Yoshua 6:15-20
Yoshua 6:15-20 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ikawa siku ya saba wakaondoka asubuhi na mapema wakati wa mapambazuko, wakauzunguka mji vivyo hivyo mara saba; ila siku hiyo waliuzunguka huo mji mara saba. Hata mara ya saba makuhani walipozipiga tarumbeta, Yoshua akawaambia watu, Pigeni kelele; kwa maana BWANA amewapeni mji huu. Na mji huu utakuwa wakfu kwa BWANA, mji wenyewe na vitu vyote vilivyomo; isipokuwa Rahabu, yule kahaba, ataishi, yeye na watu wote walio pamoja naye nyumbani, kwa sababu aliwaficha hao wapelelezi tuliowatuma. Na ninyi, msikose kujiepusha na kitu kilichowekwa wakfu; msije mkakitwaa kitu kilichowekwa wakfu, baada ya kukiweka wakfu; nanyi hivyo mtayafanya matuo ya Israeli kuwa yamelaaniwa na kuyafadhaisha. Lakini fedha yote, na dhahabu, na vyombo vya shaba, na chuma, ni vitakatifu kwa BWANA; vitaletwa katika hazina ya BWANA. Basi watu wakapiga kelele, na makuhani wakazipiga tarumbeta; hata ikawa, hapo watu waliposikia sauti ya tarumbeta hao watu wakapiga kelele kwa sauti kuu sana, na ule ukuta wa mji ukaanguka nchi kabisa, hata watu wakapanda juu, wakaingia katika mji, kila mtu akiendelea kukabili mbele; wakautwaa huo mji.
Yoshua 6:15-20 Biblia Habari Njema (BHN)
Siku ya saba, waliamka alfajiri na mapema, wakauzunguka mji huo mara saba kwa namna ileile. Ilikuwa ni siku hiyo tu ambayo waliuzunguka mji huo mara saba. Ilipofika mara ya saba, wakati makuhani walipokwisha piga mabaragumu, Yoshua akawaambia watu, “Pigeni kelele, kwa kuwa Mwenyezi-Mungu amekwisha wapeni huu mji! Mji huo utaangamizwa na kila kitu kilichomo kwani umewekwa wakfu kwa Mwenyezi-Mungu. Rahabu, yule kahaba, ndiye atakayesalimishwa pamoja na wale ambao wamo nyumbani mwake kwa kuwa aliwaficha wapelelezi wetu. Lakini msichukue chochote ambacho kimewekwa wakfu ili kiangamizwe, mkichukua kitu chochote ambacho kimewekwa wakfu ili kiangamizwe mtaifanya kambi ya Israeli kuwa kitu cha kuangamizwa, na hivyo kuiletea balaa. Lakini fedha yote, dhahabu, vyombo vya shaba na chuma ni vitakatifu kwa Mwenyezi-Mungu; hivyo vitawekwa katika hazina ya Mwenyezi-Mungu.” Basi, watu wakapiga kelele huku mabaragumu yanapigwa. Watu waliposikia sauti ya mabaragumu walipiga kelele kubwa, na kuta za mji zikaanguka chini kabisa. Mara watu wakauvamia mji, kila mmoja kutoka mahali aliposimama, wakauteka.
Yoshua 6:15-20 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ikawa siku ya saba wakaondoka asubuhi na mapema wakati wa mapambazuko, wakauzunguka mji vivyo hivyo mara saba; ni siku hiyo tu ambapo waliuzunguka huo mji mara saba. Hata mara ya saba makuhani wakayapiga mabaragumu, Yoshua akawaambia watu, Pigeni kelele; kwa maana BWANA amewapeni mji huu. Na mji huu utakuwa wakfu kwa BWANA, mji wenyewe na vitu vyote vilivyomo; isipokuwa Rahabu, yule kahaba, ataishi, yeye na watu wote walio pamoja naye nyumbani, kwa sababu aliwaficha hao wapelelezi tuliowatuma. Na ninyi, msikose kujiepusha na kitu kilichowekwa wakfu; msije mkakitwaa kitu kilichowekwa wakfu, baada ya kukiweka wakfu; nanyi hivyo mtaifanya kambi ya Israeli kuwa imelaaniwa na kuifadhaisha. Lakini fedha yote, na dhahabu, na vyombo vya shaba, na chuma, ni vitakatifu kwa BWANA; vitaletwa katika hazina ya BWANA. Basi watu wakapiga kelele, na makuhani wakazipiga tarumbeta; hata ikawa, hapo watu waliposikia mlio wa mabaragumu hao watu wakapiga kelele kwa sauti kuu sana, na ule ukuta wa mji ukaanguka chini kabisa, hata watu wakapanda juu, wakaingia katika mji, kila mtu akisonga mbele kukabili; wakautwaa huo mji.
Yoshua 6:15-20 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Siku ya saba, wakaamka asubuhi na mapema wakauzunguka mji kama walivyokuwa wakifanya, isipokuwa siku ile waliuzunguka mji mara saba. Walipouzunguka mara ya saba, makuhani walipopiga baragumu kwa sauti kubwa, Yoshua akawaamuru watu akisema, “Pigeni kelele! Kwa maana BWANA amewapa mji huu! Mji huu pamoja na vyote vilivyomo ndani yake utawekwa wakfu kwa BWANA. Ila Rahabu tu, yule kahaba na wote ambao wako pamoja naye nyumbani mwake ndio watakaosalimishwa, kwa sababu aliwaficha wale wapelelezi tuliowatuma. Lakini mjiepushe na vitu vilivyowekwa wakfu, msije mkachukua chochote katika hivyo, msije mkajiletea maangamizi katika maskani ya Israeli na kuiletea taabu. Fedha yote na dhahabu, vyombo vya shaba na chuma ni vitakatifu kwa BWANA, lazima viletwe katika hazina yake.” Wakati baragumu zilipopigwa, watu walipiga kelele, na katika sauti ya baragumu, na watu kupaza sauti, ukuta ukaanguka; hivyo kila mtu akapanda akiendelea mbele na kuuteka mji.