Walawi 6:1-7
Walawi 6:1-7 Biblia Habari Njema (BHN)
Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose, “Ikiwa mtu yeyote ametenda dhambi na kumwasi Mwenyezi-Mungu kwa kumdanganya jirani yake juu ya amana au dhamana aliyowekewa, au kumnyanganya au amemdhulumu mwenzake, au amepata kitu cha jirani yake kilichopotea, akasema kwamba hakukiona, au ameapa uongo juu ya chochote ambacho watu hufanya wakawa na hatia, mtu huyo anapokuwa ametenda dhambi na amekuwa na hatia, ni lazima arudishe alichoiba au alichopata kwa dhuluma, au amana aliyopewa, au kitu cha jirani yake kilichopotea akakipata, au chochote alichoapa kwa uongo. Atalipa kila kitu kikamilifu na kuongeza sehemu ya tano ya thamani yake. Mara atakapojua kosa lake atamrudishia mwenyewe. Kisha atamletea kuhani kondoo dume au mbuzi dume asiye na dosari amtolee Mwenyezi-Mungu sadaka ya kuondoa hatia; thamani ya mnyama huyo itakuwa ile ya kawaida ya kuondoa hatia. Kuhani atamfanyia ibada ya upatanisho mbele ya Mwenyezi-Mungu, naye atasamehewa kosa ambalo alikuwa amelifanya.”
Walawi 6:1-7 Swahili Revised Union Version (SRUV)
BWANA akanena na Musa, na kumwambia, Mtu awaye yote akifanya dhambi, na kuasi juu ya BWANA, akamdanganya mwenziwe katika jambo la amana, au la mapatano, au la kunyang'anya, au kumwonea mwenziwe; au kupata kitu kilichopotea na kutenda la uongo juu yake, na kuapa kwa uongo; katika mambo hayo yote mojawapo atakalolitenda mtu, na kufanya dhambi kwalo; ndipo itakapokuwa, akiwa amefanya dhambi, na kupata hatia, atarudisha hicho alichokipata kwa kunyang'anya, au kitu kile alichokipata kwa kuonea, au ile amana aliyowekewa, au kitu kile kilichopotea alichokipata yeye, au kitu chochote ambacho amekiapia uongo; atakirudisha hata kwa utimilifu wake, kisha ataongeza na sehemu ya tano zaidi juu yake; naye atampa huyo mwenyewe, siku hiyo ambayo atakapohukumiwa kuwa mwenye hatia. Kisha ataleta sadaka yake ya hatia kwa BWANA, ni kondoo dume wa katika kundi lake, mkamilifu, sawasawa na hesabu utakayomwandikia, kuwa sadaka ya hatia, na kumpa kuhani; na huyo kuhani atafanya upatanisho kwa ajili yake mbele za BWANA, naye atasamehewa; katika jambo lolote alifanyalo hata akapata kuwa mwenye hatia kwalo.
Walawi 6:1-7 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
BWANA akanena na Musa, na kumwambia, Mtu awaye yote akifanya dhambi, na kuasi juu ya BWANA, akamdanganya mwenziwe katika jambo la amana, au la mapatano, au la kunyang’anya, au kumwonea mwenziwe; au kuzumbua kitu kilichopotea na kutenda la uongo juu yake, na kuapa kwa uongo; katika mambo hayo yote mojawapo atakalolitenda mtu, na kufanya dhambi kwalo; ndipo itakapokuwa, akiwa amefanya dhambi, na kupata hatia, atarudisha hicho alichokipata kwa kunyang’anya, au kitu kile alichokipata kwa kuonea, au ile amana aliyowekewa, au kitu kile kilichopotea alichokizumbua yeye, au kitu cho chote ambacho amekiapia uongo; atakirudisha hata kwa utimilifu wake, kisha ataongeza na sehemu ya tano zaidi juu yake; naye atampa huyo mwenyewe, siku hiyo ambayo atakapohukumiwa kuwa mwenye hatia. Kisha ataleta sadaka yake ya hatia kwa BWANA, ni kondoo mume wa katika kundi lake, mkamilifu, sawasawa na hesabu utakayomwandikia, kuwa sadaka ya hatia, na kumpa kuhani; na huyo kuhani atafanya upatanisho kwa ajili yake mbele za BWANA, naye atasamehewa; katika jambo lo lote alifanyalo hata akapata kuwa mwenye hatia kwalo.
Walawi 6:1-7 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
BWANA akamwambia Mose: “Kama mtu yeyote akitenda dhambi, naye si mwaminifu kwa BWANA kwa kumdanganya jirani yake kuhusu kitu fulani alichokabidhiwa, au kimeachwa chini ya utunzaji wake, au kimeibwa, au kama akimdanganya, au akiokota mali iliyopotea na akadanganya, au kuapa kwa uongo, au kama akitenda dhambi yoyote ambayo watu waweza kuitenda; wakati akitenda dhambi hizo na kuwa mwenye hatia, ni lazima arudishe kile alichokuwa amekiiba au amekichukua kwa dhuluma, au alichokuwa amekabidhiwa, au mali iliyokuwa imepotea akaipata, au chochote alichokuwa amekiapia kwa uongo. Lazima akirudishe kikamilifu, na aongeze sehemu ya tano ya thamani yake, vyote ampe mwenye mali siku ile anapeleka sadaka yake ya hatia. Kisha kama adhabu lazima amletee kuhani, yaani kwa BWANA, kama sadaka yake ya hatia, kondoo dume asiye na dosari na mwenye thamani kamili kutoka kundi lake. Kwa njia hii kuhani atafanya upatanisho kwa ajili yake mbele za BWANA, naye atasamehewa kwa kosa lolote katika mambo hayo aliyoyatenda yaliyomfanya kuwa na hatia.”