Maombolezo 5:1-22
Maombolezo 5:1-22 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ee BWANA, kumbuka yaliyotupata; Utazame na kuiona aibu yetu. Urithi wetu umegeuka kuwa mali ya wageni; Na nyumba zetu kuwa mali ya makafiri. Tumekuwa yatima waliofiwa na baba; Mama zetu wamekuwa kama wajane. Tumekunywa maji yetu kwa fedha; Kuni zetu twauziwa. Watufuatiao wa juu ya shingo zetu; Tumechoka tusipate raha yo yote. Tumewapa hao Wamisri mkono; Na Waashuri nao, ili tushibe chakula. Baba zetu walitenda dhambi hata hawako; Na sisi tumeyachukua maovu yao. Watumwa wanatutawala; Hakuna mtu wa kutuokoa na mikono yao. Twapata chakula kwa kujihatarisha nafsi zetu; Kwa sababu ya upanga wa nyikani. Ngozi yetu ni nyeusi kama tanuu; Kwa sababu ya hari ya njaa ituteketezayo. Huwatia jeuri wanawake katika Sayuni; Na mabikira katika miji ya Yuda. Wakuu hutungikwa kwa mikono yao; Nyuso za wazee hazipewi heshima. Vijana huyachukua mawe ya kusagia; Na watoto hujikwaa chini ya kuni. Wazee wameacha kwenda langoni; Na vijana kwenda ngomani. Furaha ya mioyo yetu imekoma; Machezo yetu yamegeuka maombolezo. Taji ya kichwa chetu imeanguka; Ole wetu! Kwa kuwa tumetenda dhambi. Kwa sababu hiyo mioyo yetu imezimia; Kwa ajili ya hayo macho yetu hayaoni vema. Kwa ajili ya mlima Sayuni ulio ukiwa, Mbweha hutembea juu yake. Wewe, BWANA, unadumu milele; Kiti chako cha enzi ni tangu kizazi hata kizazi. Mbona watusahau sikuzote; Na kutuacha muda huu mwingi? Ee BWANA, utugeuze kwako, nasi tutageuka; Zifanye mpya siku zetu kama siku za kale. Isipokuwa wewe umetukataa kabisa; Nawe una hasira nyingi sana juu yetu.
Maombolezo 5:1-22 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Kumbuka, Ee BWANA, yaliyotupata, tazama, nawe uione aibu yetu. Urithi wetu umegeuziwa kwa wageni, na nyumba zetu kwa wageni. Tumekuwa yatima wasio na baba, mama zetu wamekuwa kama wajane. Ni lazima tununue maji tunayokunywa, kuni zetu zapatikana tu kwa kununua. Wanaotufuatilia wapo kwenye visigino vyetu, tumechoka na hakuna pumziko. Tumejitolea kwa Misri na Ashuru tupate chakula cha kutosha. Baba zetu walitenda dhambi na hawapo tena, na sisi tunachukua adhabu yao. Watumwa wanatutawala na hakuna wa kutuokoa mikononi yao. Tunapata chakula chetu kwa kuhatarisha maisha yetu kwa sababu ya upanga jangwani. Ngozi yetu ina joto kama tanuru, kwa sababu ya fadhaa itokanayo na njaa. Wanawake wametendwa jeuri katika Sayuni, na mabikira katika miji ya Yuda. Wakuu wametungikwa juu kwa mikono yao, wazee hawapewi heshima. Vijana wanataabika kwenye mawe ya kusagia, wavulana wanayumbayumba chini ya mizigo ya kuni. Wazee wameondoka langoni la mji, vijana wameacha kuimba nyimbo zao. Furaha imeondoka mioyoni mwetu, kucheza kwetu kumegeuka maombolezo. Taji imeanguka kutoka kichwani petu. Ole wetu, kwa maana tumetenda dhambi! Kwa sababu hiyo, mioyo yetu inazimia, kwa sababu ya hayo, macho yetu yamefifia, kwa ajili ya Mlima Sayuni, ambao unakaa ukiwa, nao mbweha wanatembea juu yake. Wewe, Ee BWANA unatawala milele, kiti chako cha enzi chadumu kizazi hadi kizazi. Kwa nini watusahau siku zote? Kwa nini umetuacha kwa muda mrefu? Turudishe kwako mwenyewe, Ee BWANA, ili tupate kurudi. Zifanye mpya siku zetu kama siku za kale, isipokuwa uwe umetukataa kabisa na umetukasirikia pasipo kipimo.
