Yoshua 4:1-24
Yoshua 4:1-24 Biblia Habari Njema (BHN)
Taifa zima lilipokwisha vuka mto Yordani, Mwenyezi-Mungu akamwambia Yoshua, “Chagua watu kumi na wawili miongoni mwa hao Waisraeli, yaani mtu mmoja kutoka kila kabila, uwaagize hivi, ‘Chukueni mawe kumi na mawili kutoka hapa katikati ya mto Yordani, kutoka hapa ilipo miguu ya makuhani, muyachukue mawe hayo, mkayaweke mahali pale ambapo mtalala leo hii.’” Yoshua akawaita hao watu kumi na wawili ambao alikuwa amewateua miongoni mwa Waisraeli, kila kabila mtu mmoja, akawaambia, “Litangulieni sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, mpaka katikati ya mto Yordani. Kila mmoja wenu achukue jiwe begani mwake, jiwe moja kwa ajili ya kila kabila la Israeli. Jambo hilo litakuwa ishara kati yenu; na watoto wenu watakapowauliza siku zijazo ‘Je, mawe haya yana maana gani kwenu?’ Nyinyi mtawaambia, ‘Sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu lilipopitishwa mtoni Yordani, maji ya mto huo yalizuiliwa yasitiririke!’ Kwa hiyo mawe haya yatakuwa ukumbusho kwa Waisraeli milele.” Wale wanaume wakafanya kama walivyoamriwa na Yoshua, wakachukua mawe kumi na mawili kutoka katikati ya mto Yordani, jiwe moja kwa ajili ya kila kabila la Israeli, kama Mwenyezi-Mungu alivyomwambia Yoshua, wakaenda nayo hadi mahali pale walipolala, wakayaweka huko. Yoshua akasimika pia mawe kumi na mawili katikati ya mto Yordani, mahali pale ambapo nyayo za makuhani waliobeba lile sanduku la agano zilisimama. Mawe hayo yako huko mpaka hivi leo. Wale makuhani waliobeba sanduku la agano, walisimama katikati ya mto Yordani mpaka watu walipomaliza kutekeleza kila kitu ambacho Mwenyezi-Mungu alimwamuru Yoshua awaambie watu; Yoshua alifanya yote ambayo Mose alikuwa amemwamuru. Watu wakaharakisha kuvuka mto, na watu wote walipokwisha vuka, wale makuhani wakawatangulia na lile sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu. Wanaume wa kabila la Reubeni na la Gadi na nusu ya kabila la Manase waliwatangulia Waisraeli wakiwa na silaha zao, kama vile walivyoagizwa na Mose. Watu wapatao 40,000 wakiwa na silaha tayari kwa vita walipita mbele ya Mwenyezi-Mungu wakielekea bonde la mji wa Yeriko. Katika siku hiyo Mwenyezi-Mungu akamtukuza Yoshua mbele ya Waisraeli wote, nao wakamheshimu Yoshua maisha yake yote kama walivyomheshimu Mose maishani mwake. Kisha Mwenyezi-Mungu alimwambia Yoshua, “Waamuru makuhani wanaobeba sanduku la maamuzi, watoke mtoni Yordani.” Basi, Yoshua akawaamuru wale makuhani, “Tokeni mtoni Yordani.” Hao makuhani waliokuwa wamebeba lile sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu walipotoka katikati ya mto Yordani, na kukanyaga ukingo wa mto, maji ya mto Yordani yakaanza kutiririka tena, na kufurika kama kwanza. Waisraeli walivuka mto Yordani katika siku ya kumi ya mwezi wa kwanza, wakapiga kambi huko mjini Gilgali, mashariki ya Yeriko. Yoshua akayasimika yale mawe kumi na mawili ambayo waliyachukua kutoka mtoni Yordani, huko Gilgali. Kisha Yoshua akawaambia Waisraeli, “Watoto wenu watakapowaulizeni siku zijazo, ‘Je, mawe haya yana maana gani?’ Mtawaambia hivi: ‘Taifa la Israeli lilivuka mto huu wa Yordani mahali pakavu.’ Mtawaambia kuwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, aliyakausha maji ya mto Yordani kwa ajili yenu mpaka mkavuka, kama alivyokausha bahari ya Shamu, kwa ajili yetu tukavuka, ili watu wote wa dunia wajue kuwa mkono wa Mwenyezi-Mungu una nguvu; nanyi mpate kumcha Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, milele.”
