Walawi 16:29-34
Walawi 16:29-34 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
“Hili litakuwa agizo la kudumu kwa ajili yenu: Katika siku ya kumi ya mwezi wa saba ni lazima mfunge, wala msifanye kazi yoyote, iwe mzawa au mgeni anayeishi miongoni mwenu, kwa sababu siku hii upatanisho utafanyika kwa ajili yenu ili kuwatakasa. Kisha mtakuwa safi mbele za BWANA kutokana na dhambi zenu zote. Ni Sabato ya mapumziko, na lazima mfunge; ni agizo la kudumu. Kuhani ambaye ametiwa mafuta na kuwekwa wakfu ili kuingia mahali pa baba yake kama kuhani mkuu atafanya upatanisho. Atavaa mavazi matakatifu ya kitani, na kufanya upatanisho kwa ajili ya Patakatifu pa Patakatifu, Hema la Kukutania na madhabahu, na pia kwa ajili ya makuhani, pamoja na jumuiya yote ya watu. “Hili litakuwa agizo la kudumu kwa ajili yenu: Upatanisho utafanywa mara moja tu kwa mwaka kwa ajili ya dhambi zote za Waisraeli.” Ndivyo ilivyofanyika, kama vile BWANA alivyomwamuru Mose.
Walawi 16:29-34 Biblia Habari Njema (BHN)
“Hili ni sharti ambalo mnapaswa kulifuata milele: Siku ya kumi ya mwezi wa saba, nyinyi wenyewe na hata wageni wanaoishi miongoni mwenu, ni lazima mfunge siku hiyo na kuacha kufanya kazi. Mtafanya hivyo kwa sababu siku hiyo ndiyo siku ambayo mtafanyiwa ibada ya upatanisho, msafishwe dhambi zenu, nanyi mtakuwa safi mbele ya Mwenyezi-Mungu. Siku hiyo ni siku ya mapumziko kamili nanyi mtafunga. Kanuni hiyo ni ya kudumu milele. Kuhani aliyepakwa mafuta na kuwekwa wakfu ashike nafasi ya baba yake, ndiye atakayefanya ibada ya upatanisho akiwa amevaa mavazi matakatifu ya kitani. Atafanya ibada ya upatanisho kwa ajili ya mahali patakatifu sana, kwa ajili ya hema la mkutano, madhabahu, makuhani na kwa ajili ya jumuiya nzima ya Israeli. Hili, basi ni sharti la kudumu milele; ni lazima mlifuate ili kufanya ibada ya upatanisho kwa ajili ya watu wa Israeli mara moja kila mwaka na kusamehewa dhambi zao.” Mose akafanya yote kama alivyoamriwa na Mwenyezi-Mungu.
Walawi 16:29-34 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Amri hii itakuwa amri ya milele kwenu; katika mwezi wa saba, siku ya kumi ya mwezi, mtajinyima, msifanye kazi ya namna yoyote, mzalia na mgeni akaaye kati yenu. Kwa maana siku hiyo upatanisho utafanywa kwa ajili yenu, ili kuwatakasa; nanyi mtatakaswa na dhambi zenu zote mbele za BWANA. Ni Sabato ya raha ya makini kwenu nanyi mtajinyima; ni amri ya milele. Na kuhani atakayetiwa mafuta na kuwekwa wakfu badala ya baba yake, ataufanya huo upatanisho, naye atayavaa mavazi ya kitani, yaani, yale mavazi matakatifu. Naye atafanya upatanisho kwa ajili ya patakatifu, naye atafanya upatanisho kwa ajili ya hema ya kukutania, na kwa ajili ya madhabahu; naye atafanya upatanisho kwa ajili ya makuhani, na kwa ajili ya watu wote wa kusanyiko. Na amri hii itakuwa amri ya milele kwenu, ili kufanya upatanisho kwa ajili ya wana wa Israeli kwa sababu ya dhambi zao zote, mara moja kila mwaka. Naye akafanya vile vile kama BWANA alivyomwamuru Musa.
Walawi 16:29-34 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Amri hii itakuwa amri ya milele kwenu; katika mwezi wa saba, siku ya kumi ya mwezi, mtajitaabisha roho zenu, msifanye kazi ya namna yo yote, mzalia na mgeni akaaye kati yenu. Kwa maana siku hiyo upatanisho utafanywa kwa ajili yenu, ili kuwatakasa; nanyi mtatakaswa na dhambi zenu zote mbele za BWANA. Ni Sabato ya raha ya makini kwenu nanyi mtajitaabisha roho zenu; ni amri ya milele. Na kuhani atakayetiwa mafuta na kuwekwa wakfu badala ya baba yake, ataufanya huo upatanisho, naye atayavaa mavazi ya kitani, yaani, yale mavazi matakatifu. Naye atafanya upatanisho kwa ajili ya patakatifu, naye atafanya upatanisho kwa ajili ya hema ya kukutania, na kwa ajili ya madhabahu; naye atafanya upatanisho kwa ajili ya makuhani, na kwa ajili ya watu wote wa kusanyiko. Na amri hii itakuwa amri ya milele kwenu, ili kufanya upatanisho kwa ajili ya wana wa Israeli kwa sababu ya dhambi zao zote, mara moja kila mwaka. Naye akafanya vile vile kama BWANA alivyomwamuru Musa.