu wa nyumba ya Daudi. Jina la huyu mwanamwali bikira ni Mariamu. Naye malaika akaja kwake akamwambia: “Salamu, wewe uliyebarikiwa, Bwana yu pamoja nawe!” Mariamu akafadhaishwa sana na maneno haya, akajiuliza moyoni salamu hii ni ya namna gani. Ndipo malaika akamwambia, “Usiogope, Mariamu; umepata kibali kwa Mungu. Tazama, utachukua mimba, nawe utamzaa mtoto wa kiume na utamwita jina Yesu. Yeye atakuwa mkuu, naye ataitwa Mwana wa Aliye Juu Sana. Bwana Mungu atampa kiti cha utawala cha Daudi baba yake. Ataimiliki nyumba ya Yakobo milele, na ufalme wake hautakuwa na mwisho.” Mariamu akamuuliza huyo malaika, “Maadamu mimi ni bikira, jambo hili litawezekanaje?” Malaika akamjibu, “Roho Mtakatifu atakujilia juu yako, nazo nguvu zake Yeye Aliye Juu Sana zitakufunika kama kivuli. Kwa hiyo mtoto atakayezaliwa atakuwa mtakatifu, naye ataitwa Mwana wa Mungu. Tazama, jamaa yako Elizabeti amechukua mimba katika uzee wake, na huu ni mwezi wake wa sita, yeye aliyeitwa tasa. Kwa maana kwa Mungu hakuna lisilowezekana.” Mariamu akasema, “Tazama, mimi ni mtumishi wa Bwana. Na iwe kwangu kama ulivyosema.” Kisha malaika akaondoka, akamwacha. Wakati huo Mariamu akajiandaa, akaharakisha kwenda katika mji mmoja kwenye nchi ya vilima ya Yudea. Akaingia nyumbani mwa Zakaria na kumsalimu Elizabeti. Naye Elizabeti aliposikia salamu ya Mariamu, mtoto aliyekuwa tumboni mwake akaruka. Elizabeti akajazwa na Roho Mtakatifu, akapaza sauti kwa nguvu, akasema, “Umebarikiwa wewe miongoni mwa wanawake, naye mtoto utakayemzaa amebarikiwa. Lakini ni kwa nini mimi nimepata kibali kiasi hiki, hata mama wa Bwana wangu afike kwangu? Mara tu niliposikia sauti ya salamu yako, mtoto aliye tumboni mwangu aliruka kwa furaha. Amebarikiwa yeye aliyeamini kwamba lile Bwana alilomwambia litatimizwa.” Naye Mariamu akasema: “Moyo wangu wamwadhimisha Bwana, nayo roho yangu inamfurahia Mungu Mwokozi wangu, kwa kuwa ameangalia kwa fadhili unyonge wa mtumishi wake. Hakika tangu sasa vizazi vyote vitaniita aliyebarikiwa, kwa maana yeye Mwenye Nguvu amenitendea mambo ya ajabu: jina lake ni takatifu. Rehema zake hudumu kizazi hadi kizazi, kwa wale wanaomcha. Kwa kuwa ametenda mambo ya ajabu kwa mkono wake; amewatawanya wale wenye kiburi ndani ya mioyo yao. Amewashusha watawala toka kwenye viti vyao vya utawala, lakini amewainua wanyenyekevu. Amewashibisha wenye njaa kwa vitu vizuri, bali matajiri amewafukuza mikono mitupu. Amemsaidia mtumishi wake Israeli, kwa kukumbuka ahadi yake ya kumrehemu Abrahamu na uzao wake milele, kama alivyowaahidi baba zetu.” Mariamu akakaa na Elizabeti karibu miezi mitatu, kisha akarudi nyumbani mwake. Ulipowadia wakati wa Elizabeti kujifungua, alizaa mtoto wa kiume. Majirani zake na jamii zake wakasikia jinsi Bwana alivyomfanyia rehema kuu, nao wakafurahi pamoja naye. Siku ya nane wakaja kumtahiri mtoto, wakataka yule mtoto aitwe Zakaria, ambalo ndilo jina la baba yake. Lakini mama yake akakataa na kusema, “Hapana! Jina lake ataitwa Yohana.” Wakamwambia, “Hakuna mtu yeyote katika jamaa yako mwenye jina kama hilo.” Basi wakamfanyia Zakaria baba yake ishara ili kujua kwamba yeye angependa kumpa mtoto jina gani. Akaomba wampe kibao cha kuandikia na kwa mshangao wa kila mtu akaandika: “Jina lake ni Yohana.” Papo hapo kinywa chake kikafunguliwa na ulimi wake pia, akaanza kuongea, huku akimsifu Mungu. Majirani wote wakajawa na hofu ya Mungu, na katika nchi yote ya vilima ya Yudea watu walikuwa wakinena kuhusu mambo haya yote. Kila aliyesikia habari hizi alishangaa akauliza, “Je, mtoto huyu atakuwa mtu wa namna gani?” Maana mkono wa Bwana ulikuwa pamoja naye. Zakaria, baba yake, akajazwa na Roho Mtakatifu, naye akatoa unabii, akisema: “Ahimidiwe Bwana, Mungu wa Israeli, kwa kuwa amewajilia watu wake na kuwakomboa. Naye ametusimamishia pembe ya wokovu katika nyumba ya Daudi mtumishi wake, (kama alivyonena kwa vinywa vya manabii wake watakatifu tangu zamani), kwamba atatuokoa kutoka kwa adui zetu, na kutoka mikononi mwao wote watuchukiao: ili kuonesha rehema kwa baba zetu na kukumbuka agano lake takatifu, kiapo alichomwapia baba yetu Abrahamu: kutuokoa kutoka mikononi mwa adui zetu, tupate kumtumikia yeye pasipo hofu katika utakatifu na haki mbele zake, siku zetu zote. “Nawe mtoto wangu, utaitwa nabii wa Aliye Juu Sana; kwa kuwa utamtangulia Bwana na kuandaa njia kwa ajili yake, kuwajulisha watu wake wokovu utakaopatikana kwa kusamehewa dhambi zao, kwa ajili ya wingi wa rehema za Mungu wetu, nuru inayotoka juu itatuzukia ili kuwaangazia wale wanaoishi gizani na katika uvuli wa mauti, kuiongoza miguu yetu katika njia ya amani.” Yule mtoto akakua na kuongezeka nguvu katika roho; akaishi nyikani hadi siku ile alipojionesha hadharani kwa Waisraeli.