Yoshua 4:1-24 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ikawa, hapo hilo taifa zima lilipokuwa limekwisha vuka Yordani, ndipo BWANA akanena na Yoshua, akamwambia, Haya, twaeni watu wanaume kumi na wawili katika hao watu, kila kabila mtu mmoja, kisha uwaamrishe, kusema, Twaeni mawe kumi na mawili, hapo katikati ya Yordani, mahali hapo miguu ya hao makuhani iliposimama imara, mwende na mawe hayo, mkayaweke mahali pale kambini ambapo mtalala usiku huu. Basi Yoshua akawaita hao watu kumi na wawili, aliokuwa ameteua tangu hapo awali, katika wana wa Israeli, kila kabila mtu mmoja; naye Yoshua akawaambia, Haya, piteni ninyi mtangulie mbele ya sanduku la BWANA, Mungu wenu, mwende pale katikati ya Yordani, mkatwae kila mmoja wenu jiwe moja begani mwake, kwa kadiri ya hesabu ya makabila ya wana wa Israeli; ili kwamba jambo hili liwe ishara kati yenu, hapo watoto wenu watakapowauliza ninyi katika siku zijazo, wakisema, Ni nini maana yake mawe haya? Ndipo mtakapowaambia, Ni kwa sababu maji ya Yordani yaliondoka mbele ya sanduku la Agano la BWANA; hapo lilipovuka Yordani, hayo maji ya Yordani yalisimama; na mawe haya yatakuwa ni ukumbusho kwa wana wa Israeli milele. Basi wana wa Israeli walifanya vile vile kama Yoshua alivyowaamuru, nao wakatwaa mawe kumi na mawili pale katikati ya Yordani, kama BWANA alivyomwambia Yoshua, sawasawa na hesabu ya makabila ya wana wa Israeli; wakayachukua wakavuka nayo hata mahali pale walipolala, nao wakayarundika huko. Kisha Yoshua akapanga mawe kumi na mawili katikati ya Yordani, mahali pale miguu ya hao makuhani waliolichukua hilo sanduku la Agano iliposimama; nayo yapo pale pale hata hivi leo. Kwa kuwa makuhani waliolichukua hilo sanduku walisimama katikati ya Yordani, hadi mambo yote BWANA aliyomwamuru Yoshua awambie hao watu yakaisha, sawasawa na hayo yote Musa aliyokuwa amemwamuru Yoshua; kisha hao watu wakafanya haraka wakavuka. Ikawa watu wote walipokuwa wamekwisha vuka kabisa, hilo sanduku la BWANA likavuka, na hao makuhani, mbele ya macho ya hao watu. Na wana wa Reubeni, na wana wa Gadi na hiyo nusu ya kabila la Manase, wakavuka, wakiwa wamebeba silaha mbele ya wana wa Israeli, kama Musa alivyowaambia; walikuwa kama watu elfu arubaini waliobeba silaha tayari kwa vita, waliovuka mbele ya BWANA, waende vitani, hadi nchi tambarare za Yeriko. Siku ile BWANA alimtukuza Yoshua mbele ya macho ya Israeli wote; nao wakamcha, kama walivyokuwa wakimcha Musa, siku zote za maisha yake. Kisha BWANA akanena na Yoshua, akamwambia, Haya, uwaamuru makuhani, hao waliolichukua sanduku la ushuhuda, kwamba wakwee juu kutoka mle katika Yordani. Basi Yoshua akawaamuru hao makuhani, akawaambia, Haya, kweeni mtoke Yordani. Ilikuwa, hapo hao makuhani waliolichukua sanduku la Agano la BWANA walipokwea juu kutoka mle kati ya Yordani, na nyayo za miguu yao hao makuhani zilipoinuliwa na kutiwa katika nchi kavu, ndipo maji ya Yordani yaliporudi mahali pake, na kufurika katika kingo zake zote, kama yalivyokuwa hapo kwanza. Na hao watu wakakwea kutoka Yordani siku ya kumi ya mwezi wa kwanza, wakapiga kambi Gilgali, katika mpaka wa mashariki wa Yeriko. Na yale mawe kumi na mawili waliyoyatwaa katikati ya Yordani Yoshua akayasimamisha Gilgali. Akawaambia wana wa Israeli, akasema, Watoto wenu watakapowauliza baba zao katika siku zijazo, wakisema, Mawe haya maana yake ni nini? Ndipo mtakapowaarifu watoto wenu mkisema, Israeli walivuka mto huu wa Yordani, kwa njia ya nchi kavu. Kwa sababu BWANA, Mungu wenu aliyakausha maji ya Yordani, mbele yenu, hadi mlipokwisha kuvuka kama BWANA, Mungu wenu, alivyoitenda Bahari ya Shamu, aliyoikausha mbele yetu hata tulipokwisha kuvuka; watu wote wa duniani wapate kujua mkono wa BWANA, ya kuwa ni mkono wenye uweza, na ili nanyi mpate kumcha BWANA, Mungu wenu, milele.