Maombolezo 5:1-22 Biblia Habari Njema (BHN)
Ukumbuke ee Mwenyezi-Mungu, mambo yaliyotupata! Utuangalie, uone jinsi tulivyoaibishwa! Nchi yetu imekabidhiwa wageni, nyumba zetu watu wengine. Tumekuwa yatima, bila baba, mama zetu wameachwa kama wajane. Maji yetu tunayapata kwa fedha, kuni zetu kwa kuzinunua. Tunalazimishwa kufanya kazi kama punda, tumechoka lakini haturuhusiwi kupumzika. Wamisri na Waashuru tumewanyoshea mikono, ili tupate chakula cha kutosha. Wazee wetu walitenda dhambi na hawapo tena; nasi tunateseka kwa sababu ya makosa yao. Watumwa ndio wanaotutawala, wala hakuna wa kutuokoa mikononi mwao. Chakula chetu twapata kwa kuhatarisha maisha yetu, maana wauaji wanazurura huko mashambani. Ngozi zetu zawaka moto kama tanuri kwa sababu ya njaa inayotuchoma. Wanawake wetu wanashikwa kwa nguvu mjini Siyoni, binti zetu katika vijiji vya Yuda. Wakuu wetu wametungikwa kwa mikono yao; wazee wetu hawapewi heshima yoyote. Vijana wanalazimishwa kusaga nafaka kwa mawe, wavulana wanayumbayumba kwa mizigo ya kuni. Wazee wameacha kutoa mashauri yao, vijana wameacha kuimba. Furaha ya mioyo yetu imetoweka, ngoma zetu zimegeuzwa kuwa ombolezo. Fahari tuliyojivunia imetokomea. Ole wetu kwa kuwa tumetenda dhambi! Kwa ajili hiyo tumeugua moyoni, kwa mambo hayo macho yetu yamefifia. Maana mlima Siyoni umeachwa tupu, mbweha wanazurura humo. Lakini wewe Mwenyezi-Mungu watawala milele, utawala wako wadumu vizazi vyote. Mbona umetuacha muda mrefu hivyo? Mbona umetutupa siku nyingi hivyo? Uturekebishe ee Mwenyezi-Mungu, nasi tukurudie, uturudishie fahari yetu kama zamani. Au, je, umetukataa kabisa? Je, umetukasirikia mno?
Maombolezo 5:1-22 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ee BWANA, kumbuka yaliyotupata; Utazame na kuiona aibu yetu. Urithi wetu umegeuka kuwa mali ya wageni; Na nyumba zetu kuwa mali ya mataifa. Tumekuwa yatima waliofiwa na baba; Mama zetu wamekuwa kama wajane. Tumekunywa maji yetu kwa fedha; Kuni zetu twauziwa. Watufuatiao wako juu ya shingo zetu; Tumechoka, tusipate pumziko lolote. Tumewapa hao Wamisri mkono; Na Waashuri nao, ili tushibe chakula. Baba zetu walitenda dhambi hata hawako; Na sisi tumeyachukua maovu yao. Watumwa wanatutawala; Hakuna mtu wa kutuokoa na mikono yao. Twapata chakula kwa kujihatarisha nafsi zetu; Kwa sababu ya upanga wa nyikani. Ngozi yetu ni nyeusi kama tanuri; Kwa sababu ya joto ya njaa ituteketezayo. Wanawake katika Sayuni wanashikwa kwa nguvu; Na mabikira katika miji ya Yuda. Wakuu hutundikwa kwa mikono yao; Nyuso za wazee hazipewi heshima. Vijana huyachukua mawe ya kusagia; Na watoto hujikwaa chini ya kuni. Wazee wameacha kwenda langoni; Na vijana kwenda ngomani. Furaha ya mioyo yetu imekoma; Machezo yetu yamegeuka maombolezo. Taji ya kichwa chetu imeanguka; Ole wetu! Kwa kuwa tumetenda dhambi. Kwa sababu hiyo mioyo yetu imezimia; Kwa ajili ya hayo macho yetu hayaoni vema. Kwa ajili ya mlima Sayuni ulio ukiwa, Mbweha hutembea juu yake. Wewe, BWANA, unadumu milele; Kiti chako cha enzi ni tangu kizazi hata kizazi. Mbona watusahau sikuzote; Na kutuacha muda huu mwingi? Ee BWANA, utugeuze kwako, nasi tutageuka; Zifanye mpya siku zetu kama siku za kale. Ingawa wewe umetukataa kabisa; Nawe una hasira nyingi sana juu yetu.