Yoshua 4:1-24 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ikawa, hapo hilo taifa zima lilipokuwa limekwisha vuka Yordani, ndipo BWANA akanena na Yoshua, akamwambia, Haya, twaeni watu waume kumi na wawili katika hao watu, kila kabila mtu mmoja, kisha uwaamrishe, kusema, Twaeni mawe kumi na mawili, hapo katikati ya Yordani, mahali hapo miguu ya hao makuhani iliposimama imara, mwende nayo mawe hayo, mkayaweke nchi kambini, hapo mtakapolala usiku huu. Basi Yoshua akawaita hao watu kumi na wawili, aliokuwa amewaweka tayari tangu hapo, katika wana wa Israeli, kila kabila mtu mmoja; naye Yoshua akawaambia, Haya, piteni ninyi mtangulie mbele ya sanduku la BWANA, Mungu wenu, mwende pale katikati ya Yordani, mkatwae kila mtu wenu jiwe moja begani mwake, kwa kadiri ya hesabu ya kabila za wana wa Israeli; ili kwamba jambo hili liwe ishara kati yenu, hapo watoto wenu watakapowauliza ninyi katika siku zijazo, wakisema, Ni nini maana yake mawe haya? Ndipo mtakapowaambia, Ni kwa sababu maji ya Yordani yalitindika mbele ya sanduku la agano la BWANA; hapo lilipovuka Yordani, hayo maji ya Yordani yalitindika; na mawe haya yatakuwa ni ukumbusho kwa wana wa Israeli milele. Basi wana wa Israeli walifanya vile vile kama Yoshua alivyowaamuru, nao wakatwaa mawe kumi na mawili pale katikati ya Yordani, kama BWANA alivyomwambia Yoshua, sawasawa na hesabu ya kabila za wana wa Israeli; wakayachukua wakavuka nayo hata mahali pale walipolala, nao wakayaweka nchi kuko huko. Kisha Yoshua akapanga mawe kumi na mawili katikati ya Yordani, mahali pale miguu ya hao makuhani waliolichukua hilo sanduku la agano iliposimama; nayo yapo pale pale hata hivi leo. Kwa kuwa makuhani waliolichukua hilo sanduku walisimama katikati ya Yordani, hata mambo yote BWANA aliyomwamuru Yoshua awambie hao watu yakaisha, sawasawa na hayo yote Musa aliyokuwa amemwamuru Yoshua; kisha hao watu wakafanya haraka wakavuka. Ikawa watu wote walipokuwa wamekwisha vuka kabisa, hilo sanduku la BWANA likavuka, na hao makuhani, mbele ya macho ya hao watu. Na wana wa Reubeni, na wana wa Gadi na hiyo nusu ya kabila ya Manase, wakavuka, hali ya kuvaa silaha mbele ya wana wa Israeli, kama Musa alivyowaambia; walipata kama watu arobaini elfu hesabu yao, wenye kuvaa silaha tayari kwa vita, waliovuka mbele ya BWANA, waende vitani, hata nchi tambarare za Yeriko. Siku ile BWANA alimtukuza Yoshua mbele ya macho ya Israeli wote; nao wakamcha, kama walivyokuwa wakimcha Musa, siku zote za maisha yake. Kisha BWANA akanena na Yoshua, akamwambia, Haya, uwaamuru makuhani, hao waliolichukua sanduku la ushuhuda, kwamba wakwee juu kutoka mle katika Yordani. Basi Yoshua akawaamuru hao makuhani, akawaambia, Haya, kweeni mtoke Yordani. Ilikuwa, hapo hao makuhani waliolichukua sanduku la agano la BWANA walipokwea juu kutoka mle kati ya Yordani, na nyayo za miguu yao hao makuhani zilipoinuliwa na kutiwa katika nchi kavu, ndipo maji ya Yordani yaliporudi mahali pake, na kujaa na kuipita mipaka yake, kama yalivyokuwa hapo kwanza. Na hao watu wakakwea kutoka Yordani siku ya kumi ya mwezi wa kwanza, wakapiga kambi Gilgali, katika mpaka wa mashariki wa Yeriko. Na yale mawe kumi na mawili waliyoyatwaa katikati ya Yordani Yoshua akayasimamisha Gilgali. Akawaambia wana wa Israeli, akasema, Watoto wenu watakapowauliza baba zao katika siku zijazo, wakisema, Mawe haya maana yake ni nini? Ndipo mtakapowaarifu watoto wenu mkisema, Israeli walivuka mto huu wa Yordani, kwa njia ya nchi kavu. Kwa sababu BWANA, Mungu wenu aliyakausha maji ya Yordani, mbele yenu, hata mlipokwisha kuvuka kama BWANA, Mungu wenu, alivyoitenda Bahari ya Shamu, aliyoikausha mbele yetu hata tulipokwisha kuvuka; watu wote wa duniani wapate kujua mkono wa BWANA, ya kuwa ni mkono wenye uweza, ili wamche BWANA, Mungu wenu, milele.
Yoshua 4:1-24 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Wakati taifa lote lilipokwisha kuvuka Mto Yordani, BWANA akamwambia Yoshua, “Chagua watu kumi na wawili miongoni mwa watu, kila kabila mtu mmoja, nawe uwaambie wachukue mawe kumi na mawili katikati ya Mto Yordani, palepale makuhani waliposimama, wayachukue na kuyaweka mahali mtakapokaa usiku huu wa leo.” Basi Yoshua akawaita watu kumi na wawili ambao alikuwa amewachagua kutoka miongoni mwa Waisraeli, mtu mmoja kutoka kila kabila, naye akawaambia, “Mtangulie mbele ya Sanduku la BWANA Mungu wenu, mwende katikati ya Mto Yordani. Kila mmoja wenu atainua jiwe begani mwake, kufuatana na hesabu ya makabila ya Waisraeli, kuwa kama ishara katikati yenu. Siku zijazo, wakati watoto wenu watakapowauliza, ‘Ni nini maana ya mawe haya?’ waambieni kwamba maji ya Mto Yordani yaliyokuwa yakitiririka yalitindika mbele ya Sanduku la Agano la BWANA. Wakati lilipovuka Yordani, maji ya Yordani yalitindika. Mawe haya yatakuwa kumbukumbu kwa watu wa Israeli milele.” Hivyo Waisraeli wakafanya kama Yoshua alivyowaagiza. Wakachukua mawe kumi na mawili kutoka katikati ya Mto Yordani, kulingana na hesabu ya kabila za Waisraeli kama BWANA alivyomwambia Yoshua, nao wakayabeba hadi kambini mwao, mahali walipoyatua chini. Yoshua akayasimamisha yale mawe kumi na mawili ambayo yalikuwa katikati ya Mto Yordani, mahali pale ambapo miguu ya makuhani waliobeba Sanduku la Agano iliposimama. Nayo yako huko mpaka leo. Makuhani waliobeba lile Sanduku walibakia wakiwa wamesimama katikati ya Mto Yordani mpaka kila kitu BWANA alichomwamuru Yoshua kilipokuwa kimefanywa na watu, sawasawa na vile Mose alivyokuwa amemwamuru Yoshua. Watu wakafanya haraka kuvuka, na mara tu watu wote walipokwisha kuvuka, Sanduku la BWANA na makuhani wakavuka watu wakiwa wanatazama. Wareubeni, Wagadi na nusu ya kabila la Manase wakavuka mbele ya Waisraeli, wakiwa wamevaa silaha, kama Mose alivyowaamuru. Kiasi cha watu 40,000 waliojiandaa kwa vita walivuka mbele za BWANA hadi nchi tambarare za Yeriko kwa ajili ya vita. Siku ile BWANA akamtukuza Yoshua mbele ya Israeli yote, nao wakamheshimu siku zote za maisha yake, kama vile walivyomheshimu Mose. Basi BWANA akamwambia Yoshua, “Waamuru hao makuhani wanaolibeba Sanduku la Ushuhuda, wapande kutoka ndani ya Mto Yordani.” Kwa hiyo Yoshua akawaamuru hao makuhani akisema, “Pandeni kutoka ndani ya Mto Yordani.” Nao makuhani wakapanda kutoka ndani ya Mto Yordani wakilibeba hilo Sanduku la Agano la BWANA. Mara tu walipoiweka miguu yao penye kingo, nje ya mto, maji ya Yordani yakarudi kufurika kama ilivyokuwa kabla. Siku ya kumi ya mwezi wa kwanza watu walipanda kutoka Yordani na kupiga kambi huko Gilgali, kwenye mpaka wa mashariki ya Yeriko. Naye Yoshua akayasimamisha huko Gilgali yale mawe kumi na mawili ambayo walikuwa wameyachukua katikati ya Mto Yordani. Akawaambia Waisraeli, “Wazao wenu watakapowauliza baba zao siku zijazo wakisema, ‘Mawe haya maana yake ni nini?’ Basi waambieni, ‘Israeli ilivukia mahali pakavu katika Mto Yordani.’ Kwa maana BWANA Mungu wenu alikausha maji ya Yordani mbele yenu, hadi mlipomaliza kuvuka. BWANA Mungu wenu alifanya haya kwa Mto Yordani sawasawa na kile alichoifanyia Bahari ya Shamu wakati alipoikausha mbele yetu hadi tulipomaliza kuvuka. Alifanya hivi ili kwamba mataifa yote ya dunia yapate kujua kuwa mkono wa BWANA ni wenye nguvu, na ili kwamba kila wakati mpate kumcha BWANA Mungu wenu.”